100/recent/ticker-posts
KANAANI MPYA - Lisikilizeni Neno la Bwana............. MAOMBI NA MAOMBEZI --- Tupigie; +255767-155-623 Ujumbe mfupi/Whatsapp; +255620-179-783

JE UNAMPIMA MUNGU KWA KUTAZAMA MAZINGIRA ULIYONAYO???

JE UNAMPIMA MUNGU KWA KUTAZAMA MAZINGIRA ULIYONAYO???

JE UNAMPIMA MUNGU KWA KUTAZAMA MAZINGIRA ULIYO NAYO?
 “…Kristo yu hai ndani yangu,na uhai nilio nao sasa katika mwili ninao katika imani ya mwana wa Mungu,ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.”(galatia 2:20) Paulo aliishi kwa imani. Kwa imani ya namna gani? Kwa imani katika  mwana wa Mungu? Ndiyo, lakini ni zaidi ya hiyo; aliishi siku kwa siku akiamini katika mambo yote kwamba Yesu Kristo alimpenda na akajitoa yeye mwenyewe kwa ajili yake, pasipo kujali chochote kinachoweza kutokea! Hii ni imani ambayo pengine yaweza kuonekana haibadili mazingira yetu mara moja, au pengine haitabadilisha mazingira yetu kabisa, lakini hii ndiyo imani inayotubadilisha sisi wenyewe katika mazingira yetu! Ni imani inayoushinda ulimwengu. Ni imani inayotufanya sisi kuvumilia katika majaribu na matatizo na hutuleta katika ufahamu halisi kuona kuwa Kristo anaishi ndani yetu, na huyafanya mambo yote yafanye kazi kwa uzuri! Ni imani ambayo hutubadilisha sisi na kumtukuza Mungu. Ni imani inayompendeza Mungu! Sasa inakuwaje basi baadhi ya waamini wanafikiri mara moja kuwa Mungu hapendezwi nao kwa sababu tu eti mambo yao wakati mwingine hayaendi sawa au kwa sababu wanakutana na shida? Hiyo siyo imani. Hizo ni imani za kishirikina. Bila sababu yoyote  tunafikiri kuwa majeshi ya giza fulani yapo kinyume nasi na kwamba yanataka kutuadhibu.Tunapokuwa tunafanya aina hii ya hofu na mitazamo ya hasi, tunakuwa hatumheshimu Mungu. Paulo anasema, “Mara tatu nalipigwa na bakora, mara moja nalipigwa kwa mawe, mara tatu nalivunjikiwa jahazi, kuchwa kucha nalipata kukaa kilindini, katika kusafiri mara nyingi, hatari za mito, hatari za wanyang’anyi, hatari kwa taifa langu, hatari kwa mataifa mengine, hatari kwa mjini, hatari za jangwani hatari za baharini, hatari kwa ndugu za uongo. Katika taabu na masumbufu katika kukesha mara nyingi, katika njaa na kiu, katika kufunga mara nyingi, katika baridi na kuwa uchi.(2Kor,11:25-27. Paulo alivunjikiwa na jahazi mara tatu. Je hii inamanisha kuwa Mungu alikuwa kinyume naye? Je Mungu alikuwa anamwadhibu? Bibilia iko wazi kwamba jibu lake ni ‘Hapana’. Paulo anasema, “…twajua yakuwa hakika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema yaani wale walioitwa kwa kusudi lake..”(Warumi 8:28) Kwa hiyo Paulo aliweza kusema, “Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” (Wafilipi 4:12,13) Paulo alikutana na matatizo pamoja na majaribu mengi lakini ushuhuda wake na mafundisho yake ni kuwa tunajua kuwa mambo yote hufanya kazi pamoja kwa wema kwa wao wampendao Mungu! Hii ni yenye nguvu. Hii huingia moja kwa moja kwenye mizizi ya mahusiano yetu pamoja na Mungu. Je, kumtumaini Mungu kwetu kuna zama ndani zaidi kuliko yale yanayotutokea?Je, imani ni kumwamini Mungu katika kufanya mambo tu? Ni zaidi ya hapo. Kujaribiwa kwa imani yetu ni kitu cha thamani kuliko hata dhahabu. Imani ni kumwamini Mungu pale ambapo hakuna chochote kinachotokea, au mambo yanapoonekena kutuendea vibaya. Hii ndiyo imani ya kweli, inaingia ndani zaidi kuliko mazingira ya aina yoyote.Tunashawishika kikamilifu kuhusiana na wema Wake na umaminifu kuliko mazingira yoyote yanayotufanya tutie shaka pendo lake kwaajili yetu. Hii ndiyo imani. Wasikilize watu hawa watatu toka katika Agano la Kale. “Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia anaweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto, naye atatuokoa na mkono wako ee mfalme. Basi kama si hivyo, ujue ee mfalme, sisi hatutakubali kuitumikia miungu yako wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha, (Daniel 3:17-18). Ni mistari ya ajabu namna gani hii! Ndiyo tunajua kuwa Mungu aweza kutuokoa sisi kutoka katika moto huu uwakao, wanasema. Lakini hata kama hatafanya hivyo, haitabadilisha lolote! Tutaendelea kumwabudu Yeye bila kujali kitakachotokea. Baadhi ya wakristo wanaanza kumtiliashaka Mungu na pendo lake eti kwa kuwa tu haonyeshi kuingilia mazingira yao. “Yeye ni mwenye nguvu zote, kwa nini hafanyi lolote? Je, ni kweli anatupenda? Haya ni aina ya mawazo yanayozalishwa na kutokuamini, na yanaungwa mkono na shetaani. Meshak, Shadraki na Abdinego wao hawakusita, wala hawakukaribisha mawazo kama hayo, pasipokujali kilichowatokea wao waliendelea kumwabudu Mungu. Hii haiwezi kutengenezwa au kuiga! Imani hii inatoka ndani kabisa ya moyo wa mtu. Inatokana na kuendelevu wa kujitoa na kumpenda mwokozi wetu kila siku, kwa ajili ya utukufu wa Mungu! Ndiyo sababu Paulo anasema, “Wala si hivyo tu, ila na tufurahi katika dhiki pia, tukijua yakuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi, na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo, na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini, na tumaini halitaharishi, kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa ndani yetu na Roho Mtakatifu tuliye pewa sisi.” (Warumi 5:3-5). Ni ule uzoefu wa kupita katika matatizo ndio unaotufundisha  sisi kuweka  mategemeo yetu tumaini letu katika Mungu, na hii hutusababishia sisi kumjua kwa undani zaidi kuwa yeye ni Mwaminifu, Mwema na wakutegemewa! Ni imani hiyo iliyotokana na majaribu hayo, hiyo ni yenye thamani zaidi kuliko dhahabu. Imani hii inamtukuza Mungu na haitoi nafasi kwa shetani. Mungu aliwaahidi Waisraeli kuwapatia nchi inayo miminika maziwa na asali, na watu wa Mungu walikusudia kufurahia huku wakimwona Mungu akiwafanyia mambo kwa niaba yao, kwa kuwafungulia njia katika bahari ya shamu na kuwashindia dhidi ya Wamisri. Lakini mara tu shida ilipowajia waliangukia katika kutokuamini, na sio tu walimlaumu Musa, bali walimlaumu Mungu mwenyewe kwa kusimama kinyume nao. Wao walimshtaki Mungu hata kusema kuwa Mungu aliwachukia wao na kwamba amewaleta hadi jangwani ili kuwaangamiza humo! (Kumb.1:27) Hapo ndipo kutokuamini kwaweza kutuleta sisi kama tutairuhusu! Je kukoje moyoni mwako? Kwa sababu ya kutokuamini kwao Waisraeli wengi hawakuweza kuingia katika nchi ile ya ahadi. Walimpima Mungu kwa kujilinganisha na mazingira yao kwa nje. Lakini Mungu amekwisha kuridhia pendo lake kwa ajili yetu, na amelionyesha pendo lake kwa kutukomboa kutoka katika nguvu za adui! Hatupaswi kumpima Mungu kwa mazingira ya nje.Tunapaswa kumtegemea yeye kwa sababu ya kile ambacho amekwisha kukifanya kwa ajili yetu. Na kwa sababu yeye ni Mungu. Mazingira yetu yanayobadilikabadilika hayambadilishi Yeye! Wala imani yetu katika yeye isibadilike kwa sababu tu eti mazingira yetu ni magumu. Kama unataka kumpima Mungu kwa kuangalia mazingira yako kwa nje, basi mpime yeye kwa mazingira haya – Pale Calvari! Kama unataka kufahamu jinsi Mungu anavyojisikia kukuhusu wewe, tazama pale Calvari. Mungu alitoa kitu cha thamani zaidi ambacho angeweza kutoa kwa ajili yako – alimtoa mwanae pekee. Alitupenda sisi zaidi hata akamtoa mwanae pekee Yesu Kristo afe pale Calvari! “Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi” (Warumi 5:8). Haya ndiyo mazingira yanayoonyesha pendo la Mungu kwa ajili yetu. Ni tukio kubwa zaidi ambalo halijawahi kutokea! Umpime Mungu kwa mazingira haya, yaani ya Calvari, na mazingira mengine yote yawayo katika maisha yako utayaona na macho mapya! Kwa hiyo Paulo anaenda mbali zaidi katika kusema kuwa… “Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu, kama utukufu ule utao funuliwa kwetu”(warumi 8:18) Kila siku maisha yetu yanapaswa kuwa ni dhabihu iliyo hai ya upendo, kutafakari, utii, sifa na kumtegemea Mungu kikamilifu yeye aliyetupenda na ambaye huyafanya mambo yote yafanye kazi kwa wema. Paulo aliishi namna hiyo na hata alidiriki kusema… “Basi tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu ni nani aliye juu yetu? Yeye asiye mwachia mwanawake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili ya sisi sote atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakaye washitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakaye wahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiyo alikufa, naam, na zaaidi ya hayo amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu tena ndiye anaye tuombea. Ni nani atakaye tutenga na upendo wa Kristo? Je ni dhiki, au shida au adha, au njaa, au uchi, au hatari au upanga? Kama ilivyo andikwa ya kwamba, ‘Kwa ajili yao tuanauawa mchana kutwa. Tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.’ Lakini katika mambo hayo yote tunashinda. Na zaidi ya kushinda kwa yeye aliyetupenda. Kwaa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayo kuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chochote, hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo yesu Bwana wetu.(Warumi 8:31-37) Uitazame Calvari ukaone kuwa Mungu ni kwa ajili yako, yupo kazini ka ajili ya kila mazingira, ili kukufananisha wewe na mimi kwa sura ya Mwanae. Hili ni jambo lenye utukufu; hili ni jambo jema lile alilofanya Mungu ndani yetu, yaani, tufananishwe na mfano wa Mwana Wake! Hicho ndicho kinachosemwa katika warumi 8:29 ambao unafuatia baada ya ule mstari wa 28. Yawezekana unajiuliza, ni jambo gani jema laweza kutoka katika mazingira yenye shida? Jibu la Biblia ni, ‘Yesu Kristo.’ Yesu Kristo ndani yako tumaini lenye utukufu! Kibinadamu tungeweza kusema kuwa mambo mabaya yamemtokea Yakobo. Alimpoteza mtoto wake mmoja. Na tena akatokewa na ukame wa kutisha. Kisha mwanae mwingine akawa amechukuliwa utumwani. Ndipo alipofikiria kuwa anaweza kuwapoteza wanawe wote iwapo atawapeleka Misri tena, na kwa huzuni alipiga kelele.. “Yakobo baba yao akawaambia, ‘Mmeniondolea watoto wangu! Yusuphu hayuko, wala Simioni hayuko, na Benjamini mnataka kumchukua nae. Mambo haya yote yamenipata mimi. (Mwanzo 42:36) ‘Mambo yote haya yako kinyume nami.’ Haya yalikuwa maneno yake. Je umewahi kujaribiwa namna hii? Ukweli ni kwamba Mungu mwenyewe ndiye aliye kuwemo katika mazingira hayo yote ya Yakobo. Mungu alikuwa kazini ilikuletea baraka kubwa Yakobo, pamoja na familia yake yote. Kile ambacho Yakobo alikuwa anakiona kama ni adui, kama ni tishio, kama ni hatari kwake, kumbe ilikuwa ni uhalisia wa mkono wa Mungu mwenyewe katika kumwongoza kuelekea kwenye baraka kubwa. Wakristo wengine wanapoingia katika matatizo huanza kwa urahisi tu kumlaumu shetani, au pale mambo yanapokuwa hayafanyiki kama wanavyopenda yawe. Wanavurugikiwa badala ya kujitoa maisha yao kama dhabihu iliyo hai katika mazingira yao ili kwamba ipate kuthibitisha kile kilicho chema, chenye kukubalika na mapenzi makamilifu ya Mungu katika maishaa yao (Warumi 12:2) Usifikiri kuwa Mungu yu kinyume nawe. Jikabidhi kwake, ujitoe kwake, pasipo masharti. Yeye anakupenda, na kama ilivyo kuwa kwa Yakobo, ni vilevile kwako wewe . Ataendelea kufanyakzi katika maisha yako ili kukuletea baraka timilifu katika Kristo Yesu. Mungu hayupo pale ili kutimiza matarajio na ndoto zetu, au hata mipango yetu. Yeye hufanya kazi ili kutubariki katika Kristo Yesu. Kwa vyovyote shetani yupo kazini, na hufanya mambo kujaribu kuangamiza kazi za Mungu, na kuwanyanganya watu wa Mungu ule urithi wao ulimo katika Kristo Yesu. Lakini wewe utaweza tu kuelewa nini ni nini katika maisha yako, na katika mazingira yako pale tu utakapojitoa maisha yako kama dhabihu iliyo hai kikamilifu na pasipo malalamiko au masharti kwa Mungu kila siku! Vinginevyo unaweza kujikuta wewe mwenyewew ukipambana kinyume na Mungu, huku ukifikiria labda ni shetani katika mazingira yako, kama vile ilivyo kuwa kwa Yakobo. Yusufu mwana wa Yakobo alipitia katika kuushuhudia uovu mwingi kinyume naye, na mazingira ambayo kwa uhakika yalikuwa magumu na yasiyo ya haki – alichukiwa na hatimaye akauzwa utumwani na ndugu zake yeye mwenyewe, alisingiziwa na mke wa bosi wake, pasipo haki akatupwa gerezani, lakini mwisho wa hayo yote, yeye alisema nini? “nanyi kweli mlikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa kama ilivyo leo.” (Mwanzo 50.20). Ni maneno ya ajabu ya jinsi gani! Hakuna uchungu. Hakuna malalamiko. Yusuph aligundua mkono wa Mungu katika mazingira yake yote. Sio maombo yote yaliyomtokea Yusuph yakuwa sawa; mambo yasiyo kweli yalimtokea Yusufu. Alipitia katika mambo ya  mateso, alivumilia na kuwa mnyenyekevu, lakini alikabidhi maisha yake na roho yake kwa Mungu katika mambo yote na akamwabudu Mungu. Hakupambana au kufanyia ushawishi katika mazingira yake ili kupata kile alichotaka apate. Mungu alifanya kazi kwa niaba yake ili kumletea utimilifu wa baraka. Basi na Mungu afanye hivyo katika maisha yetu yote.

Post a Comment

0 Comments