SOMO: AINA ZA MAARIFA YA UTUKUFU WA MUNGU NA FAIDA ZAKE - Mwakasege
UTANGULIZI
Lengo la somo hili ni kutaka kumsaidia kila mtu anayesoma somo hili kujua aina za maarifa zinazohusiana na utukufu wa Mungu ili aweze kunufaika na utukufu wa Mungu.
JAMBO LA KWANZA
1. UTUKUFU WA MUNGU UNAPOTOKEA HUWA UNABEBA KITU KWA ULIOWATOKEA
Yesu alikuja akiwa amebeba utukufu, na maandiko yanazungumza kwenye Yohana 1:14 yanasema “tukauona utukufu wake utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”
Kwa hiyo ndani ya ule utukufu uliofunuliwa ambao Yesu aliubeba kulikuwa na neema na kweli. Japo kulikuwa na vitu vingine ndani yake lakini haya maneno mawili yaani neema na kweli yamebeba vitu vingi sana ndani yake.
Hesabu 16:41-50 inatuonyesha siku Bwana aliposhuka kwa ajili kuwapiga wana Israel kwa tauni baada ya kunung'unika. Siku ile lilishuka wingu na kufunika hema lakini na utukufu wa Bwana ulionekana.
Hapa tunaona ya kuwa si kila mahali ambapo utukufu wa Mungu unapofunuliwa si kila mahali unakuja na baraka, kuna muda unakuja kuleta adhabu kwa watu. Kwa hiyo ni muhimu sana uwe na maarifa ya utukufu wa Mungu.
Biblia inazungumza kuwa kuna wakati utukufu wa Mungu unakuja ukiwa umebeba adhabu. Usipokuwa na maarifa ya kuzuia hiyo adhabu isikupate au ukachelewa kama Haruni alivyochelewa kwa dakika chache walikufa watu 14,700. Japo kuna watu waliopona kwa toba aliyoifanya wakati ule.
JAMBO LA PILI
2. YESU AMEWAPA WATU WAKE UTUKUFU WA MUNGU KAMA ALIOPEWA YEYE NA MUNGU
Katika Yohana 17:5,22 nataka uone hiki kipengele kinachosema utukufu ule ulionipa nimewapa wao kwa hiyo Yesu katupa utukufu ambao na yeye alipewa na Mungu.
Kama usipoelewa utukufu maana yake nini hautajua thamani ya kitu ulichopewa. Biblia inasema aliuvua ule utukufu ili aweze kufanya kile ambacho Mungu alikuwa amekikusudia kutokana na neema aliyokuwa akitembea nayo.
2 Wakorintho 3:18
“Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.”
Kuna mabadiliko ambayo Mungu huendelea kubadilisha ndani yako ambayo anayabadilisha kwa muonekano wa utukufu aliokupa. Biblia inasema tunabadilishwa ili tuweze kufanana na mfano wa uo utukufu toka utukufu kwenda utukufu
Kazi ya utukufu ambao Yesu katupa ni ili tuwe na umoja kama yeye alivyo na umoja na Baba yake.
Kuna tofauti ya utukufu unaotokea tunapokuwa na umoja na utukufu ule ambao unakuja kutusaidia ili tuwe na umoja. Utukufu ambao anaouzungumza kwenye mstari huu ni ule utukufu ambao unakuja ili kutusaidia tuweze kuwa na umoja.
Kwa hiyo ni rahisi sana kuweza kujua kama umoja haupo katikati ya watu wa Mungu basi utukufu haupo au umepungua, kwa sababu kazi mojawapo ya utukufu huu ambao tumepewa ni ili tuwe na umoja
JAMBO LA TATU
3. TUNAHITAJI MAFUNDISHO YA ELIMU YA UTUKUFU WA MUNGU ILI TUPATE MAARIFA YAKE
2 Wakorintho 4:6
“Kwa kuwa Mungu, aliyesema, Nuru itang'aa toka gizani, ndiye aliyeng'aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo.”
Habakuki 2:14
“Kwa maana dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa Bwana, kama maji yaifunikavyo bahari.”
Mstari ule wa Wakorintho unazungumza juu ya elimu ya utukufu wa Mungu na mstari ule wa Habakuki unazungumza juu ya maarifa ya utukufu wa Mungu.
Elimu imebeba vitu vitatu ndani yake:
- Masomo
- Mfumo wa kufundisha hayo masomo
- Lengo la kufundisha hayo masomo.
Kwa hiyo anaposema elimu ya utukufu wa Mungu ina maana kuna masomo yanayoendana na utukufu wa Mungu, kuna mfumo wa kuyafundisha na kuna lengo lake la kufundisha.
Kwa hiyo kila elimu kutokana na ngazi yake kuna vitu inabeba. Kazi ya elimu ni kumsaidia mtu ili siku akihitaji maarifa ayapate. Elimu yako inaweza ikakusaidia kufaulu masomo darasani, lakini haiwezi kukusaidia kufaulu mtihani wa maisha.
Ndio maana ukisoma Hosea 4:6 inasema Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa haisemi wanaangamizwa kwa kukosa elimu.
Huwezi kuwa na maarifa bila kuwa na chanzo fulani ambacho kinakuletea vitu ndani ambavyo vitakusaidia ndani yake upate maarifa.
JAMBO LA NNE
4. KUKOSA MAARIFA YA UTUKUFU WA MUNGU KUNAWEZA KUKUKWAMISHA KIMAISHA
Habakuki 2:14
Kwa maana dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa BWANA, kama maji yaifunikavyo bahari.
Ukisoma hapo bahari sio maji, bahari ni mahali maji yanakaa. Katika uumbaji kuna kipindi fulani kulijaa maji kabisa. Biblia inasema Mungu akayatenga maji, mengine yakaenda juu na mengine chini.
Yale yaliyoenda chini akayaamuru yajikusanye na sehemu kavu ikatokea. Mungu aliumba viumbe ambavyo vitaishi ndani ya maji yaliyoko baharini na mazingira ya baharini ambayo yatasaidia hivyo viumbe viweze kuishi na kustawi. Jambo hilo limefananisha na utukufu wa Mungu.
Biblia inasema dunia itajazwa na maarifa ya utukufu wa Mungu, sasa haiwezi kujazwa na maarifa ya utukufu wa Mungu kama utukufu wa Mungu haupo na unahitaji kutumika.Mungu hafanyi kazi ya hasara hawezi kukupa maarifa ambayo huyahitaji.
Biblia inazungumza kuwa Dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa Mungu. Inamaanisha utukufu wa Mungu utakuwepo. Anapozungumza juu ya kuwepo kwa utukufu wa Mungu anazungumza juu ya mazingira ya kiroho ambavyo yatafunuliwa kwa jinsi ya mwili. Neno Utukufu linatokana na jamii ya neno tukuka, julikana, fahamika, heshimika.
Utukufu wa Mungu kwa lugha ya kawaida ni Mungu kujifunua kwa namna ambayo inajulikana yeye ni Mungu na hauwezi kuwa utukufu bila kuonekana upande huu kwa jinsi ya mwili. Naye Neno akafanyika mwili nasi tukauona utukufu wake. Utukufu unaonekana.
Kwa Mungu mazingira ni muhimu kuliko kitu kinachoishi kwenye mazingira. Kabla hajatengeneza kitu kwenye yale mazingira lazima akitengenezee kwanza mazingira la sivyo hana sababu ya kukiumba hakitaishi; kitakufa ndio maana mwanadamu ana umuhimu wake, hakuumbwa tu siku ya kwanza. Mwanadamu angeumbwa siku ya kwanza ingekuwa shida tupu.
Biblia inasema hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na nchi nayo nchi ilikuwa ukiwa utupu na giza na Roho Mtakatifu akatulia juu ya uso wa maji hakukuwa na mahali pa kukaa kwa hiyo isingekuwa sahihi kwa jinsi tunavyotazama maandiko, kumuumba mwanadamu siku ya kwanza, pili, tatu, nne na tano. Bali alisubiri siku ya mwisho ya sita ndipo alipomuumba mwanadamu kwa sababu alihitaji amtengenezee mazingira yote anayoyahitaji kwa ajili ya kuishi vizuri ndipo akamweka.
Mungu hakuumba mbegu mpaka alipohakikisha nchi kavu imetokea na jua limekaa mahali pake.
Nataka ufahamu, Mungu alimuumba mwanadamu aishi kwenye mazingira yanayoitwa utukufu wake, kama vile Samaki alivyoumbiwa kukaa kwenye mazingira yanayoitwa maji. Ukimtoa Mwanadamu kwenye Utukufu wa Bwana anakufa maana yake hawezi kufikia kiwango ambacho Mungu anataka.
Sasa unapokosa kujua Utukufu wa Mungu ukoje hata ukitokea utaujuaje? Licha ya kwamba unaweza usijue hata maarifa ya aina ngapi yanayoweza kukusaidia. Ngoja nikupe Mifano yake kidogo
Katika 1 Samweli 4:21 tunaona neno “Ikabodi” likitokea. Walikuwa wanajua kabisa Mungu akiingia katikati ya vita wanayopigana mazingira ya ushindi yanabadilika ni lazima washinde kwa hiyo walipoenda kupigana na Wafilisti wakapigwa. Kwa hiyo wakaagiza sanduku la agano liletwe. Sanduku lilikuwa linawakilisha uwepo wa Mungu na sanduku lilipoingia walipiga kelele mno kiasi ambacho kambi ya Wafilisti wakajua kuwa Mungu wao ameingia kambini, wakatiana moyo.
Baada ya kujipa moyo Wafilisti wakaenda tena kupigana vita na Wayahudi, na Wayahudi walishindwa na sanduku lile likatwaliwa na wale vijana wa kuhani Eli wakafa. Habari ilipopelekewa kwa Kuhani Eli akaanguka na kufa.
Kilichomuua kuhani Eli sio mtoto wake kufa bali sanduku la agano kutwaliwa. Mkwe wake mmoja alikuwa mjamzito akapata uchungu hapo hapo akazaa. Mtoto akamwita Ikabodi maana yake utukufu umeondoka. Haikusema Mungu ameondoka imesema Utukufu umeondoka
Mungu aliamua kunyamaza, kwa sababu kazi mojawapo ya utukufu ni kudhihirisha upande huu kwa njia ya mwili uwepo wa Mungu kwa ajili yao na wale Wafilisti wakalichukua sanduku wakalipeleka kwa Mungu wao dagoni ili kumsifia kwamba amewasaidia na kesho yake asubuhi wakamkuta dagoni wao ameanguka.
Kwa sababu walifikiri kwa kuwashinda watu wa Mungu wamemshinda Mungu wao, kwa sababu Mungu wa watu wa Mungu kaamua kunyamaza asiwapiganie shetani asije akafikiri Mungu ameenda Likizo. Mungu alikuwa ni Mungu wao Mungu wa Agano. Kama utukufu unaweza kuondoka inamaanisha unaweza kurudi.
Warumi. 3:23
kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;
Haijasema hivi “wote wamefanya dhambi wanaenda Jehanamu” kuna adhabu yake lakini hapa anasema wamepungukiwa na utukufu wa Mungu, na kama hujui utukufu maana yake nini basi huwezi kuelewa kupungukiwa maana yake nini pia. Na huwezi kujua hasara yake kwa hiyo utatembea bila kujua.
Watu wengi sana hawajajua kwa sababu kama ni dhambi utukufu unaweza kuongezeka kama ukitubu. Hutubu kwa ajili ya kwenda mbinguni bali kwa ajili ya kurudisha utukufu wa Mungu. Ukiletewa huu mstari wakati unaomba anazungumzia kwa ajili ya utukufu na kama unakuja kukusaidia, anasema umejaa neema na kweli inamaanisha kutakuwa na kitu adimu kimepungua Biblia inazungumza wazi kabisa kwamba utukufu wa Bwana unabeba kitu na unabeba sauti au ujumbe wa Mungu.
1 Wafalme 8:10 - 11
Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya BWANA ikajaa wingu; hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya BWANA ilikuwa imejaa utukufu wa BWANA.
Sulemani anaweka wakfu hekalu na wingu likatokea likaijaza ile nyumba, Makuhani walishindwa kufanya kazi kwa sababu ya lile wingu na ule utukufu. Sidhani kama ule utukufu na lile vilikuja kuwanyima wasifanye kazi lakini ninakuambia utukufu wa Mungu unaweza kukufanya ukashindwa kufanya kazi wakati Mungu alikuja kukusaidia kufanya kazi.
USHUHUDA
Nilikuwa mahali fulani tulikuwa na mkutano wa ndani na sehemu kubwa ilikuwa ni Wachungaji na Wakristo wa kawaida wa eneo lile na tulikuwa tunafanya semina ilipofika mchana tunatakiwa kwenda kula Roho Mtakatifu akaniambia nisiende kula niende kuomba.
Kwa hiyo nikawaeleza wenzangu kuwa siwezi kula chakula na wao wanasema “njoo upate chakula kwa sababu umesimama muda mrefu.” Nikawajibu kuwa “Mungu ameniambia nikaombe,” sikutaka kubishana nao nikaondoka kwenda kuomba.
Tuliporudi kipindi cha mchana na kuendelea na somo nililokuwa ninafundisha, ghafla nikaona wingu likiingia mlangoni (hapo tulikuwa mlimani na ni rahisi sana kusema ni ukungu). Nilitazama nje sioni ila naona wingu likiingia pole pole na likaanza kuwafunika wale waliokuwepo nyuma na kadri unapowafunika ninaona wametulia na sura zimebadilika (wengine machozi yanawatoka huku mimi nikiendelea kufundisha).
Nikaendelea kufundisha na wingu ikasongea mpaka mbele nilipokuwa nimesimama kufundisha na ghafla nikashindwa kufundisha, nguvu za Mungu zikaachilia kitu ambacho Mungu amebeba kwa ajili ya watu wale kwa saa ile na wakati ujao na nikaanza kuona vitu vinavyowahusu kwa kuona maisha yao ya baadae na mipango Mungu aliyoyakusudia na vitu ambavyo havijakaa sawa.
Ratiba iliyokuwepo ilibadilika kabisa ni kwa sababu nguvu na utiisho wa Mungu umeshuka pale ndani. Mungu alinipa kuzungumza na wachungaji wawili ambao wamepanga kuwa wakirudi nyumbani kwao wameamua kuacha wake zao na Mungu akasema tatizo lile linatatulika. Hawakuruhusiwa kuachana kwa sababu wameshajiandaa kuacha wake na utumishi. Nikasema mtu kama huyo ni uamuzi wake atoke hapa mbele au abaki na nilipoita wakatoka wachungaji wawili wakaja mbele.
Sasa usiwashangae hao makuhani kwamba utukufu wa Bwana unakuja na wao wanazubaa hawajui wafanyeje. Si kila mtu anaona ila wako wachache wanaona.
MFANO WA MWISHO
Luka 9:28 - 36
Inaelezea habari za Yesu kuwachukua wanafunzi wake Petro, Yohana na Yakobo. Katika kusali kwao wakashuka Musa na Eliya walioonekana katika utukufu wa Bwana na utukufu wa Bwana ukishuka utajazwa maarifa ya Mungu ukijifunua kuwa Mungu yupo muda wote.
MFANO.
Wakati ule George Bush akiwa Rais wa Marekani alipokuja Tanzania alikaa kwa siku nyingi kidogo lakini angalia watu wa Dar es Salaam walipata kazi kwani lilitoka tangazo la kwamba waliopo bara kama hakuna sababu ya kwenda Dar es Salaam wasiende. Barabara nyingi zilifungwa na mji ukasafishwa na dawa za mbu zilipigwa hata maeneo ambayo Bush hatafika, hii yote ni kwa sababu mfalme anaposhuka mahali inadaiwa mazingira kuandaliwa.
Sasa pale alikaa siku 5 hadi 6 je! akihamia itakuwaje na wengine watakuwa hawaendi Dar es Salaam na sasa akihamia lazima uwe na maarifa ya kukaa Dar es Salaam.
Sasa Biblia inazungumza juu ya Yesu kuwa tuliona utukufu wake nao ukakaa kwetu na akishusha utukufu wake nyumbani kwako hakutabaki kama kulivyo na kila sehemu utakapoenda Naye yumo na utukufu wake utakuwa pamoja nawe baada ya muda ule utukufu ukiisha na Yesu akawaambia wasimwambie mtu yeyote kwa yaliyotokea.
Nikienda Israeli na kupanda kwenye ule mlima nakumbuka sana hili kwa sababu Petro aliposema wajenge vibanda Mungu alimkemea pale pale kuwa asimfananishe Mungu na akina Musa na Eliya na akawaondoa ili heshima Yake pekee ibaki.
USHUHUDA
Nilikuwa naenda mahali kwa kukaribishwa na mtu kwenda kwenye kikundi chao cha huduma. Siku moja kabla ya kwenda waliniambia wametaka kubadilisha ratiba kidogo kwa sababu ya ujio wa kiongozi wa serikali nikawauliza wanabadilisha kwa sababu gani?
Wakasema kwa sababu ana shughuli nyingi, akishamaliza kusema kitu chake ataondoka nawe utaendelea. Ndipo nikawaambia “Hapana! kwa nini aseme tu na asije kusikiliza neno la Bwana? Nikawaambia hakuna kubadilisha ratiba mimi nitaanza naye ndio atanifuata kwa sababu kwenye ratiba hakuwepo” wakabisha na nikawaambia hamna shida wanaweza wakamtafuta mtu mwingine.
Wakaniuliza ni kwa nini? nikawajibu kuwa yeye anawakilisha serikali yake na mimi nawakilisha ufalme wa Mungu (kama utukufu wa Bwana hauko juu yako usiseme hayo maneno).
Na niliposema hayo maneno nikawaambia uamuzi uko juu yao kwa sababu yeye ana maneno ya kwake nami nina maneno ya kwangu baadae wakasema hawatabadilisha ratiba. Baada ya hapo nikaingia maombi maalum nikapanda gari mwenyewe huku nikiendesha naendelea kuomba kuwa wasisikie tu maneno bali wauone utukufu wa Bwana na Mungu ajidhihirishe.
Nikiwa njiani nguvu za Mungu zilifunika ile gari zima kama ukungu na ghafla nikaanza kutokwa na machozi na nikapaki pembeni nikiendelea kuomba muda mrefu kidogo halafu ndipo nikaondoka.
Nilipofika kule tukaingia chumba kimoja na huyo waziri na tukasalimiana vizuri na muda ulipofika tukachukuliwa wote, tukaenda meza kuu (high table) nikaangalia ratiba nikakuta hawajabadilisha na nilipokuja kupewa nafasi nikasimama na nikachapa ile injili ya kumalizana na nikazungumza “umuhimu wa mtu kuokoka.” Kwa sababu nguvu za Mungu zilikuwa zimenifunika hapo nikamgeukia kiongozi huyo na nikasema “Mheshimiwa hutaenda mbinguni kwa sababu umekuwa mwaminifu kwenye kazi unayofanya kwa sababu ukiwa mwaminifu namna hii utapata heshima kwa viongozi wako na kwa wananchi lakini mbinguni ni lazima kuokoka.”
Nikaendelea kuhubiri na baadae kidogo nikaita watu kuokoka na yeye waziri hakuwahi kusikia hata siku moja kuwa kuna kuokoka. Ndipo akamwuliza mwenyekiti wa huo mkutano kuwa hapa Mwakasege anaposema kuokoka sasa ndio anamaanisha nini? Akamjibu hicho anachoeleza hapo ndicho chenyewe kwa hiyo kama na wewe unataka kuokoka usimame tu. Akasimama nikaongoza sala ya toba na yeye akaokoka na akauona utukufu wa Bwana aliyejaa neema na kweli.
Baada ya kumaliza akaomba ya kusema alichopenda kusema na ile haraka waliyosema kuwa anayo sikuiona. Baadae nikamwambia mwenyekiti kuwa umeona inawezekana anaenda sehemu na akifika huko watu hawaelezi habari za kuokoka.
Palipo na utukufu wa Mungu pia kuna utiisho wake, unapompokea Yesu Kristo anajifunua pia.
UTUKUFU KAMA MAZINGIRA YA UWEPO WA KIROHO YALIYO DHIHIRIKA KATIKA ULIMWENGU WA KIMWILI KWA MALENGO MBALIMBALI YA MWENYE UTUKUFU HUO ULIODHIHIRIKA.
Ukisoma Biblia unaweza kuona ya kwamba roho ambazo zinaweza zikaachilia mazingira ya kiroho kuna:-
1.Mungu
2.Mtu
3.Shetani
Na ukiendelea kusoma kwenye Biblia utakuta kuna:-
1.Utukufu wa Mungu huyu aliye hai
2.Utukufu wa mwanadamu
3.Utukufu wa shetani
Utukufu maana yake ni pana sana lakini tuangalie suala la utukufu kama mazingira ya uwepo wa kiroho yaliyo dhihirika katika ulimwengu wa kimwili kwa malengo mbalimbali ya mwenye utukufu huo.
Malengo yako mawili makubwa ambayo unahitaji kukumbuka:-
LENGO LA KWANZA
I. NI KURAHISISHA NA KUWEZESHA UJULIKANAJI WA MWENYE UTUKUFU HUO ULIO DHIHIRIKA
Neno utukufu limetokana na jumuiya ya maneno kadhaa. Ndani ya jumuiya hiyo utakuta kuna neno “tukuka”, “tukuza”, “tukuzo”, tafsiri nyingine maana yake “amejulikana”. “ameheshimika”, “amesifiwa”, “anafahamika”, kwenye Kiswahili chetu hiki cha kisasa tunasema “huyu mtu ni mzito” na kwenye Kiingereza tunasema ana “influence”
LENGO LA PILI
II. NI KURAHISHA NA KUWEZESHA UTEKELEZAJI WA MAKUSUDI NA MIPANGO YA MWENYE UTUKUFU HUO ULIODHIHIRIKA
Mungu anapofunua utukufu wake, cha kwanza anataka ajulikane yeye ni nani, na cha pili anataka kusudi lake na mipango yake itekelezwe. Na kwa shetani ni hivyo hivyo.
Habakuki 2:14
“Kwa maana dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa Bwana, kama maji yaifunikavyo bahari.”
Hosea 4:6 inasema “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa;” inamaanisha maarifa kazi yake ni kutusaidia tusije tukaangamia, bali tufanikiwe, kutumia vitu tunavyopewa vya kutusaidia Kwa hiyo kama Mungu ametupa maarifa hayo yatatusaidia kutumia alichotupa kwa utukufu wake.
Kwa tafsiri hiyo tunaweza tukasema bahari ni eneo na maji ni kile kijazacho mazingira ya eneo liitwalo bahari.
Sasa anaposema “Dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa Bwana” kwa hiyo Dunia ni eneo na utukufu wa Bwana ni kile kijazacho mazingira ya eneo liitwalo Dunia.
Kwa hiyo tukienda kwa tafsiri ya utukufu maana yake ni uwepo wa kiroho wa Bwana Mungu uliodhihirishwa katika eneo linaloitwa Dunia.
MFANO
Kama ni mfanya biashara au unafuatilia masuala ya biashara si tu hapa Tanzania na nje ya nchi kuna kitu kinaitwa mazingira ya kibiashara. Kati ya kipimo kimojawapo ambacho watu wa Benki ya Dunia wanakiangalia na kukifuatilia katika nchi mbalimbali Duniani ni mazingira ya kibiashara, yaani ni rahisi kiasi gani kwa ajili ya kufanya biashara kwa mfanya biashara kufanya biashara yake na wanapima vigezo vingi sana.
Tuangalie kwa ngazi kama mbili hivi:
NGAZI YA KWANZA
1. NI MIFANO ILIYOPO KATIKA AGANO LA KALE
Kwa hiyo ungezungumza kwa lugha ya ki muda wa kiagano, Yesu alipozaliwa na Yohana kutangulia mpaka kufika msalabani kilikuwa kipindi cha Agano la kale kwanini? Kwa sababu Biblia inasema pasipo kumwaga damu hakuna agano.
MFANO WA KWANZA
Kutoka 40:34-38
“Ndipo lile wingu likaifunikiza hema ya kukutania, na huo utukufu wa Bwana ukaijaza maskani. Wala Musa hakuweza kuliingia hema la kukutania, kwa sababu lile wingu lilikaa juu yake, na huo utukufu wa Bwana ukaijaza maskani. Na hapo lile wingu lilipoinuliwa kutoka juu ya maskani, wana wa Israeli wakaenda mbele katika safari zao zote, bali kama lile wingu halikuinuliwa, wakati ule hawakusafiri hata siku ile lilipoinuliwa tena. Kwa maana lile wingu la Bwana lilikuwa juu ya maskani wakati wa mchana, na mlikuwa na moto ndani yake wakati wa usiku, mbele ya macho ya nyumba ya Israeli katika safari zao zote.”
Kwenye kitabu cha Kutoka, Kutoka 25:1-8 utaona Mungu akizungumza na Musa awaambie wana wa Israeli juu ya utoaji wa sadaka kwa kila ambaye moyo wake unapenda. Ule mstari wa 8 hasemi wanijengee hema bali anasema wanifanyie Patakatifu nipate kukaa kati yao
Alipomaliza kujenga, wingu lilikuja na kufunika lile hema na sio tu lilifunika lile hema lakini ndani yake kulionekana utukufu. Kwa hiyo waliweza kutofautisha wingu la kawaida na ule utukufu uliotokea pale.
USHUHUDA
Wakati fulani tulikuwa Dar es Salaam kwenye semina na hakikuwa kipindi cha mvua lakini mvua ikaja. Na hema tulilonalo ni hema la kuzuia jua na si la kuzuia mvua, labda ziwe mvua ndogo ndogo.
Kwa hiyo mvua ilipoanza kuleta shida, na kawaida yetu ya maombi ya asubuhi tulipokuwa tukiomba na kuzunguka ghafla mvua ikaanza, na tukaomba kwa Mungu kwamba mvua ile isubiri na isinyeshe lile eneo mpaka tutakapo maliza semina.
Wakati tunaendelea kuzunguka na kuomba ghafla kwenye kona ya hema niliona upinde wa mvua ukiwa umejikita juu ya hema, nikaangalia kwanza mahali unapoelekea sikuona bali niliona ukiwa umekuja na kujikita juu ya hema.
Nikaichukua simu yangu na kupiga picha na picha ikanasa (maana si kila wakati nikipiga picha vitu vingine huwa vinanasa). Nilielewa ni kitu gani maana haukuwa upinde wa mvua wa kawaida, kwa sababu wakati Mungu ananiita kwenye utumishi kitu kimojawapo ambacho nilikiona ni upinde wa mvua ukinizungumza (niliuona kwa macho haya ya nyama na niliuona kwenye ndoto).
Kwa hiyo nilipouona pale nilijua kabisa si upinde wa kawaida bali ni Mungu anajaribu kunieleza kwa kisinisumbue yeye yupo na Mvua ikanyamaza wakati huo huo.
2 Nyakati 7:1-3
Basi Sulemani alipomaliza maombi hayo, moto ukashuka kutoka mbinguni, ukateketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; utukufu wa BWANA ukaijaza nyumba. Wala makuhani hawakuweza kuingia nyumbani mwa BWANA, kwa kuwa utukufu wa BWANA umeijaza nyumba ya BWANA. Wana wa Israeli wote walipoona ule moto ukishuka, utukufu wa BWANA ulipokuwa katika nyumba, wakasujudu kifudifudi mpaka sakafuni, wakaabudu, wakamshukuru BWANA, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele.
Biblia inakupa kujua ya kwamba utukufu huo unaweza ukajaa nyumbani kwako, ile ilikuwa ni nyumba ya ibada inaweza ikawa ni nyumba binafsi, ofisi, mahali popote pale Mungu anaweza kudhihirisha utukufu wake ukajaa hapo.
Zaburi 63:1-2
Ee MUNGU, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, Mwili wangu wakuonea shauku, Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji. Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu, Nizione nguvu zako na utukufu wako.
Anasema ninapotazama kwenye madhabahu vitu viwili nipate kuviona cha kwanza nataka kuona nguvu zako cha pili utukufu wako. Na unaona kabisa ametofautisha nguvu za Mungu na utukufu wa Mungu.
Kuna watu wanafikiri kwa sababu pana nguvu za Mungu basi utukufu wa Mungu uko hapo! Utukufu ni kujulikana, kuna watu wengine wanataka nguvu za Mungu zifanye kazi lakini utukufu wanachukua wao.
Kutoka 24:15-18
"Musa akapanda mlimani, lile wingu likaufunikiza mlima. Na huo utukufu wa BWANA ukakaa juu ya mlima wa Sinai; lile wingu likaufunikiza siku sita; na siku ya saba akamwita Musa toka kati ya lile wingu. Na kuonekana kwake ule utukufu wa BWANA kulikuwa kama moto uteketezao, juu ya mlima machoni pa wana wa Israeli. Musa akaingia ndani ya lile wingu, akapanda mlimani; Musa akawa humo katika ule mlima siku arubaini, mchana na usiku."
Musa aliona wingu wana wa Israel waliona kama moto ili Kuwazuia wana wa Israel wasije wakathubutu kuingia huko, kama na yeye Musa angeona kama moto unafikiri angeweza kuingia!
Zaburi 85:9-13
Hakika wokovu wake uko karibu na wamchao, Ndipo utukufu wake ukae katika nchi yetu.
Nilitaka nikuonyeshe pia unaweza kujaa ndani ya nchi. Nchi nzima ikajazwa na utukufu wa Mungu. Na nchi ikishajazwa utukufu wa Mungu angalia kinachotokea.
"Fadhili na kweli zitakutana, Haki na amani zitakumbatiana. Kweli itachipuka katika nchi, Haki itachungulia kutoka mbinguni. Naam, BWANA atatoa kilicho chema, Na nchi yetu itatoa mazao yake. Haki itakwenda mbele zake, Na kuzitayarishia hatua zake mapito."
Sio tu Mungu atajulikana yeye ni nani kwa nchi, lakini kuna kitu ambacho nchi itafaidi kama vile utukufu wa Bwana ukifunuliwa katika ofisi yako.
MIFANO YA AGANO JIPYA
Soma Waebrania 8:6, Warumi 8:14, 2 Wakoritho 5:7 na Waefeso 1:15 - 20
Roho wa Mungu alipokuwa akiwaongoza wana wa Israeli alikuwa anakuja kwenye hema, walikuwa wanaangalia uelekeo wa hema ndio wanajua Mungu yuko huko, katika Agano jipya Roho Mtakatifu yuko ndani yetu miili yetu imefanyika hema na hekalu.
Yohana. 17:22
"Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja."
Hakusema ameupunguza alisema “Nimewapa” kama ametupa inamaanisha hatukuwa nao. Angalia
Zaburi 8:4 - 6
"Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima; Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake."
Biblia inazungumza juu ya uumbaji wa mtu, anasema “Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;” Inazungumza juu ya ngazi za uumbaji ukisoma Biblia utaona kuna Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu.
Biblia inatuambia sisi ni wabeba utukufu, katika Agano la Kale utukufu ulibebwa kwenye hema na kwenye hekalu, katika Agano jipya kila mtu alieokoka amebeba utukufu ule ule.
kazi mojawapo ya utukufu ni kubadilisha mazingira ya kiroho, maana yake ukiingia mahali hata usiposema kitu wewe ni tishio
Zaburi 106:19 - 20
Walifanya ndama huko Horebu, Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka. Wakaubadili utukufu wao Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani.
Ukibadilisha miungu unabadilisha utukufu na unajishushia hadhi kwa sababu utukufu una heshima, kwa nini ukatafute utukufu ulio mdogo unaacha wa Yesu alie Bwana wa Mabwana Mfalme wa wafalme?.
USHUHUDA
Nilikuwa mkoa mmoja nikaja kuambiwa kuna msichana mmoja anataka kuja kukuona alikuwa ameongozana na mama mmoja, nikasema ngoja niangalie kama naweza pata nafasi lakini mwishoni nikapata nafasi nikamkaribisha na nilikuwa simjui kabisa.
Akaniambia amekuja kuniomba msamaha, nikamwuliza amekosa nini maana simjui, akaniambia “kabla ya kuokoka nilikuwa namwabudu shetani na tulipewa kazi ya kukuua kwa namna yoyote”. akanieleza yeye mwenyewe, akanieleza jinsi ambavyo nilienda kwenye hoteli nikawa nakula na akajifanya ni mfanyakazi wa pale bila wao kujua akaniwekea sumu kwenye chakula na ile sumu ingeweza kuniua ndani ya dakika tano tu. Na wakanitazama nife lakini sifi wakaamua kutoroka pale na hawakukata tamaa ya kunifuatilia.
“Na siku moja tulikufuatilia tukagundua kuwa ulikuwa unatoka Moshi unaenda Arusha na ulikuwa unaendesha gari peke yako tukakusubiri Bomang'ombe kwenye kituo cha polisi ili watuombee lifti na tulijua huwezi pakia mtu njiani ndio maana tuliomba polisi watusaidie kwa sababu walikuwa hawatujui. Na nia yetu ilikuwa ungeturuhusu tuingie kwenye gari tungesababisha ajali ili ufe.” Basi nilipokuwa naendesha gari na kufika Bomang'ombe Polisi wa Usalama barabarani akanisimamisha na nikasimama.
Yule polisi akaja moja kwa moja nikaona anachungulia nyuma, akasema “Naona mmejaa nilitaka kuwaombea lifti hawa" nikamtazama yule polisi nikasema “kweli tumejaa” mimi sikumbuki kama nilisema bali Roho ndani yangu ndiye aliysema kuwa tumejaa.
Utukufu wa Mungu ukiingia mahali hauji peke yake unakuja ukiwa umejaa Roho Mtakatifu.
Wakati mwingine utakuta Roho Mtakatifu anakuonesha viashiria.
UHURU NA UMOJA
KWA MFANO.
Kwenye 2 Wakorintho 3:17-18 inasema “palipo na Roho wa Bwana pana uhuru” na juu ya wanadamu walipo ndani ya Kristo, kubadilishwa kutoka utukufu hadi utukufu
Sasa ukisoma Yohana 17:22 inasema “Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja.”
Kazi mojawapo ya umoja ni ili tupate kumwinua Kristo apate kujulikana. ili utukufu wa Bwana umejulikana katika mji au kanisa Mahali po pote penye utukufu wa Bwana tofauti hizo zinaweza zikawepo lakini haziwezi zikawa kikwazo cha kuzuia kusimama na mwenzako kuhakikisha jina la Yesu linatukuzwa.
Kiashiria kingine ni
AMANI
Wafilipi 4:6 - 7
“Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
Saa nyingine utakuta unapita mahali pagumu sana na kati ya kitu kifakachokuwa kinatesa na kumwumiza sio hicho kitu bali fikra anazofikiri juu ya hicho kitu kinachomsumbua.
Yakobo kwenye ile Mwanzo 28 alipokuwa anasafiri alilalia jiwe akaota ndoto Mungu akijifunulia kwake kuwa Yeye ndiye Mungu wa agano
Sasa ukisoma Mwanzo 28:16 - 17 inasema “Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli BWANA yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni.”
Wakati anaenda kulala hakuwa na hofu Mungu akaifunua kwa njia ya ndoto na alipoamka ile hofu ya Mungu imezunguka eneo lote kudhihirisha kuwa Bwana amejifunua apate kujijulisha kwa Yakobo na ndio maana Yakobo akamwambia “mimi sikujui)
Mwanzo 28:20 - 21
“Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo BWANA atakuwa Mungu wangu.”
Utukufu wa Bwana ulijifunua kwa njia ya ndoto ili apate kujijulisha kuwa Yeye ni Mungu wa agano.
Zaburi 29:9
“Sauti ya BWANA yawazalisha ayala, Na kuifichua misitu; Na ndani ya hekalu lake Wanasema wote, Utukufu.”
Kama ndani ya hekalu kusingekuwa na utukufu kwa vinywa vyao wasingesema utukufu (glory). (Watu wanafikiri wakati tunahubiri tukisema Glory to God wanadhani ni kibwagizo na yeye sasa kama kesho anahubiri anachomekea ndani).
Kwenye Isaya 6 baada ya mfalme Uzia kufa aliona wale maserafi na alipowaona walikuwa wanasema “Mtakatifu, Mtakatifu” ukikaa kanisani unaona nguvu za Mungu zinashuka na Mungu anajifunua kwako na kukutengenezea ka-utukufu ka-kwako ambako watu wengine hawauoni na huku ukimtukuza Mungu kwa sababu ndani yako ulishafahamu kuwa Mtakatifu anakuzunguka na kuna kitu anakitazama.
Kuna muda ukiwaambia watu wanyanyue mikono juu na nguvu za Mungu zikishuka utakuta wananyanyua mikono juu zaidi. Hii inaashiria kuwa wanasema “ninakuabudu Wewe Mungu uliyehai” na wengine wanaweza wakaona na wengine wanaweza wasione.
Ubarikiwe sana na BWANA Yesu Kristo wa Nazareth.
0 Comments