JINSI YA KUOMBA MWENYEWE NA KUPATA JIBU
YOHANA 16:24
“Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu: OMBENI, NANYI MTAPATA; furaha yenu iwe timilifu”.
<><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><>
Maneno haya aliyasema Yesu Kristo mwenyewe akiwaambia Wanafunzi wake. Tunaona katika maneno haya kwamba, kila mwanafunzi wa Yesu au mtu aliyeokoka, ana haki ya kumwomba Baba yetu aliye mbinguni kwa Jina la Yesu Kristo na akapokea jibu. Yesu hasemi kwamba mtu fulani tu aliyeokoka akiomba, ndiye atakayepata jibu, bali YEYOTE.
MARKO 11:23
“Amin, nawaambia, YEYOTE atakayeuambia mlima huu, ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.”
Maandiko mengi yanadhihirisha jinsi ambavyo kila mtu aliyeokoka alivyo na haki ya kuomba na kupokea jibu na wala siyo mtu fulani pekee. [Angalia mifano katika YOHANA 14:12-14; MATHAYO 7:8-11].
ANGALIA TENA LUKA 11:10; “ Kwa kuwa KILA AOMBAYE HUPOKEA…….”.
Unaona! Kila mtoto wa Mungu, yaani kila mtu aliyeokoka, akiomba, hupokea. Huu ni UHONDO maalum kwa watoto wa Mungu tu. Mtu ambaye hajaokoka, ametenganishwa kabisa na Mungu kutokana na maovu yake. Kutokana na dhambi za mtu ambaye hajaokoka kumfarikisha au kumtenganisha na Mungu, sala zake ni machukizo mbele za Mungu na hazisikilizwi kabisa. [SOMA ISAYA 59:2; MITHALI 28:9; MITHALI 15:29; YOHANA 9:31]. Sala pekee ambayo inasikilizwa na Mungu inapotoka kwa mtu ambaye hajaokoka, ni pale anapotubu dhambi zake na kuwa tayari kuziacha na kuomba damu ya Yesu imsafishe uovu wake; ili aokolewe kutoka katika mauti ya milele [1 YOHANA 1:7-9]. Mtu ambaye hajaokoka, akimpokea Yesu Kristo kuwa Bwana au Mtawala wake na mwokozi wake ndipo anapofanyika MTOTO WA MUNGU na kuanza kufaidi uhondo wa kujibiwa maombi na Baba yetu aliye mbinguni [YOHANA 1:12]. Kabla ya kuokoka, mtu anakuwa ni mtoto wa Ibilisi, na siyo mtoto wa Mungu [YOHANA 8:44]. Kwa sababu hiyo ili uingie katika mpango wa Mungu wa kukupa majibu ya maombi, kwanza ni lazima ukubali kuokolewa na kuwa mtoto wake.
KUTEGEMEA KUOMBEWA NA MWINGINE WAKATI WOTE
Ni huzuni kwamba, wako watoto wa Mungu ambao wanafikiria kwamba wao hawawezi kusikilizwa na Mungu na kujibiwa; mpaka waombewe na mtoto wa Mungu mwingine. Huku ni kukosa ufahamu. Hakuna upendeleo kwa Mungu. Mtoto yeyote katika familia ya Mungu anakubaliwa na Baba aliye Mbinguni. Hakuna mtoto anayekubaliwa na Mungu zaidi anapoomba kuliko mwingine [SOMA MATENDO 10:34-35; WARUMI 2:10-11; KUMB.10:17]. Biblia inasema Mungu hapokei uso wa mwanadamu, yaani hamuoni mtoto wake mmoja kuwa ni bora kuliko wengine kiasi ya kwamba wengine asiwajali [WAGALATIA 2:6]. Eliya alipoomba mvua isinye kwa miaka 31/2; halafu akaomba tena mbingu zikatoa mvua; alikuwa katika hali ya mtoto wa Mungu kama yeyote yule. Alikuwa mwenye tabia moja na sisi, na Mungu hakufanya hayo kwa sababu aliomba Eliya! [YAKOBO 5:17-18].
Watu wengi waliookoka, wanatembea huko na huko katika mikutano wakihitaji kuombewa na watu wengine. Miongoni mwao, wako wanaofikiri sala ya mzungu fulani kutoka Marekani au Uingereza ndiyo ataisikia Mungu zaidi kuliko sala yake. Huku ni kukosa ufahamu. Mungu hapokei uso wa mwanadamu wala hana upendeleo. Kila aaminiye, akiomba hupokea. Ukifanya utafiti, utagundua kwamba, mara nyingi watu ambao wanapokea miujiza wanapoombewa na wengine; ni wale ambao hawajaokoka kabisa, au wale waliookoka lakini wakiwa na muda mfupi sana katika wokovu. Sababu ni kwamba, baada ya mtu kuwa na muda mrefu katika wokovu; unatazamiwa na Mungu kuchukua mwenyewe chakula na kukila bila kungoja kulishwa. Biblia inasema uponyaji ni chakula cha watoto wa Mungu[MATHAYO 15:26]. Katika hali ya asili, mtoto anapozaliwa, katika uchanga hulishwa kwa kijiko na mtu mwingine, kwa sababu hawezi kujilisha mwenyewe. Mtoto huyo anapokua, anatazamiwa achukue kijiko na kula mwenyewe. Haitapendeza kumwona mtoto mwenye miaka kumi, akilishwa chakula na mtu mwingine. Vivyo hivyo katika maombi, kila mtu aliyeokoka anatazamiwa kuomba mwenyewe na kuchukua jibu lake. Kwa kukosa maarifa, watu wengi wa Mungu wameangamia [HOSEA 4:6]; na kukosa majibu ya maombi yao. Yafuatayo ni maarifa unayopaswa kuwa nayo ili upate majibu ya maombi yako kila mara.
A: MAMBO MANNE YA KUYAFAHAMU KABLA YA KUMWOMBA MUNGU LOLOTE
1. Mfahamu Vizuri Mungu Baba na Mungu Mwana
Kwa kuwa tunamwomba Mungu Baba kwa jina la Mungu Mwana-Yesu Kristo, ni vema sana kuwafahamu vizuri ili tuwe na hakika ya kujibiwa. Ufahamu ulio nao kuhusu mtu unayekwenda kumwomba hitaji lako, unaweza ukakupa imani ya kupokea kwake au ukakupunguzia imani hata ya kwenda kumweleza hitaji lako. Ukifahamu kwamba mtu fulani ni katili, ufahamu huo unatosha kuondoa ujasiri wa kumwomba lolote. Kwa kukosa kuwafahamu vizuri Mungu Baba na Mungu Mwana, watu wengi waliookoka wamekosa msingi mzuri wa kujibiwa maombi yao. Kinyume na inavyopasa, msingi wao wa kuomba unakuwa ni manung’uniko ambayo huleta maangamizo badala ya mafanikio [SOMA 1 WAKORINTHO 10:10]. Ukiwafahamu vizuri Mungu Baba na Mungu Mwana, ufahamu huo pekee, utakufanya uwe na hakika ya mambo unayotarajia kuyapata; ingawa hayajaonekana bado. Hii ndiyo inayoitwa IMANI ambayo ni msingi muhimu wa kupewa majibu yetu [WAEBRANIA 11:1,6]. Imani ni kuamini jinsi Neno la Mungu linavyoeleza kuhusu Mungu alivyo kwetu. Ukiwafahamu Mungu Baba na Mwana walivyo huwezi kunung’unika, kubabaika na kukata tamaa. Kunung’unika, Kubabaika na Kukata tamaa; ni kinyume kabisa na Imani. Watu wanaonung’unika, kubabaika na kukata tamaa, ni watu wasiomfahamu Mungu alivyo. Usiwe miongoni mwa watu wa jinsi hiyo, ambao hawawezi kupata majibu ya maombi yao.
Inakubidi basi, kuyafahamu yafuatayo na kuyaamini kabla ya kuomba; ili upate Majibu ya Maombi yako:
Mungu Baba hujishughulisha SANA na kila jambo tunalolihitaji, liwe dogo au kubwa. Wakati wote, fahamu kwamba hitaji ulilonalo anapenda kulishughulikia mno. Anataka tu, umtwike YEYE fadhaiko ulilo nalo. [SOMA 1 PETRO 5:6-7].
Kwa kuwa tunamwomba Mungu Baba kwa jina la Mungu Mwana-Yesu Kristo, ni vema sana kuwafahamu vizuri ili tuwe na hakika ya kujibiwa. Ufahamu ulio nao kuhusu mtu unayekwenda kumwomba hitaji lako, unaweza ukakupa imani ya kupokea kwake au ukakupunguzia imani hata ya kwenda kumweleza hitaji lako. Ukifahamu kwamba mtu fulani ni katili, ufahamu huo unatosha kuondoa ujasiri wa kumwomba lolote. Kwa kukosa kuwafahamu vizuri Mungu Baba na Mungu Mwana, watu wengi waliookoka wamekosa msingi mzuri wa kujibiwa maombi yao. Kinyume na inavyopasa, msingi wao wa kuomba unakuwa ni manung’uniko ambayo huleta maangamizo badala ya mafanikio [SOMA 1 WAKORINTHO 10:10]. Ukiwafahamu vizuri Mungu Baba na Mungu Mwana, ufahamu huo pekee, utakufanya uwe na hakika ya mambo unayotarajia kuyapata; ingawa hayajaonekana bado. Hii ndiyo inayoitwa IMANI ambayo ni msingi muhimu wa kupewa majibu yetu [WAEBRANIA 11:1,6]. Imani ni kuamini jinsi Neno la Mungu linavyoeleza kuhusu Mungu alivyo kwetu. Ukiwafahamu Mungu Baba na Mwana walivyo huwezi kunung’unika, kubabaika na kukata tamaa. Kunung’unika, Kubabaika na Kukata tamaa; ni kinyume kabisa na Imani. Watu wanaonung’unika, kubabaika na kukata tamaa, ni watu wasiomfahamu Mungu alivyo. Usiwe miongoni mwa watu wa jinsi hiyo, ambao hawawezi kupata majibu ya maombi yao.
Inakubidi basi, kuyafahamu yafuatayo na kuyaamini kabla ya kuomba; ili upate Majibu ya Maombi yako:
Mungu Baba hujishughulisha SANA na kila jambo tunalolihitaji, liwe dogo au kubwa. Wakati wote, fahamu kwamba hitaji ulilonalo anapenda kulishughulikia mno. Anataka tu, umtwike YEYE fadhaiko ulilo nalo. [SOMA 1 PETRO 5:6-7].
(b) Ni mapenzi ya Mungu Baba, kukupa haja za moyo wako na kukuona una furaha baada ya kujibiwa maombi [SOMA ZABURI 37:4; YOHANA 16:24].
(c) Mungu Baba anawahurumia watu waliookolewa kama vile Baba awahurumiavyo watoto wake[SOMA ZABURI 103:13]. Linalofurahisha zaidi ni kwamba, Mungu Baba; ni Baba mwenye uwezo wote, tofauti na baba wa duniani ambao wanaweza kuwa na huruma kwa watoto wao, lakini wakakosa uwezo wa kuwasaidia; wakabaki kusema “POLE”, bali huruma ya Mungu huambatana na UWEZO wa kutupa mahitaji yetu; hata yakiwa mazito kiasi gani. [ANGALIA MFANO LUKA 7:13-15].
(d) Mungu kamwe hawasahau, hawaachi, hawapungukii wala hawatupi watoto wake yaani watu waliookoka. Unapokuja mbele za Mungu ukiwa unajiona umeachwa, umesahauliwa au umetupwa; basi ujue unampa nafasi shetani ya kukuangamiza kwa kukosa maarifa ya Neno la Mungu. Tunaweza tu kumshinda shetani kwa “Imeandikwa” yaani kwa Neno la Mungu, kama Yesu alivyomshinda alivyokuwa anajaribiwa na Ibilisi nyikani. Mbinu kubwa ya Ibilisi anayotumia kumshinda mtu aliyeokoka, ni kumfanya akiri tofauti na “Imeandikwa”. Unachotakiwa kufahamu kuanzia leo ni kwamba, Imeandikwa kuwa Mungu hawezi kumsahau, kumuacha au kumtupa mtoto wake, yaani mtu aliyeokoka. Wewe unaweza kumwacha, lakini yeye hawezi kukuacha katika mahitaji unapokaa ndani yake. [SOMA KWA MAKINI ZABURI 94:14; KUMBUKUMBU 31:8; ISAYA 49:14-16; ZABURI 37:25; 1 SAMWELI 12:21-22; 1 WAFALME 6:13; ZABURI 37:28].
(e) Ikiwa Mungu Baba alimtoa mwanawe wa pekee Yesu Kristo ili afe kwa ajili ya dhambi zetu, je hatazidi sana kutupa mambo mengine tunayoyahitaji, ambayo thamani yake siyo kubwa kama thamani ya mwanae wa pekee? [SOMA WARUMI 8:32].
(f) Yesu Kristo ni mzaliwa wa kwanza katika uzao wa Adamu wa pili yaani uzao wa watu waliookoka. Ni kusema kwamba, Yeye ni NDUGU yetu. Yeye ni KAKA YETU wa kwanza kuzaliwa. [SOMA WARUMI 8:29; WAEBRANIA 2:11]. Tafakari jinsi alivyo ndugu wa kwanza kuzaliwa katika familia, hasa anapokuwa wa kiume. Mahitaji yote ya wadogo zake, huyabeba yeye. Ni kaka yupi mwenye uwezo wote wa kuwasaidia wadogo zake, ambaye atawaacha ndugu zake bila msaada? Ikiwa kaka wa duniani wasiokuwa na uwezo wote, wanajitahidi kuwasaidia wadogo zao; ni zaidi sana kwa kaka yetu Yesu Kristo mwenye upendo wote na uwezo wote mbinguni na duniani. Anahusika MNO NA KILA HITAJI walilo nalo wadogo zake. Ndiyo maana anamwita mdogo wake yeyote mwenye kusumbuka na kulemewa na mzigo wowote, aende kwake ampumzishe. [MATHAYO 11:28]. Yesu anataka tumtwike mizigo yetu yote na masumbufu yetu yote, kama jinsi ambavyo Baba anavyotaka tumtwike fadhaa zetu zote!
2. Fahamu jinsi ulivyo wa thamani mbele za Mungu
(a) Wewe ni TAJI YA UZURI katika mkono wa BWANA [ISAYA 62:3]. Jiulize mwenyewe, taji ya uzuri utakubali ichafuliwe na tope au ichanwe? Utaitunza na kuiangalia namna gani?
Wewe ni KILEMBA CHA KIFALME mkononi mwa Mungu wako [ISAYA 62:3]. Kilemba cha kifalme ni kitu cha thamani mno. Kinazidi thamani yake kinapokuwa ni kilemba cha kifalme cha Mungu. Wewe ni kilemba cha Kifalme cha Mungu. Wewe ni wa thamani mno machoni pa Mungu. Jiulize mwenyewe, Mungu ataacha kukitunza kilemba chake cha kifalme?
(b) Anayekugusa wewe na kukutesa, kukuonea, au kukukosesha furaha, anakuwa anaigusa mboni ya jicho la Mungu [ZEKARIA 2:8]. Ikiwa wewe huwezi kukubali kuweka kidole kwenye mboni ya jicho la Mungu. Atafukuzwa kwa utisho mkuu.
(c) Katika mpango wa Mungu, Yesu alikuokoa wewe na kukutoa mahali palipokuwa pakame na jangwa tupu lisilokuwa na matumaini; na kukulaza kwenye majani mabichi. Hataki tena upungukiwe na kitu [ZABURI 23:1-2]. Zaidi ya hayo, kwa kuwa wewe ni wa thamani mno kwake, anakuzunguka na kukulinda kwa uwezo wake wote. Mpango wake, ni kukutunza na kukuhifadhi kama mboni ya jicho[SOMA KUMBUKUMBU 32:10]. Jiulize mwenyewe, Je, unaitunza namna gani mboni ya jicho lako? Kipande kidogo tu cha mchanga kikiingia jichoni, utahangaika mno mpaka kitolewe. Utairuhusu miiba ikaribie kwenye mboni ya jicho lako? Mboni ya jicho ikiingiwa na vumbi kidogo tu, jicho lote hujaa machozi na mwili wote kuhuzunika. Furaha huja tu pale vumbi linapotoka. Ndivyo alivyo Yesu pia unaposumbuliwa wewe mboni ya jicho lake, yeye pia hulia machozi pamoja nawe na kuhakikisha kila kinachokusumbua kinatoweka [YOHANA 11:33-36, 43-44].
(e) Wewe ni KITO AU JIWE LA THAMANI LINALOMETAMETA katika nchi ya Mungu [ZEKARIA 9:16]. Jiwe la thamani linaangaliwaje? Hazina inashughulikiwaje?
(f) Wewe ni HAZINA YA MUNGU [SOMA MALAKI 3:16]. Hazina inalindwaje? Hazina inaangaliwaje? Hazina inatunzwaje? Hazina inashughulikiwaje?
(g) Wewe ni MALI ILIYONUNULIWA KWA THAMANI KUBWA. Ulinunuliwa kwa damu ya YESU ya thamani. [SOMA 1 WAKORINTHO 7:23; 1 WAKORINTHO 6:20]. Jiulize mwenyewe! Mali uliyoinunua kwa thamani kubwa, unailinda na kuitunza namna gani? Mwanadamu anaweza kuwa mzembe, asijue sana kutunza mali; lakini Mungu asiye mzembe kamwe, hakika atakutunza. Wewe ni wa thamani mno kwake!
Wewe ni BIBI-HARUSI, MKE WA MWANA-KONDOO yaani MKE WA YESU [SOMA UFUNUO 21:9]. Biblia inasema, “Kama Bwana-Arusi amfurahiavyo Bibi-Arusi, ndivyo Mungu anavyokufurahia wewe.” [SOMA ISAYA 62:5]. Ikiwa Yesu anakufurahia hivi kama Bibi-Arusi wake, je atakuacha kabisa na asikujali au asikupe mahitaji yake? Dalili ya kumfurahia Bibi-Arusi, ni kuhusika sana na mahitaji yake. Bibi-Arusi anapoomba lolote kwa Bwana-Arusi, mara moja Bwana-Arusi hufanya jitihada yote ili ampe na kumfurahisha. Mabwana-Arusi wa duniani hawana uwezo wote, hivyo hukwama katika kuwatekelezea mahitaji yao yote Mabibi-Arusi wao; lakini Bwana-Arusi Yesu Kristo mwenye uwezo wote, kamwe hashindwi. Lolote unalolihitaji kwake, atakupa ili akufurahishe. Mungu ni MUME WAKO![SOMA YEREMIA 3:14]. Huu ni ukweli wa ajabu! Ikiwa mumeo ni Rais wa Nchi, utakuwa na hakika ya kutunzwa, kuangaliwa na kupewa mahitaji yako! Hata hivyo Rais wa Nchi ana mpaka. Hawezi kukupa mahitaji yako yote. Sasa tafakari ukweli huu kwamba Mungu aliye muumba wa mbingu na nchi ni mumeo! Una haki ya kuringa, kuwa na mume wa namna hii mwenye uwezo wote. Je atashindwa kukupa nini? Ana uwezo wa kutuma watumishi wake malaika, wakuletee chochote ukitakacho.
3. Fahamu kwamba hakuna gumu lisilowezekana kwa Mungu:
Usiupime kamwe uwezo wa Mungu kwa kuulinganisha na uwezo wa mwanadamu. Kufanya hivyo, ni kama kuulinganisha uwezo wa kuangaza kwa JUA na KOROBOI! Kulinganisha kiasi cha uwezo wa Mungu wa kufanya jambo na uwezo wa mwanadamu, ni kama kulinganisha kiasi cha maji kinachotosha kuijaza bahari, na kile kinachotosha kujaza kikombe. Kwake Mungu, hakuna neno ‘HAIWEZEKANI’. Hili ni neno la kibinadamu tu! Mungu anasema ingawa jambo linaweza kuwa haliwezekani mbele za wanadamu na kuwa gumu mno lakini siyo mbele za Mungu. Angalia maandiko.
ZEKARIA 8:6
“Bwana wa majeshi asema hivi, Ingawa hili ni neno lililo gumu mbele ya macho ya mabaki ya watu hawasiku hizo, je! liwe neno gumu mbele ya macho yangu? asema BWANA wa majeshi.
“SOMA PIA YEREMIA 32:17, 27; AYUBU 42:2; MATHAYO 19:26; LUKA 1:37”.
4. Fahamu kwamba magonjwa na umasikini siyo mapenzi ya Mungu kwako:
Magonjwa na umasikini au kutofanikiwa, ni sehemu ya LAANA juu ya mtu asiyetaka kuisikiliza sauti ya BWANA Mungu na kufanya maagizo yake [KUMBUKUMBU 28:15-28]. Yesu alifanyika laana kwa ajili yetu kwa kupigiliwa msalabani ili baraka zitufikie [WAGALATIA 3:13-14]. Kwa kupigwa kwake Yesu na hatimaye kusulubishwa msalabani, alitukomboa kutoka katika:-
(a) Dhambi [MATHAYO 26:28; 1 PETRO 2:24].
(b) Magonjwa na udhaifu wote [MATHAYO 8:14-17; ISAYA 53:4-5;
1 PETRO 2:24].
(c) Umasikini [ 2 WAKORINTHO 8:9].
Magonjwa na udhaifu wote, umasikini na dhambi; zote ni kazi za Ibilisi ambazo zilivunjwa na Mwana wa Mungu [1YOHANA 3:8]. Watu tuliookolewa, hatuko tena chini ya laana. Hivyo kama unavyozikataa na kuzipinga dhambi,vivyo hivyo inakupasa kuyakataa na KUYAPINGA MAGONJWA na Udhaifu wote, na kuukataa umasikini. Hivyo usiseme “Labda ni mapenzi ya Mungu niugue” au “Huenda anataka kunifundisha kwa ugonjwa”. Ni mapenzi ya Mungu UWE MZIMA WA AFYA – Yeye anaitwa YEHOVA-RAPHA AU “BWANA NIKUPONYAYE” [SOMA KUTOKA 15:26; YEREMIA 30:17; YEREMIA 33:6; ZABURI 103:3; YOHANA 10:10; 3 YOHANA 1:2].
Mungu ana njia nyingi za kukufundisha. Hakufundishi kwa kumruhusu shetani akuletee magonjwa! Ukisema ni mapenzi ya Mungu uugue, basi ujue unazidi kumpa nafasi shetani akutese zaidi. Mapenzi ya Mungu, ni Neno la Mungu. Shetani akijua kwamba hulijui neno lililoandikwa, atakutesa! Usimpe nafasi Ibilisi kwa kuzungumza yaliyo kinyume na Neno la Mungu. Mara zote, yapinge magonjwa ukijua kwa kufanya hivyo unampinga shetani; naye atakimbia. Shetani ndiye mleta magonjwa yote. Shetani ndiye aliyeleta magonjwa juu ya Ayubu na kutofanikiwa kote. Ayubu hakujua akasema ni Mungu! Usiwe kama Ayubu. Mjue mbaya wako Shetani! [Angalia WAEFESO 4:27; YAKOBO 4:7; AYUBU 1:12-16; AYUBU 2:2,7]. Hivyo kumbuka kwamba usitumie “Ikiwa ni mapenzi yako” katika kuomba juu ya ugonjwa. Tunatumia maneno haya pale tu tusipokuwa na uhakika wa jambo. Uhakika juu ya ugonjwa uko tayari katika Neno. Ni mapenzi ya Mungu uwe mzima.
B. UKIYAJUA HAYA MWELEZE MUNGU HAJA ZAKO KWA MAOMBI:
Bila mashaka ya kupokea majibu, wewe kama Bibi Arusi mwendee Mume wako Mungu, na kumwelezea unalolihitaji. Maombi ni mazungumzo na Mungu. Zungumza naye kama jinsi ambavyo unavyoweza kuzungumza na mumeo, Rafiki yako, Baba yako au Kaka yako. Usimwendee huku ukinung’unika, ukilia na kubabaika; kiasi ya kwamba hata unalolihitaji halifahamiki! Usiseme yeye anajua yote, hivyo huna haja ya kumweleza kitu. Hivyo siyo sawa na Neno la Mungu. Utampa nafasi Shetani kukupiga kwa kusema hivyo, maana hulijui Neno la Mungu. Mpango wa Mungu wa sisi kupokea, ni KUMWOMBA tukimweleza mambo yote tunayoyahitaji [ISAYA 43:26; YOHANA 16:23-24; YOHANA 15:7]. Kumbuka Neno linavyosema “Kila aombaye hupokea.” Ni kwa sababu hii huna haja ya kutaka watakatifu fulani waliokufa wakuombee! Siyo Bikira Maria, Petro, Paulo au yeyote. Yesu mwenyewe kwa pendo lake, ndiye pia Mwombezi wetu kwa Baba. Hakuna mwingine mbinguni! [1 YOHANA 2:1]. Kwa Imani tu, zungumza na Mungu bila kutumia vitu vingine na kuviweka kati yako na Mungu kwa mfano Rozari, Maji ya Baraka n.k. Aliye kati yetu na Mungu anapaswa kuwa YESU tu! Watu wengine husema kwamba hawajui kuomba kwa kutokujua maana ya maombi. Kama ulivyotangulia kufahamu, maombi ni mazungumzo. Mke anazungumzaje na Mumewe? Ebu angalia mfano huu:- “Mume wangu, naomba fedha nikanunue mafuta ya kujipaka. Ngozi imechubuka sana kutokana na jua kali. Nimeona mafuta mazuri yanauzwa kwa shilingi mia moja.”
Kwa jinsi hii hii, ndivyo tunavyozungumza na Mungu. Ni jinsi ile ile mtoto anavyomwomba Baba yake kalamu ya kuandikia shuleni.
C. TUMIA MAMLAKA ULIYO NAYO JUU YA SHETANI KATIKA MAGONJWA NA ONDOA VIZUIZI VYAKE VYOTE VYA MAJIBU.
Hapo mwanzo, Adamu alikuwa na mfano wa Mungu katika utakatifu mpaka pale alipotenda dhambi kwa kutumia vibaya hiari yake ya kuchagua jambo la kufanya. Akachagua kuliasi Neno la Mungu, tendo ambalo ndilo linaloitwa dhambi. Kabla Adamu hajafanya dhambi, alikuwa ni MTAWALA. Chochote katika nchi kilipaswa kumtii Adamu. Hii ni pamoja na Shetani. Adamu alipofanya dhambi na kukubali Neno la Shetani, alipoteza mamlaka ya utawala aliyokuwa nayo na akayachukua Shetani. [MWANZO 1:26-27]. Alipokuja Yesu na kututoa katika utumwa wa dhambi, na kuzivunja kazi za Ibilisi aliyetutumikisha wote tuliozaliwa kutokana na Adamu; alifanya jambo jingine zuri. Aliturudishia mamlaka aliyotunyang’anya Shetani. Ndiyo maana Yesu alisema “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani baada ya kufufuka [MATHAYO 28:18]. Sasa mamlaka hii aliyoichukua Yesu ni ile aliyokuwa ametunyang’anya Shetani. Kwa kumshinda Shetani na kazi zake zote, Yesu alimnyang’anya mamlaka Shetani na kutupa mamlaka hiyo ambayo pia inaitwa “AMRI”. Kwa mamlaka hii au “AMRI” aliyoturudishia kila mtu aliyeokoka ana uwezo wa kumkanyanga nyoka yuleyule aliyetukanyaga mwanzo. Nguvu zote za Shetani, hazina uwezo juu ya mtu aliyeokoka.
LUKA 10:18-19
“Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama nimewapa AMRI ya kukanyanga nyoka na nge, na NGUVU ZOTE ZA YULE ADUI (SHETANI), wala hakuna kitu kitakachowadhuru.”
Nguvu zozote za Shetani hata kama zingekuja kwa vitisho kama umeme, ziko chini ya “AMRI” au “MAMLAKA” ya mtu aliyeokoka. Unapolitumia Jina la Yesu kwa Mamlaka au Amri juu ya pepo wanaosababisha tatizo ulilo nalo, pepo hao watakutii na kuondoka [SOMA LUKA 10:17]. Magonjwa mengi husababishwa na pepo wa udhaifu [SOMA LUKA 13:11; MATHAYO 12:22;MARKO 9:17, 25; LUKA 11:14]. Unapokuwa umeelemewa na ugonjwa wowote iwe ni homa au ugonjwa wowote, au unapokuwa unaomba kwa ajili ya ugonjwa alio nao mwenzio; haitoshi tu kumwomba Mungu auponye ugonjwa huo, ila inakubidi pia UTUMIE MAMLAKA ULIYO NAYO JUU YA SHETANI NA KUUKEMEA UGONJWA HUO NA KUUAMURU KWA AMRI KWAMBA UHAME. [Angalia mfano katika [LUKA 4:38-39].
MFANO WA MAMLAKA KATIKA ULIMWENGU HUU:
Waangalie askari wa Usalama Barabarani au askari wa trafiki. Hata kama umbo la askari ni dogo namna gani, kwa kutumia mamlaka aliyopewa na Serikali, anaponyosha mkono mtupu usio na chochote, gari kubwa lenye tela nyuma na linaloendeshwa na mtu mwenye umbo kubwa husimama pale pale. Vivyo hivyo kwa mtu aliyeokoka. Hata kama ukiwa na umbo dogo namna gani au umeokoka leo tu au jana, unapoamuru pepo wa udhaifu au kazi yoyote ya Shetani ikuachie bila mashaka yoyote, kazi hiyo ya Shetani itahama. Mamlaka uliyopewa na Yesu ni kubwa mno. Unapolitumia Jina la Yesu, ni kwamba unamwakilisha Yesu mwenyewe kama jinsi ambavyo askari wa Usalama Barabarani anavyoiwakilisha Serikali. Askari wa Usalama Barabarani anaponyosha mkono kuamuru gari kusimama, huwa hana mashaka ndani yake kwamba labda gari hilo litaendelea kwenda. Ni lazima dreva huyo atatii na kulisimamisha gari. Vivyo hivyo kwako, inakupasa kutoa mashaka unapomkemea Shetani kuhama; naye lazima atakutii [LUKA 10:17]. Unapokuwa pia ukiomba, kumbuka kukemea namna zozote za vizuizi vya Shetani juu ya majibu ya maombi yako. Shetani hutumia wakuu wake wa giza walio chini yake KUCHELEWESHA MAJIBU ya Maombi ya Watakatifu [ANGALIA MFANO KATIKA DANIEL 10:12-13].
D. BAADA YA MAOMBI, AMINI KWAMBA UMEPOKEA MAJIBU NA USIKUBALI KUTEGWA NA SHETANI KWA MANENO
Biblia inasema katika MARKO 11:24, “Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote myaombayo mkisali, AMININI YA KWAMBA MNAYAPOKEA nayo yatakuwa yenu”. Hali unayokuwa nayo BAADA ya maombi ni muhimu sana kama unataka kuona muujiza wako au jibu la maombi yako. Kamwe usikubali kuongozwa na milango mitano ya fahamu baada ya maombi. Usiongozwe na KUONA AU HISIA! Ya kwamba unajisikiaje au unajionaje baada ya maombi, hayo siyo muhimu. Hatuenendi kwa kuona bali kwa imani [SOMA 2 WAKORINTHO 5:7] Wakati mmoja, Yesu aliulaani mtini usiokuwa na matunda. Wanafunzi wakasikia alivyotoa amri juu ya mti ule, lakini halikuonekana badiliko lolote la kuonekana machoni wakati huo huo. Kesho yake asubuhi wanafunzi wale ndipo wakashangaa kuona mtini ule umenyauka kutoka shinani. Wakamwambia Yesu kwamba mtini ule umenyauka (BAADA YA KUONA!) . Yesu akawajibu “MWAMININI MUNGU”. [SOMA MARKO 11:12-14, 20-21]. Maana yake nini? Palepale Yesu alipotoa amri, mti ule ulinyauka kutoka kwenye MIZIZI! Macho hayaoni mizizi ya mti maana iko chini ya udongo. Kesho yake, kunyauka huko kulikwisha fika kwenye shina na kwenye matawi mahali ambapo macho yanapoona. Jina la Yesu katika amri linashughulikia MZIZI WA TATIZO ili kukuweka huru kabisa. Macho yanachukua muda kuona wakati mwingine. Macho hungoja kuona shina na matawi. Kungoja kuona kwa macho siyo Imani na huua kabisa matokeo ya maombi. Kumbuka baada ya maombi kwamba hata kama majani kwenye matawi yanaendelea kuwa kijani kibichi, yatakauka tu kwa kuwa mizizi ya mti imenyauka. Usikiangalie kichwa au tumbo linaloendelea kuuma baada ya maombi. Mzizi umenyauka! Tumbo lazima litaacha kuuma.
Unalotakiwa kufanya baada ya maombi ni KUKIRI USHINDI kwa maneno ya kinywa chako. Mungu aliumba mbingu na nchi kwa Neno. Na iwe hivi ikawa hivyo. Neno la Mungu lina uwezo wa kuumba. Kwa jinsi hiyo hiyo, mtoto wa Mungu ana uwezo wa kuumba kwa maneno yake. Kwa maneno yako, utashiba mema au mabaya [SOMA KWA MAKINI MITHALI 18:20-21]. Baada ya maombi, Shetani hungoja kukutega kwa maneno ya kinywa chako. Maneno yako yasiyokiri ushindi humfanya mwindaji au mtega mitego Shetani kukushinda tena na kuendelea kukuonea. Kujiponya katika mtego wake, ni kukiri ushindi.
MITHALI 6:2,5:
“Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako. Ujiponye kama paa na mkono wa mwindaji, na kama ndege katika mkono wa mtega mitego”.
Jambo muhimu la kukumbuka ni kwamba kukiri ushindi kwa maneno ya kinywa chako siyo kibali cha kusema uongo. Ikiwa ulikuwa unaomba nyumba na hujaipata baada ya maombi, usiseme “Nimekwisha pata nyumba nzuri sana iko Sinza, Dar es Salaam.” Huo ni uongo ambao unampa nafasi zaidi Shetani ya kukukosesha muujiza. Kama bado kichwa kinauma na homa inaendelea baada ya maombi unapoulizwa usiseme “Kuuma kichwa na homa, vyote vilikwisha toweka zamani”. Kama bado ni kipofu baada ya maombi usiseme “Ninaona sasa bila matatizo.” Huo wote ni uongo. Biblia inatukataza kumtetea Mungu kwa kusema uongo kwa ajili yake. [AYUBU 13:7-8].
Kukiri ushindi kwa maneno yako baada ya maombi, ni kukiri maneno ya Mungu ya ushindi bila kujali mazingira uliyo nayo au hali uliyo nayo baada ya maombi. Kwa mfano, “ Kwa kupigwa kwake,mimi niliponywa”[1 PETRO 2:24]; “Aliyachukua masikitiko yangu na huzuni zangu. Kwa kupigwa kwake mimi nilipona” [ISAYA 53:4-5]; “Siku za njaa nitashiba, sitaaibika wakati wa ubaya.” [ZABURI 36:19]; “Wamtafutao BWANA hawatahitaji KITU CHOCHOTE kilicho chema”. [ZABURI 34:10]; “Yesu amekuja ili niwe na uzima, tena niwe nao tele”. Mungu anapenda nifanikiwe katika mambo yote. Kwa maneno haya, tatizo langu limekwisha.” [YOHANA 10:10; 3 YOHANA 1:2] n.k.
Usiseme maneno kama yafuatayo, ukatengwa na kukamatwa na Shetani na kushindwa: “Labda nitapona”. “Mungu akipenda nipone, nitapona.” “Hali yangu imezidi kuwa mbaya baada ya maombi, nafikiri ugonjwa huu utaniua.” – Ukisema hivi, utakufa kweli, utapata matunda ya kinywa chako! Baada ya maombi, kiri maneno ya Mungu ya Ushindi bila kuangalia maumivu yanayoendelea au mazingira yanayokukabili wakati huo.
VIZUIZI KUMI VINAVYOFANYA MAMLAKA YAKO ISITENDE KAZI KUBWA
NA KUWEZA KUPATA MAJIBU YA MAOMBI KWA KIWANGO CHA JUU
NA KUWEZA KUPATA MAJIBU YA MAOMBI KWA KIWANGO CHA JUU
Yesu alisema kwamba yeye amwaminiye, atazifanya kazi alizozifanya yeye na hata kubwa zaidi kuliko alizozifanya Yesu. [SOMA YOHANA 14:12]. Lakini leo utaona kwamba watu wengi wanaomwamini Yesu, wanasumbuliwa na kazi ndogo tu za Shetani na mamlaka yao inashindwa kutenda kazi. Viko vizuizi vinavyosababisha mtu asione miujiza mikubwa inayotokana na maombi na mamlaka yake juu ya Shetani:-
(1) Kutaka miujiza tu na ukawa hutaki kumfuata Yesu katika mambo yote
[MATHAYO 6:33; YOHANA 6:24-27; ZABURI 91:14-16].
(2) Yesu alikuwa chini ya amri ya Baba wakati wote. Baba alivyomwamuru ndivyo alivyofanya. [YOHANA 14:31]. Hii ndiyo iliyokuwa siri kubwa ya Yeye kutenda kazi kubwa na kuwa na mamlaka yote juu ya Shetani. Leo watu wengi waliookoka hawataki kuwa chini ya amri ya Baba yaani kufuata amri zote katika Neno la Mungu. Wanaongeza na kupunguza katika Neno la Mungu na kuchagua yale yaliyo rahisi kwao kuyafanya. Kufanya hivyo ni machukizo na kutafuta kupigwa na Shetani. [KUMBUKUMBU 4:2; 12:32; MITHALI 30:5-6; UFUNUO 22:18-19]. Kufanya yote aliyoamriwa, ndiyo ilikuwa siri ya Yoshua kufanya kazi kubwa na kuwa na mamlaka kuu juu ya Shetani. Alipoamuru Jua kusimama, lilitii. Siri ya ushindi huo, ni Yoshua kufanya YOTE aliyoamriwa na Mungu kupitia kwa Musa. [YOSHUA 11:15]. Ukitaka kuona mamlaka yako inatenda kazi kubwa, mtii aliyekupa mamlaka na kuyafanya yote anayokuamuru. Usiseme kufanya hili na hili siyo lazima. Usiseme kubatizwa katika maji tele baada ya kuamini siyo lazima; usiseme kutoa fungu la kumi katika mapato yako yote siyo lazima. Usiseme kuvaa mavazi ya kidunia na kufanana na mataifa siyo tatizo. Ukichagua ya kufanya, mamlaka yako inakuwa dhaifu sana. Hakikisha siku zote maisha yako yote yanakuwa sawa naHESABU 23:26. Siku zote wafukuze watenda mabaya wanaokushawishi kuacha kuyatenda maagizo yote ya Mungu [SOMA ZABURI 119:115].
(3) Kutafuta kuwapendeza wanadamu badala ya Mungu. Yesu siku zote
alihakikisha anafanya kila njia kumpendeza Mungu siku zote. Hii ndiyo siri nyingine ya nguvu yake ya maombi. [SOMA YOHANA 8:29]. Tatizo kubwa kwa watu wengi waliookoka, wanatafuta kuwapendeza wanadamu na kuonekana wazuri kwao, badala ya kutafuta kumpendeza Mungu. Mashujaa wote waliokuwa na uwezo mkubwa katika maombi yao, walikuwa wanatafuta kumpendeza Mungu kabla ya yeyote. Hii ndiyo iliyokuwa siri ya ushindi kwa Daudi na kuwa na uwezo wa kumpiga Goliathi kwa jiwe MOJA tu lililokuwa kwenye kombeo. [SOMA ZABURI 73:25].
(4) Kuigeukia miungu mingine. Kazi yako, biashara yako, mchumba wako, ndugu
zako, wazazi wako, masomo yako au vitu vyako vinaweza kuwa ni miungu yako ikiwa vinakufanya ukose nafasi ya kumwabudu Mungu, kufanya kazi yake, na kuwa na usharika naye. Jambo hili husababisha uso wa Mungu ufichwe kwako, na usione majibu ya maombi. [SOMA KUMBUKUMBU 31:18].
(5) Ikiwa viungo vyako vya mwili vinatumika kutenda dhambi, Mungu anapoviangalia, anaviona vimejaa damu na uchafu. Vidole vinavyoshika sigara, mikono inayotumika kushika bia, midomo inayotumika kusema uongo na kusengenya, miguu na viuno vinavyotumika kucheza Disco na Ngoma, viungo vyako vya siri vinavyotumika kufanya uasherati na uzinzi, macho yako yanayotumika kuangalia sinema na video za kidunia, masikio yako yanayojistarehesha kwa kusikia miziki ya kidunia katika radio n.k. Kila kiungo kinachotumika kutenda dhambi, mbele za Mungu kinakuwa kimejaa damu na uchafu na kinafanya uso wa Mungu ufichwe kwako na usione majibu ya maombi kwa kiwango cha juu[SOMA ISAYA 1:15; EZEKIELI 39:24; ISAYA 59:2-3].
(6) Kutokuwa tayari kujifunza Neno la Mungu na kulitenda. Wako watu wengi waliookoka ambao baada ya kuokoka, hawaoni umuhimu wa kutafuta mafundisho kwa bidii bali wanazunguka huko na huko kutafuta mikutano ya Injili tu. Baada ya kuokolewa, hupaswi kutafuta Injili ya kukuokoa tena! Inakupasa kutafuta mafundisho au maarifa. Ukichukia maarifa, majibu ya maombi yako yanakuwa hafifu[SOMA MITHALI 1:28]. Yesu alinena kama Baba ALIVYOMFUNDISHA [ANGALIA YOHANA 8:29]. Ikiwa Yesu alikubali kufundishwa, ni zaidi sana sisi. Hiyo ndiyo iliyokuwa siri ya ushindi wake na kwa unyenyekevu anatuonyesha siri hiyo. Unapokubali kutafuta mafundisho ya KWELI hata yakiwa magumu namna gani, ujue kweli hiyo ndiyo itakayokuweka huru wakati wote. Maneno ya Mungu yakiwa kwa wingi ndani yako, majibu ya maombi yako yatakuwa dhahiri. [SOMA YOHANA 8:31; YOHANA 15:7]. Kumbuka pia kwamba kulijua Neno la Mungu bila kulitenda ni kuwa sawa na Shetani. Yeye analijua Neno la Mungu lakini halitendi. Ili uwe tofauti na yeye na kumshinda kwa mamlaka, sikiliza lolote katika neno na kulitenda au siyo, utalia na usisikilizwe na BWANA (SOMA KUMBUKUMBU 1:43, 45).
(7) Mashaka kabla au baada ya maombi, huzuia kabisa majibu ya maombi. Bila mashaka au kusitasita, mwendee Mungu ukijua hakika atafanya. [SOMA YAKOBO 1:6-7; WAEBRANIA 10:38; MARKO 11:23].
(8) Makusudi yako ya maombi ni lazima yawe ya kupata na kulitumia jibu kwa
utukufu wa Mungu na siyo kwa tamaa tu! [YAKOBO 4:3; 1 WAKORINTHO 10:31].
(9) Kumpiga mkeo, kutompa heshima na kumuonea tu kwa kuwa ni chombo
kisicho na nguvu; jambo hili husababisha pia maombi yako kuzuiliwa na kutopata majibu
[SOMA 1 PETRO 3:7].
(10) Kutohubiri Injili kwa watu ambao hawajaokoka pia husababisha mamlaka yako
kupungua na majibu yako ya maombi kuwa mbali. Watu ambao hawajaokoka ni maskini wanaohitaji habari njema. Yesu aliwahubiria maskini hawa habari njema. Ukiziba masikio usisikie kilio chao cha kutaka habari njema, na kuwaacha waende Jehanum, wewe pia maombi yako hayatasikiwa [SOMA MITHALI 21:13]
Ukikaa katika mafundisho haya, utajua kwamba Mungu wetu yuko karibu mno na anajibu kila tumwitapo[SOMA KUMBUKUMBU LA TORATI 4:7].
0 Comments