100/recent/ticker-posts
KANAANI MPYA - Lisikilizeni Neno la Bwana............. MAOMBI NA MAOMBEZI --- Tupigie; +255767-155-623 Ujumbe mfupi/Whatsapp; +255620-179-783

SEHEMU YA SADAKA YAKO KATIKA MUNGU KUJIFUNUA KWENYE MSIMU MPYA KWA AJILI YAKO - C.Mwakasege

SOMO: SEHEMU YA SADAKA YAKO KATIKA MUNGU KUJIFUNUA KWENYE MSIMU MPYA KWA AJILI YAKO - C. Mwakasege

UTANGULIZI 

Kuna mambo kama manne hivi ambayo nitazungumza na wewe kupitia somo hili 

JAMBO LA KWANZA UHUSIANO WA IMANI NA KUTOA SADAKA NA MAJIBU YA MAOMBI YAKO KATIKA MSIMU MPYA

Tambua jambo hili siku zote, sadaka yako inabeba moyo wako na moyo wako unabeba Imani yako na Imani yako inabeba jibu lako

 Na ni kwa maana ifuatayo:-

 1.Sadaka inabeba moyo wako. Mathayo 6:21 Kwa hiyo hazina inabeba moyo, moyo wako unafuata sadaka yako ilipo.

2.Moyo wako unabeba Imani yako Warumi 10:9, Marko 11:23-24 imani inakuwa moyoni.

 3.Imani yako inabeba jibu lako Mathayo 8:13 Hapa utaona Yesu alivyomjibu Yule akidai ambaye mwanae alikuwa anaumwa aliambiwa  “na iwe kwako kama ulivyo amini”. Kwa hiyo majibu yake yalikuwa ndani ya Imani yake. 


Marko 5:34  habari za Mwanamke ambaye  aliyekuwa na shida ya kutoka damu miaka 12. Mstari wa 34 Yesu akasema Imani yako imekuponya. Kwa hiyo uponyaji ulikuwa ndani ya Imani yake. Imani yake ndiyo iliyomponya ilibeba ndani yake jibu la kitu alichokuwa akitaka. Hata hawa watu ambao walikuwa wanaomba, Yesu alikuwa haangalii maombi tu bali aliangalia Imani zao za maombi.

 Soma Waebrania 11:4, Imani inabeba kile unachokitarajia kabla ya kukipata. Wale walioenda kwa Yesu kuponywa haisemi walioenda kwa Yesu kuombewa bali walikuwa wanaenda kuponywa. Na Biblia inasema aliwaponya wale waliokuwa na haja ya kuponywa. 

Sasa kuna watu wengi sana Imani zao zipo kwenye kuombewa. Kwa hiyo majibu yao yapo kwenye kuombewa. Wakiombewa huwa wanaridhika haijalishi maombi yamejibiwa au hayajajibiwa.

Sehemu nyingi sana katika Biblia Yesu hakutumia Imani yake bali alitumia Imani ya watu ambao walikuwa wanaenda kwake kutafuta msaada.  Pia  Imani huwezi kuificha. Na maandiko yanatuambia wazi kabisa Imani inaonekana kwenye maneno na pia kwenye matendo.

Imani isipokuwa na matendo imekufa nafsini mwake maana yake haiwezi kutoa kilichoko ndani. Imani ni kibebeo huwa na kitu ndani. Kwa hiyo unaweza kuchanganya maneno na matendo pia kama vile yule dada aliyekuwa akitokwa damu alivyofanya, maandiko yanasema alisema moyoni mwake kwamba “ikiwa nitashika pindo nitapokea uponyaji wangu”. Kwa hiyo alipokuwa akienda kwa Yesu kushika pindo alikuwa haendi kujaribu bali alikuwa anaenda kuchukua uponyaji.

Warumi 10:17 inatuambia kuwa Chanzo cha Imani si neno bali ni kusikia Neno la Kristo. Na ndiyo maana watu wengi sana wana neno lakini hawana Imani. Kwa hiyo ni lazima ukipata neno ujifunze kulitafakari, kuliombea mpaka ndani yake usikie na ukisha sikia kuna kitu kitaachiliwa ndani yake ambacho kinaitwa uhakika. Uhakika ndiyo unaoitwa Imani.

Kwa hiyo sadaka ni njia mojawapo ya kuonyesha Imani yako kimatendo kwa Mungu wako. Sadaka ina ugomvi mkubwa sana katika ulimwengu wa roho kwa sababu sadaka inauwezo wa kubeba mioyo. Unaweza kuhamisha moyo kutoka kanisani na kupeleka kwa mganga wa kienyeji, yaani mwili uko kanisani lakini moyo uko kwa mganga.

Sulemani alitoka sadaka kwa ajili ya kujenga madhabahu ya ile miungu ya wake zake, maandiko yanasema moyo wake ulibanwa na hakuenenda tena kama vile Mungu alivyokuwa akitaka. Biblia inasema “akarudi nyuma hakumfuata Mungu ipasavyo”

Waebrania 11:4 inatuonesha tofauti ya sadaka ya Kaini na Habili. Sadaka ile haikuwa kwanza kwenye vitu walivyotoa bali ilikuwa kwenye imani waliyokuwa nayo wakati wanatoa ile sadaka.

Katika utafiti wa sadaka Mungu haangalii kwanza unachotoa bali anaangalia Imani unayokuwa nayo muda ule wa kutoa. Na ukifanya namna hiyo sadaka yako itaenda na sauti ya Imani hata kama ukiondoka ile sauti itaendelea kunena kwenye madhabahu.

Ukisoma habari za Kornelio Biblia inasema alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi na kuomba daima. Maandiko hayatuambii alichokuwa akiomba. Lakini ukitaka kujua alichokuwa akiomba angalia majibu ya maombi yake. Kwa sababu Imani inabeba majibu.

Mungu akiona Imani anajua unachokitaka. Ndani ya imani kuna jibu.Sasa kuna umbali mrefu sana na umbali mfupi sana kati ya neno unalosikia na Imani. Kwa sababu Imani huja kwa kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo.

Kama unasoma neno la Kristo kwenye Biblia lakini  huna  au hapati Imani katika neno ulilosoma. Hapo ujue kubwa umebanwa kwenye kusikia na ndiyo maana maandiko yanasema kwenye kile kitabu cha Mathayo 13 wakati Yesu akitoa mifano juu ya ufalme wa Mungu na wanafunzi wakiuliza kwanini akisema nao kwa mifano.

Yesu aliwaambia ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa Mungu lakini si kila mtu amejaliwa. Akawaambia hao watu watasikia lakini hawatasikia, watatazama lakini hawaoni, mioyo yao imekuwa mizito kiasi ambacho kile wanachosikia na wakitazamacho hawawezi kuelewa. Halafu Biblia inazungumza sentensi ngumu kidogo kwamba ili wasije wakasikia na wasije wakaona ikawaokoa. Kwa hiyo hii ni adhabu. 

Kama unaona katika kusoma Biblia hakujengi Imani ndani yako nenda mbele za Bwana na umuulize shida iko wapi kwa sababu inawezekana ni shetani amekupofusha fikra zako ili nuru ya injili isije ikakuzukia.

Inawezekana kabisa shetani ameshika masikio yako kama alivyowashika wana wa Israeli wakati akiwatengenezea ndama. Haruni  aliwaambia walete pete za kwenye masikio. Maana yake ili abane kusikia kwao wasiweze kumsikia tena Mungu.

Ukienda kutoa sadaka kwa miungu yoyote kitu cha kwanza  itakachofanya ni kubana kusikia kwako. Kwa sababu ikibana kusikia kwako basi imefanikisha kufunga imani yako. Na ikishafunga Imani yako basi imeshazuia majibu ya maombi yako labda Mungu anyanyue mtu mwingine mwenye Imani aweze kukusaidia au rehema za Mungu zikutembelee mahali uliko la sivyo hautavuka.

Baada ya dhambi kuingia katika bustani ya Edeni ilitunyang’anya Imani. Yesu akiingia ndani yetu baada kuoka huwa anatupa kiasi cha Imani.

Watu wengi sana wanapotoa sadaka zao huangalia mara nyingi upande mmoja tu yaani aina ya sadaka lakini hawangalii aina ya Imani inayokwenda na sadaka. 

Kuna wakati huwa tunasoma kwenye meseji kwenye simu ambazo wafu wanatumia kutuma meseji na sadaka. Mtu mmoja aliandika alisema "kama ni sadaka nimetoa ,kama ni kuomba nimeomba lakini tatizo liko wapi?Ninaweza nisijue tatizo lako lakini ninachojua ni Imani haijakaa mahali ambapo inatakiwa ikae.


MAOMBI:

Mungu naomba rekebisha imani za watoto wako zirudi mahali pake maana huu sio mwaka wa kukosa kabisa.Yesu anauliza hili swali maana yake kuna mahali imani alitaka asione na sasa haioni mahali pake.

*********************************

Ukitoa sadaka inaenda na moyo wako na ndio maana ni rahisi sana Yesu kwenda kuchungulia katika sanduku la hazina maana akiangalia sadaka yako anaona moyo wako. Yesu alisema huyu mjane ametoa vingi kuliko hawa maana alikuwa haangalii mkononi kimetolewa nini bali alikuwa anaangalia imani iliyobebwa ndani ya moyo.

Baada ya kuangalia Yesu aliona imani iliyobebwa na moyo wa mjane ilikuwa ni kubwa kuliko ile ambayo wamatajiri walitumia kutolea sadaka. Kwa hiyo mbele za Mungu ikaandikiwa thamani kubwa zaidi kwa sababu ya imani yake lakini matajiri waliandikiwa kidogo haijalishi wametoa pesa nyingi kiasi gani.

Ukishatoa sadaka tu moyo wako unaonekana. Kila wakati chunga sana saa ya kutoa sadaka maana Mungu huwa anaangalia moyo. Hii iliwagharimu Anania na Safira maana walijua Mungu anangalia kiwanja kumbe Mungu aangalia moyo na ndani ya moyo wao aliona udanganyifu.Sadaka yako inafungua moyo wako kwa hiyo jipange kutoa sadaka yako.


MAFUNDISHO MENGINEYO

 SOMO:UMUHIMU WA MALEZI -Sehemu Ya Pili

NENO LA SIKU:THAMANI YAKO INATEGEMEANA NA ULICHOKIBEBA

NENO LA SIKU:UTAKATIFU UNAANZIA DUNIANI


JAMBO LA PILI 

MSIMU MPYA UNADAI KUMJUA MUNGU ZAIDI KULIKO KUMJUA MTU

Ukisoma Mwanzo 46:1-5 utaona Hii ni  habari ambayo inazungumzia familia ya mzee Yakobo, wakati huo watoto wake walikuwa wanaongozwa na Ruben. Wakati huo tayari njaa ilikuwa imeingia Duniani na tayari Yusufu alikuwa ni waziri mkuu wa nchi ya Misiri na tayari alikuwa kwanza kugawa chakula kwa watu maana njaa ilikuwa tayari imeanza.

Tayari walikuwa wameenda safari kama mbili hivi Misri. Pia wakati huo walikuwa tayari wameambiwa kuwa waende wakamlete baba yao yaani mzee Yakobo. Yusufu alikuwa kajitambulisha kwao kuwa yeye ni Yusufu waliyemuuza.

Taarifa ilikuwa imeshatolewa kwa Farao ili  ndugu zake Yusufu waje wakae Misri kwa hiyo Farao akatuma ujumbe wa magari ili wakaichukue  Familia ya mzee Yakobo ili aje akae Misri katika eneo la Gosheni yeye na mifugo yake.

Akina Rubeni na wenzake baada ya kupewa ile misafara ili wakamchukue baba yake na familia zao walifurahi sana. Basi walipo fika walimweleza baba yao mzee Yakobo kuwa Yusufu yupo hai kwa hiyo aende nao ili ahamie Misri. Soma sura yote 45 utaelewa zaidi.

Kuna mstari pale unasema hakuwasadiki. Maana ilikuwa ni ngumu sana kuwaamini. Yusufu aliuzwa akiwa na miaka 17. Alikuja kuwa  waziri mkuu akiwa na miaka 30. Kwa hiyo 30-17=13. Ukijumlisha na  ile miaka miwili ambayo tayari njaa ilikuwa imetokea utapata miaka 15. Yaani 13+2 miaka ya njaa =15. Kwa hiyo miaka 15 walikuwa wanajua kuwa Yusufu kafa.

Akina Rubeni hawa hawa ndio  waliochovya vazi lake katika damu ya kondoo na wakasema kuwa kauawa na wanyama wakali. Kwa hiyo waliitisha msiba wakalia na kilio wakaanua matanga na wakamaliza msiba.

Sasa leo wanakuja kumuambia kuwa  Yusufu yupo hai anatawaaminije sasa? Je wanajielezaje kuwa Yusufu yupo hai baada ya miaka 15 kupita tangu waliposema amekufa?. Wakamueleza na maneno ambayo Yusufu aliwambia. Biblia inasema hakuwasaidiki lakini alijitia moyo akasema sawa ntaenda kumuona mwanangu ningali hai.

Nia yake ilikuwa akamuone mtoto wake angali hai lakini moyoni alikuwa haamini. Sasa tuendelee kusoma katika sura ya 46.

Mwanzo 46: 1

Akasafiri Israeli, pamoja na yote aliyokuwa nayo, akaja Beer-sheba, akamchinjia sadaka Mungu wa Isaka babaye.

Hii ilikuwa ni safari ya miaka 400 ambayo ilikuwa inaanza. Maana Yusufu alisema  njaa ina miaka 5 iliyobaki. Alisema baada ya hapo  mnaweza kurudi. Lakini Mungu aliwaambia mtakaa Misri kwa miaka 400.

Mzee Yakobo alichukua hatua japo alikuwa haamini kuwa kweli Yusufu yupo hai. Baada ya kuchukua hiyo hatua hofu iliingia ndani yake. Chanzo cha hofu yake ilikuwa  kutokuwaamini wale watu alioongozana nao safari. Maana hakuwa na watu wengine wa kuwaamini kwasababu watoto wake hawaamini tena na hata Farao hamjui kwa hiyo hawezi kuwaamini wale watu wa Farao.

Japo walimweleza kuwa Yusufu anasema hivi lakini ndani ya mzee Yakobo Yusufu alikuwa amekufa kwa miaka 15. Pia hao hao waliosema Yusufu amekufa leo ndio wanasema Yusufu yupo hai.

Kwa hiyo hakikuwa kitu chepesi sana. Ilibidi afanye maamuzi maana imani ni maamuzi. Kama anaendelea na safari basi asiweke imani kwa watoto wake, au Yusufu, au yeye mwenyewe na wafanyakazi wa Farao. Sasa alipofika Beer-sheba akatoa sadaka maana ule ulikuwa ndio mwanzo mpya wa msimu kwake.

Mahali alipopitia mzee Yakobo hapakuwa pepesi sana kuweza kuwaamini wale watu kirahisi rahisi tu. Maana ingekuwa kama sasa hivi angesema ngoja nimpigie simu niongee nae lakini wakati ule hakukuwa na simu.

Ndani yake alikuwa na hofu kwa hiyo alienda akaachilia sadaka pale Beer sheba. Ile sadaka ilibeba moyo wake. Na ile sadaka ilipobeba moyo wake maana yake ilibeba na imani ndani yake 

Kwa hiyo imani yake kuna kitu alikuwa inatafuta. Akasema Mungu katika mazingira haya niliyonayo katika msimu huu mpya hamna mtu naweza kumuamini. Lakini naomba katika saa hii na zamu huu naomba ujifunue maana hamna namna naweza kuwaamini hawa watu.

Ndio maana Mungu alisema na Yakobo kwenye ndoto alisema mimi ni Mungu. Je unafikiri ni kwanini Yakobo alitoa sadaka kwa Mungu wa baba yake na sio kwa Mungu wake? 

Mzee Yakobo miaka 15 iliyopita alikabidhi mtoto wake ili aende akawasalimie ndugu zake huko machungani. Akambariki akisema Mungu wangu wa Ibrahimu na Isaka ambaye ni Mungu akusafirishe salama uende urudi. Akamletea nguo Yusufu ili aende. 

Wale wengine nao pia huenda aliwaombea baraka akisema Mungu wangu awasafirishe salama huko machungani mwende na mrudo salama. Lakini Yusufu hakurudi wale wengine walirudi. Huenda Yakobo akiwa anajiuliza maswali je  kama Mungu katika madhaifu kwangu je kwanini hajanijibu?

Je umewahi waona watu wanapitia mahali pagumu sana na wanasema Mungu kama hujajibu maombi yangu sawa lakini je hata wale ambao wananiombea nao umeamua kutowajibu?. 

Yakobo akasema  ngoja nimtafute Mungu wa Isaka maana nina uhakika namna alivyotembea na Isaka lakini sina uhakika namna anavyotembea na mimi. Mungu alipojifunua alisema mimi ni Mungu. Alisema mimi ni Mungu kwasababu ndani ya sadaka au ndani ya moyo wa mzee Yakobo alikuwa anamtaka Mungu wa kuwa nae njiani.

Mungu aliongeza tena alisema mimi ni Mungu wa baba yako Isaka  usiogope. Ndani yake Yakobo alikuwa  na hofu maana alikuwa haamini.

Sio kwamba alikuwa hataki kwenda lakini yake alikuwa na hofu. Maana alikuwa kwanza safari lakini alikuwa anafikiria kurudi asiendelee na safari.

Je hujawahi kuona mtu anafika stendi na yupo na mizigo yake lakini anasema haloo mimi siendi narudi nyumbani.


USHUHUDA 

Wakati fulani tulikuwa tunasafiri kutoka Israel kurudi Tanzania kwa Shirika la ndege la Ethiopian airlines.

Tulipofika Adis Ababa Ethiopia ilibidi tuconnect na ndege nyingine ya Shirika hilo hilo kuja Tanzania kupitia Kilimanjaro. 

Sasa tulipokuwa tunajiandaa kuondoka tukiwa ndani ya ndege. Wakati huo ndege ilikuwa tayari imeshafungwa na milango imefungwa.

Kulikuwa na abiria wawili wakaanzisha purukushani wakisema sisi tunataka kushuka maana kuna wenzetu wawili mmewaacha. 

Maana walisikia tangazo likitolewa kuwa abiria wote waliotakiwa kukaa ndani ya ndege wameingia. Tangazo hilo na wao walilisikia. Sasa wakati marubani wanataka kuondoa ndege ndipo abiria hao wawili  wakasimama na kuanza kusema sisi hatuendi.

Walipoulizwa wakasema kuna wenzao wawili ameachwa. Wakaulizwa je  sasa ndio mmekuwa kuwa hao wenzenu mmewaacha? Maana mliona kabisa tangu mwanzo kuwa hao wenzenu hawapo wakati mnafanyiwa ukaguzi.

Wakaulizwa je ni kitu gani kimewafanya sasa ndio mnataka  kushuka na kusema tumewaacha hao wenzenu wawili?. Basi wakaendelea kuwa wakali.

Askari wakaitwa wakaja na bunduki. Wakawauliza sasa mnatakaje nyie? Wakasema sisi tunataka kushuka. Kama unasafiri kwenye ndege hilo sio jambo jepesi. kabisa.

Askari waliamua kung'oa mpaka zile sponji ambazo zipo kwenye siti ambazo walikaa wale watu. Pia walitangaza kwenye ndege kila mtu aoneshe mzigo wake. Na kila mzigo ulioonekana hauna wetu ulitolewa.

Basi tulijikuta tunakaa tena dakika 45 pale uwanja wa ndege na ndipo tukandoka. Lakini shida hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya watu wawili tu ambao waliamua kushuka.

Askari walikuwa anakuagua kila kitu maana hawakuwa na uhakika kama hawajaacha bomu ndani ya ndege maana walikuwa wanafikiria kwanini waingie alafu watake kushuka?

Sasa turudi kwa mzee Yakobo,Mungu alimwambia usiogope kushuka maana Yakobo alitaka aishie pale Beer sheba alafu arudi tena nyumbani kwake. Lakini kilichomfanya ashuke kwenye Misri ni pale Mungu alisema mimi nitashuka na wewe 

Hapo ilikuwa haimsumbui hata kama watoto wake wako pamoja naye ambao hawaamini tena lakini kwasababu Mungu alisema ntashuka pamoja na wewe alipata ujasiri wa kuendelea na safari hata kama hatakutana na Yusufu lakini yuko Mungu anayemuamini.

Msimu huu mpya unadai ndani ya watu wanaoingia kwenye huu, imani zao ziwe kubwa kwa Mungu na si watu. Unaweza ukawaamini hao watu lakini usiwaweke kwenye ngazi sawa na Mungu kwa maana unaweza usijue watabadilisha mawazo yao saa ngapi. 

Ndani yako weka kiu ya kumtaka kwani ni bora kumjua Mungu kuliko watu. Katika mapito yako inawezekana unawategemea watu na wamekuangusha, sasa unabaki kuwalaumu (unaweza ukawalaumu mpaka uchoke). Sasa hivi sio muda wa kulaumu bali tafuta kwenda mbele za Bwana. 

Watu wengi mwanzoni mwa mwaka huwa wanatoa sadaka lakini wengi sana hawaendagi mbele za Mungu na sadaka kwa ajili ya Mungu ili ajifunue katika maisha yao.

MAFUNDISHO MENGINEYO

NENO LA SIKU:NI MUHIMU KULINDA KUSUDI LA MUNGU

NENO LA SIKU:MUNGU WAKO NI MKUU KULIKO KILICHO MBELE YAKO

SOMO:NGUVU YA IMANI


JAMBO LA TATU

3. MSIMU MPYA UNADAI KUMJUA MUNGU ZAIDI KULIKO WINGI WA MALI ULIZONAZO

Luka 6:38

Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.

Na ukiendelea kusoma kwenye Biblia huu mstari umejirudia-rudia kwamba kile unachotoa ndicho unachopokea yaani kile unachopanda ndicho unachovuna. 

Muhimu: Imani yako inaweza ikabadilisha DNA ya (aina ya mbegu iliyojengwa na) sadaka yako. 


Mfano wa kwanza:

NUHU BAADA YA GHARIKA KUISHA 

Ukisoma  Mwanzo 8:15 na kuendelea Nuhu alipotoka kwenye safina baada ya Mungu kumwambia atoke, alipofungua mlango hakuikuta ile dunia aliyoiacha kabla ya gharika. Sasa fikiria ile safina ingekuwa ndio Scania yake ambapo amehifadhi vile vyombo Mungu kamwambia ahifadhi ili viwe mbegu, wakati anabeba alibeba na vyakula vyao. 

Uwe na uhakika ile ulikuwa muujiza mgumu sana kwa Nuhu kwenda kukusanya wale wanyama wote kule maporini halafu akajua na jinsi zao, mfano kujua nyoka huyu ni jike na huyu ni dume, kwa sababu ukijaribu kumchungulia anaweza kukung'ata. 

Unaweza ukasoma habari za Nuhu ukakuta ni kitu chepesi yaani kuanzia kuwapata hao wanyama, ndege, wadudu, n.k kwa kila jinsi na vyakula vyao halafu vitoshe kwa siku zote hizo na wakawa hai mpaka siku ya kutoka kwenye safina. 

Nuhu alikuwa ana kila kitu kwenye safina lakini hakuwa na maisha (future)

Maana yake ni kuwa itakusaidia nini ukapata ulimwengu wote na kukosa uzima wa milele. Kuwa na kila kitu haimaanishi una maisha. 

Watu wengi ni matajiri lakini hawana maisha. Nuhu alikuwa ana ahadi ya Mungu kabla ya gharika lakini mazingira ya msimu mpya yalidai kwanza Mungu ajifunue ndipo atimize ahadi. 


MFANO WA MUSA

Unajua kwa nini Musa alipoambiwa na Mungu kuwa malaika ataenda pamoja nao hadi Kanaani ila Mungu Yeye hatashuka, Musa aligoma? Alitaka Mungu aende pamoja nao. Lakini sasa watu wengi wakishapokea mistari ya Biblia au ahadi za Mungu wanataka waende nazo tu bila ya kwenda na Mungu. 

Majira na msimu mpya yanadai Mungu ajifunue, zaidi ya mtu kuwa na ahadi zake. Nuhu alikuwa ana ahadi lakini Mungu alikuwa hajajifunua kutembea pamoja naye pamoja na ile ahadi kwenye msimu mpya. 

Nuhu alikuwa ana mbegu kwa ajili ya kupanda lakini majira ya kupanda na kuvuna yalishavurugwa (kwani ile gharika ilipiga kwa jinsi ya rohoni na si kwa jinsi ya kimwili) sasa zile mbegu hazitafaa kutokana na majira kubadilika. 

Ukisoma 

Mhubiri 3:1

Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.


1 Mambo ya Nyakati 12:32

Na  wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao.

Kile ambacho walitakiwa wafahamu kilifungwa kwenye nyakati. 

Matendo ya Mitume 17:26 - 28

Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake.

Kwa hiyo nyakati ziliumbwa yapasa watu wamtafute Mungu na si vitu alivyoviumba, na bila Mungu hakuna maisha. 

Watu wengi wakiokoka wanafurahia tu wokovu lakini ukifurahia tu wokovu kuna vitu unapunjwa sawasawa na 

Yohana 17:3

Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.

Kitu cha kwanza kinachokuja moyoni mwako kinatakiwa kiwe ni uzima wa milele na sio wokovu kwa sababu uzima wa milele ndio unakujulisha Mungu ni nani kwako.

Sasa ukiukulia wokovu halafu usikue katika kumjua Mungu kuna vitu utakwama. 

Kwani maandiko yanasema: 

Ayubu 22:21

Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.

Na

Isaya 55:6

Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu;

Sasa watu wanatafuta mema kwanza halafu wakiyapata ndipo wanamtafuta Mungu na wakati huo Mungu yupo karibu na sisi zaidi kuliko pumzi zetu. 

Mungu aliamua ashuke ili afanane na sisi ili iwe rahisi kumfikia lakini watu inapofika msimu mpya hawajui taratibu za kumpata Mungu. 

Nuhu alikuwa ana ahadi lakini Mungu bado hakujifunua; sasa kama Mungu hajajifunua nani atafunua hizo ahadi. Nuhu alikaa pale na hakujua kitu cha kufanya kwa sababu Mungu angekuwepo angemwambia kitu cha kufanya katika majira yale. 

Ukishamjua Mungu utapata vitu ndani mwake. 

Sasa Nuhu alipojua Mungu hayupo naye akajenga madhabahu na akaandaa wanyama waliosafi ambao waliachwa kwa ajili ya mbegu. Alifanya hivi kwa sababu ndani yake kulikuwa na ujumbe kuwa haijalishi ana mbegu kiasi gani ili bila Mungu ni bure! Kwani hata akitoa mbegu hizo kuwa sadaka, Mungu atatengeneza kitu kingine. Muhimu thamani ya Mungu ionekane kuwa ni kubwa kuliko vitu anavyovimiliki, sadaka na mbegu alivyonavyo. 

Ndipo Mungu akafurahia harufu ya manukato ya sadaka ile na akaanza kurudisha majira kwanza? 

Swali: Kwanini Mungu alisubiri mpaka sadaka itolewe? Kwa sababu maelezo ya kutengenezwa safina alipokea bila yeye kutoa sadaka lakini kutoka ndani ya safina hakusema hadi sadaka ilipotolewa. 

Hii ilitokana na imani aliyoipokea iliyotokana na maelezo ya nini cha kufanya. 

Watu wengine wanasema wana imani ila hawajui kitu cha kufanya. Ukishakuwa na uhakika ndani yako hautamwuliza mtu nini cha kufanya. 


USHUHUDA

Nilienda mkoa mmoja na nikakutana na baba mmoja (ni mchungaji) alikuwa anataka kuoa. Akaniomba nikiwa na nafasi tuonane ndipo nikatafuta nafasi katika shughuli nilizonazo tukaonana na akanielezea kuwa anataka kuoa. 

Akasema amepata wasichana kama watatu ila hajui yupi ndiye mke wake. Kwa hiyo anahitaji maombi yangu ili ampate aliye sahihi. Na akasema kile ambacho Mungu atanisemesha nimwambie. 

Nilimtazama kwa muda! Na kumwuliza kuwa kama Jumapili iliyopita alihubiri akasema Ndio! Sasa nikamwuliza mbona hakuniuliza kuhusu mstari wa kuhubiri na kama alimwomba Mungu na kumpa mstari huo, kwanini asiulize kuhusu mke? Nikamwambia kwanini asiende kwa utaratibu huo huo kwa Mungu ili amwambie mwanamke wa kumwoa ni yupi? 

Kwanini anataka kunitwisha hivyo halafu wakishindwana huko ndani aseme hata mtumishi aliniambia ni huyu? 

Hata kama una wanawake 20, kaa mbele za Bwana ili awachuje. Na saa nyingine anaweza akwachuja asibaki hata mmoja, ila hilo lisikusumbue nenda tena kawakusanye kawapeleke mbele za Bwana. Lakini katika kuwakamata huko usimwambie kila mmoja kuwa unatarajia kumwoa wakati huna uhakika kuwa hata mmoja ni girl friend wako halafu mwishoni ukishampata mmojawao hata hao wengine huwafungui na wanabaki kupata shida huko. 

Kwa Nuhu imani ilikuwa inafanya kazi kwani ilikuja na maelekezo; aina ya imani inakupa aina ya maisha nayo hukupa aina ya jibu na kwa sababu hiyo alipokuwa anatoa sadaka ya vitu hakuwa anataka vitu. Nuhu alipokuwa anatoa ndege safi hakuwa anataka wengine bali alikuwa anamtaka Bwana.

Mfano wa pili 

RAHABU YULE KAHABA

Waebrania 11:31 inasema Kwa imani Rahabu, yule kahaba, hakuangamia pamoja na hao walioasi; kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi kwa amani. Biblia haituambii Yeriko walikuweko wangapi lakini walikuwepo watu wengi.

Rahabu alikuwa kahaba lakini hakuangamia kwa sababu ya ile imani aliyokuwa nayo na aliipata kwa kusikiliza shuhuda. Alizungumza na wale wapelelezi anasema tumesikia habari za Mungu wenu, lakini mimi najua kuwa Mungu amewapa nchi hii anaposema mimi najua maana yake kuna uhakika umeingia ndani. 

Ile imani ilipoingia ndani ikampa macho, kwani huwezi kuwa na imani halafu usione,  kwa sababu imani ni bayana ya mambo yasiyoonekana, Ni jicho la ndani, huwezi kuwa na imani halafu usione fursa hii ndio iliyomsaidia kuwatofautisha wale  wanaume wapelelezi na wanaume wengine.

Rahabu wakati anatoa ile sadaka hakuwa na shida ya vitu hakuwa maskini; alikuwa tajiri sana mwenye nyumba kubwa tu,  na hakuwa na shida ya kazi maana alikuwa kahaba. Sikuambii kutoa sadaka ili upate kazi ni vibaya ninachotaka tufuatane juu ya majira mapya.

Itakusaidiaje hata ukipata kazi nzuri sana na hauna Mungu ndani yako, haya majira bila kuwa na Mungu haufiki mbali, na sio suala la nchi moja bali ni la dunia nzima ni kipindi cha ulimwengu mzima.

Ukisoma kwenye maandiko, majira yote makubwa yaliyotokea katika ulimwengu hayakuanza pazuri. 

➖ Majira ya kwanza yalianza kwenye Mwanzo 1:2, inasema Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji;

Huwezi kuita mahali ukiwa kama hakukuwa na watu halafu wakaondolewa, huoni mahali popote Mungu akisema pawe giza kwa hiyo inamaanisha hakuumba giza lakini lilikuweko, huo msimu haukuanzia pepesi ulianzia pabaya.

  • Msimu mwingine ulianzia baada ya Habili kufa halafu Adamu apate mtoto mwingine, ni mpaka Kaini amekuwa  na vizazi 6 vikateketea vyote na hakuna kizazi hata kimoja kilicholiitia jina la Bwana, na mpaka alipozaliwa mtoto mwingine ndio tunaona akiliitia jina la Bwana.
  • Msimu mwingine ulianzia kwa Nuhu, ulikuja na Gharika ukapiga kila kitu.
  •  Msimu mwingine umeanza baada ya Yusufu kuuzwa. Hakuna mahali unaona msimu unaanzia mahali pazuri.
  •  Hata msimu wa agano jipya umeanza kwa Yesu kufa msalabani. Kwa hiyo usishangae sana kwamba 
  •  huu msimu umeanza na Corona (COVID-19), ukisoma Biblia ni rahisi sana kujua kilichoko. Mhubiri aliandika hakuna jambo jipya duniani.


Rahabu alipokuwa anatoa sadaka hakuwa na shida na vitu bali alikuwa na shida na Mungu kumsaidia ili atoke kwenye hali aliyokuwa nayo, Mungu aliekuwa anamwabudu hakuweza kumtoa lakini imani iliyojengeka ndani yake aliposikia nini Mungu wa Israeli amefanya akajua hata yeye anaweza kumsaidia.

Rahabu hakuweka imani kwa wale wapelelezi akaweka kwa Mungu, kwa sababu haijalishi kama ni watumishi wa Mungu alikosa uhakika kama watarudi tena akawaambia wamwapie kwa Mungu wao. Alitaka kujifungamanisha na Mungu wao moja kwa moja. Maana yake wao wangeweza kumwaibisha lakini Mungu asingeweza, wangeweza kumsahau na kumwacha lakini Mungu asingeweza.

Ikabidi wale wapelelezi wampe Rahabu alama ya uaminifu ya kamba nyekundu akawa na uhakika hata wakiondoka bado Mungu atatuma wengine kuja kumchukua na familia yake.

Pamoja na ukahaba wake alijua isingekuwa rahisi kukubaliwa na wana wa Israeli wenye miiko yao kwa makahaba ndio maana alipopokelewa aliwekwa nje ya kambi mpaka Yoshua alipokuja. Rahabu alijua kabisa kule anakoenda anamhitaji Mungu ili amtengenezee kibali kipya.

Inawezekana na wewe umeingia mwaka huu na msimu huu, hauna kibali yupo Mungu anayeweza kukutengenezea kibali kipya, haijalishi kama wanadamu wamekuharibia sifa kwenye mtaa yupo Mungu atakutengenezea kingine.

Tofauti ya Rahabu na watu wengine kwenye ule mji wa Yeriko ipo kwenye sadaka ya imani, maana hakuna alieokolewa kwa sababu ya matendo yake Mungu aliamrisha wote waondolewe kwenye ule Mji, lakini ile Sadaka ya Rahabu aliyoitoa kwa imani iliweka tofauti na kumtengenezea msimu mwingine. 

Haijalishi una vitu vingi kiasi gani msimu mpya unadai umjue Mungu zaidi, haina maana ukitoa sadaka ya pesa Mungu hatakupa pesa No, lakini ninakuonyesha kitu kilicho bora zaidi, kuna sadaka ambazo watu walitoa na ziliachilia Mungu kujifunua zaidi kwa upya,  nataka uende kwenye hiyo ngazi kwa sababu ukishampata Mungu hivi vingine vinakuwa rahisi. Unaweza kuwa na vitu na ukakwama.


SOMO:VITU VITAKAVYOKUWEZESHA UITUMIE IPASAVYO MAMLAKA ULIYOPEWA NA MUNGU

SOMO:UPONYAJI WA NDOA YAKO

SOMO:FAIDA YA KUWA MTENDAJI WA NENO LA MUNGU


JAMBO LA NNE

4.TOA SADAKA ILI KUSUDI MUNGU AJIJULISHE YEYE NI NANI KWAKO KATIKA MAZINGIRA YA MSIMU MPYA UNAYOPITIA

Kuna Siri ya ajabu sana ambayo Mungu anawaongoza watu kwenye utoaji sadaka. Tumeahaanza msimu mpya kama vile Israeli (Mzee Yakobo)alivyoanza ule msimu mpya lakini ndani yake amejaa hofu, Roho wa Mungu akamuelekeza juu ya kutoa  sadaka akiwa njiani ili Mungu ajijulishe yeye ni nani kwake.

1 Wafalme 18:36-39 hapa unamuona Eliya mtishibi akipambana na manabii wa Baali na nchi kuwa na ukame. Unaona maneno aliyosema pale baada ya zamu yake kufika. Wale manabii wa Baali na Eliya walikubaliana Mungu atakaejibu kwa moto huyo ndio awe Mungu na wamuabudu yeye.

Manabii wa Baali walipokwama kumfanya mungu wao aje, Eliya akatengeneza madhabahu ambayo kwa hali ya kawaida usingetegemea moto kuwaka, maana yaliletwa mapipa saba ya maji yakamwagwa juu ya zile sadaka, yakawekwa na mawe juu yake,  ili moto utakapowaka wasije wakasema ni moto wa kibinadamu ambao utaisha kesho, wasijaribu kusema ni mwanadamu kaanzisha. 

Na ndio maana moto ulipowaka ulilamba kila kitu mpaka maji na mawe ili  ijulikane kuwa Mungu ni Mungu mkuu. Ombi la Eliya lililokwenda na ile sadaka lilikuwa limebeba ndani yake jibu la kitu alichokuwa anataka na ule moyo wake ulibeba imani, ndani ya hiyo imani kulikuwa na jibu alilokuwa analitarajia kuliona 

Eliya akaanza kumuomba Mungu akisema "na ijulikane leo ya kwamba wewe ni Mungu juu ya Israeli" hicho ndio cha kwanza alichoanza nacho. Unajua Hakimbadilishi Mungu kuwa Mungu anabaki kuwa Mungu lakini huku anaweza asipewe heshima kwamba ni Mungu ngoja nirudie tena 

Mungu ameinuliwa hakuna namna unavyoweza kumuinua zaidi ya kuinuliwa kwake haiwezekani, ila haijalishi ameinuliwa kiasi gani huko aliko wewe unaweza ukamshusha chini kwenye maisha yako. 

Kwa hiyo ni lazima ucheki ndani yako kila wakati, hata unapokuta wanadamu wanasema "Mungu tunakuinua" usiseme tu, lazima yawe ni maneno ya imani kutoka ndani ya moyo ywako kwamba Mungu anapata heshima kuliko kitu kingine chochote ndani ya moyo wako na kile kinachokuzunguka, ni kukiri kwa imani yako kwamba Mungu ana nafasi.

Wana wa Israeli hata wangesema Mungu sio Muda hawawezi kumbadilisha Mungu ya kwamba sio Mungu, lakini hapo ugomvi ulikuwa ni nani awe Mungu juu ya Israeli, sehemu kubwa walichagua awe Baali.

Baali aliingia mahali ambapo hakutakuwa kuingia. Israel halikuwa taifa mwanzoni  Mungu alilitengeneza taifa toka ndani ya taifa.  Alimtoa Ibrahimu kutoka katika Uru ya Walkadayo na alimchukua hatua kwa hatua.

Mungu alijifunua hatua kwa hatua kwa wana Israel mpaka aliwapa ardhi ya Kaanani na aliwarithisha maana ilikuwa ni ya kwake. Pia aliwapa na baraka kuwa kila watakachofanya Mungu atawabariki. Pia aliwaambia kuwa watakuwa vichwa na si mikia. Na atawakuwa anawatumia  kwa ajili ya kujifunua ili waweze kumwona Mungu kwa upya.

Lakini ghafla hawa watu walirudi nyuma. Maana baada tu ya mabadiliko ya uongozi yaliwavuruga kabisa kiroho chao.  Yule kiongozi ambaye alikuwa ni mjakazi wa Sulemani alitengeneza ndama. Moja akiweka Dani na  Nyingine Betheli, shida ilianzia pale na  kuleta shida kutoka vizazi na vizazi..

Baada ya   hayo Elia ndipo alikuja kutokeza. Na alipotokea tu aliachilia adhabu kwa miaka mitatu na nusu kukosa mvua. Pia alifikiri kuwa akiachilia adhabu itawabadilisha watu ili wamgeukie Mungu.

Lakiji haikuwa hivyo maana waliendelea kumuabudu Baali. Ndio maana si kila adhabu inaweza kumrudisha mtu katika njia iliyonyooka. Ukisoma habari za Musa utaona Musa aliporudi toka katika mlima kuomba alikuta watu wanaabudu ndama..


Aliwaambia kuwa sikujua kama mmefanya kosa kubwa sana namba  hii. Kwa hiyo aliye upande wa Mungu na aje upande huu.

Alishangaa sana kuona walijitokeza watu wachache sana. Wengi wao walibaki kwenye upande wa ndama.

Musa alichukia sana na akaamuru wachukue napanga ili kuwaua wale watu wote ambao walikuwa upande ule wa kuabudu ndama. Walikufa watu elfu tatu siku ile ambao waliamua kuifia dini. Walimkataa Mungu ambaye aliwatoa Misri na wakaamua kuabudu ndama ambayo walijitengenezea wao wenyewe kwa mikono yao.

Hapa sasa unaweza ukaelewa kwanini Mungu alimwambia Musa kuwa waache hawa jamaa ili niwamalize na nitengeneze taifa lingine maana wana shingo ngumu maana hawataogopa adhabu.

Hii ndio shida ya imani, imani ikikaa ndani yako haijalishi Nebukadreza anawasha tanuri la moto bado uko tayari kuingia ndani ya moto na sio kuabudu sanamu yake. Hii pia inafanya kazi hata kwa upande ule mwingine maana hata watu wanasema bora wafe kwa kuabudu ndama kuliko kwa Mungu.

Ile sala ya Elia alipotoa ile sadaka yake pale ilikuwa na uzito sana. Maana utaona katika ulimwengu wa roho ilifungua kitu kikubwa sana. 

Wale watu waliishi kwa shida sana kwa miaka mitatu na nusu bila mvua. Ahabu alijua kuwa lile tatizo lilitokea kwasababu ya Elia. Elia alikuwa amefichwa kwa kipindi chote cha miaka mitatu na nusu. Lakini bado hali ilikuwa vile vile.

Elia alianzisha malumbano ya dini. Alisema mtasita sita mpaka lini? Kama Bwana ndiye Mungu mfuateni pia kama Baali ndiye Mungu mfuateni. Wale watu walikuwa tayari wameamua kumfuata Baali. Kwa hiyo hakukuwa na sababu ya kuanzisha malumbano ya kidini.

Ni hatari sana kuanzisha  malumbano ya dini maana kama mtu ana dini yake ina maana kaamua Mungu wake. Pia ni vizuri sana  kuwa na katika kama yetu ambayo mtu anaruhusiwa kuabudu dini yoyote ili mradi asivunje sheria za nchi. Kuliko kuwa na Katiba ambayo inasema watu wote wawe Wakristo.Maana kuna watoa wataamua wawe Wakristo ili waweze kuishi katika hiyo nchi ila sio kwa kumtaka Yesu.

Suala la imani ni suala la mtu binafsi. Kwa hiyo wale watu walinyamaza maana waliamua kuwa baali ndio  mungu wao. Roho wa Mungu alimuongoza Elia kuwa aache malumbano ya dini bali awaambie watoe sadaka ili kumaliza ubishi.

Wafuasi wa Baali walikubali hilo wazo maana walijua mungu wao atatokea na kujibu kwa moto. Walisahau ya kuwa  akija Mungu mkuu yule mungu wao hawezi kutokea. Hata kama  walitoa ile sadaka na kujichana chana kwa wembe lakini hakutokea. Alijua kabisa Mungu wa Israel sio saizi yake ni mkuu sana hawezi hata kupambana nae. Kwa hiyo akaamua kutokutokea kabisa katika lile pambano.

Ukisoma Biblia yako utaona kuwa alipoona wameshindwa kumuita mungu wao ili aje, Biblia inatuambia kuwa Elia alijenga madhabahu ya Bwana iliyobomoka. Kile kulikuwa ni kitendo cha unabii maana pale alikuwa mlimani na hakuwa hekaluni. Alikuwa anatengeneza madhabahu ya Bwana ndani ya mioyo ya watu ili kurudisha heshima ya Mungu ndani ya watu.

Alipoanza kuomba alisema Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, *na ijulikane leo* ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako.

Maana yake alikuwa anasema Mungu naomba jijulishe maana hawa watu wanakusikia tu jijulishe leo ili ujulikane. Elia alisema Mungu ajulikane leo.

Mungu wako akidharauliwa na utumishi wako unadharauliwa. Kwa hiyo aliomba yale maombi ili ijulikane kuwa Mungu ndiye kamtuma na kafanya yale yote kwa neno la Mungu. 

Baada ya kutoa sadaka kulikuwa na mazingira ambayo yanadai Mungu ili ajulikane.  Pia Mungu wako akidhauriliwa na neno lake nalo linadharauliwa pia. Kwa hiyo alisema na  ijulikane leo kuwa wewe ndiye umenituma na ninafanya yote haya ninafanya sawa na neno lako.

Mungu akijitokeza watu wanabadilishwa mioyo yao ili kumfuata Mungu. Pia alisema na ijulikane leo kuwa umewageuza mioyo yao ili wakufuate. Kwa hiyo aliachilia mbegu katika lile taifa baada ya kutoa ile sadaka ili watu warudi kwa Mungu.

Kama umetoa kwa imani ina maana unakuwa na uhakika na matokeo ambayo yataletwa na hiyo mbegu. Maana yake hutakuwa na wasi wasi tena.

Sijajua mahali unapopita ila naomba Mungu ajijulishe kwako, kwa ndugu zako na rafiki zako kuwa yeye ni Mungu.

Mungu akijijulisha na kupata heshima na watu watakuheshimu na wewe.

Tunaona baada ya Mungu kujijulisha katika ile sadaka ya Eliya na kujibu kwa moto. Wale wanabii wa Baali hamna mtu aliyewafundisha kusujudu walisujudu na wakasema Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.

Mungu akijijulisha nyumbani kwako, hutawakumbusha watu kuwa na ibada. Maana wataanza leo ibada vipi?. Pia Mungu akijulikana ofisini kwako watu wataanza kusema hebu tusianze kazi bila maombi. Hata watu wa dini nyingine watakuwa wanakuja hapo. Hata ukiwapa nafasi ya  kuomba na wao watasema inatosha maana wewe umeomba tayari.

Mungu akipata nafasi katika basi ambalo mnasafiri nalo, utashangaa wakisema kuwa kama kuna mtu hapa yuko tayari aombe kwa ajili ya safari siku ya leo. Na huko mbele tunakoelekea kila basi ambalo wanasafiri atakuwepo mtu aliyeokoka. Kwa sababu huu ni msimu mpya.

Sasa katika nchi huu uamsho mkubwa sana umeanza kutokea. Sisi ambao tunazunguka katika huduma tunaona. Maana watu wakiniona napita mahali huwa wanakuja na kusema Bwana Yesu asifiwe baba, wanajitambulisha pale na kuna wengine wanasema wameoka kwenye semina zetu au wengine mahali pengine. Ila wanakuja kunisalimia kwasababu ya Mungu na wanataka kumtambulisha Mungu. Kama ana shida anasema nimuombee na akisema namuombea hapo hapo.

Leo je unataka kumuona Mungu kwa namna gani katika utoaji wako wa Sadaka ili Mungu ajulikane.

Tamani Mungu ajitambulishe aende na wewe kama Yakobo alivyokuwa anaenda Misri. Tamani sana Mungu aende na wewe katika mwaka huu na msimu mpya huu…


Ukishakuwa na Mungu wako mazingira hayajalishi. Mungu hakuona shida kuwapitisha wana Israel jangwani maadamu yeye alikuwepo.

Hapa ndio mwisho wa semina hiyo karibu sana na omba Mungu akuongoze kutoa sadaka hii sawa sawa na maelekezo yake.

       Amen, Amen

NENO LA SIKU:MAOMBI YA YATIMA NA MJANE

NENO LA SIKU:JINSI ZAKA INAVYOWEZA KUBORESHA AU KUVURUGA HALI YAKO

NENO LA SIKU:MAZINGIRA UNAYOYAPITIA YASIONDOE TUMAINI LAKO KWA MUNGU


Post a Comment

0 Comments