SOMO: HATUA ZA KUCHUKUA MSIMU MPYA UNAPOYUMBISHA IMANI YAKO
Mwl.Christopher Mwakasege
UTANGULIZI
MALENGO YA SOMO
- Imani yako ikae mahali ambapo itakuwa rahisi Mungu kuitumia anapokusaidia.
- Ikiwa imani yako iko mahali isipotakiwa uirudishe na kuiweka inapotakiwa.
- Thamani ya imani uliyonayo katika Mungu kwa njia ya Yesu Kristo iongezeke zaidi.
Na haya ni mafundisho ya mazungumzo ambayo Mungu anazungumza na mtu binafsi, Taasisi na nchi mbalimbali.
HATUA YA KWANZA
FANYA MAAMUZI YA KUVUKA SALAMA NA KWA USHINDI KATIKA MSIMU HUU MPYA KWA MSAADA WA MUNGU KATIKA YESU KRISTO
Kutoka 10:8-9
Musa na Haruni wakaletwa tena kwa Farao; naye akawaambia, Nendeni, mkamtumikie Bwana, Mungu wenu; lakini ni kina nani watakaokwenda? Musa akamjibu, Tutakwenda na vijana wetu na wazee wetu, na wana wetu, na binti zetu, tutakwenda na kondoo zetu na ng'ombe zetu; kwa kuwa inatupasa kumfanyia Bwana sikukuu.”
Hapa tunaona Musa akisema juu ya uamuzi ambao alikuwa anafanya ambao na sio tu ulikuwa ni wake pamoja na wa wazee wa Israeli ( Kutoka 3:7-9 ) Mungu alitaka kuona maamuzi ya wazee wa Israel kama walikuwa tayari kuondoka Misri.
Mungu alizungumza na Musa lakini hakumtumia mpaka pale Musa alipokubali ndani yake kuitenda na kufanya kazi hiyo. Pamoja na ubishi aliokuwa nao Mungu alimkabidhi Haruni kwa ajili ya kumsaidia. Mungu alitaka kwanza kabla hajaenda kwa Farao aende kwanza kuzungumza na wazee na wana wa Israel kuona kama wako tayari kutoka Misri.
Ili wakishakubali ndipo aende kwa wana wa Israel kuwaeleza juu ya Mungu kusikia kilio chao juu ya mazingira magumu ya kazi waliyokuwa nayo. Maamuzi ya Mungu hayakuwa kukarabati mazingira ya kazi lakini ni kuwatoa Misri na kuwapeleka Kaanani.
Mungu alitaka wafanye maamuzi ndani yao, waamue kama walikuwa wakitaka huo msaada au hawataki. Ndio maana wakati Musa akizungumza na Farao alimuuliza Musa ataenda na akina nani. Musa alisema atondoka na watu wote na vitu vyao vyote.
Na maamuzi haya ambayo walikuwa wamefikia hayakuwa maamuzi mepesi sana kwao kwa sababu kufuatana na mazungumzo yake na Mungu kwenye kile kitabu cha Kutoka 3 Mungu aliashiria kabisa ya kwamba kuna msimu mpya uliokuwa ukija juu yao. Na ndio maana ile Kutoka 12:1-2 inasema Bwana akanena na Musa na Haruni katika nchi ya Misri, akawaambia, Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu.” Mungu alikuwa akitangaza msimu mpya kwanza kwao.
Tunajifunza haya ili ujue kuwa Mungu anazungumza na wewe katika kipindi cha msimu mpya kwa ajili ya Dunia nzima na watu wote. Mungu ametumia watumishi wake mbalimbali kwa namna mbalimbali ili Dunia na mataifa yote yapate kujua kuwa Dunia imeingia kwenye msimu mpya.
Pia Mungu angetaka kuhakikisha ya kwamba watu wake wanapata msaada unaostahili katika kipindi hiki cha msimu mpya. Kwa sababu hiyo amekuwa akizungumza na sisi kwa njia mbalimbali na njia mojawapo ni haya maneno ninayokueleza ili uweze kujua hatua zilizopo. Kwa sababu kati ya tabia mojawapo ya msimu mpya ni kuyumbisha imani
Imani ikiyumba msaada wako unaoutegemea kutoka kwa Mungu unaweza usiupate kiusahihi na unaweza usidumu hata ndani ya huo msaada kama akikufanyia maana hutajua msingi wake.
Je Musa aliupata wapi ule uhakika? Aliwezaje kumjibu Farao bila kusita? Maana alivyomjibu Farao alikuwa na uhakika kabisa na kile kitabu cha Waebrania 11:1 inasema Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.”Na huo uhakika au hiyo imani aliipataje? Warumi 10:17 inasema Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.”
Kwa hiyo Mungu alisema naye na ikamuwekea uhakika ndani, akasema na wale wazee na ikawawekea uhakika ndani pia alisema na wana wa Israeli wakawekewa uhakika ndani na kwa pamoja ndani yao wakaamua kwamba wanaondoka.
Imani hii ilikuwa ikitokana na Neno la Mungu juu ya kuondoka kwao bila kujali mazingira yaliyokuwa yakiwazunguka. Haijalishi mazingira yalikuwa yanasema kuwa hawawezi kuondoka ama si kitu rahisi wao kuondoka pale maana wameshakaa sana na kuanza maisha pale lakini suala ya msimu si uamuzi wa mtu bali ni suala ambalo Mungu ameshaliweka kwenye kalenda zake na anapoachilia Neno lake halitegemei mazingira tuliyonayo bali linategemea uaminifu wake na maagano yake na ratiba alizonazo.
Mungu akitaka kusaidia watu kati ya kitu kimojawapo anachofanya ni kuwaunganisha na Neno lake ili wapate uhakika ule ule ambao anao wa kuangalia neno lake badala ya kuangalia mazingira waliyonayo.
Na hivyo nataka ufahamu hili litakusaidia ya kwamba Imani ni ya moyoni ukiangalia Marko 11:23 inazungumzia juu ya ukiamini moyoni mwako. Hivyo imani ni ya moyoni. Hata Warumi 10:9 pia inatuambia imani ni ya moyoni. Kwa hiyo Mungu akitaka kujenga imani yako atajenga ndani ya moyo wako kwa kutumia Neno lake.
Sasa kama ukijua ya kwamba imani ni ya moyoni ni rahisi sana nikakutafsiria kwa tafsiri iliyo nyepesi kabisa ya kwamba Imani ni nia uliyonayo/kusudio ulilonalo juu ya unachokitarajia bila kujali mazingira yanayokuzunguka hata kama mazingira uliyonayo yanapingana na tarajiao lako. Ndio maana Imani inakuwa ni uamuzi kabla ya kuwa kitendo/neno katika kinywa chako
Warumi 9:11
Kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye
Maana yake ni kwamba uchaguzi wake ulitegemea nia yake. Uchaguzi wa Mungu juu ya kitu au kwa nini amchague huyu amtumikie hapa na yule anatumikia pale na kwa nini akuokoe wewe leo na mwingine kesho, inategemea nia yake Yeye aitae.
Biblia inatuambia tunaitwa katika kazi ya Mungu si kwa sababu ya matendo yetu bali kwa sababu ya kusudi la Mungu kwake yeye aitaye. Maana yake kunakuwa na nia ndani yake ni nia ndiyo inayomsaidia kufanya maamuzi. Ili aweze kufanya maamuzi sahihi ni lazima kuwe na Neno la Mungu ambalo linatokana na nia aliyonayo na ndiyo Mungu anavyofanya mpaka leo na kwetu pia.
Fikiria wana wa Israel wangesema sisi hatutaki kuondoka! Kwa sababu walikuwa na uamuzi wa kukataa pia. Hakikuwa kitu rahisi sana kwao kwa sababu walipofika njiani walikutana na mazingira ambayo hayakufanana na jinsi walivyokuwa wanatarajia na kila wakipiga hatua wanafananisha mazingira na msimu uliopita na wanatamani kurudi Misri.
Kama hutaki kwenda safari kwa nini Mungu akuandae na akuvike kwa ajili ya safari?. Ndani yako lazima ufahamu kuwa neno la Mungu likija ndani yako, linakarabati nia yako ili uweze kuwa na nia na kusudio lile lile la kufanya kitu kwa ajili ya mapenzi ya Mungu na kwa ajili yake Yeye.
Katika maamuzi hayo unaamini ya kwamba nitavuka salama na kwa ushindi kwenye msimu huu na hayo maamuzi ugawe mara mbili.
UAMUZI WA KWANZA
i). Fanya hayo maamuzi kama vile Musa alivyofanya.
Hii ni ili kwamba Mungu ajue kuwa unataka kuvuka salama, kuwa na ushindi na kwenda na Bwana katika msimu mpya au hutaki. Sasa ukishafanya maamuzi hayo, fikiria juu ya wengine wanaokuzunguka na kukutegemea je ukiondoka na ukawaacha itakuaje?. Kwa hiyo zungumza nao kama Musa alivyosema tutakwenda wote hatuachi kitu lazima uende nao. Na neema ya Mungu itakuwa juu yako ili uweze kuongea nao vizuri.
Pia Fanya kama kwa Rahabu, alipotaka kuondoka alisema pale kuna baba yake, kuna ndugu zake wa kike na wa kiume hakutaka abaki hata mmoja kwa hiyo wanatakiwa waende wote pamoja na vitu vyao vyote viingie kwenye agano.
USHUHUDA
Kuna siku tulikuwa tunasafiri (mimi na mke wangu) tukakutana na watu sasa wakati wa mapumziko tukiwa hapo, wanakula chakula wakafungua mfuko wa salfet akatoka paka. Wakati mama anawagawia watoto vyakula, akamtengea na paka wake alipomaliza kula na safari ikaanza tena akamrudisha Paka wake ndani ya mfuko huo. Ile ilimaanisha hakutaka kuacha paka nyuma yake.
Wakati shetani anafika kwa Ayubu alikuta
hadi kuku wanalindwa hii ni kwa sababu Ayubu aliwaweka kuku kwenye agano, akaweka mbuzi, vijiko, sufuria, viatu nk hata kama vimechakaa viweke kwenye agano siache kitu.
UAMUZI WA PILI
ii). Amua kuwa na imani sahihi kwa ajili ya kuitumia mahali sahihi katika msimu sahihi.
Mungu anataka uwe na vitu sahihi ili aamue kutembea na wewe. Mfano ni: Wana Israeli walipoamua kuondoka Misri.
Waebrania 11:28
Kwa imani akaifanya Pasaka, na kule kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wao.”
Imani ilihusika ilipofika saa ya kuondoka. Adhabu zote zilizotukia hazikuhitaji imani za Waisraeli ila hapa mwishoni wakati wa kuanza kuondoka (take off time) kwa sababu walihitaji imani. Ukiona pameandikwa imani ya Musa ujue ni kwa wale wote waliolisikia lile neno.
Yesu wakati anawaombea wanafunzi wake kwenye Yohana 17, aliwaombea wale 11 na akasema hakupoteza hata mmoja ila ni yule mmoja ndipo akaanza kuwaombea wale 11 ndipo akasema hawaombei hao tu bali na wengine wote watakaoamini kwa sababu ya kuliamini neno lake. Hii inamaanisha katika maombi yale na sisi tumo.
Musa alifanya kitendo hicho kwa kila familia kushiriki Pasaka ili ajue ni wangapi wapo tayari kuondoka. Katika mfano huu kuna vitu vitatu vya msingi sana vya kuangalia. Ambavyo walivionyesha walipokuwa wanashiriki ile karamu kila familia.
JAMBO LA KWANZA
A. WALIPOKUWA WANAONYESHA IMANI YAO, KIMOJA WALICHOONYESHA NI MAAMUZI YA IMANI YAO WALIYOFANYA KWA NJIA YA VITENDO.
Ndio maana hata kula kwao Pasaka walipewa taratibu kuwa huku wamejifunga viunoni ili waondoke. Imani iliwafanya wakae mkao wa kusafiri.
JAMBO LA PILI
B. WALIKUWA WANAMWONYESHA MUNGU KUKUBALIANA NAYE KUWA SI SUALA LA KUHAMA KUTOKA NCHI MOJA KWENDA NYINGINE BALI NI KUHAMA MSIMU MMOJA KWENDA MWINGINE.
Ndio maana unapokuwa unashiriki sakramenti kanisani watasema yale maneno ya Yesu kuwa kikombe hiki ni ishara ya agano jipya, inamaanisha ilikuwa inafungua msimu mpya.
Halikuwa suala la kutoka Misri kwenda Kanaani, nchi moja kwenda nyingine bali lilikuwa suala la kuhama msimu mmoja kuingia mwingine, na ile imani ndani yao ilikuwa inawaambia kukubaliana na msisitizo wa Mungu wa kuhama msimu. Sio tu suala la kubadili kazi, mahali pa kuishi bali ni kubadili msimu mpya.
Mungu alipolikumbuka agano lake ilikuwa ni kwa ajili ya kuhama msimu. Na inapofika masuala Mungu anakusemesha mambo ya msimu mpya, watu wengi wanapata shida sana, sio suala la kubadili kazi, Mahali pa kuishi lakini ni msimu mpya. Huo ndio msisitizo wa Mungu.
JAMBO LA TATU
C. WALIKUWA WAPO TAYARI KWA MABADILIKO YA MFUMO WA KUISHI
Waliikubali hilo lakini sijui kama walielewa gharama yake, kwa sababu hawakuwa wanataka mabadiliko ya nchi, ya kuishi bali walitaka mabadiliko ya utendaji kazi maana walikuwa wanafanya kazi kitumwa. Lakini Mungu alipoleta neno kwao ya kwamba siji kuwabadilishia mazingira ya kazi bali kuwapa msimu mpya utakaokuwa na maisha mapya tofauti kabisa, je wako tayari?
Waliposhiriki ile pasaka siku ile maana yake walikuwa wanamwambia Mungu kuwa wapo tayari, sijajua kama walijua gharama za maamuzi hayo. Sijui kama unajua kuwa walipokuwa Misri walikuwa na Mungu lakini Mungu hakuwa kiongozi wa nchi hiyo, kwa sababu Mungu alisema atakuja kuwatoa sasa anawatoaje kama wapo kwake?. walikuwa wanatumikia miungu mingine.
Mungu alikuwa anawapeleka kwenye msimu mwingine na taifa ambalo Yeye atakuwa ndio Mungu. Wakiwa jangwani Mungu akaanza kusema nao juu ya mabadiliko na mfumo wa kuishi, wakapewa sheria nyingi kiasi ambacho wakaanza kuzikumbuka sheria za Farao kwa sababu zilikuwa chache.
Lakini kama Mungu anakutengenezea mfumo ambao ni bora zaidi kuliko mfumo ulikotoka, uwe na uhakika kuna vitu atakavyosema na wewe na kukusukuma uvifanye ambavyo itakulazimu uwe na mazoezi mazito zaidi kuliko mazoezi mengine kwa sababu unaenda ngazi nyingine.
Katika msimu huu tunakabiliwa na maswali na mamuzi hayo hayo na kila mtu ndani yake na kumuomba Mungu ukitaka kusonga mbele akuvushe kwenye msimu huu na kutaka uvuka kwenye biashara, kazi, uchumi, kipato, utumishi, imani nk, unapofanya hayo maamu
zi Mungu anachungulia ndani yako kuiangalia nia yako inayoonyesha maamuzi uliyonayo na tarajio ulilonalo. Mungu akikuita anataka uitike lakini hakulazimishi ni uamuzi wa kwako kwenda kutaka kwenda kwenye msimu mpya na Mungu na neno lake au na mkumbo wa watu na neno la wanadamu.
Wana wa Israeli walipokuwa wanahama msimu, ule msimu ulikuwa na vipindi vitatu. Kama vile unapoenda kwenye chuo wanakwambia kuna msimu wa mwaka wa kwanza, lakini kwenye msimu huo kuna vipindi viwili ambavyo vina mitihani, ili uvuke kuingia msimu wa mwaka wa pili ni lazima ufaulu mitihani yote.
Kwa hiyo wana wa Israeli walikuwa na vipindi vitatu, Cha kwanza ilikuwa kutoka Misri kwenda mpaka bahari ya shamu wakakutana na mtihani na wakavuka. Cha pili kilikuwa kutoka bahari ya shamu mpaka Yordani, Mungu akaamua kuwapa mtihani wa kuvuka Yordani kupitia jangwani wakafeli, walipita wawili tu Joshua na Kalebu.
Mungu aliwazuia maelfu ya wale wengine si kwa sababu alitaka bali maandiko yanasema ni kutokuamini kwao, kwenye hatua ya mwisho kabisa. Sio kwamba hawakuwa na Mungu, walikuwa na Mungu lakini hawakuwa na imani sahihi.
Shetani anamwamini Mungu kwamba yuko na anatetemeka lakini hana imani sahihi ya kumuogopa. Wana wa Israeli walipewa siku 40 za kukaa jangwani walikuwa na Mungu na aliwasaidia kuzunguka Jangwani lakini hawakuwa na imani ya kuvuka Yordani. Kuna watu ambao watakuwa wanamuona Mungu akiwafanyia mambo makubwa lakini hawavuki kuingia msimu mpya kwa sababu ya kukosa imani sahihi ya kuvuka.
Mungu alikuwa na wana wa Israeli jangwani miaka 40 lakini hakuwavusha Yordani maandiko yanatuambia ni kwa sababu ya kutokuamini kwao na alikaa pamoja nao kwa sababu walikuwa na mtaji wa imani waliyokuwa nayo iliyowatoa Misri mpaka hapo, hawakusikia neno la kuwasaidia waende ng’ambo nyingine. Ndio maana nakuambia fanya maamuzi sahihi ili Mungu anapotazama nia uliyonayo atakusaidia tu utakaposema unaihitaji imani sahihi maana yake neno la saa la wakati linalokufaa wewe kwenye nafasi ya kwako maana neno analosema kwako halifanani na la mwingine.
Mungu atakupa neno ambalo linafanana na mahali ulipo. Maana ukisema Bwana naomba nisaidie kutokuamini kwangu basi uwe na uhakika kubwa atashuka katika ngazi uliyopo na kukusaidia. Ndio maana Mungu alishuka kutoka Mbinguni akaja Duniani kwa ajili yako.
Mtu yeyote ambaye anayetubu huwa anavuta uwepo wa Mungu uje kwake hapo hapo alipo hata kama ni kwenye matope Mungu atamfuata alipo na kumsaidia.
Leo nataka tuombe ili Mungu akusaidie uvuke uingie katika msimu mpya. Maana unajiuliza kuwa je nitavuka kweli hapa kwenye mazingira niliyonayo? Maana unaona Mungu anakusaidia katika mambo mbalimbali ila katika kuvuka kwenye msimu mpya bado huoni kama unavuka unaona umekwama.
HATUA YA PILI
MJUE SANA MUNGU NI NANI KWAKO KATIKA MAZINGIRA YANAYOWEZA KUIYUMBISHA IMANI YAKO
Ayubu 22:21
“Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.”
Aina ya maisha ambayo Mungu alikuwa amemuahidi Ibrahimu hayakuwa Misri wala jagwani bali yalikuwa Kanaani kwenye msimu mwingine.
Kama unasoma Biblia yako vizuri maandiko yanatuambia wale waliotoka Misri waliokuwa watu wazima ilikuwa ni Joshua na Kaleb peke yao walioingia.
Hesabu 14:30-38
“hakika yangu hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo niliinua mkono wangu ya kwamba nitawaketisha humo, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni. Lakini Watoto wenu, ambao mlisema watakuwa mateka, ndio nitakaowaleta na kuwatia ndani, nao wataijua nchi ninyi mliyoikataa. Lakini katika habari zenu, mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili. Kisha watoto wenu watakuwa wachungaji jangwani muda wa miaka arobaini nao watauchukua mzigo wa uasherati wenu, hata mizoga yenu itakapoangamia jangwani. Kwa hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani, siku arobaini kila siku kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu, ndiyo miaka arobaini, nanyi mtakujua kufarikana kwangu. Mimi Bwana nimekwisha nena, hakika yangu ndilo nitakaloutenda mkutano mwovu huu wote, waliokusanyika juu yangu; wataangamia katika nyika hii, nako ndiko Watakakokufa. Kisha hao watu, ambao Musa aliwatuma waipeleleze nchi, waliorudi, na kufanya mkutano wote kumnung'unikia, kwa walivyoleta habari mbaya juu ya nchi, watu hao walioileta habari mbaya ya nchi wakafa kwa tauni mbele ya Bwana. Lakini Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, wakabaki hai miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza nchi.”
Ukisoma Biblia yako utaona yakwamba alipomaliza kuongea nao namna hiyo tauni ikawajia wale wapelelezi 10 na kufa saa ile ile. Binafsi nilisoma ile habari halafu ikanisumbua maana ilikuwa ni adhabu kali namna ile ilitokana na nini ?.
Waebrania 3:16-19
“Maana ni akina nani waliokasirisha, waliposikia? Si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa? Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arobaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka katika jangwa? Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika raha yake, ila wale walioasi? Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.”
Wale walioshindwa kuingia hawakuweza kuingia si kwa sababu Mungu hakuwa pamoja nao bali kwa sababu ya kutokuamini kwao pamoja na kwamba walikuwa na Mungu. Si majitu wala shetani aliowazuia lakini ni kutokuamini kwao.
Anaposema kutokuamini kwao ana maana gani?.
Hesabu 14:11
BWANA akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hata lini? Wasiniamini hata lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao.
Hapa nilitaka kujua kisa hiki, kutokuamini kwao kulikuwa kuna maana gani. Maana kwenye Kitabu cha Waebrania kinasema "Tuangalie sana na sisi tusije tukakosa".
Hii imani inatakiwa tuijue na tusipojua ni rahisi tukakwama Jangwani. Hesabu 14 :11 inatoa jibu.
Kwenye mfumo huu wa msimu mpya kuna vitu vipya vitaachiliwa na wengi watatamani warudi kwenye hali ya zamani. Kitu cha muhimu sana ni hiki, UMJUE SANA MUNGU WAKO ILI USIMAME NA IMANI YA KWAKO.
Mambo yatakayokusaidia kupanua imani yako hapa:
I. UNAWEZA USIWE NA IMANI YA KUMJUA MUNGU NI NANI KWAKO NA USIJUE KUWA HUNA.
Unaweza usiwe na imani ya kujua Mungu ni nani kwako na usijue kuwa huna imani hiyo.
Mfano:
Matendo ya Mitume 17:22-23
“Paulo akasimama katikati ya Areopago, akasema, Enyi watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini. Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua.”
Kuna watu wanaokwenda ibada kwenye madhabahu fulani na hawamjui Mungu wa ile madhabahu ila wanaona watu wakiwepo hapo, miujiza, nk.
Tatizo la hao ndugu ilikuwa si Mungu anayeabudiwa bali mahali pa ibada. Kuna watu wengi sana wanaenda ibadani hawana shida na Mungu bali wana shida na ibada.
Yesu alisema hivi “Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima.” (*Yohana 5:39-40*)
Kwa hiyo unaweza ukalijua neno lakini usijue Mungu ndio neno lenyewe. Watu wengi sana wana neno lakini hawana Mungu.
Kuna tofauti ya kuamini neno na kumwamini Mungu ambaye ni neno kwa sababu hii ndio inazaa mapokeo ambayo yanamwondoa Mungu kwenye nafasi yake.
Unaweza ukawa na maandiko (maneno na maelekezo kama wana wa Israeli walivyo na sanduku) lakini hauna Mungu.
Yohana 5:8-11
“Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo. Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwambia yule aliyeponywa, Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro. Akawajibu, Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, Jitwike godoro lako, uende.”
Si kila anayejua miujiza anamjua Mungu wa miujiza. Unaweza usiwe na imani ya kumjua Mungu, na usijue kwamba huna. Huyo jamaa aliponywa lakini akasema hamjui aliemponya.
Musa alimuomba Mungu ajitambulishe kwake ili amjue kwa sababu miungu ilikuwa inafahamika kwa majina, na Mungu akasema yeye yuko ambae yuko.
Mungu anapojifunua hapo na unatembea nae inakuwa sio suala la kazi aliyokupa bali ni suala la yeye aliekupa kazi, sio suala la msimu mpya ni suala la nani aliekupa msimu mpya.
2.IMANI ULIYONAYO JUU YA MUNGU NI NANI KWAKO, NDIO ITAKAYOAMUA HALI YA MAISHA YAKO KATIKA MSIMU HUU MPYA
Kwenye msimu mpya wengi sana wameingia bila kumjua Mungu ni nani kwao, wanaweza wakajua kabisa Mungu yupo lakini wasijue ni nani kwao.
Imani ni kibebeo haiji peke yake, Warumi 10:17 inasema "Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo." lile neno linaloweka imani ndani yako linapokuja haliji tu lenyewe linakuja na vitu vingi.
Imani ni kama gari kubwa iliyobeba vitu vingi sana na hivi ni Vitu vilivyoko ndani ya imani
1.Cha kwanza
AINA YA IMANI, AINA YA IMANI INAKUPA AINA YA MAISHA
Habakuki 2:4 inasema, mwenye haki wangu ataishi kwa imani yake, kwa hiyo maisha ni matokeo ya aina ya imani aliyonayo.
Kwa hiyo unahitaji kumjua Yesu ni nani kwako binafsi.Maana kama uko ndani ya Boti na mawimbi yakapita je Yesu ni nani kwako? Maana unaweza ukamuona shetani katika dhoruba hiyo lakini kama hukumuona Yesu maana yake huna imani ambayo Yesu anaweza itumia kukusaidia.
KIPENGELE CHA KWANZA.
1.AINA YA IMANI INAKUPA AINA FULANI YA MAISHA.
Huenda umetazama sasa aina ya imani uiliyonayo ndio imekupa aina ya maisha uliyonayo.
Biblia inasema katika Matendo ya mitume 17:26-28. Hapa anazungumza juu ya umbali ambao Mungu kuweka kuwa Mungu akiisha kuwawekea Nyakati na mipaka. Pia Biblia inaendelea kusema ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake
Sasa wewe kwanini unataka kuishi kwa uzoefu badala ya kuishi kwa imani?. Kumbuka kuwa aina ya imani uliyonayo inakupa aina fulani ya maisha.
KIPENGELE CHA PILI
2.KIWANGO CHA IMANI NDICHO KINAKUPA KIWANGO CHA MAISHA.
Soma Warumi 12:3-8 Biblia inasema mtu asinie makuu kupita imani yake. Lakini Pia inasema mtu anie kwa kadri ya kiwango cha imani alichonacho.
Biblia inasema mwenye kufundisha kwa kadri ya imani. Maana yake huwezi kufundisha zaidi ya imani ambayo unayo.
Ukisoma kitabu cha Mathayo katika habari za wanafunzi kuwa katika Boti ambayo ilipata dhoruba ya bahari. Anasema Enyi wenye imani haba maana yake wenye imani kidogo, imani kidogo maana yake inaweza ikapimika.
Katika somo la mfululizo unaofuata tutatazama vitu kama 11 katika imani. Lakini hivyo vitu vitakufundisha kuwa aina ya imani ambayo ikiyumba inayumbisha na vitu ulivyonavyo na kiwango cha maisha ulichonacho.
Ugomvi wa Mungu na wana Israel ulikuwa ni imani waliyokuwa nayo na sio ya majitu kuwepo.
Pia tunaona wana Israel walikuwa wanataka kurudi nyuma yaani mahali ambapo wametoka. Badala ya kusonga mbele katika msimu mpya.
Je hujawahi kuona watu ambao huwa wanatazama nyuma kurudi katika msimu wa zamani badala ya kusonga mbele kuingia msimu mpya.
Dunia nzima iko katika msimu mpya na kilichosukuma msimu mpya ambao tunaingia ni ugonjwa wa Corona. Unaweza ukawa unafikiria Corona badala ya kumjua Mungu ni nani kwako katika msimu mpya baada ya Corona.
MIFANO MICHACHE JINSI AMBAVYO KATIKA MSIMU MPYA MUNGU ALITUMIA IMANI ZA WATU KUWASAIDIA
Tuanze na kuangalia watu watatu kwenye kitabu cha Waebrania. Mifano ya watu ambao katika kipindi chao na si jambo jepesi sana kulisikia maana wakati Mungu akinisemesha jambo hili halikuwa jepesi kwangu kulisikia na sidhani nawe litakuwa jepesi sana kulisikia. Kuna msimu kama vile tulivyokuwa tukiangalia si watu wengi sana wanavuka salama na kwa ushindi.
MFANO WA HABARI ZA NUHU
Tukisoma kitabu cha Waebrania 11:7 tunaona hapa habari za Nuhu katika kizazi chake walipona watu nane tu. Unaweza ukasema alivuka kwa sababu alionekana mwenye haki kizazi chake…Hapana! Kumbuka Mungu alimtembelea kwa sababu katika kizazi chake alionekana mwenye haki lakini ili atoke alihitaji imani. Mungu alimtoa si kwa sababu alikuwa mwenye haki bali maandiko yanasema “Kwa imani Nuhu akiisha kuonywa na Mungu”
Nuhu alitii kile ambacho Mungu alimwambia kufanya kwenye ule msimu maana ulikuwa ni msimu mwingine wa kuingia. Na kwa ajili ya imani ya mtu mmoja alivusha familia yake.
MFANO WA HABARI ZA RAHABU
Pia ukisoma Waebrania 11:31 utaona ya kwamba Rahabu alikuwa akitokea kwenye jiji la Yeriko na ni jiji peke yake Duniani limekuwa na watu muda wote mpaka leo. Na ilipofika juu ya msimu mpya kwao na kwa Rahabu alivuka yeye na wazazi wake na ndugu zake Biblia haijatuambia walikuwa wangapi.
Maandiko yanasema kilichomsaidia Rahabu kutokuangamia ni imani. Kwa hiyo wengine waliokuwepo waliangamia kwa sababu ya kukosa imani.
Sasa kwenye msimu huu mpya tulionao sikuambii kwamba watu watakufa ila ujue ya kwamba kuna watu wengi sana hawatavuka kimaisha kwa sababu tu hawakusimama kwenye imani kumpa Mungu nafasi anayostahili kwenye maisha yao na kuacha imani zao zinayumba na kutozirudisha mahali zinapotakiwa.
Lakini Mungu ametupa nafasi hii kwa makusudi kabisa somo hili ili tujue ya kwamba ameamua kutusaidia ili tujue namna ya kukanyaga na kushirikiana naye. Kumbuka kuwa imani ni kibebeo
Soma pia kitabu cha Warumi 12:3,6 Watu wengi wanachanganya kati ya kazi ya neema na imani ndani ya mtu. Wanafikiri tunapewa vitu kwa neema na tunapokea kwa neema. Unapewa vitu kwa neema lakini unapokea kwa imani!
Usije ukafikiri kwa sababu ya msimu huu ni tofauti na msimu wa akina Rahabu, ni tofauti na akina Musa na Joshua utapokea vitu kwa mteremko tu kwa sababu kuna neema! No! Neema inakupa imani inapokea kitu ambacho neema imetoa.
Kwa hiyo kiwango cha maisha, utumishi au nyanja yeyote uliyonayo ni kwa kadri ya imani uliyonayo! Usikusudie kufanya kitu kikubwa zaidi ya imani uliyonayo, kwanini? Kwa mfano, gari ni la tani 1 unalibebesha mzigo wa tani 5 unategemea nini? Sasa watu wana imani tani 1 wanataka kubeba vitu vya tani 5 wakati uwezo wao ni kubeba tani 1 unafikiri watafika wapi? Watachoka, wataumia, watamchukia Mungu, watanung'unika, watashangaa wakijiuliza kwanini Mungu hatusaidii? Lakini ni kwa sababu wamebeba vitu vikubwa zaidi ya imani yao,
Biblia inasema Kuweni katika kumjua yeye kwa sababu kadri unavyokuwa anaangalia imani yako na kukuongezea vitu na pia maandiko yanasema Mrithi awapo mtoto hata kama ni mrithi wa yote lakini yuko sawa sawa na mtumwa mpaka ule muda utakaoamriwa na baba maana yake wewe huamui kwamba umekua, kwa sababu Mungu haangalii umri wa kukua kwako kwa muda uliokaa kwenye wokovu kuna vitu anaangalia ndani na kwa sababu hiyo anakupa hivyo vitu. Imani ina vitu vingi miongoni mwa hivyo ni:-
1.Aina ya imani inakupa aina ya maisha, Habakuki 2:4, Matendo 17:26-28,Marko 4:35-40
2.Kiwango cha imani kinakupa kiwango cha maisha Warumi 12:3-6, Mathayo 8:26
3.Mahali ulipoiweka imani panakupa mipaka ya maisha. Luka 8:22-25
Luka anaandika kitu kingine tena anaandika anauliza imani yenu iko wapi maana yake imani yao wameiweka mahali isipotakiwa na ndio maana haijawasaidia. Imani yako ikiyumba inaenda mahali isipotakiwa kwa hiyo haitakusaidia hata kama unayo 1 Wakoritho 4:6.
Paulo anaandika tujifunze kutokupinga yaliyo andikwa, imani ina mipaka, Joshua 1:7 aliambiwa juu ya kufuata maelekezo yote aliyopewa na Musa kuwa asiende kushoto wala kulia, maana yake asivuke mipaka, imani isiyo na mipaka sio imani.
KITU CHA NNE
UHAKIKA WA IMANI UNAKUPA AMANI KIMAAMUZI YA KUITEGEMEA KIMATUMIZI.
Unaweza kuwa na imani lakini usiitegemee japo Imani ndani yake imebeba uhakika. Ule uhakika ulioko ndani ya imani kazi yake ni kukupa amani, ndio maana siku zote imani inafanya kazi na amani Wakolosai 3:15 inasema amani ya kristo iamue mioyoni mwenu Warumi 5:1-2 inasema Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu.
Imani inafanya kazi na amani. Ndio maana yule dada aliyetokwa na damu alipopona Yesu alimwambia imani yako imekuponya halafu akamwambia enenda kwa amani Ukisoma kwenye Biblia inasema mtatoka kwa furaha mtaongozwa kwa amani. Amani ndio inakupa maamuzi ya kuitengemea imani kimatumizi, unaweza kuwa na imani lakini usiitegemee kimatumizi.
KITU CHA TANO
TAFSIRI YA IMANI INAKUPA TAFSIRI YA MAISHA
Ukisoma Waebrania 11:3 utajua ya kwamba Imani humpa mtu ufahamu na palipo na ufahamu amani ipo.
Na ukiongezea kusoma Mithali 23:7 utaona ikisema kwa tafsiri nyingine Maana yake ni kwamba atafsirivyo moyoni mwake. Ndio maana Biblia inajitafsiri yenyewe ingawa unaweza ukapata msaada wa tafsiri kutoka sehemu mbalimbali lakini imani ikishaingia inakupa na tafsiri ndio maana ikiingia imani ndani yako unajua huo mstari una maana gani kwa sababu imani inakupa ufahamu.
KITU CHA SITA
NGAZI YA IMANI INAKUPA KIPINDI CHA MAISHA HAYO
Warumi 1:16-17 Anaposema …toka imani hata imani… ni kama ngazi yaani kuna ngazi ya kwanza, kuna ngazi ya pili; yule aliyeko kwenye ngazi ya pale juu na wa chini unaona maisha yanatofautiana. Ngazi ya imani inakupa kipindi cha maisha, ukipanda kidogo inakupa kipindi kingine cha maisha kwa sababu unapokanyaga namna hiyo tafsiri ya ngazi hiyo inaendana na ngazi hiyo.
Ukishapata tafsiri sahihi hofu inahama (sio kama kwa wana wa Israeli kwani wao walitafsiri isivyo na ikasababisha wapate hofu).
KITU CHA SABA
UWEZO WA KUSHINDA UNAKUPA USHINDI DHIDI YA UPINZANI UNAOKUTANA NAO KATIKA MAISHA YAKO
1 Yohana 5:4-5 Tuangalie mifano michache.
MFANO WA ISAKA
Mwanzo 26:1-6 Ila soma Mwanzo 26 yote utapata kitu zaidi. Na Ukisoma habari yote kwenye Mwanzo 26 kuna mambo matatu makubwa niliyoyaona ambayo yatakusaidia katika msimu huu:-
JAMBO LA KWANZA
I). SI SUALA LA KUFANYA UNACHOTAKA KUFANYA KWA SABABU WENGINE WANAKIFANYA BALI LA MUHIMU NI KUMJUA YESU NI NANI KWAKO KIMAMLAKA KATIKA MSIMU ULIONAO
Hapa unaona Isaka alitaka kufanya kitu alichotaka kufanya kwa kuiga kutoka kwenye makundi mawili
—1. Kwa baba yake - njaa iliwahi kutokea kipindi chake naye akaenda Misri.
—2. Wenyeji wa pale Gerari - nao huenda Misri kipindi cha njaa.
Kikubwa kinachowapeleka kule ni tatizo la kiuchumi na kuwepo kwa ukame na kusababisha njaa kuanzia kwa binadamu hadi wanyama kwani majani na mazao hukauka.
JAMBO LA PILI
SI SUALA LA ULICHONACHO KIUCHUMI WAKATI WA MSIMU MPYA BALI NI SUALA LA ULIENANE NI NANI KATIKA MAZINGIRA UNAYOPITIA KIUCHUMI
Angalia ule msitari kwenye Mwanzo. 26:3
anasema "Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki," kwa hiyo usitafute baraka za Mungu kwenye msimu mpya bali mtafute Mungu mwenye baraka. Maana zile baraka hazikumjia Isaka kama mpira uliorushwa tu, alisema kwa sababu atakuwa na yeye atambariki.
JAMBO LA TATU
SI SUALA LA KUMKASIRIKIA MUNGU KWANINI UCHUMI WAKO SI MZURI, BALI NI SUALA LA KUMSHUKURU MUNGU AMEJIFUNUA SASA AKUSAIDIE
Anaposema "nitakuwa pamoja na wewe" kwenye hiyo Mwanzo 26:3 Maana yake sikua pamoja na wewe hapo mwanzo, kwa hiyo uchumi wa Isaka uliharibika kwa sababu hakuwa na Mungu toka mwanzo.
Kwa sababu unaweza kupoteza muda kulalamika kiasi ambacho Mungu akasema na wewe usisikie.
Sasa angalia ule msitari wa 24 anasema "BWANA akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu."
Hapa hasemi "mimi nitakuwa pamoja nawe" anasema "mimi ni pamoja na wewe nitakubarikia" kwa hiyo tayari yuko pamoja nae, lakini bado anamwambia Isaka kilichomfanya aje pale ni kwa sababu ya Ibrahim baba yake. Baada ya hapo Isaka akatengeneza madhabahu akatoa na sadaka kujiungamanisha na Mungu, na ndio maana baada ya pale Mungu akaongeza akasema yeye ni Mungu wa Ibrahim na Isaka.
Ndio maana unatakiwa uwe na imani ya Mungu ni nani kwako kibinafsi, anaweza kukusaidia kwa msaada wa mwingine lakini kuna cha zaidi kinakuja ukijiunganisha pamoja nae.
SWALI
UNAFANYAJE ILI MUNGU AWE WAKO KIUCHUMI?
Kitu cha kwanza ni kwamba usitafute tu baraka za Ibrahimu bali mtafute kwanza Mungu wa Ibrahimu na baraka za Ibrahimu zitakuwa zako bila hata kuzitafuta.
Maandiko yanasema ukitii neno langu baraka hizi zitakufuata na kukupata. Maana yake huwezi kukwepa baraka hizo. Kwa hiyo lazima uwe mtii wa neno na ndio maana ya imani.
Unaweza sema sasa nitaanza kutafuta baraka kila mahali maana unaweza anza kwenda kwa watumishi wakubwa wakubariki na wewe. Je una uhakika kuwa wana hizo baraka?
JIBU
OMBA MUNGU AKUPE MTU KAMA YUSUFU.
Mwanzo 39:1-23 Hapa katika huu mstari bado msisitizo ni Bwana kwanza ndipo kunakuja kustawi. Pia hata kwa Potifa Biblia inasema Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake.
Kwa hiyo hata naye alijua kwanza huyu mtu anafanikiwa kwa sababu ya Bwana aliyekuja nae. Japo vilitokea visa vya shetani Yusufu alienda Jela. Lakini nako huko jela alienda na Bwana baraka zikahama kwa Potifa na zikaenda Jela kule alikokuwa Yusufu.
Biblia inasema Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza. hata yule mkuu wa gereza akamuona kwanza Bwana kwa Yusufu. Maandiko yanasema Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa, waliomo gerezani; na yote yaliyofanyika humo ndiye aliyeyafanya. Wala mkuu wa gereza hakuangalia neno lililoko mkononi mwa Yusufu; kwa kuwa BWANA alikuwa pamoja naye. BWANA akayafanikisha yote aliyoyafanya.
Kwa hiyo hata wewe weka kwanza imani yako kwa Bwana na sio kwenye vitu. Hata unapotafuta wafanyakazi mwaka 2021 watafute kwanza kwa sababu wana Bwana kwanza na ndipo angalia ujuzi wao.
Pia usipate shida hata kama wanakufukuza kazi maana wao ndio watapata hasara kwa sababu Bwana ambaye anawafanikisha anakuwa ameondoka na wewe. Ndugu zake Yusufu wakati wamemuua hawakujua kuwa wanamuuza na Yesu wake. Ukiona unanung'unika baada ya kufukuzwa kazi basi ujue huna Yesu kama unae basi humjui yeye ni nani kwako. Maana sio wewe utakayepata hasara bali ni wao ndio watapata hasara.
Ukimkaribisha Yesu katika biashara yako hamna namna atajificha. Hata watu wengine watamuona Mungu kwako.
Hili tunaliona kwa Potifa kuwa alimuona Bwana akiwa pamoja na Yusufu. Pia je mkuu wa Gereza alijuaje kuwa Bwana alikuwa pamoja na Yusufu?
Kwa hiyo Bwana akiwa pamoja na wewe binafsi hata watu wengine wanamuona Bwana kwako. Hata kama hawataki kukiri kuwa wameona lakini wataona tu.
Biblia inatuambia huyu Mungu ndiye atufundishaye ili tupate faida. Kwa hiyo atakufundisha pia hata namna ya kupiga hesabu za biashara vizuri. Atakusaidia ili upate wateja na mtaji wako wa biashara usikatike.
HATUA YA TATU
USIKUBALI TABIA MBAYA ULIYONAYO IIZUIE IMANI NZURI ULIYONAYO KUMPA MUNGU FURSA YA KUKUTOA KWENYE MAISHA ULIYONAYO SASA ILI AKUINGIZE KWENYE MSIMU MPYA
Tabia mbaya inaweza kukukwamisha usiingie kwenye msimu mpya kwa sababu itadhoofisha imani yako.
Waebrania 11:31
“Kwa imani Rahabu, yule kahaba, hakuangamia pamoja na hao walioasi; kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi kwa amani.”
Katika huu mstari unaozungumza maisha ya Rahabu, nataka tutazame mambo kadhaa kama ifuatavyo;
JAMBO LA KWANZA
I. AINA YA IMANI INAYOKUPA TABIA NZURI NI TOFAUTI NA IMANI INAYOKUPA MAISHA MAZURI
Kuna watu ambao wana tabia nzuri lakini uchumi wao sio mzuri. Katika mstari tuliosoma, tunaona imani aliyopata Rahabu na ndugu zake ilibadilisha tabia yao kuwa nzuri lakini haikubadilisha uchumi wao.
Hii inategemea Neno walilosikia kwa sababu imani huja kwa kusikia na kusikia huja kwa Neno la Kristo. Na sasa kama tukisisitiza tabia nzuri bila kuwa na maisha mazuri. Maana yake watu watakuwa na tabia nzuri bila kuwa na maisha mazuri.
Kwa hiyo lazima tuende sawasawa na 3 Waraka wa Yohana 1:2 Ni mapenzi ya Mungu ufanikiwe rohoni, kwenye nafsi yako na mwilini mwako, katika maisha yako sawasawa na vigezo ambavyo Mungu ameweka. Rahabu alifanikiwa kiuchumi lakini kitabia hakuwa mzuri.
Kwa mfano Watumishi, je umewahi kujiuliza kwa nini wewe unawaombea wagonjwa wanapona lakini wewe ukijiombea ukiugua wakati mwingine huponi? Ni kwa sababu neno linalokupa imani ya kuwaombea wengine wapone ni tofauti na neno linalokupa imani wewe ili uweze kupona.
Unaweza kuwaombea watu wengine wakafanikiwa kiuchumi lakini wewe ukakwama. Tofauti yake ni neno unalosimamia kuwaombea wengine wafanikiwe ni tofauti na neno ambalo Mungu atakakupa wewe kwa ajili ya kufanikiwa kwako. Sasa wewe unatarajia mwingine afanikiwe kwa hiyo unamwombea afanikiwe lakini wewe hutarajii kufanikiwa.
JAMBO LA PILI
II. TABIA MBAYA NA IMANI NZURI VINAWEZA KUKAA MAHALI PAMOJA NDANI YA MTU KWA PAMOJA, LAKINI KUSUDIA IMANI NZURI KUISHIDA TABIA MBAYA
Ukisoma Galatia 5 utaona inasema twende kwa Roho ili tusitimize tamaa za mwili. Anaendelea kusema Roho yaani Roho Mtakatifu anashindana na mwili. Kwa sababu hiyo mwili unashindana na Roho aliyeingia ndani yako ambaye anataka mapenzi ya Mungu yatimizwe kwenye maisha yako.
Wewe ndiye unayeamua kipi kishinde si shetani wala si Mungu bali ni wewe! Kilichowazuia wana wa Israeli kuvuka mto Yordan na kuingia Kaanani si Mungu, Shetani wala majitu bali ni kutokuamini kwao. Walivuka watoto waliozaliwa Jangwani na Joshua na Kalebu tu.
Ubishi uliopo kati ya tabia na imani nzuri vitapigana huko ndani mpaka kimoja kife sasa ni uamuzi wako wa kuamua kipi kife. Lakini kusudia ndani yako mwaka huu 2021 tabia mbaya inakufa, ukishakusudia namna hiyo unakuwa upande wa imani nzuri.
JAMBO LA TATU
III. TUMIA JICHO LA IMANI NZURI NA USITUMIE JICHO LA TABIA MBAYA KUONA MAISHA YAKO YA BAADAYE YATAKUWAJE
Maandiko yanatuambia kwenye 2 Wakoritho 5:7 ya kwamba _twaenenda kwa imani, si kwa kuona._Kama tunaenda kwa kuona maana yake jicho pia lipo ndani ya imani.
Ukisoma Waebrania 11:1 katika Kipengele cha - "bayana ya mambo yasiyoonekana" maana yake ukiwa na imani unaona vitu vingine ambavyo wengine hawavioni. Kwa hiyo ukiwa na imani ndani yako una jicho ambalo Mungu anakusudia kuona kwa sababu dhambi ilipofusha jicho ambalo tulitakiwa kuwa nalo ndani likafa na ndio maana Paulo alikuwa anawaombea Waefeso ili macho yao yatiwe nuru waweze kuona.
Waefeso 1:17-18 “Roho wa hekima na ufunuo awatie nuru katika macho yenu ya ndani” Kuna macho ya ndani ambayo yanatiwa nuru na neno.
Neno likikaa ndani yako ukapokea imani nuru inatokea ndani yako na kukuwezesha kuona vitu unavyovitarajia.
Maana yake inakuwezesha kuona maisha yako ya baadaye. Rahabu alikuwa na uchaguzi wa maisha imani ilipoingia ndani yake kuwa atazame maisha yake ya baadaye kwa jicho la tabia aliyonayo au atazame kwa jicho la imani.
Imani kabla ya imani haenda kwa Rahabu ndani yake hakuwa na uchaguzi juu ya tabia yake mbaya. Aliona maisha yake yote ndivyo yatakavyokuwa kwa hiyo aliishi kwa kutegemea ukahaba.
Hoi utaona alipowaambia wale wapelelezi kuwa ana ndugu zake na lazima na wao aondoke nao. Pia alikuwa anatazama maisha yake ya baadae kuwa lazima aendelee na ile tabia ili aweze kuishi.
Unaweza kuona mtu akiwa mlevi au kahaba na haamini kwamba anaweza kutoka kwenye hiyo tabia. Maisha yake yanategemea hiyo tabia aliyonayo.
Katika Joshua 2:8-11 utaona ya kuwa jicho la imani humpa mtu kuona mabadiliko ambayo yanakuwa kuona tabia nzuri ambayo ulikuwa huoni mwanzoni.
Rahabu alikuwa anaona mabadiliko ya kumwabudu Mungu mwingine ambaye kwa jinsi ya mazingira aliyokuwa nayo alikuwa anajua akihamia kwa Mungu huyo hatakubali akae na ukahaba.
Kwa jinsi ya kibinadamu asingetaka hayo mabadiliko yule dada alikuwa tajiri sana, unajuaje? Soma Biblia! Lazima alikuwa na nyumba kubwa sana maana aliweza kuwaingiza wazazi wake, ndugu zake na vyote walivyokuwa navyo pia. Waisraeli hawakumwambia watamtembelea lini lakini alikuwa ana bajeti ya kuwalisha na kuwapa huduma zote watu wote wale kwa siku zote. Pia aliishi kwenye nyumba ya kifahari kutokana na kujengwa kwenye ukuta wa mji kama walivyo matajiri. Kwa sasa tungesema anaishi uzunguni maana ni sehemu yenye hewa fresh.
Kukubali kwake kubadilisha maisha alimaanisha haijalishi atapita kwenye misukosuko ya aina gani wakati anabadilisha maisha, lakini akifika huko mbele kwa sababu ya Mungu aliyeamua kumfuata maisha yake yatakuwa mazuri tu.
Unaposoma habari hii haijalishi una tabia ya aina gani, jipe moyo kwa Bwana; hata kama una moyo wa aina gani, utakuja kubadilika tu. Wewe mwaminini Mungu na uwe na imani hiyo ya kuja kubadilika.
JAMBO LA NNE
IV. IMANI NZURI INAPOKUPA FURSA YA KUPATA MSAADA KWA MUNGU ITUMIE
Ndani ya imani kuna fursa na hizo fursa si za kutumia peke yako zinampa Mungu ili uweze nafasi ili aweze kuzitumia vizuri.
Ukahaba wa Rahabu ulikuwa hautafuti hata fursa; fursa zilimzunguka tu kwani alikuwa anafahamika nchi nzima hadi kwa mfalme wa Yeriko. Pia ilifahamika nani anaingia kwake na hata wageni walipoingia kwake ilifahamika kuwa wameingia pale.
Ndani ya Rahabu kuliingia imani baada ya kupata habari za Mungu wa Israeli kwa sababu aliona ndani yake kuna tarajio. Na wale wapelelezi walienda nyumbani kwake na wala si kwa watumishi wa Mungu wanaofahamika pale.
Haiwezekani ukafika eneo fulani halafu ukalala kwa kahaba na asubuhi ukatokea hapo, utafikiri wapendwa wataongea nini?
Rahabu alipowaona wapelelezi jicho la imani lilichukua nafasi yake na kuwapa tafsiri nyingine kabisa kwa sababu hakuwachukulia wa kawaida na ndipo akapokea jibu lisilo la kawaida.
Imani ilipoingia kazini ikayeyusha ule ukahaba kwa sababu Mungu alikuwa ameingia kazini kwa kuwapokea wapelelezi kwa amani, kwani palipo na imani pana amani ya Mungu.
Kama ilivyo kwenye Wakolosai 3:15 Na maneno ya Yesu Kristo katika Luka 10:5-7
Rahabu lazima nafsi yake ilikuwa inapiga kelele na wapambe waliokuwa wanamzunguka na makahaba wenzake walikuwa wanamzunguka. Yeye alikuwa ni na ni kahaba mkubwa inawezekana kuna wengine alikuwa anawaongoza. Sasa yeye akiacha ukahaba inamaanisha na hao watakuja kukosa kazi. Kwa hiyo lazima walikuwa wanamshabikia asije akaondoka na kupokea hiyo imani.
Hujawahi kuona kuna mlevi kanisani wanaomzunguka wanamwona kama anapoteza muda tu. Nimeona walevi wakiokoka wakiwa wamelewa chakari na makahaba wameokoka wakiwa kazini, walikuwa wanapita ofisini kwangu niwaombee kuepuka mikosi ya kukosa mabwana katika shughuli zao.
Ni rahisi sana kuwakatia tamaa, lakini kama unatembea kwa imani unajua kabisa hakuna lisilowezekana kwa Mungu na kwake aaminiye.
JAMBO LA TANO
TABIA MBAYA ISIKUNYIME KUILISHA IMANI YAKO ILI IZIDI KUWA NA NGUVU
Ili imani inaposhindana na tabia mbaya, imani iweze kushinda, kunapotokea fursa imani itumike.
Watu wa Mungu kwenye masuala ya maisha ya kiroho, kikazi, kibiashara, n.k maandalizi ni muhimu ili imani inapokuja ikutayarishe kwa ajili ya mambo yajayo.
Rahabu hakujua wale wapelelezi watakuja lini lakini imani yake ilikuwa tayari, na alikuwa peke yake hakukuwa na mtu wa kumtia moyo alijitia moyo kwa Bwana.
Ukisoma maandiko utajua hiyo imani aliilishaje na aliipataje, ukisoma kwenye Yoshua 2:8-11, anasema "tumesikia habari za huyu Mungu wenu alivyowapigania." Rahabu alikuwa anatafakari shuhuda na ishara za Bwana.
Ni muhimu kutafakari shuhuda na matendo makuu ya Bwana hata kama hajafanya kwako, hata Rahabu alikuwa anatafakari matendo makuu ya Mungu aliyoyasikia.
Ukienda kwenye Zaburi 78:51-57 utaona inasema walimwekea mipaka Mungu wa Israeli kwa sababu hawakuyakumbuka matendo yake makuu, kwa hiyo wakaweka mpaka Mungu asiwasaidie.
Watu wengi wanacheza na imani kwa sababu hawajui ndani yao Mungu ameweka nini. Hakuna aliyejua Rahabu angeingizwa kwenye ukoo wa Yesu, sasa utaelewa kwa nini ule ukahaba ulimbana ili akose ile fursa, ugomvi wa shetani anapokuletea tabia mbaya ujue anataka kuyumbisha imani yako, kwa sababu anajua imani yako ikiyumba maisha yako yanayumba na nafasi yako kwa Mungu inayumba.
Mwangalie yule Sauli ambaye ndiye Paulo, aliandika Nyaraka nyingi sana kwenye agano jipya, lakini ile mbegu ilikuwa ndani yake alipokuwa anafurahia kufa kwa Stephano. Pia alipokuwa analiudhi na kulitesa kanisa la Mungu.
Anaandika kwenye Wagalatia anasema aliliudhi kanisa lakini Mungu aliyemtenga toka tumboni mwa mama yake alimwokoa. Lakini ile mbegu ya imani ilikuweko ikisubiri tu muda wa kutokea. Shetani alimletea kitu cha ajabu sana, alipita kwenye dini na kuanza kuzungumza habari za wokovu.
Shetani alikuwa anawinda kuyumbisha imani ya Paulo ili asisimame kwenye nafasi yake. Kwa hiyo kuna namna mkono wa Bwana ulisimama juu yake katika ulimwengu wa roho.
Wakati wa Musa, shetani lazima alikuwa anafuatilia katika ulimwengu wa roho kwa ajili ya watoto ambao watazaliwa na wanawake wa Kiebrania. Kwa hiyo alijua kuwa kuna mtoto wa kiume ambaye atazaliwa na kuwa tishio kwake. Kama hakujua kwa nini alimwagiza Farao kuwa aue watoto wa kiume badala ya watoto wa kike.
Pia inawezekana wewe usijue lakini katika ulimwengu wa roho Mungu anajua na ndiyo maana shetani naye anakufuatilia ili kukuvuruga kwa sababu anajua katika ulimwengu wa roho Mungu kakuwekea alama na anakufuatilia.
Kwa maana hiyo hutakiwi kumkatia tamaa mtu yeyote au mtoto wako. Mama fikiria Rahabu ndiye mtoto wako na ukamkatia tamaa, unashangaa baada ya muda anakuingiza katika Royal Family (Ukoo wa Yesu) na yeye ndiye anayekuja kukuhubiria injili.
Kwa hiyo usimkatie tamaa mtoto wako maana iko nguvu ndani ya damu ya Yesu ambayo inaweza ikavunja minyororo. Mungu anachofanya ni imani yako isije ikakatishwa tamaa au ukakata tamaa. Haijalishi kuna Mafarisayo ambao wanakatisha tamaa lakini jua kuwa kuna mbegu ndani yao ambayo Mungu kaweka katika watoto wako. Kwani nani angejua kuwa Yakobo mtoto wa Isaka atakuja kuwa baba wa taifa la Israeli?
Yakobo alikuwa ni mlaghai na mwongo lakini Mungu alimfanya kuwa taifa kubwa maana ndani yake kulikuwa na kabila 12 za Israeli. Unaweza ukamdharau mtu kwa sababu ya tabia aliyonayo na hujui mbegu aliyonayo. Ndio maana hutakiwi kukata tamaa kwa ajili ya wototo wako au mzazi wako hata kama ni mzee kiasi gani.
Ukisoma Mwanzo 25:23 utaona mbegu ilipandwa ndani ya mama yake na Yakobo; kulikuwa na kabila 12. Alipokuwa anamkimbia Esau kwa sababu alijua kuwa atamwua Yakobo alikuwa anakimbia kutoka Kanaani kwenda mahali pengine Mungu alimkamata njiani. Mungu alijitambulisha kuwa “mimi ni Mungu wa baba yako Ibrahimu na Isaka”.
Yakobo alikuwa hamjui Mungu wa baba yake. Sababu ya Mungu kujitambulisha kwake ilikuwa ni kumwambia kuwa hawezi kukimbia na mbegu ambayo amemwekea ndani yake.
Hata wewe haijalishi una tabia mbaya kiasi gani huwezi kukimbia na mbegu nzuri ambayo Mungu kaweka ndani yako.
USHUHUDA
Kuna muda najitazama mimi mwenyewe na natamani kujifinya kwa maana huwa natazama na najiuliza hivi Mungu mimi nilikuwaje?. Wakati ule nasoma chuo Sokoine Morogoro. Wakati ule ilikuwa ni Faculty of Agriculture Sokoine chini ya chuo kikuu cha Dar es Salaam. Nilikuwa Disco Joker DJ nikipiga mziki katika kumbi za burudani. Lakini ndani yangu kulikuwa na zaidi ya vitabu 32 ambavyo nimeandika mpaka sasa. Lakini nilikuwa napiga mziki Disco.
Pia usiku tulikuwa tunaenda kunywa gongo na wenzangu. Siku ambayo Mungu aliniokoa alisema “haianzii hapa tulikubaliana na mama yako kuwa wewe na wadogo zako mtakuwa watumishi wangu.”
Kwa hiyo Mungu alinitoa huko nikiwa na mbegu yake ndani yangu. Na hii semina ya leo ilikuwepo pia maana ilikuwa ndani ya mbegu. Hii ni sawa na mti ambao huwa unatoa matunda kila mwaka katika shina hilo hilo. Kwa hiyo wewe endelea kuupalilia huo mti ili uendelee kuzaa matunda.
Huwa nikiona kijana akipata shida na kuwa na tabia mbaya huwa siwakatii tamaa maana najua kitu ambacho Mungu kaweka ndani yako.
USHUHUDA
Wakati fulani nilikuwa kwenye semina mkoa fulani. Nilisikia moyoni kuwa niite watu ambao wana tabia za wizi na wanashindwa kuacha.
Siku hiyo alikuwepo na RPC na mkuu wa mkoa walikaa mbele kabisa. Walitoka vijana wengi na mtoto mmoja nae pia alitoka. Wahudumu walienda kumwuliza kuwa hapa wameitwa watu ambao wana tabia ya wizi.
Yule mtoto akasema na mimi ni mwizi huwa namwibia mama yangu. Baada ya ile semina RPC alisema sikutarajia wale watu watoke maana wananifahamu na nilikuwepo pale kwenye semina nikiwa nimekaa mbele.
Unaweza kuwatazama wale watu na ukawaona kama hawafai. Kama umewahi kutembelea jela wakati ule wa Yusufu ukaona wale wafungwa wote walikaa pale kama hawafai. Kumbe alikuwepo Yusufu ambaye ana mbegu ya Mungu ndani yake kwa ajili ya taifa la Misri.
Kwa hiyo usikate tamaa kuwa hata kama umewaona wana tabia mbaya, nakuambia yuko Yesu ambaye atawasaidia maana huu ni msimu mpya. Utatembea na utavuka kabisa na Mungu atakusaidia.
USHUHUDA
Huyu mtu kaandika anasema "Mwaka 2015 nilikuwa naumwa lakini baada ya kupima katika vipimo mbalimbali haikujulikana naumwa nini.
Mwaka 2017 baada ya kupimwa tena nilijulikana kuwa nina Saratani (Cancer) ya mifupa. Kwa hiyo nilikuwa naishiwa damu mara kwa mara na ilikuwa inashuka mpaka 5. (Kwa wale wanajua vipimo vya damu wataelewa).
Pia nilikuwa naongezewa damu mara kwa mara na miguu ilivimba na kuwa mieusi. Lakini namshukuru Mungu sana katika semina iliyoanza tarehe 5 -12 January 2020 iliyofanyika katika uwanja wa reli Arusha. Nilihudhuria siku zote na wakati wa maombi uliomba sana juu ya wagonjwa wa Cancer (Saratani)".
Namshukuru Mungu sana kwa mwaka jana wote na mpaka leo matatizo yote ambayo nimeyataja hayajanisumbua tena mpaka leo.
Anaendelea kusema "nimeenda katika hospitali mbalimbali kwa ajili ya check up mbali mbali na wanasema ugonjwa wa cancer hawauoni tena. Pia anasema damu sasa imerudi kawaida na iko juu ya9".
Baada ya huo ushuhuda sasa tuangalie hatua ya nne
HATUA YA NNE
4.TUMIA MBINU ZA MAOMBI YA KULIA INAPOHITAJIKA
Nataka tutazame mambo kadhaa ili iwe rahisi sana kwako kuweza kulitekeleza hili jambo.
JAMBO LA KWANZA
I) JE UMEWAHI KUKUTANA NA MAZINGIRA AMBAPO ULISIKIA MSUKUMO WA KUOMBA KWA KUTUMIA MAOMBI YA KULIA. JE ULIFANYEJE?
Waebrania 5:7
Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu
Ikiwa Yesu alipita katika mazingira ambayo yalifanya atumie mbinu ya maombi ya kuongea na kulia, hiyo inatufanya na sisi tujue mbinu za maombi ya aina zote na si tu kuomba kwa maneno bali na mbinu ya maombi ya kulia machozi.
JAMBO LA PILI.
II) MUNGU HUWA ANAJIBU MTU ANAPOOMBA KWA MBINU YA KULIA
Zaburi 145:18 - 19
BWANA yu karibu na wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu. Atawafanyia wamchao matakwa yao, Naye atakisikia kilio chao na kuwaokoa.
Anaposema atasikia kilio chako hiyo ni mbinu mojawapo ya maombi. Ni zaidi ya kuomba kwa maneno kawaida.
Kutoka 3:7-9
BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi.
Kilichomfanya Mungu ashuke ni kwa sababu ya kulia. Nilitaka uone ya kwamba Mungu huwa anajibu kama utaamua kutumia mbinu ya kuomba kwa kulia inapohitajika na uwe na uhakika Mungu atajibu.
JAMBO LA TATU
III) MUNGU ANAJUA KUSOMA LUGHA YA MACHOZI YETU NA KUJIBU
Maana yake ndani ya machozi kuna lugha ambavyo Mungu anaijua. Machozi hayafanani kwa lugha yake japokuwa yanaweza kufanana kwa kuonekana kwake lakini hayawezi kufanana ujumbe uliobebwa na yale machozi.
Zaburi 6:6
Nimechoka kwa kuugua kwangu; Kila usiku nakieleza kitanda changu; Nalilowesha godoro langu kwa machozi yangu.
Analia usiku, kitu gani kinachomfanya alie? Uchungu! Kwa hiyo ukilia ukiwa na uchungu namna hiyo, yale machozi yanapoenda mbele za Bwana yanaachilia hali ya moyo wako ambayo huna maneno ya kujieleza kwa Mungu ili aweze kupata jinsi unavyosikia ndani.
Haijalishi ni tone moja, kila chozi lina jibu sawasawa na kitabu cha Ufunuo 21:4 _Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita._
Unamkumbuka Hana mama yake nabii Samweli aliyemlilia Mungu alimsikia yule mama na uchungu kwenye moyo wake kwenye machozi yake. Yule mama alimlilia Mungu kwa namna ambavyo mdomo wake ulikuwa hauwezi kuumba tena maneno lakini maandiko yanasema ule uchungu ulikuwa moyoni mwake. Katika ulimwengu wa Roho yale machozi yalienda mbele za Mungu yakaeleza uchungu wa yule mama aliyeona kama amesahauliwa katika kile ambacho alikuwa anaomba kila mwaka na akawa anapata dhihaka.
Ukisoma Kutoka 2:23-24 utaona maandiko yanatuambia ya kwamba walimlilia Mungu kwa uchungu na Mungu akakumbuka agano.
Wagalatia 4:19
“Vitoto vyangu, ambao kwamba nawaonea utungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu;”
Unapopita kwenye mazingira ambayo Mungu anakuwekea wazo jipya au ngazi mpya ya kitu unachofanya au ya ushirika wako wa kumjua Mungu zaidi lakini unakutana na upinzani mkubwa wa kuzuia kile cha Mungu na mapenzi ya Mungu yakasimama, utakuta Roho Mtakatifu anakushukia na anateremsha ndani ya moyo wako maombi ambayo ndani yake yana kilio ili kupambana na ule upinzani.
Wagalatia walikuwa wanapambana na mapokeo ya dini yao ndio maana Paulo aliwaandikia akisema, "Enyi Wagalatia nani kawaloga"?. Maana yake kuna roho ya kichawi ambayo iliingia ndani ya kanisa na kusisitiza mapokeo mabaya badala ya neno la Bwana.
Saa nyingine wazo jipya linakuja sawasawa na Isaya 55:8,11
“Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA…… ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.”
Na utakuta hilo wazo linaloletwa likapingana na la kwako lakini Mungu anakuletea wazo jipya kwenye ngazi hiyo halafu ndani yako ubishi unaanza. Sasa kila ukitaka kufanya hicho kitu unakuta machozi yanakutoka tu kwa kusikia uchungu ndani.
Pia unaweza ukakutana na upinzani kutoka kwa watu au mwilini kwako (kama ilivyotokea kwa Yesu - 'roho i radhi lakini mwili ni dhaifu') ujue sio mabadiliko kwa ajili yako tu bali kwa ajili ya kanisa na ulimwengu kwa ujumla.
Yesu alipata upinzani kutoka kwa shetani, mwili wake na kwa Yuda ila mwili ndio ulichukua sehemu kubwa ndicho kilichopelekea kuingia katika maombi mpaka matone ya damu yakamtoka, ili apate ushindi wa kile kilichokuwepo ndani yake.
Hata wewe katika kipindi hiki kipya Mungu atakuwekea nguvu za Roho Mtakatifu ndani yako na saa nyingine utakuwa unasikia kulia tu na hujui kitu gani kinatokea - ujue Mungu anakusaidia ukae kwenye maombi. Sawasawa na Warumi 8:26 inayotuambia hivi_“Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.”_
USHUHUDA
Kuna muda nilikuwa ninasafiri kwenda nchi ya Madagascar kwenye semina ya maaskofu kwenye nchi hiyo, nilipandia ndege Nairobi. Nilipoingia kule ndani nilikaa katikati kwa hiyo kulikuwa na watu kulia na kushoto kwangu.
Nikamshukuru Mungu kwa ajili ya safari; ndani yangu nikasikia kuugua na hakukuwa na namna ninaweza kuzuia yale machozi kwani yalikuwa yanatoka tu. Ni rahisi sana ukatazama kushoto na kulia ukiwaza hao watu watakuelewaje lakini kama unajua una Roho Mtakatifu kisikusumbue kwani yeye ameshakuzunguka.
Maombi ya kulia ni gia kubwa sana na kama unaionea aibu kazi kwako
Niliendelea kuomba namna hiyo na saa ilipofika ndege ya ndege kuondoka walifunga milango lakini baada ya muda ndege haikuondoka na muda ukaendelea kupita. Ndipo nikaanza kumwuliza Mungu kuna shida gani (wakati naendelea kuomba). Akaniambia mbele kuna ajali kwa sababu ndege ina shida. Akaniambia niombe ili waone tatizo lililoko kwa hiyo nikaanza kuomba pamoja na kunena kwa lugha na kuomba kwa ufahamu nikisema Mungu rubani asiondoke na ndege kabla hajagundua kitu.
Baada ya muda rubani akaomba msamaha kwa kuchelewa kuondoka halafu akasema wamegundua ya kwamba ile ndege imepata shida kwenye matairi. Wakati huo wametokea Ufaransa 🇫🇷 kama saa moja iliyopita. Endapo wangeendelea na safari ile ndege wakati wa kutua matairi yasingetoka na ingetua kwa tumbo na ingesababisha ajali.
Ndipo akasema wameita mafundi ili waendelee kutengeneza hivyo wafanyakazi wa ndege watatoa breakfast kwa sababu ilikuwa asubuhi. Ndipo wakagawa hiyo chai nami sikunywa ila ndani yangu kuugua kukaendelea na nikaendelea kuomba hadi masaa mawili yakapita.
Ndipo tangazo likatoka kuwa mafundi hawawezi kutengeneza kilichoharibika hadi spea itoke Ufaransa kwa hiyo tutateremka na kulala Nairobi kwa gharama ya shirika la ndege - Air France. Na wote tukateremka tukalala hapo hotelini hadi kesho yake ndipo safari ikaendelea.
Ningeweza kuona aibu kabisa na kusema nitaomba nikifika huko lakini ningekuwa nimeshachelewa. Kwa sababu saa hiyo Mungu anakusemesha mbele yako kuna upinzani.
Ukisoma kitabu cha Luka 7:36-50 ni habari nzuri, nitasoma mistari michache
Luka 7:37-38 Na tazama, mwanamke mmoja wa mji ule, aliyekuwa mwenye dhambi, alipopata habari ya kuwa ameketi chakulani katika nyumba ya yule Farisayo, alileta chupa ya marimari yenye marhamu. Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza kumdondoshea miguu machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, akiibusu-busu miguu yake na kuipaka yale marhamu.
Angalia msitari wa 44 unasema "Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, Wamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi miguu yangu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake."
Angalia mstari wa 47 "Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana;" sawa amesamehewa lakini ametubu saa ngapi? Machozi yalibeba toba. Nimekwambia machozi yana lugha na Mungu anajua kusoma.
Ukienda kwenye Luka 22:62 inazungumza habari ya Petro baada ya kumkana Yesu mara tatu, Petro alilia kwa machozi na hakusema kitu. Machozi yake yalibeba toba ya kumkana Yesu mara tatu, maana baada ya Yesu kufufuka aliwaambia kuwa ‘kawaambieni wanafunzi wangu pamoja na Petro …’ kwa sababu Petro alikuwa ameshajitoa kwenye list ya wanafunzi.
Kwenye kitabu cha Esta 8:3-4 unaona Esta akienda kwa mumewe (mfalme) wakiwa wamezuiwa wote pamoja na yeye mwenyewe, Alipoenda pale alitoa machozi akaomba, Mfalme akamnyooshea fimbo yake ya dhahabu. Machozi yanaweka msisitizo wa ombi lako.
Mhubiri 4:1
"Kisha nikarudi na kuona madhalimu yote yanayotendeka chini ya jua; na tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo, walakini wale walikuwa hawana mfariji."
Kwa hiyo unaweza kulia na Mungu akajua unatafuta haki ulipodhulumiwa.
Pia tunaipata hiyo kwenye Luka 18:7 anasema "Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?" anazungumza juu ya yule mama aliyeenda kwa Mungu kama hakimu alitoa mfano wa kadhi, Yesu naye anasema, na Mungu je hatawapatia haki wale wanaomlilia mchana na usiku,?
Maandiko yanasema pia jihadhari kwenda mbele za Mungu na machozi ya kinafiki maana Mungu anasoma machozi ujumbe katika machozi. Hiyo utaipata katika Waebrania 12:17.
JAMBO LA NNE.
IV) UNAWEZA KUMSAIDIA KUOMBA ALIAYE KWA WEWE KUOMBA PAMOJA NAYE KWA KULIA NA WEWE
Hii unapata katika kitabu cha Warumi 12:15_Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao._
USHUHUDA
Siku moja tulikuwa katika Mlima Karmeli Nchini Israel kwa ajili ya maombi. Kila tukienda Israel lazima twende pale na ni mahali ambapo Mungu alitusemesha kuwa tuwe tunaombea mambo ya kitaifa.
Na hakuna maombi ambayo tumeombea pale hayajajibiwa. Sasa usiulize ni maombi yapi bali wewe tambua tu kuwa maombi yote ya kitaifa ambayo tumeomba pale yamejibiwa.
Kuna mwaka fulani kulikuwa na jambo fulani la kitaifa ambalo lilikuwa linajadiliwa bungeni la halikupata majibu katika kipindi cha siku mbili.
Na tuliomba kama Eliya alivyofanya alivyosema na ijulikane leo. Kwa hiyo na sisi tulichukua bendera ya Tanzania na tukaweka katika madhabahu ya kanisa ambalo lipo pale katika mlima Karmeli. Tukatoa na sadaka kama Eliya alivyofanya tukaanza kuomba, na ile sadaka tuliiacha pale kwa ajili ya wale watu ambao ndio wanatunza lile eneo.
Tulipoanza kuomba ukashuka upako wa kulia. Tulilia kwelikweli pia hata baada ya pale sikumbuki tena kama tiliruhusiwa kuingia tena kule ndani. Huwa wanatupa tu sababu kuwa sasa kuna mabadiliko ya uongozi kwa hiyo huwa wanatupa chumba kimojawapo cha pembeni pale ila sio ndani ya kanisa tena.
Siku ile alikuja baba Paroko pale kutazama wakati tunaomba kwa kulia. Alijaribu kutunyamazisha na aliona hamna mtu ananyamaza kwa hiyo aliamua kuondoka tu.
Wakati tumeatamia pale tunaomba na watu wengine walikuwa wamelala kabisa pale wanalia, tulipokuja kufungua macho tulimuona mzungu mmoja na yeye yupo katikati yetu na yeye analia na kubandika mikono katika bendera ya Tanzania.
Tulimuuliza wewe umetokea wapi? Alisema nilikuwa napita nje ya kanisa hili na nilisikia mnalia. Roho Mtakatifu akaniambia na mimi niungane nanyi kuja kulia. Tulimuuliza je unajua kiswahili akasema hapana sijui. Ila mimi ninachojua kuwa Roho Mtakatifu aliniambia kuwa nije nilie nanyi maana najua hiyo bendera ni ya nchi yenu. Kwa hiyo Mungu alijua ana mzigo wa kuomba pamoja na na sisi na akampa.
Yeremia 9:17-18,21
BWANA wa majeshi asema hivi, Fikirini ninyi, mkawaite wanawake waombolezao, ili waje; mkatume na kuwaita wanawake wenye ustadi, ili waje; na wafanye haraka na kutuombolezea, ili macho yetu yachuruzike machozi, na kope zetu zibubujike maji. Kwa maana mauti imepandia madirishani mwetu, imeingia majumbani mwetu; Ipate kuwakatilia mbali watoto walio nje, na vijana katika njia kuu.
Maana yake unaweza ukapata watu wa kuja kulia pamoja na wewe katika hilo hitaji ambalo Mungu kakupa.
Mungu akubariki sana tuonane tena katika wakati na somo lijayo.
MWISHO
0 Comments