100/recent/ticker-posts
KANAANI MPYA - Lisikilizeni Neno la Bwana............. MAOMBI NA MAOMBEZI --- Tupigie; +255767-155-623 Ujumbe mfupi/Whatsapp; +255620-179-783

Mwl:C.Mwakasege - UDHIHIRISHO WA NGUVU ZA MUNGU UNAPOMSHUKURU MUNGU

 UDHIHIRISHO WA NGUVU ZA MUNGU UNAPOMSHUKURU MUNGU

MALENGO YA SOMO

Malengo 3 makubwa ya somo hili ni haya yafuatayo:-

1.Ujue aina mbalimbali za kumshukuru Mungu.

2.Uimarishe imani yako ili unapo mshukuru Mungu udhihirisho wa Nguvu za Mungu uonekane na uongezeke.

3.Ukue katika imani ya kumjua Mungu zaidi katika Yesu Kristo. 

(Mungu ni Neno na Yesu ni Neno kwa hiyo kila Neno limebeba sura ya Mungu na sura ya Yesu. Hivyo kadri unavyolisoma zaidi linakusaidia kumjua Mungu zaidi katika Yesu Kristo na kwa sababu hiyo imani yako inaongezeka)
 

Na kwa kujifunza somo hili tutakwenda kujifunza kwa mifano ili iwe rahisi zaidi kulielewa.
 
MFANO WA KWANZA
KUMSHUKURU MUNGU WAKATI AHADI ALIYOKUPA YA KUKUSAIDIA BADO HUJAIONA IKITOKEA
 
Soma: 2 Mambo ya Nyakati 20:1-25
Katika mfano huu wa kwanza tutaangalia mambo machache ambayo Mungu anataka tuone.
 

JAMBO LA KWANZA
1. TATIZO LINAPOKUSUKUMA KUOMBA KWA JUHUDI NA KWA BIDII
 

Biblia inazungumza juu ya kuomba kwa juhudi,bidii na bila kukoma pia inazungumza misingi tofauti tofauti ya kuomba.
 
Ukisoma mstari wa 1-4 katika 2 Mambo ya Nyakati 20, utaona kabisa maombi ya namna hii unayapata tu pale ukifika mahali  hakuna plan B. Ni Mungu kukusaidia  na bila hivyo umekwama. Huwezi kuomba kwa bidii kama hujafika mahali hapo maana kama una  Plan B basi huwezi kuwa na msukumo wa kuomba kwa bidii.
 
Lazima ujue ya kwamba ukitaka kutoka hapo ulipo ni lazima awe ni Mungu peke yake kakusaidia. Na kama kuna mtu anaweza kukusaidia basi atatoa upepo kwenye maombi yako. Sio vibaya kupata msaada kutoka kwa watu maana Mungu anaweza kukunyanyulia watu wengi sana. Lakini hapa tunazungumzia masuala ambayo watu wengi sana wanaofuatilia somo hili wanapitia.
 
Yehoshafati kwa jinsi ya kibinadamu angeweza kuitisha jeshi lake na angeweza kuita Wafalme marafiki ili wamsaidie katika ile vita. Lakini unaona Yehoshafati katikati ya kuzungukwa na majeshi ya maadui hakuogopa kutafuta nafasi ya kuomba msaada kwa Mungu wake.
 
Watu wengi sana wanapokumbwa na matatizo makubwa sana huwa wanapoteza utulivu  ndani yao na hawawezi hata kuomba wala kumtafuta Mungu kwanza.

Katika mazingira hayo unakuta mtu anatafuta watu wa kumsaidia na msaada kila mahali anapoweza ili asaidie.  Kutafuta misaada kwa watu si vibaya lakini angalia wenzetu walichofanya cha kumtafuta Mungu na kutafuta msaada wake kwanza.

Maandiko yanatuonyesha kabisa Yehoshafati pamoja na kuogopa na ile hofu aliyoipata ndani yake ilimsukuma kwenda kwa Mungu.
 
Yehoshafati alipoanza kuomba (ukisoma mpaka ule mstari wa 12) unaona kabisa ni mtu ambaye alikuwa na utulivu. Kwa sababu alipangilia maombi yake vizuri akimkumbusha Mungu safari zote walizofanya na jinsi ambavyo wale Mungu alisema ni ndugu zao hivyo wasiondolewe.

Ndipo akamwambia Mungu waondolewe kwa sababu ya wanachowafanyia na akamweleza Mungu mahali walipo na hata akiwaambia wapigane nao hawawezi kwa sababu ya wingi wa jeshi lile la maadui zao.

Na akasema Mungu akiwauliza kitu watajibu hawajui bali macho yao yanamwangalia Yeye peke yake. Hii ni sawa na mtu aliyeamua kupambana yeye mwenyewe kwa kila mbinu halafu akikwama anarudi kwa Bwana na kujieleza namna hiyo.

Yehoshafati alikuwa kiongozi wa kabila la Yuda sasa walipofika Yerusalemu watu wake walifikiri watapata suluhisho kutoka kwake, ila yeye akawaambia watafute uso wa Bwana. Sasa unapofika mahali kama hapa unapaswa uombe kwa Bwana na hautakiwi uombe huku umechanganyikiwa au una hofu (panic). Omba ukiwa na utulivu kutoka kwa Mungu, hata kama utakuwa unalia huku ukiomba haina shida, bali usiwe umemkasirikia  Bwana.


JAMBO LA PILI
2. MAOMBI YALIWAPA JIBU LA AHADI ISIYO NA UDHIHIRISHO WAKATI WANAJIBIWA.

Ukisoma pale mstari wa 13 utaona kuna maelezo ya muhimu pale, sasa tatizo langu linakuja hapa kuwa kwa nini Mungu asiwajibu pale pale badala ya kusubiri hadi hiyo kesho?

Watu wengi wanapoomba Mungu anawajibu kwa kuwapa maandiko lakini huoni udhihirisho wa hilo andiko la ahadi. Wengine wameshapokea neno linalosema Mungu atawatetea bila wao kupigana lakini anawaambia kesho huku majeshi ya maadui yamewazunguka.

Unaweza ukakutana na mstari kwenye Biblia ambao umebeba ahadi na ukatambua kabisa Mungu anasema nawe lakini unakuta haujadhihirishwa .

Na neno linakuja kuwa “simameni muone wokovu wa BWANA” wakati huo jeshi la adui limewazunguka. Mstari kama huo unaweza ukausoma na kuuhubiri lakini ni kazi sana kuuweka kwenye matendo.

Haijalishi Mungu anakupa ahadi ya namna gani, kama unajua hujafikia nafasi (kiwango cha imani) kama ya wenzetu lazima hofu itakuwepo. Kwa wengine ni rahisi sana kutafuta mpango mbadala na wengine watazimia wakiwa huko ndani kabla adui hajafika. 



JAMBO LA TATU
3. SI KILA MTU ANAWEZA KUSEMA MANENO YA KUINUA IMANI YAKO UNAPOTAZAMANA NA TATIZO AMBALO ULITEGEMEA MUNGU AWE AMELIMALIZA, LAKINI BADO LIPO.


Kwenye mstari wa 20 - 21 utaona maneno ya muhimu hapa kuwa akina Yehoshafati walipopewa ule ujumbe wa ahadi, ndani ya mioyo yao walipokea lile jibu lao kwa imani kabla hawajaiona.

Marko 11:24
Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.


Biblia inasema ili mpokee lazima muamini kwanza mnapokea. Maana yake tunapokea kwanza ndani ya mioyo yetu ndipo yanadhihirishwa kwa nje. Kwa hiyo inatakiwa tuyapokee kwanza ndani yetu kwa imani ndipo yanakuwa yetu.

Kwa maana hiyo tunapokea kwanza ahadi kwa imani ndani ya mioyo yetu kabla Mungu hajayadhirisha kuwa halisi. Sasa ukirudi kwenye hii habari inaonyesha hawa Watu walipokea kwa imani. Maana walipokea kabisa na katika habari hiyo utaona vitu vitatu pale kuanzia mstari wa 17-18.

Katika mstari wa "18 Yehoshafati akainama kichwa, kifulifuli; wakaanguka mbele za Bwana Yuda wote na wakaao Yerusalemu, wakimsujudia Bwana". Maana yake ni kitu ambacho kilitoka moyoni kwao maana waliamua kumuabudu Mungu wakati wamezungukwa na maadui.

Unapokuwa umezungukwa na tatizo na Mungu anakusemesha na ndani ya moyo wako unajua uaminifu wa Mungu jinsi ulivyo. Unasema hata kama sijaona uaminifu wa Mungu ulivyo lakini najua ambacho Mungu umesema ni halisi na hakika. Ndani yako imani ikipokea kuna kitu kinakuwa halisi kwako ambacho wakati mwingine unakuwa unajiuliza je nina akili yangu sawa sawa maana kwa  mazingira niliyonayo sitakiwi kufanya kitu cha jinsi hii.

Hapa tunaona namna ambavyo Yehoshafati alipopokea ule ujumbe alianguka kufulifuli na kumsujudu Mungu. Japo alikuwa kazungukwa na maadui .

2 Mambo ya Nyakati 20:19
Na Walawi, wa wana wa Wakohathi na wa wana wa Wakorahi, wakasimama ili wamsifu Bwana, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana.


Sasa fikiria wanafanya hivyo wakati wamezungukwa na maadui. Ni rahisi kusema maadui watasikia na kuja kutuvamia maana watajua tulipokaa kwa sababu watajua tupo katika ibada na hatujajiandaa kwa ajili ya vita.

Moyo wako unapopokea kwa imani na kumwangalia Mungu kuwa yeye ni mkuu kuliko kuangalia matatizo ambayo yamekuzunguka. Moyo ukiisha kubali ndani yako inatoka hali kuu ya kumsifu Mungu mpaka watu wengine watakushangaa.

Moyo wako ukipokea  kwa imani

1.Utaabudu

2.Utasifu

Kusifu hutahitaji kwaya kukusaidia pia hata waimbaji hawatasukumwa kusifu. Maana kutakuwa na namna fulani ndani yako nzuri ya kumsifu Mungu kwa sababu kajibu maombi yao.

Mstari wa 20 kilitokea kitu cha ajabu kidogo maana unasema "Wakaamka asubuhi na mapema". Huwezi kuamka kama hukulala hili ina maana walipata amani ya kwenda kulala. Je unawezaje ukalala katika mazingira ya namna hiyo. Lazima awe ni Mungu peke yake ambaye atakuwa kakupa usingizi katika mazingira ya namna hiyo.

Katika mazingira hayo kama si Mungu kukusaidia huwezi kulala. Maana inaweza ikafika mpaka asubuhi  hujaweza kupata hata usingizi yaani unageuka huku na huku bila kulala.

Kama ukiona namna hiyo na hauna namna nyingine ya kufanya, unamwambia Mungu kuwa  Mungu mimi sina uwezo wa kutatua hili tatizo maana ni kubwa sana macho yangu yanakutazama wewe tu.

Sasa kwanini unaanza tena kupanga namna ya kutoka wakati umesema unamtegemea Mungu?

Ukiwa katika hali ya namna hiyo endelea kutafakari ahadi ya Bwana ndani yako. Ukiona katika nafsi yako maswali yanakuja kutoka katika kona moja achilia ahadi kutokea kona nyingine sema  nafsi yangu usisahau kuwa tumeahidiwa na Bwana kuwa vita si vyetu ni vya Bwana na tutaona wokovu wa Bwana.

Upande mwingine wa nafsi yako unaweza ukawa unasema Bwana kaahidi na kusema ni kesho. Lakini upande mwingine utakuwa unasema  nani kasema acha kesho ijisumbukie yenyewe na  tunataka leo. Japo mtabishana sana huko  lakini ukiwa na maandiko ya kutosha ndani yako ya kunyamazisha hiyo kona ya nafsi ambayo inapiga kelele mwishoni itanyamaza tu.

Wafilipi 4:6-7
Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.


Matokeo ya kwamba umekabidhi jambo mikononi mwa Bwana amani itakuja ndani yako. Amani inayopita akili na fahamu inakuja kwako.

Japo mwili utapiga kelele lakini moyo utatulia ndani yako na kuambia mwili kuwa  nyamaza maana tumeshapokea. Mawazo yanaweza yakaja kwako lakini endelea kuisemesha nafsi yako na kuikiri ahadi  ya Bwana. Maana utauambia mwili kuwa nisingeweza kupata utulivu wa jinsi hii katika changamoto hizi.

Ukirudi kwenye hiyo habari utaona kuwa walipoamka asubuhi walifikiri hawatayakuta majeshi ila walishangaa baada ya kuona majeshi yako pale pale.

2 Mambo ya Nyakati 20:20
Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini Bwana, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.

Baada ya kutiwa moyo, waliabudu, walisujudu na kumsifu Mungu kwa sauti kubwa sana. Maana walipata amani mpaka shetani aliwashangaa sana maana waliweza kulala katikati ya maadui kwa sababu Mungu aliwaambia kesho wataona wokovu wake.

Kulipokucha asubuhi waliona wale askari yaani maadui zao wanawatazama kwa hiyo uwe na uhakika kuwa mioyo yao iliinama tena. Ndio maana Yehoshafati alisema mwaminini Mungu ina maana imani yao iliyumba. Waaminini manabii wake ina maana walipuuzia ile ahadi ambayo walipewa jana.

Si rahisi kupata watu ambao wanaweza wakakutia moyo katika mazingira ya namna hiyo. Pia ukisoma habari za Ayubu utaona kuwa mambo yalipokuwa mazito kuna watu waliacha imani zao ziyumbe.

Mke wa Ayubu alipoona uvumilivu umemshinda alimwambia Ayubu amtukane Mungu. Maana sasa kama yeye ndio anataka kufanya hivyo si angemtukana yeye mwenyewe tu!. Kwanini anataka na mume wake naye amtukane Mungu? Yeye alifikiri imani ya Ayubu imeloa kama yake.

Walipokuja marafiki wa Ayubu wakamtazama  na walimsemesha maneno magumu sana kiasi ambacho Ayubu akawaita ni marafiki wataabishaji. Walimsemesha maneno magumu sana ya kumrudisha nyuma ili asiendelee na Mungu wake na Ayubu alikuwa na kila sababu ya kumuacha na kumdharau Mungu wake.

Ayubu alijisemea "Bwana alitoa na Bwana ametwaa" ni maneno mazuri sana, Ayubu anatuambia yeye hajui kilichotokea lakini anachojua yuko mikononi mwa Mungu na ameruhusu kama hajaruhusu basi kuna mahali kakosea lakini kwa vyovyote vile hamuoni Shetani kama msababishaji.

Shetani anakasirika sana usipompa utukufu, na Mungu hakumuonyesha  sababu ya yeye kuwa katika hali ile. Na ndio maana kuna vitu vingine Mungu hawezi kukuruhusu uone maana vitamaliza imani yako kabisa.

Unaweza ukawa unapita kwenye kipindi kigumu sana unamwambia Mungu uombeje alafu unasikia moyoni "shukuru kwa kila jambo" kinaweza kuwa kigumu sana kukitekeleza. Unaweza kujifanya wa kiroho sana ukaanza kushukuru na Mungu anajua tu unaiga unashukuru mdomoni lakini moyoni hamna shukrani.

USHUHUDA
Katika uzazi tulionao nyumbani mwetu, tulipoteza mimba moja. Wakati ule nilikuwa naenda Canada kihuduma na nilijua kilichokuwa kinatokea nikaomba sana lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote.

Lakini nikiwaombea wengine wenye shida ya namna hiyo na Mungu anawavusha ila mimi sikuvuka.

Baadae nikampigia simu mke wangu kumuuliza anaendeleaje, akaniambia mimba imeharibika. Sasa fikiria kesho yake nilikuwa naanza semina ya kuhubiri kuwa Mungu anajibu maombi. Nilimuuliza mke wangu kama yeye ana amani akaniambia anayo, akaniuliza kama nina amani nikamwambia wazi "sina". Akaniuliza sasa ndio nafanyaje, nikamjibu kweli sijui.

Yule mwenyeji wangu aliponitazama akajua kuna habari mbaya nikamueleza, akaniuliza sasa ndio nafanyaje? Nikamjibu pia sijui. Nikaingia chumbani, nikamuuliza Mungu sasa ndio naombaje? Akaniambia nishukuru kwa kila jambo, nikamjibu Mungu siwezi. Sikuwa na sababu ya kuficha kwa sababu Mungu ananijua vizuri labda anisaidie tu nashukuruje.


Na ndipo aliponisemesha maneno magumu sana, la kwanza akasema                                                         1. Yeye ni Mungu na atabaki kuwa Mungu hata kama hajajibu ninavyotaka. La pili akasema 

2. Mimi na yeye tumetoka mbali sana kwa hiyo hili lisitugombanishe.                                     Nikamwambia Mungu kama anataka nimshukuru anisaidie. Nikapiga magoti na nguvu za Mungu zikanishukia na moyo wangu ukaanza kububujikwa kwa shukrani.

Lakini ukijuliza unashukuruje maana kwa jinsi ya kawaida ulichokuwa unaomba huna. Hawa watu wamemsifu Mungu na wakalala waliweka imani yao kwenye matendo wanaamka asubuhi Tatizo bado lipo. Ndio maana walipewa neno la kuwatia moyo.



JAMBO LA NNE
5.KUMSHUKURU MUNGU UNAPOSIKIA MOYONI KUMSHUKURU ILI AGEUZE JIBU LA AHADI LIWE JIBU HALISI


2 Mambo ya Nyakati. 20:21-22
"Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia BWANA, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni BWANA; kwa maana fadhili zake ni za milele. Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa."

Walipokuwa wanaendelea kusogea wakiimba na kusifu na ili kuonyesha kwamba imani yao imerudi wakatanguliza waimbaji mbele ya askari wakawekwa nyuma kwa sababu walikuwa wanajiandaa kupigana Mungu akawaambia vita si yao na wataangalia tu wokovu wa Bwana.

Sasa kitu kinachonifikirisha zaidi ni huu msitari wa 22 unaosema "Nao walipoanza kuimba na kusifu,.." ndipo udhihirisho wa Bwana ukaja. Kwanini Mungu alisubiri waimbe na kusifu ndio adhirishe nguvu zake? Kwa sababu walipoamka asubuhi imani yao ilifika mahali ambapo haiwezi kusukuma upako wa Mungu uingie kazini kwa ajili ya kudhihirisha neno ambalo Mungu kaweka.

Ukisoma Biblia utajua kuwa kinachovutia muujiza wako ni imani yako. Ukisoma miujiza mingi ambayo aliifanya Yesu alipokuwa akitembea hapa Duniani alikuwa anasema imani yako imekuponya, imekuokoa. Nguvu zilikuwa  zinatoka ndani yake lakini alikuwa anasema imani ndio imevuta upako mahali ulipo.

Imani huja kwa kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo. Neno lile ambalo umepewa yaani ahadi na ukianza kuliweka katika matendo kama mtu yule aliyepokea ndipo unaona matokeo.

Hawa watu katika mistari tuliyosoma tunaona kuwa  jana yake waliimba na kumsifu Mungu sana. Lakini ule muda wa udhihirisho ulikuwa bado ambao Mungu aliwaambia maana alisema kesho.

Lakini imani yao ilikuwa imelala tena. Sasa kama Mungu anakuambia unasafiri kesho na unajaza gari yako mafuta tayari kwa ajili ya safari. Lakini kuna kitu ambacho kinatokea asubuhi unaona matairi ya gari yako hayana upepo na oil iko chini. Katika mazingira hayo Mungu akisema anza safari huwezi kuanza safari kwasababu imani uliyokuwa nayo jana ya safari leo hauna tena na huwezi chukua safari. Mpaka hapo utengeneze gari lako ndipo imani yako iweze kukaa sawa sawa.

Katika habari hii tunaona tena Yehoshafati akisema mwaminini Mungu na mtathibitika. Hii ni kwa sababu waliacha tena kumwamini Mungu. Pia alisema waaminini manabii wake nanyi mtafanikiwa. Lile neno la ahadi lilotoka pale lilikuwa la kwao lakini asubuhi walipoamka waliacha kumwamini Mungu na lile neno ambalo walipewa.

Mungu alikuwa anawasubiri na Yehoshafati alianza kuwashauri wenzie kuwa tusiharibu hapa Mungu alisema kesho na ndio imefika sasa.

Katika mazingira haya tuliyonayo basi tuanze tena kuamsha ile imani tuliyokuwa nayo jana.

Ukisoma unaona jana yake walimsifu Mungu na wakalala. Lakini asubuhi imani ilipata shida. Lakini walipoanza kuimba tena waliimba kutoka moyoni na imani yao ikajengeka kwa  upya maana ilikuwa imetoka moyoni mwao kabisa. Kwa hiyo waakachilia imani ndani yao ambapo walipoanza kuimba Mungu akaweza waviziao. Maana tunaona walipokuwa wanaendelea kuomba walishangaa kuona Watu wameuana wao kwa wao bila wao kurusha mkuki hata mmoja. Pia Biblia inasema walikaa pale siku tatu wakichukua nyara ambazo zilikuwa pale.

Kuna kushukuru kwa imani ambako kunaachilia nguvu za Mungu zidhihirishe ahadi ambayo umepewa lakini bado hujaiona katika maisha yako. Mungu anasubiri hatua yako ya kutoka moyoni ili umshukuru  ili aweze kuachilia nguvu zake.



JAMBO LA TANO
5.TATHIMINI MAOMBI YOTE AMBAYO UMEKUWA UKIYAOMBA TANGU MWAKA UANZE

Jitathimini wewe mwenyewe ndani yako kama Mungu alishakujibu. Wengine wanaandika mistari hiyo na wengine wanakumbuka kabisa kuwa Mungu alinisemesha mstari huu. Mungu alipokusemesha mistari hiyo kuna mambo mawili yalitokea. Kama Mungu alikusemesha na anataka moyo wako upokee maana yake unakuta mzigo wa kuomba ulikatika na ukaingia mzigo wa kumuabudu  na kumsifu Mungu. Kwa hiyo ukapata amani ipitayo fahamu zote  japo mazingira hayajabadilika lakini ndani yako una amani ambayo unashindwa hata kuieleza.

Japo unataka kuliombea hilo jambo lakini ndani yako kunaingia kushukuru. Ukifika mahali pa namna hiyo basi ujue kabisa kuwa Mungu kajibu katika ulimwengu wa roho. Kwa hiyo endelea kushukuru kwa imani na Mungu ataachilia udhihirisho ndani yako.

Ukiona ndani yako umeacha kuomba na umepoteza kumuabudu Mungu na kumsifu Mungu ulikokuwa nako na amani imeanza kupotea ndani yako. Sasa kama  lile jambo likija tena unashindwa kuomba na kumshukuru Mungu ndani yako basi ujue kuwa umezira na umeumia ndani yako. Rudi kwa Bwana akusaidie ili atengeneze tairi ambalo limepata pancha. Maana huwezi endelea na safari wakati upepo unatoka.


 
MFANO WA PILI
2. KUMSHUKURU MUNGU KWA ALIYOKUTENDEA MSIMU ULIOPITA KUNAKOMFANYA AKUSAIDIE KWENYE MSIMU MPYA
 

Neno la kusimamia ni kutoka katika kitabu kile cha Kutoka 18:8-12
 
Kwa kuangalia mfano huu wa pili nataka tuangalie mambo kadhaa pia ili uweze kuelewa na kupata kile Mungu alichokusudia.
 
JAMBO LA KWANZA
1. ULIMWENGU MZIMA (MATAIFA YOTE) UPO MWANZONI MWA MSIMU MPYA
 

Mataifa yote ulimwenguni tupo kwenye msimu mpya lakini mwanzoni. Na katika msimu mpya kuna mabadiliko makubwa sana ambayo yapo na yanakuja. Na kati ya eneo mojawapo ambalo litaguswa kwa ajili ya mabadiliko ni mifumo (systems).
 
Na ninachosikia kukueleza leo ni kwamba mojawapo ya Mifumo ambayo itabadilika ni pamoja na:-

1.Upimaji wa utendaji kazi.
 
2.Mifumo ya kimaamuzi inayodai mgawanyo wa kimaamuzi (nani aamue nini)
 
3.Mifumo ya ajira hasa kwenye vigezo vya kuajiri

 
Na haya mabadiliko pamoja na mengine mengi yatagusa mioyo ya watu, akili zao, miili yao, muda wao na mazingira wanayoishi wakubwa kwa wadogo, viongozi pamoja na wale wanaoogozwa Na kila Taifa litaguzwa kivyake kivyake.


 
JAMBO LA PILI
2. UMEINGIA MSIMU MPYA UKIWA NA HALI GANI UKILINGANISHA NA HALI ULIYOKUWA NAYO MSIMU ULIOPITA
 

Tumesoma yale mazungumzo katika kitabu cha Kutoka 18 kati ya Musa na Mkwewe kuhani mkuu wa Midiani, mzee Yethro.
 
Tuangalie kwanza Kutoka 19:1 pia linganisha na ile Kutoka 12:1-2 Katika Kutoka 19 Biblia inasema ni mwezi wa tatu.  Hapa Kutoka 12 unaona kuwa Mungu alisema mtaanza kuhesabu miezi upya maana yake ulikuwa ni msimu mpya kwao.
 
Sasa angalia Kutoka 12:41-42 Mungu aliwatangazia pia kuwa sasa wanaingia katika msimu mpya na mfumo  wa kalenda  zao nao unaenda kubadilika. Mungu alifuta ile miaka ya ile kalenda iliyokuwepo ambayo walikuwa wanaitumia.
 
Kutoka 19 unaona kuwa ilikuwa imepita miezi mitatu. Sasa wana wa Israel sijajua kama walijua maana yake nini hayo mabadiliko mpaka pale ambapo waliona wanaanza kujikusanya kwa ajili ya kuondoka. Walitamani sana kuona mazingira yao yanabadilika  wakiwa Misri maana  hawakua na mpango wa kwenda Kanaani.
 
Katika ile sura ya 15 ghafla walianza kuona mabadiliko makubwa sana. Kitu cha kwanza walikutana na kukosa maji maana walisafiri siku 3 bila maji kwa hiyo walikuwa na kiu. Lakini walipokuta maji yalikuwa machungu.  Katika hali hiyo walianza kumnung'unikia Musa na Mungu.
 
Katika sura ya 17 walifika Refudimu. Napo hapo hawakukuta maji, wakapata msaada na wakapata maji. Katika hali hiyo napo waliendelea kulalamika na kunung'unika. Baada ya hapo walikutana na Waamaleki wakapigania vita na wakashinda.
 
Katika sura ya 18 tunaona mzee Yethro akienda kumsalimia Musa na akiwapeleka binti yake na wanawe wawili. Musa alimsimulia Baba mkwe wake matendo makuu ambayo Mungu aliyafanya kwa Farao na namna ambavyo aliwatoa Misri. Pia alimwambia namna ambavyo Mungu aliwasaidia katika safari walipokuwa njiani.
 
Mzee Yethro alisema na ahimidiwe Bwana Mungu wa Israel. Mungu alimsukuma kusindikiza Shukrani zake na sadaka. Ilikuwa ni busara sana wamshukuru Mungu kwa sababu  ya alichowafanyia jana, mioyo yao ingefunguka na kujua kama aliwasaidia na pale, angewasaidia na hapo pia. Lakini kwa sababu ndani yao walikuwa wanalinganisha na hali ya sasa kiasi ambacho wanaona kama vile hakukuwa na sababu ya kuja pale.

Angalia ndani ya moyo wako je unamuona nani zaidi? Unaona mazingira unayopitia au unamuona Mungu alie pamoja nawe katika hayo mazingira? Kipi unakisikia zaidi kati ya sauti inayotoka kwenye hayo mazingira magumu au unasikia sauti ya neno ulilopewa kupita nalo kwenye hayo mazingira magumu, kipi kina sauti ndani yako kwa sababu ndicho kitakachoamua hatua zako mbele yako.


 
JAMBO LA TATU
3. MUNGU ALITUMIA MAZINGIRA YA MWANZO YA MSIMU MPYA KUJIJULISHA ZAIDI KWA WANA WA ISRAELI

 
Mungu alijitambulisha kwa Musa kama Mungu wa baba zake, Wa Ibrahim, Isaka na Yakobo, Musa akauliza atakapoenda kule na wakamuuliza ametumwa na nani asemeje, Mungu akamwambia yeye ni Mungu Niko ambae niko.
 
Kwa hiyo Musa alikuwa sahihi kabisa kumuuliza Mungu yeye anaitwa nani?. Na tangu wakati ule Mungu alikuwa anatumia mazingira yote na kupita jangwani kujijulisha kwao yeye ni nani waendelee kumjua zaidi kabla hawajafika Kanaani,  kwa sababu Mbele yako kuna mafanikio lakini usipomjua Mungu katika shida hautamjua kwenye mafanikio.
 
Walipovuka tu bahari ya Shamu, walipoanza tu kutembea hakukuwa na maji na waliyoyapata yalikuwa machungu, lakini Mungu akajifunua kwao kama Mungu mponyaji akayatibu yale maji, yaani Jehova Raphar, wao walikuwa wanafurahia muujiza wa maji lakini Mungu alifurahia kwa sababu amepata fursa ya kujitambulisha kwao lakini hawakumtambua walitambua maji kama vile watu wengi wanafurahia muujiza hawataki kumtambua Mungu aliyewaletea muujiza.
 
Kwenye msimu mpya watu wanajawa na kiu ya kutoka kwenye shida bila kujali nani anawatoa kwenye shida,  wana wa Israeli kwenye sura ya 15 walikuwa na shida na maji bila kujali nani anawaletea maji, na Mungu alitaka kutumia hiyo shida ili wajue yupo Mungu ni Mungu mponyaji, ili watakapokuwa wanaenda huko watakapopata shida yoyote wajue yupo Mungu Jehovah Rapha katikati yao, imani isitindike, lakini wao walifurahia maji. Ndio maana walipopata tena hiyo shida ya maji kwenye sura ya 17 walilalamika kwa sababu wameshasahau.
 
Kwenye sura ya 16 katika mazingira ya kukosa chakula Mungu alijifunua kwao kama Adonai yaani Mungu Mkuu,  alijifunua kama Elohim, Yehova-yire (God is my provider) ili wapate kujua kuwa yule Mungu aliyemsaidia Ibrahimu kwa ajili ya kupata sadaka, Mungu alimpatia kondoo, ndiye atakayewapatia chakula.
 
Sasa kwa sababu walichelewa kumjua Mungu, walichelewa kufika Kanaani na kuna wengine hawakufika kabisa. Hii si kwa sababu Mungu aliacha kufanya miujiza, ni kwamba hawakudaka kile Mungu alikuwa anawafundisha mwanzoni.
 
Mazingira magumu ni fursa kwa Mungu kujijulisha kuwa Yeye ni nani. Hata kama hayo mazingira ni magumu kiasi gani, Mungu hujijulisha hapo. Kwenye mazingira unayopitia usijaribu kumtafuta shetani au mtu kwa sababu utamwona kwa haraka, bali umtafute Mungu. 


 
JAMBO LA NNE
4. SHUKRANI YA YETHRO ILIYOAMBATANA NA SADAKA ILIFUNGULIA HEKIMA YA MUNGU KWA AJILI YA MSIMU UJAO
 

Ukisoma kuanzia Kutoka 18:13 utaona baada ya sadaka kutolewa, asubuhi iliyofuatia Musa aliendelea kutoa huduma (atoe hukumu, ajibu maswali ya watu, asome sheria, n.k kwa watu wanaomzunguka) akiwa peke yake na ilikaa foleni ndefu.
 
Mzee Yethro akapita pale akamwuliza Musa, unafanya nini hapa, na Musa akamweleza anachokifanya. Na majibu ya Mzee Yethro yapo kwenye Kutoka 18:17
 
Kitu kilichotokea ni kwamba mabadiliko yaliingia kwenye mfumo wa kutathmini kazi. Jambo hilo hilo Musa alipolifanya huko nyuma lilikuwa bora, zuri na watu walikuwa wanalifuata ila muda hakujua kuwa msimu mpya umeanza na umekuja na mabadiliko. Mabadiliko yaliyokuja ni namna ya kutathmini mabadiliko ya utendaji wa kazi.
 
Kutoka 18:21-22 Ukisoma hapa utaona kuwa kuna  ajira mpya ambazo zitakuja maana msimu mpya unadai mgawanyo wa majukumu kimaamuzi. Kilichosukuma huo mgao ni kupunguza uwezo wa Musa kuamua kila kitu  na likapelekwa kwa wengine katika makundi tofauti tofauti na yakapewa uwezo wa kuamua. Lakini walibakiza mambo machache ambayo yataamuliwa na Musa.
 
Katika msimu mpya pia kutawepo na msisitizo wa vigezo vya namna ya kuwapata watu ambao watakuwa katika hizo nafasi ambavyo hukuvizoea kuviona.

Kutatokea kupanuka kwa huduma na kazi na ndio maana Mungu anakuinulia watu mapema ambao watakusaidia maana mbele yako kunapanuka.
 
Mungu aliwaambia wana wa Israel kuwa  huu ni msimu mpya kwa hiyo wanatakiwa waondoke kule Misri. Japo wangeweza kufunga na kuomba kuwa Mungu tunaomba tubadilishie mazingira ya hapa, wangeweza kukaa pale na wasione baraka za Mungu maana  Mungu anataka waende mahali pengine.
 
Kwa hiyo katika msimu mpya unahitaji kutega sikio kitu ambacho Mungu anakuambia. Kuna watu watadhoofika akili  kwa sababu watakuwa wanafurahia sana kitu ambacho mtumishi anafanya kuliko kujiendeleza kielimu au kusoma. Haijalishi kuwa ni wahubiri wazuri kiasi gani lakini hawapati wao  muda wa kusoma Biblia na wa kutafuta nguvu za Mungu ili awajaze tena kwa sababu nguvu zimepungua. Lakini watakuwa wako busy sana kwenye huduma kiasi ambacho hawatajua ni wakati gani nguvu za Mungu zimeisha ndani, au neno la Mungu walilokuwa nalo limetumika tayari na hawajaona kitu kipya ambacho Mungu anataka waone.
 
Kuna watu wanajivunia kufanya kazi bila kupumzika na hiyo sio kwamba uko kiroho. Kupumzika ni kiroho maana maandiko yanatuambia kuwa Yesu aliwaita wanafunzi wake pembeni ili waweze kupumzika kidogo maana hata chakula walikuwa hawajala. Maana walipoenda mahali pengine walikuta makutano wanawasubiri.
 
Mstari wa 23 Kutoka 18 anasema Kwamba utafanya jambo hili, na Mungu akikuagiza hivyo, basi utaweza kusimama wewe, na watu hawa wote nao watakwenda mahali pao kwa amani. Maana yake kutatokea kukosa amani kwa sababu ya uzito wa ile kazi kiasi cha kuona hajui tena kitu cha kufanya. Hii ni  kwa sababu hajui kilichotokea katika msimu mpya au Mungu kamsemesha kitu cha kufanya na yeye hayupo tayari kwenda mbele za Mungu kutafuta msaada. Lakini hataweza kusimama na kuendelea na hilo jukumu wenyewe.
 
Kuna watu ambao wataacha huduma au kazi wenyewe maana mzigo utakuwa mzito na ndani yao watakuwa hawana amani, maana Biblia inasema amani ya Kristo na iamue ndani yenu. Itafuteni amani na muifuate. Mtatoka kwa furaha na mtaongozwa kwa amani. Amani ipitayo fahamu zote itakusaidia. Kukosa amani ni ishara ya kwamba huendi sawa sawa na Mungu anavyotaka.
 
Kukosa amani kukizidi nyumbani kwako kutaambukiza mtaani. Hii ni Dunia jaribu kutafuta watu ambao wamekosa amani nyumbani, ofisini utawakuta wako mtaani. Kwa hiyo lazima liwepo neno la Bwana maana Yesu ni Mfalme wa amani ambalo litawasaidia watu katika mazingira ya kukosa amani na Yesu ataleta amani, furaha na tumaini ndani yako.
 
Kwa sababu tunaona tofauti hulazimiki kuona jangwa ukiwa jangwani. Unaweza ukaona Kaanani ukiwa jangwani maana Jangwani ni mahali pa kuangalia Kaanani. Musa alionyeshwa Kaanani akiwa mwishoni mwa jangwani katika mlima Nebo.
 
Kuna kitu Mungu kapanga kwa ajili yako kizuri lakini  kitaamuliwa hapo unapitaje mwanzoni mwa msimu mpya. Je moyo uko tayari kushukuru?. Kama huwezi kushukuru hapo mahali ulipo basi shukuru kwa kile ambacho kilifanyika jana na juzi. Kama leo umekosa maji lakini juzi Mungu alikupa maji. Jifunze kushukuru kwa hilo na mshukuru Mungu kwa ajili ya msimu uliopita.
 

MFANO WA PILI
2. KUMSHUKURU MUNGU KWA ALIYOKUTENDEA MSIMU ULIOPITA KUNAKOMFANYA AKUSAIDIE KWENYE MSIMU MPYA


Tulisoma Kitabu cha Kutoka 18:8-12  Kutoka 18 imeanza kuelezea habari za Mzee Yethro baba mkwe wa Musa ambaye ni Kuhani wa wa Midian. Alipokuwa anarudi nyumbani kwa Musa baada ya kukaa nao mbali kidogo.

Baada ya hapo unaona yule mzee akisindikiza shukrani yake kwa kutoa sadaka.

Pia tulitazama jambo la nne

JAMBO LA NNE
4. SHUKRANI YA YETHRO ILIYOAMBATANA NA SADAKA ILIFUNGULIA HEKIMA YA MUNGU KWA AJILI YA MSIMU UJAO


Ile hekima ambayo Mungu alimpa Yethro iligawanyika kwenye vipengele kadhaa.

Ukirudi sasa katika ile habari ya kutoka 18 unaona asubuhi yake Musa aliwapanga watu foleni kama kawaida yake. Maana huoni akipiga mbiu ya kuwa  watu waanze kwenda.  Lakini tunaona tu asubuhi yake watu wakijipanga foleni.

Biblia inatuambia kubwa Mzee Yethro alimwambia Musa kwa kufanya vile atadhoofika, atashindwa kusimama, atakosa amani, hatakuwa na nafasi ya kutosha.

Kwa hiyo akipata watu wa kumsaidia wataenda  ule mzigo ambao msimu uliopita ulikuwa mwepesi  kwake ghafla msimu mpya umekuwa mzito. Na Mungu ameweka kwa maksudi kabisa ili kupata nafasi ya watu wengine kuja.

Kwa lugha nyingine hili jambo lilikuwa linalazimisha kupanua wigo wa imani ya Musa iongezeke.

KUNA MAENEO MATATU AMBAYO IMANI YA MUSA  ILITAKIWA IONGEZEKE

Eneo la kwanza 

  • .Kumwamini Mungu anaweza kumpa watu sahihi.


Eneo la pili  

  • Kuweza  kuwaamini watu wengine kuwa wanaweza kutumiwa na Mungu kama wewe.


Hiyo ni changamoto ngumu sana kwa watu wengi. lazima ujue namna ya kwenda mbele za Mungu kwa maombi ili aweze kukupa watu.

Luka 6:12
Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu
.

Tunaona Yesu alikesha usiku kucha akiomba Mungu apate wanafunzi. Na baada ya kutoka mlimani Yesu aliwaita wanafunzi wake wengi na akachagua kumi na mbili ambao aliwaita mitume.

Kwa hiyo pia ni lazima ujifunze kuwaamini watu wengine kuwa Mungu anaweza  kuwatumia. Kama vile Musa alivyoambiwa achague watu wa kumsaidia maana Mungu anaweza kuwatumia na wao.



JAMBO LA TANO
5. ANAYEMSHUKURU MUNGU KWA AJILI YA ALICHOFANYA KWA MSIMU ULIOPITA, NDIYE ANAYEPEWA HEKIMA YA KUKABILIANA NA KUFANIKIWA KATIKA MSIMU MPYA

Swali linakuja:
Kama Mungu alijua Musa anahitaji hekima hiyo kwa nini alimpa Yethro? Wakati Musa ndio kaitwa na amepewa upako wa kazi hiyo.

Sasa kwa nini Mungu hakumwambia Musa hilo jambo moja kwa moja?

Yethro alipewa kwa sababu NDIYE ALIYEONA UMUHIMU WA KUMSHUKURU MUNGU KWA IMANI KWA AJILI YA KITU KILICHOFANYIKA MSIMU ULIOPITA.

SWALI: Kwanini Yethro alisukumwa kuambatanisha ile shukrani na sadaka?,

JIBU, Kilichomsukuma Yethro kuunganisha shukrani yake na sadaka ni ile imani iliyokuwa ndani yake

Biblia inasema Imani ni kuwa na hakika ya mambo uyatarajiayo na imani isipokuwa na matendo imekufa, Imani ndio inayokusukuma kuchukua hatua.

VITU VILIVYO TENGENEZA IMANI NDANI YA YETHRO AU VILINIFANYA NIONE IMANI NDANI YA YETHRO AMBAVYO WATU WENGI HUWA HAWANA WANAPOTOA SADAKA.

1. YETHRO ALIMPA MUNGU WA MUSA NAFASI YA KWANZA MOYONI MWAKE KULIKO MIUNGU MINGINE

Kutoka. 18:11
"Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa unyeti.".


Anasema,  "Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa unyeti." Huyu mzee aliichukua nafasi ya mungu wake ndani ya moyo wake akampa Mungu wa Musa.

Kujua maana yake kuwa na uhakika, uhakika maana yake kuwa na imani.

Na kwa imani twafahamu.

Ukisoma Zaburi 50:23 Atoaye dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.. Maana yake anayetoa sadaka za Shukrani kwa Mungu ndiye anayefanya Mungu ajulikane.

Kwa hiyo kule kutoa kwake sadaka ina maana kuna imani ambayo ilitumika ndani yake.



JAMBO LA PILI.
2.MUDA WA KWENDA KUTAFUTA SADAKA YA KUILETA ILIYO SAHIHI.

Hili utalijua kuwa kati ya mstari wa 11 na 12 Biblia ilinyamaza.

 Kutoka. 18:11-12
Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa unyeti.Yethro mkwewe Musa akamletea Mungu sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; na Haruni akaja, na wazee wote wa Israeli, wale chakula pamoja na mkwewe Musa mbele za Mungu

Swali  linakuja, hii sadaka mzee Yethro alimletea Bwana kutoka wapi? Maana alikuwa amekuja kwa mkwe wake  kumsalimia na alisimuliwa ule ushuhuda akiwa pale kwa Musa. Kwa hiyo hakujiandaa kuwa na sadaka muda ule.

Aliposikia ule ushuhuda, ulitengeneza imani ndani yake. Baada ya pale alitoa shukrani ya maneno ambayo ilianza kumsukuma kupeleka sadaka.

MFANO:
Fikiria Mkristo ambaye anasali kanisani na huwa anatoa sadaka zake vizuri tu. Ghafla anaugua au anataka kupata cheo. Sasa anaamua kuchanganya mambo yaani aende kwa Mchungaji au anataka kwenda kwa mganga. Na anaenda kwa mganga usiku na wanamwambia aina ya sadaka ambayo wanataka kwa mfano Beberu mwenyewe kidevu mweupe. Mtu huyo atazunguka katika minada kutafuta huyo beberu na akipata anampeleka kwa  mganga.

Akimpata  anampeleka kwa mganga huenda naye yuko mbali kwa hiyo anasafiri masaa manne au matano. Na watamchinja ili apate kukabiliwa lakini wakati kanisani kachukua tu noti moja tu na anatumia dakika tano au kumi kufika hapo. Alafu atagemee kupata majibu kwa Mungu? Hapana kule alikotoa sadaka ya beberu ndipo katoa kwa imani na ndipo atakapoona udhihirisho wa nguvu za mapepo kumsaidia.


Musa hakujua  kama ni msimu mpya kwake.Baada ya kuvuka bahari ya shamu watu wake walikuwa wanamng'unikia tu juu yake na mpaka aliweza kupoteza kibali kwa watu kabisa.

Hata Ndugu zake yaani Haruni na Miriam waliuliza kama  alisikia vizuri katika habari za kuoa kwake. Kwani mwanzo alipooa hawakuona mpaka walipovuka bahari ya shamu ndipo wanaanza kupata walakini katika kuoa kwake?.


MFANO WA TATU.
3.KUMSHUKURU MUNGU KWA VICHACHE ALIVYOKUPA INGAWA HAJAKUPA KWA KIWANGO ULICHOOMBA AU ULICHOTARAJIA

Soma Luka 17:11-19
Katika mfano huu wa tatu nataka tutazame mambo matatu katika eneo la kumshukuru Mungu kwa vichache ambavyo amekupa..

JAMBO LA KWANZA
1. SI KILA WAKATI MUNGU ATAKUPA CHOTE ULICHOMUOMBA KWA WAKATI MMOJA ULE ULE.

Inawezekana kabisa saa ambayo Mungu anakutembelea akakuponya kwa asilimia 10% na 90% zikabaki. Na wakati mwingine uponyaji ukaongezeka na kufika asilimia 50%. Lakini wewe ulitaka upate yote 100% wakati huo huo. Hivyo ndivyo mtu yeyote anayeomba anataka apewe majibu yake.

Kuna kipofu Yesu alimgusa mara moja akaona miti kama inatembea na akamgusa tena mara ya pili na akaona wazi wazi. Lakini kuna Kipofu mwingine Yesu alimgusa mara moja tu na akapata kuona.

Kwa hiyo ni rahisi sana Yesu akatatua shida ya mtu kwa mara ya kwanza, mtu mmoja  akipewa 50% na mwingine akapata 100% siku ile ile. Huyu aliyepata 50% ni rahisi kuuliza hali ya kiroho ya Yesu kuwa siku ile ilikuwaje yeye aombe na ampe 50% wakati mwingine alipewa zote 100%.

Je umewahi kufikiria ukiomba Mungu laki 1 lakini akakupa 10,000. Alafu mwingine anasimama kushuhudia kuwa  nilimuomba Mungu Laki moja na akanipa laki mbili. Sasa utajaribu kufikiria kuwa  je  ni Mungu yule yule ambaye mimi nilimuomba au?.

Kwa mfano fikiria mtu anaomba  kwa Mungu apate kazi ambayo atakuwa anapata mshahara mkubwa. Lakini anapata kazi ambayo inamlipa  mshahara mdogo. Ndani yake anaendelea na mawindo ya kazi nyingine.

Katika mazingira hayo  ni watu wachache sana ambao watakuwa na hali ya kumshukuru Mungu kwa hicho kidogo walichonacho. Lakini wengine wataendelea kuomba ili wapate kazi nyingine na kusema Mungu umesema tuombe bila kuchoka. Na wachache sana ambao watakuwa na moyo wa kushukuru kwa hicho kidogo waliochopata.

Kuna watoto wengine ambao tunawalea wanaweza wasijue umuhimu wa kumshukuru Mungu kwa hali ambazo wanazo na neema ya Mungu ambayo ametupa.

Usipowafundisha wanaweza wakashindwa kumshukuru Mungu hata kwa ngazi ambayo wamekutana nayo ya maisha wanapokuja Duniani.

USHUHUDA.
Wakati fulani tulipita katika mkoa mmoja hapa nchini na wakati huo mjukuu wetu alikuwa ni mdogo. Aliona wanafunzi wakienda shule asubuhi wakiwa wamevaa kandambili (Ndala).

Akachungulia nje ya kioo cha gari akawaona akatuuliza. Ivi wale watoto hawana baba zao? Tukamuuliza kwa ajili ya nini akasema wanaendaje shule kwa mguu. Yeye alikuwa anapelekwa shule na gari. Kwa hiyo haelewi  kuwa kuna wengine wanaenda shule kwa miguu.

Wakati tunafikiria tunamjibuje akatuuliza swali lingine akasema kwanini hawana viatu. Wanaendaje shule wakiwa wamevaa Ndala za kwendea bafuni. Yeye alikuwa haelewi kwanini wale watoto wanaenda shule wakiwa wamevaa Ndala. Maana mazoea kuona Ndala tunaendea bafuni  ila wengine wanaenda shule.

Ilibidi tuseme nae katika ule.umri mdogo aweze kuelewa neema ya Mungu ili ajue namna ya kumshukuru Mungu. Wakati mwingine tunakuwa na mafundisho ndani ya kanisa kubwa ukiisha okoka unatakiwa utoke hapa chini na uende hapa juu.


Mungu hakutuumba ili tupande lift, tukipanda lifti hatutengenezi msuli! Lazima tupande ngazi. Tunatoka imani kwenda imani, utukufu kwenda utukufu, nguvu juu ya nguvu, neno juu ya neno, amri juu ya amri, kanuni juu ya kanuni ili njiani tuwe tunatengeneza msuli.

Saa Mungu amekusogeza hatua utamshukuru kwa hiyo hatua moja.

Biblia inasema hatua za mwenye haki zinaongozwa na Bwana inamaanisha anategemea ukanyage hatua.

Wakolosai 3:15
Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukran
i.


Ukiona amani ya kristo ipitayo akili zote, amani ya Mungu iko ndani ya moyo wako basi jua kubwa Mungu anategemea uwe na moyo wa shukurani. Inawezekana huna chakula cha kutosha lakini kama una amani moyoni mwako wewe ni mtu ambaye unatakiwa kwenda mbele za Mungu kwa shukrani. Haijalishi chakula ni kidogo kiasi gani kuna wengine wanalala hawajala.

Mara kwa mara tunapokuwa mezani na watoto wangu wakija kutusalimia maana sasa kila mtu anaishi kwake. Mara nyingi tunajaribu kuzungumza nao maisha tuliyoishi huko nyuma ili wasije wakafikiri tuliteremka kama uyoga.

Siku moja tulikuwa tunakula mikate mezani tunaweka na siagi juu halafu ikaja picha tulipokuwa wadogo kwa sababu tulikuwa tunapenda mikate mno na saa nyingine baba au mama alikuwa anakosa hela ya mkate. Kwa hiyo kama wazazi walikuwa wanafikiria watoto wake wakikosa mkate itakuwaje?. Kwa hiyo mama alikuwa akata ugali wa jana kwa slices , halafu zinapangwa kama mikate sasa tulikuwa tunapaka blueband juu yake. Na tunakula kama mkate kabisa ila ni ugali.

Haijalishi maisha uliyonayo kama unakula kiasi kidogo sana ila jua kuwa kuna watu wanalala bila kupata chakula. Ukiona Mungu amekusudia umepata chakula kidogo na bado una amani, hulalamiki Biblia inasema uwe mtu wa shukurani.

Kama huna pesa za kutosha lakini unayo amani una kitu kikubwa kwa sababu kuna watu hawana pesa na hawana amani inakuwa ngumu sana kwa sababu maamuzi yao hayatakuwa sahihi kwa kuwa Biblia inasema amani ya kristo iamue mioyoni mwenu. Ukikosa pesa na ukakosa amani utakosa utulivu na unaweza kufanya kitu chochote kile kwa sababu umekosa amani.

Mungu alikusaidia ukafika mahali huna pesa za kutosha lakini ukafika mahali Mungu anakupa amani yake ujue katikati ya kukosa pesa Bwana yuko pamoja na wewe. Huwezi kufanya maamuzi ambayo hajakaa sawa. Kama biashara yako haiko sawa. Kama huna pesa ya kutosha na una amani moyoni, umshukuru Bwana hicho ndio kitu kikubwa.

Kuna watu hawana pesa, hawana amani; wana hali ngumu sana kwa sababu maamuzi yao hayatakuwa sahihi.

USHUHUDA
Nikiwa mkoa mmoja tulikuwa tunajiandaa kwa ajili ya semina, nikapata nafasi ya kuongea na baadhi ya watu pale mjini wakiwemo wafanyabiashara ili wapate kuokoka kwa sababu wengi walikuwa hawajaokoka.

Roho Mtakatifu akaniambia nisihubiri hicho, nikamwuliza nihubiri nini akaniambia kichwa somo "UMUHIMU WA KUNIPOKEA KWENYE BIASHARA ZAO". Nikamwuliza hiyo imeandikwa wapi, akanieleza jinsi alivyoingia kwenye boti ya Petro. Akasema waambie wamkaribishe kwenye boti zao na sio kwenye mioyo yao halafu atawapatia samaki na wakishapata samaki watamjua yeye ni nani.

Nikafurahi kwa kupata mahubiri mazuri kabisa na nikachapa injili hiyo na mwishoni nikauliza wanaohitaji kumkaribisha Yesu kwenye biashara zao wakatoka wengi na nikawaongoza sala ya toba. Na nikawaalika kuja kwenye semina tuliyoenda kuifanya pale halafu nikaondoka.

Baada ya siku mbili tatu za semina hiyo, wakaja baadhi yao na nilipoita watu kuokoka nikaona na wao wanatoka. Baadaye mmoja aliniomba kuonana naye kuwa kuna kitu anataka kuniambia.

Huyo mtu akasema hanifahamu na hajawahi kuja kwenye semina zetu. Lakini kilichomsukuma kuja ni  kile kitu alichosikia kutoka kwangu. Aliniambia kuwa kesho yake asubuhi alikuwa amejipanga kwenda kwa mganga. Nikamwuliza kwa shida gani, akasema ana wiki ya pili hajauza kitu watu wanafika dukani kwake na wanaondoka bila kununua.

Nikamwuliza kama yeye ni Mkristo akanijibu ndiyo. Nikamwuliza sasa ni kitu gani kinamfanya aende kwa mganga akajibu kuwa kuna watu walimshauri kuwa ili afanikiwe kwenye biashara lazima aende kwa mganga wa kienyeji.

Nikamwuliza sasa nini kimetokea? Akasema baada ya kufanya ile sala ya kumkaribisha Yesu kwenye boti (dukani) sasa kesho yake asubuhi akaona watu wanaingia na kununua bidhaa.

Pia alikuwa haongei na mke wake sasa watu walipoanza kununua ikawafanya waanze kuongea na wakaanza kujiuliza kulikoni?

Ukiona unapita kwenye hali ya namna hiyo huku una amani moyoni mwako, unatakiwa uwe na moyo wa shukrani kwa sababu si kila mtu anayepitia hali kama hiyo anakuwa na amani moyoni mwake.

Ndoa yako inaweza isiwe na amani lakini hakikisha moyo wako uwe na amani. Kuna wengine ndoa zikikosa amani na wao wanakosa amani halafu wanafanya vitu ambayo havijakaa sawa.

Ukienda mbele za Mungu na ukamkabidhi hilo jambo na akakupa amani ipitayo fahamu zote, Biblia inasema umshukuru Mungu.

Inawezekana una vita kubwa na Mungu hakupi ushindi wa vita hivyo ndani ya muda huo na akakupa ushindi kwa sehemu ndogo tu na ukawa na uhakika kuwa amekupa ushindi, halafu vita vingine vikiinuka Mungu anakufungulia ushindi.

Mungu akikushindia vita kwenye sehemu ya kwanza umshukuru kwa kusema “Wewe ni Mungu ambaye umenisaidia kwenye vita hii na uko pamoja nami, haijalishi vita nyingine itaibuka huko mbele kwa sababu najua wewe ni Jehova - nisi UTANIPIGANIA TENA.”

 

JAMBO LA PILI
2. UNAPOPATA KITU KIDOGO KUTOKA KWA MUNGU KULIKO ULICHOOMBA MOYO WAKO UNAKUWA NA HALI GANI

Luka 17:16 - 17
“akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria. Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi?”

Ikimaanisha ndani ya wale 10 kuna Wayahudi .Nilimuuliza Yesu kuhusu hili swali kuwa alijuaje kuwa wametakaswa 10? Kwa sababu maandiko yanasema walipokuwa wanampigia kelele wakiwa wamesimama mbali na wala wasingemwona kwa ukaribu kutokana na sheria ya wakati ule. Kila wakiwaona watu lazima wawatamkie mapema kuwa wao wana ukoma, ni najisi kwa hiyo watu wanakaa nao mbali.

Sasa ile Yesu kusema “hawakutakaswa 10?” Sasa unaweza ukamuuliza kama aliwaona wapi kwa sababu walikuwa mbali. Pia walipokuwa wakienda walitakasika ikimaanisha walitakasika baada ya kuondoka mbele ya Yesu. Walitoka na ukoma sasa alijuaje kama wametakasika wote 10? Na pale hakukuwa na mtu wa kujibu swali hilo. Sasa kwa nini aliuliza?

Uwe na uhakika alikuwa haulizi swali ambalo mimi nilifikiri kuna swali hapo. Jibu: Alichokuwa anauliza hali za mioyo yao kwa sababu walipotakaswa ndani ya mioyo yao walitakiwa kuwa na moyo wa shukrani. Haijalishi ile mioyo ilikuwa inaenda kwa makuhani kwa shukrani (kwenda kupata certificate of clearance) kwamba wanaruhusiwa kuingia na kukaa na jamii lakini hawakuwa na moyo wa shukrani.

Unapoenda kumshukuru Mungu si kitu kidogo ingawa anaweza kukufanyia kidogo lakini yeye anaangalia hali ya moyo wako ikoje pale anapokupa kitu; una shukrani kwa kiwango kipi.

Hesabu 11:4-6
"Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule? Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu; lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu."


Unaelewa maana yake nini mbele za Mungu? Ukisoma ule mstari wa 10 unasema hivi "Basi Musa akawasikia watu wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema yake; na hasira za BWANA zikawaka sana; Musa naye akakasirika."

Mungu alikasirika sana akawapa pigo, aliwakasirikia kwa sababu Ile sura ya 16 ni msimu mpya uliingia na Mungu alikuwa anazungumza nao walipokuwa wamekumbuka masufuria ya Misri. Mungu akawaletea MANA na kware wale. Mungu alisema anawalatea Mana ili awajaribu kama watatii sheria yake au la, na hapo ndipo alipoanza kuwatengenezae nidhamu ya kuiheshimu siku ya sabato.

Walianza kulalamika kuwa Mana inawakausha kiroho chao na Mungu alikasirika, kwa sababu Mungu alikuwa anatumia ile mana kufanya kitu kingine bora zaidi na hawakukiona.

Kama Mungu anaweza kumsaidia mtu 100% wewe akakusaidia 20% usikasirike, inawezekana yule kuna kitu hataona kama utakachoona wewe, hatajua kumvumilia na kutembea na Bwana, kushikwa mkono hatua kwa hatua yeye anaweza asijue hicho kitu. Wewe unakuwa na ushuhuda wa kutembea na Mungu hatua kwa hatua.

Wana wa Israeli waliwezaje kuona duni kitu alichowapa Mungu,  kwa sababu kama unakiona duni basi na Mungu unamuona duni na yeye. Haijalishi ni kitu kidogo kiasi gani kama umepewa na Mungu inamaanisha na Mungu yupo ndani yake, ukikidharau umemdharau Mungu pia, na kwa sababu Mungu amekupa Mshukuru yeye.



JAMBO LA TATU
3. YESU ALIKUWA NA KITU GANI CHA ZAIDI ATAKE WARUDI KUSHUKURU KWA MZIGO NAMNA ILE

Ukisoma ile Luka 17:18 na wa 19 inasema
"Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu? Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa." ukisoma msitari wa 17 kuna anauliza kwa mzigo sana anasema "je hawakutakaswa wote 10,  je 9 wameenda wapi?"

Ukiangalia ule msitari wa 19 unatupa kitu kingine, inasema "Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.". Nilipokuwa nasoma haya maneno "imani yako imekuokoa" nikaenda kuyatafuta kwenye miujiza mingine ya Yesu nikakuta yamejrudiarudia nikajua hazungumzii wokovu tulio nao sasa kwa sababu usingeweza kutokea bila msalaba.

Nikaanza kutafuta kwenye Biblia za kiingereza, niliipenda sana Tafsiri ya Amplified Bible wao yale maneno "Imani yako imekuokoa" wameandika wanasema "Your Faith has restored you to health" maana yake Imani yako imekurudishia tena afya yako.


Biblia inasema alirudishiwa   maana yake kuna kitu kiliondolewa katika katika maisha yake na ule ugonjwa lakini sasa kimerudi tena. Kwa hiyo waliokuwa wakienda ule ukoma uliisha lakini walibaki hawana vidole. Lakini yule mmoja aliporudi kushukuru Yesu aliona imani yake imeongezeka ndani ya yule mtu.

Hii ni sababu ambayo Daudi anasema anatafakari shuhuda za Bwana kitandani kwake. Ili akiamka asubuhi awe na kitu ndani yake. Shuhuda ni neno lililowekwa kwenye matendo. Na kwasababu hiyo lina kazi ya kukuwekea imani ndani yako

Kwa hiyo ile imani iliyotoka ndani yako kuna kitu cha zaidi imekuongezea na kukurudishia vile vitu ulivyopoteza. Kwa hiyo vikatokea tena  vidole ambavyo vilipotea.

Pia akamwambia unarudishiwa afya yako. Maana yake wale walipona  tu lakini huyu alirudishiwa na afya yake. Kuna tofauti kati ya uponyaji na afya. Uponyaji Mungu anashughulika na ugonjwa tu lakini afya Mungu anashughulika na mfumo wako wa kuishi.
 
Afya ni mfumo wa maisha. Yaani Yesu alimfanya yule aliyeugua ukoma asirudi tena kwenye maisha yaliyomfanya augue ukoma. Wale wengine wakifurahia uponyaji lakini wataenda kuishi maisha yale yale ambayo yaliwaletea ugonjwa. Kwa hiyo yanaweza wakatae tena ugonjwa.

Lakini yule alirudishiwa mfumo wa kuishi ambao unatunza afya yake. Yote haya aliyapata alipoenda kushukuru kwa ajili ya uponyaji kidogo aliopata akapata cha zaidi ambacho hakutegemea.

Fikiria kesho yake wanakutana na wale ambao walikuwa wakoma.Maana waliachana bila kuagana. Alafu wale 9 wanamtazama  mwenzao sura yake iko tofauti maana sasa ana afya.Ukiwa na afya  unakuwa tofauti hata sura yako inaonesha.

Sasa baada ya kukutana wote pamoja na yule mwenzao aliyeenda kumshukuru Yesu. Wanaona mwenzao ana afya nzuri na ana vidole vyake tena. Lakini wao hawana vidole, wanaweza wakakimbia, ila baada ya kupata ujasiri wanaweza kuuliza mwenzao kuwa sasa wewe hivi vidole umepata wapi?.

Yule mtu aliyeshukuru atasema nilirudi tena kwa Yesu na nilianguka miguuni pake kumshukuru. Akaniambia enenda zako amani yako imani imekuokoa. Basi nikaona vidole vyangu vimerudi. Wale wengine watasema  mbona tulikuwa tunapiga kelele wote pale kusema wewe mwana wa Daudi uturehemu. Yaani wewe katika kushukuru tu ndio umepata hivi?

Walisahau kuwa baada ya kumwomba Yesu pale aliwajibu kwa asilimia 50%. 50% ya ule uponyaji wao ulibaki kwenye shukrani.

Ghafla wale 9 waliobaki ndipo wanaona umuhimu wa kushukuru.  Sijajua kama wale watu walikuwa na uhuru kama tulionao sasa wa kama unataka kwenda kwa Mungu unaenda katika roho na kweli. Sio kama wakati ule ulikuwa lazima uende Yerusalemu au katika mlima ule. Maana unaweza ukamshukuru Mungu mahali popote ulipo na ukapata kitu kutoka kwa Yesu.

Yule mmoja aliyekwenda kushukuru alipata cha zaidi cha kurudishiwa afya yake baada ya kwenda kushukuru.

Na mimi niliona hilo, kwa hiyo huwa nawaambia Watanzania  tusiache kushukuru kwa mwaka huu 2020. Kama ulimwomba Mungu vitu 10 na kakupa viwili mshukuru kwa kupata hivyo hivyo viwili. Hata kama hajakupa kitu mshukuru kwa kuwa  kakutegea sikio.

Fanya zoezi la kumshukuru Mungu ili imani yako inyanyuke ndani yako. Ukijifunza utashangaa vitu ambavyo Mungu atakuongezea. Kama kuna uponyaji wa 100% na Mungu kakupa asilimia 10%. Mshukuru kwa hizo asilimia 10%. Na uwe na uhakika Mungu atakupa cha asilimia 20%.

Hapa ndio mwisho wa somo letu na endelea kumshukuru Mungu toka moyoni mwako.


Mungu akubariki sana

Post a Comment

0 Comments