100/recent/ticker-posts
KANAANI MPYA - Lisikilizeni Neno la Bwana............. MAOMBI NA MAOMBEZI --- Tupigie; +255767-155-623 Ujumbe mfupi/Whatsapp; +255620-179-783

USHUHUDA UTAKAOKUSAIDIA KUKUA KIROHO

 USHUHUDA UTAKAOKUSAIDIA KUKUA KIROHO 

USHUHUDA 

http://draywadray.blogspot.com
Huu ni ushuhuda ulioandikwa na
Mchungaji John Mulinde wa Uganda
kutokana na kile alichosikia kutoka kwa
mhusika mwenyewe. Mhusika huyo,
mchungaji hajamtaja, lakini alikuwa ni
kijana ambaye alimtumikia shetani tangu
angali tumboni mwa mama yake.
Baadaye, kwa neema ya Bwana kijana
huyo aliokolewa, ndipo akaanza kueleza
siri hizi za ufalme wa giza na ufalme wa
nuru.
Mamilioni ya Wakristo duaniani
tunamwomba Mungu wetu kwa ajili ya
mahitaji mbalimbali tuliyonayo. Lakini
liko swali moja kubwa linalojirudiarudia
ndani ya mioyo yetu karibu kila siku.
Tunajiuliza, “Nimeomba sana na kwa
muda mrefu. Mbona Mungu hajibu...?”
Tunabaki bila majibu, tunavunjika moyo,
na tunaanza kudhani labda sisi ni wenye
dhambi sana ndio maana hatujibiwi.
Ukiifahamu siri iliyomo kwenye ushuhuda
huu, utatiwa nguvu sana za rohoni;
maana maarifa ndiyo yanayotufanya tuwe
na nguvu za Mungu. Tunaenenda kiimani
kwa kadiri ya kiwango cha maarifa au
ufahamu uliomo ndani yetu. Tukijua
sana, tunaweza sana; tukijua kidogo,
tunaweza kidogo.
Karibu ujipatie maarifa ambayo Bwana
wetu ameruhusu yatufikie. Nami na
hakika utamfurahia Bwana kwa
kukupigisha hatua nyingine ya imani.
Utafanya vema kama ukiweza kuwapatia
na wengine somo hili la muhimu sana
kwa ajili ya mwili wa Kristo.
******************
Yafuatayo ni maelezo ya Mchungaji John
Mulinde:
Napenda nikushirikishe ushuhuda wa
kijana mmoja ambaye aliokoka; kijana
ambaye alikuwa akimtumikia ibilisi. Na
mtu yule alipotoa ushuhuda wake, ulinitia
changamoto kubwa sana. Sikutaka
kuamini. Ilinibidi nifunge kwa muda wa
siku kumi mbele za Bwana, huku
nikimuuliza, "Bwana, hivi mambo haya ni
kweli? " Na ilikuwa ni katika wakati huo
ndipo Bwana alipoanza kunifundisha kile
kinachotokea kwenye ulimwengu wa roho
pale tunapoomba.
Kijana huyu alizaliwa baada ya wazazi
wake kuwa wamejiweka wakfu wao
wenyewe kwa lusifa. Wakati bado akiwa
tumboni, walifanya matambiko mengi na
kumweka wakfu awe mtumishi wa lusifa.
Alipozaliwa na kufikisha miaka minne,
tayari alianza kutumia nguvu zake za
kiroho. Hata wazazi wake walianza
kumwogopa! Akiwa na miaka sita, baba
yake alimkabidhi kwa wachawi ili
akapatiwe mafunzo. Na akiwa na miaka
kumi, alikuwa akifanya mambo makubwa
katika ufalme wa ibilisi. Alikuwa
akiogopwa hata na wachawi wa kawaida.
Alikuwa bado ni kijana mdogo, lakini
mambo aliyokuwa anafanya yalikuwa ni
mabaya mno. Alikua hadi kufikia miaka
ya ishirini akiwa na damu nyingi ya watu
mikononi mwake. Aliua watu kila
alipotaka. Alikuwa na uwezo wa kutoka
nje ya mwili wake kupitia taamuli ya
kinjozi (transcendental meditation), yaani
kitendo cha kutuliza mawazo na mwili
kama wafanyayo Wahindukatika yoga.
Tazama mfano HAPA . Katika huko
kutaamuli, angeweza hata kunyanyuka
kimwili kutoka ardhini pale alipokaa na
kuelea hewani (levitate). Tazama mfano
HAPA . Wakati mwingine aliweza kutoka
nje ya mwili; akauacha mwili wake na
kwenda nje huko na kule kufanya mambo
mbalimbali (astro-travelling). Na kijana
huyu alitumiwa na shetani kuharibu
makanisa mengi; na kuwaharibu
wachungaji wengi.
Siku moja, alipangiwa kwenda kuharibu
kanisa moja ambalo lilikuwa na maombi
ya kutosha. Kulitokea na migawanyiko
mingi kanisani na kuchanganyikiwa
kwingi. Alianza kufanya kazi kwenye
kanisa hili; lakini mchungaji wa kanisa lile
aliitisha mfungo wa kanisa zima. Kanisa
lilipoanza kufunga, watu walitubu sana
na kufanya mapatano mengi. Na watu
wakawa kitu kimoja, na wakaanza
kuomba kwa ajili ya kazi ya Bwana
katikati yao. Na wakaendelea kufanya
maombezi na kumlilia Mungu ili
awarehemu na kuingilia kati maishani
mwao. Na kadiri siku zilivyoendelea,
bwana huyu alikuwa akija tena na tena
akiwa na mapepo kinyume na kanisa hili.
Lakini lilitoka neno la kinabii likiwaambia
Wakristo wasimame pamoja na kufanya
vita dhidi ya nguvu za giza ambazo
zilikuwa zinashambulia kanisa lile.
Siku moja, kijana huyu aliuacha tena
mwili wake chumbani kwake na akatoka
nje. Aliongoza jeshi kubwa la mapepo
moja kwa moja hadi kwenye kanisa lile ili
kwenda kufanya vita vya kiroho.
Sasa, ufuatao ni ushuhuda wake.
Roho yake ilikuwa inapaa hewani juu ya
kanisa lile na kujaribu kulishambulia,
lakini kulikuwa na kifuniko cha nuru juu
ya kanisa hilo. Wakati waliendelea na
mapambano, ghafla, kulikuja jeshi la
malaika ambalo liliwashambulia na
kukawa na mapambano makali pale
hewani. Hatimaye, mapepo yalikimbia,
lakini yeye alikamatwa na wale malaika.
Ndiyo, alikamatwa na malaika! Alijiona
akiwa ameshikiliwa na malaika sita. Na
wakamleta kwa kumpitisha kwenye paa
hadi kwenye madhabahu ya kanisa.
Akawa yuko pale huku watu wanaendelea
kuomba. Walikuwa wamezama kwenye
maombi, wakifanya vita vya kiroho;
wakifunga na kuvunja, na kutupa nje.
Mchungaji alikuwa kwenye madhabahu
akiongoza maombi hayo na vita. Roho wa
Bwana akaongea na mchungaji, akisema,
"Nira imevunjika, na mhusika yuko hapa
mbele yako. Msaidie kwa kumfungua. "
Mchungaji alipofungua macho yake,
alimwona yule kijana akiwa ameanguka
pale hajitambui. Mwili wake ulikuwa
pamoja naye! Kijana yule anasema kuwa
haelewi ni kwa vipi mwili wake uliungana
naye; maana alikuwa ameuacha
nyumbani. Lakini ndio alikuwa pale; hajui
ni kwa vipi aliingia, isipokuwa tu malaika
walimpitishia kwenye paa.
Sasa, mambo haya ni magumu kuamini,
lakini mchungaji alinyamazisha kanisa na
kuwaambia kile ambacho Bwana
alimwambia. Kisha akamwuliza yule
kijana, "Wewe ni nani? " Kijana yule
alikuwa anatetemeka wakati mapepo
yalipoanza kumtoka.
Kwa hiyo, waliomba kwa ajili ya
kufunguliwa kwake, na hatimaye baadaye
alianza kusema ushuhuda wake. Hivi
sasa kijana huyu ameshaingia kwa
Bwana na ni mwinjilisti, akihubiri Injili.
Anatumiwa sana na Bwana kuwaweka
huru watu wengine.
Usiku mmoja, mimi (John Mulinde)
nilienda kwenye chakula cha usiku mahali
fulani. Sababu hasa ya kwenda pale ni
kwa vile kuna mtu alinieleza habari za
huyo kijana; na nilikuwa na shauku
kubwa sana ya kumwona, na kuona kama
kweli hadithi yake ina ukweli wowote.
Kwa hiyo, nilipofika, nilikaa mezani. Na
jioni ile, kijana huyu alipewa nafasi ya
kutoa ushuhuda wake. Alizungumza juu
ya mambo mengi sana. Mara nyingine
alilia kutokana na mambo aliyoyafanya.
Alipomaliza kusema, alitoa ombi.
Kulikuwako na wachungaji wengi pale
kwenye ukumbi. Alisema, "Ninawaomba
ninyi, wachungaji. Tafadhalini, wafundisheni
watu namna ya kuomba.” Watu ambao
hawaombi, wanaweza kuchukuliwa na
chochote, katika chochote na ibilisi; na
ziko hata njia za adui za kutumia maisha
yao na maombi yao. Adui anajua hata
namna ya kutumia kwa faida yake
maombi ya watu wasiojua kuomba.
"Wafundisheni watu namna ya kutumia
silaha za kiroho ambazo Mungu amezitoa. "
Kisha alieleza jinsi ambavyo alikuwa
akiongoza mapambano kwenye anga.
Alikuwa akienda pamoja na maajenti
wengine wa shetani na mapepo mengi
hadi angani. Ilikuwa kama zamu. Inabidi
kwenda kutekeleza zamu yako. Kwa hiyo,
ni mara nyingi tu alikuwa na muda wa
kwenda kwenye anga ili kufanya vita. Na
akasema kuwa kule angani, kwenye
ulimwengu wa roho, kama anga
limefunikwa na blangeti la giza, blangeti
hilo linakuwa ni nene sana; na ni kama
jiwe. Na linakuwa limefunika eneo lote.
Na mapepo haya yanaweza kwenda juu
yake na chini yake. Na yakiwa huko,
yanaweza kuathiri matukio
yanayoendelea duniani.
Pale mapepo wachafu pamoja na
maajenti wa shetani wa kibinadamu
wanapomaliza zamu yao, wanashuka
duniani kwenye maeneo ya kimaagano,
iwe ni kwenye maji au ardhini, ili kuweza
kurejesha upya nguvu zao, maana
zinakuwa zimepungua kutokana na
kufanya kazi angani wakati wa zamu yao.
Na wanarejeshaje nguvu zao? Ni kupitia
kafara ambazo watu wanatoa kwenye
madhabahu hizi. Kafara zinaweza kuwa
ni uchawi wa wazi, damu za aina zote,
ikiwa ni pamoja na utoaji mimba, vita, na
utoaji wa kafara za wanadamu na
wanyama. Zinaweza pia kuwa ni kafara
za uzinzi, pale ambapo watu wanafanya
uzinzi na uashetati wa kila aina. Na
matendo haya maovu yanaleta nguvu
kwenye ulimwengu wa giza. Na ziko aina
nyingi za kafara.
Kijana huyo alisema kuwa, maajenti wa
shetani wanapokuwa juu kwenye anga, na
Wakristo wakaanza kuomba hapa
duniani, maombi ya Wakristo huonekana
kwa namna tatu. Maombi yote huonekana
kama moshi ambao unapaa kuelekea
mbinguni.
Baadhi ya maombi huonekana kama
moshi, na yanaenda juu kiasi na
kupotelea hewani. Maombi ya aina hii
hutoka kwa watu ambao wana dhambi
maishani mwao na hawako tayari
kushughulika nazo. Maombi yao ni dhaifu
sana, kiasi kwamba yanapeperushwa na
kupotelea angani.
nyingine ya maombi nayo ni kama moshi
ambao unainuka juu hadi unapofikia
kwenye ule mwamba, lakini hayana nguvu
ya kupenya mwamba huo. Kwa kawaida,
hawa ni watu ambao hujaribu kujitakasa,
lakini hawana imani juu ya kile ambacho
wanakifanya pale wanapoomba, yaani
wanaomba lakini moyoni hawana ujasiri
kwamba kile wanachokiomba
watakipokea. Mara nyingi huwa
wanapuuzia mambo mengine ya muhimu
yanayotakiwa wakati mtu anapoomba.
Aina ya tatu ya maombi ni kama moshi
ambao umejaa moto. Yanapokuwa
yanapaa, yanakuwa ni ya moto sana kiasi
kwamba yanapoufikia ule mwamba,
unaanza kuyeyuka kama nta. Yanapenya
mwamba huo na kuendelea hadi juu.
Mara nyingi watu wanapoanza kuomba,
maombi yao huonekana kama aina ya
kwanza ya maombi. Lakini kadiri
wanavyoendelea kuzama, yanageuka na
kuwa ya aina ya pili. Na wakiendelea
zaidi, ghafla yanalipuka moto. Na
maombi hayo yanakuwa yana nguvu sana
kiasi kwamba yanapenya kabisa ule
mwamba.
Mara nyingi maajenti wa uovu hubaini
kwamba kuna maombi yanabadilika na
kuelekea kwenye kuwa moto. Kisha
huwasiliana na viumbe vingine vilivyoko
duniani na kuwaambia, "Mvurugieni mtu
huyo maombi! Mfanyeni aache kuomba!
Mwondoeni kwenye maombi! "
Mara nyingi Wakristo hushindwa na
mbinu hizi. Wanakuwa wanaomba kwa
nguvu; wanatubu; wanaruhusu Neno
kukagua nafsi zao; imani inaanza
kujengeka. Maombi yao yanaanza kuwa
na shabaha zaidi. Kisha ibilisi anaona
kuwa maombi yao yanaanza kukusanya
nguvu. Ndipo vurugu zinaanza ili kuharibu
maombi hayo. Mara simu inalia. Wakati
mwingine, katikati ya maombi ambapo
mtu alikuwa amezama kabisa, , simu
inaweza kulia na unawaza kuwa, ngoja
niende nikaipokee kisha nitarudi
kuendelea na maombi.
Mbinu zingine za kuvuruga maombi nazo
zinaweza kutumika; hata kama ni
kukugusa mwili wako na kuleta maumivu
mahali fulani. Hata pia kukufanya ujisikie
njaa ambapo utajisikia kwenda jikoni
kutengeneza japo chakula kidogo.
Ilimradi tu wakiweza kukufanya utoke
mahali pale, wanakuwa
wameshakushinda. Wachungaji, ni lazima
muwafundishe watu jinsi ya kuomba.
Tengeni muda, si tu kwa ajili ya maombi
ya juujuu. Mara moja kwa siku, Wakristo
wanatakiwa kuwa na muda wa
kujielekeza kwa moyo wote kwa Mungu,
bila kuwapo kwa kitu chochote cha
kuwaharibia umakini wao.
Na kama watu waking’ang’ana kabisa
kwa njia hii ya maombi na kuruhusu
kupata mwongozo wa kiroho, kisha
wakawa wanaendelea na kuendelea,
lazima kitu kitatokea rohoni. Moto
utalipuka na kugusa ule mwamba na
kuuyeyusha! Kuyeyuka kunapoanza, ni
moto sana kiasi kwamba hakuna pepo
ambaye anaweza kustahimili. Wala
hakuna roho ya mwanadamu inayoweza
kustahimili pia. Wote wanakimbia.
Kama mtu atajitoa kuomba kwa bidii na
kwa kumaanisha namna hiyo, hatimaye
kutafuata kufunguka kwa ulimwengu wa
roho. Na mara hili linapotokea, matatizo
yote haya katika maombi yanafikia
mwisho! [Yaani ule ugumu na ule uzito
unakwishilia mbali!] Yule ambaye
anakuwa anaomba duniani anakuwa sasa
anajisikia kuwa maombi ni kitu kilaini
kabisa, cha kuburudisha, na chenye
nguvu.
Na nimegundua kuwa wakati huo, huwa
tunapoteza kabisa hisia za muda na
mambo mengine. Si kwamba tunakosa
mpangilio; la hasha! Mungu anakuwa
anashughulika na muda wetu. Lakini
inakuwa ni kama unaachilia kila kitu, na
unaunganishwa moja kwa moja na
Mungu. Maombi yako yanapopenya,
kunakuwa hakuna kizuizi tena kuanzia
hapo; na mtu anayeomba anaweza
kuendelea kwa muda mrefu kama
apendavyo. Hakuna kabisa kizuizi.
Na mara anapomaliza kuomba, lile tundu
linabakia wazi.
Kijana huyu pia alisema kuwa, watu wa
namna hii wanapomaliza kuomba na
kuondoka mahali hapo, lile tundu
linakuwa linaondoka pamoja nao.
Wanakuwa hawaenendi tena chini ya lile
blangeti la jiwe. Wanakuwa wanaenenda
chini ya mbingu zilizo wazi. Na akasema
kwamba, katika hali hiyo, ibilisi hawezi
kufanya kile anachokitaka kwao. Na
uwepo wa Mungu unakuwa kama nguzo
kutoka mbinguni ikiwa iko juu ya maisha
yao. Wanalindwa; na kunakuwa na nguvu
kubwa sana ndani ya hiyo nguzo kiasi
kwamba kadiri wanavyotembea huku na
kule, uwepo huo unakuwa unagusa hata
watu wengine. Nguzo hiyo inakuwa
inatambua kile ambacho adui amefanya
kwa watu wengine. Na pale watakatifu
hao wanapozungumza na watu wengine,
na wale watu wakawa wamesimama nao,
wanaingia ndani ya nguzo hiyo. Na mradi
tu wakiwa ndani ya ile nguzo, vifungo
vyote vya adui vinadhoofika.
Kwa hiyo, watu hawa wenye mpenyo huu
wa kiroho wanapowashuhudia wenye
dhambi habari za Yesu Kristo, upinzani
wa wenye dhambi unakuwa wa chini. Ni
rahisi kuwaleta wenye dhambi kwa Kristo.
Wanapoomba kwa ajili ya wagonjwa, au
kwa ajili ya mambo mengine, maombi
yao yanakuwa na nguvu sana.
Na kama kuna sehemu ambako maombi
ya namna hii huombwa mara kwa mara,
uwepo wa Mungu unakuja mahali pale na
hauondoki. Hivyo, hata watu wasiomjua
Mungu wanapokuja kwenye sehemu kama
hizo, ghafla vifungo vyao vinakatika.
Na kama atatokea mtu wa kusema nao
kwa uvumilivu na kwa upendo, wanaweza
kugeuka haraka sana; si kwa nguvu au
kwa uwezo, bali ni kwa Roho wa Mungu,
ambaye anakuwa yuko pale. Na kama
hakuna mtu atakayewajali watu hawa,
wanakuja kwenye uwepo wake na
kujisikia hatia, wanaanza kujadili kama
wakubali au la. Pale watakapoondoka,
vifungo vinakuwa na nguvu zaidi kwao.
Na ibilisi anajihadi kwa kila njia
kutowaruhusu kurudi tena kwenye
sehemu kama hizo.
Je, shetani anakaa kimya tu baada ya mtu
kupata mpenyo?
Kijana huyu alisema kuwa, ibilisi
anawachukia sana watu wa namna hiyo,
yaani wale waliopata mpenyo wa
maombi.
Sasa unaweza kupiga picha, sote
tulikuwa tumekaa chini tunamwangalia
kijana huyu akieleza ushuhuda wake.
Alikuwa anatueleza mambo ambayo yeye
mwenyewe alikuwa akiyafanya na
aliyoyashuhudia kwa macho yake.
Alitueleza kile ambacho walifanya kwa
watu ambao walipata mpenyo katika
maombi. Alisema kuwa waliwaweka
akilini sana watu kama hao. Kisha
waliwafuatilia sana na kujifunza kuhusu
wao ili kuwajua vizuri. Walitafuta kila kitu
kuwahusu. Hivyo, walifahamu udhaifu
wao wote, na ikitokea mtu akawashinda
kwenye maombi na kupenya,
wanawasiliana na wengine kwenye
ulimwengu wa giza na kusema,
"Mumlenge mtu huyu kwenye eneo hili na
hili. Udhaifu wake uko hapa na hapa."
Kwa kuwa mtu wa aina hii anapotoka nje
ya kifuniko cha maombi, roho ya maombi
inakuwa juu yake, uwepo wa Mungu upo
juu yake, roho yake inakuwa iko juu, na
furaha ya Bwana ndiyo nguvu zake;
anapokuwa anaenda, adui anajaribu kila
njia kuleta yale mambo ambayo
yatamvuruga ili asielekeze macho yake
kwa Bwana.
Kama, kwa mfano, imeshajulikana kuwa
udhaifu wake uko kwenye eneo la hasira,
basi adui atasababisha watu watende
mambo ambayo yatamfanya akasirike.
Na kama hayuko makini kumsikiliza Roho
Mtakatifu, na akaingiwa na hasira, basi
ataondoa macho yake kwa Bwana. Na
anapokuwa na hasira hivyo, ghadhabu
zinamjaa. Baadaye anapokuja kujirudi,
anakuwa anataka kutupilia mbali hali
hiyo na kuendelea na furaha ya Bwana,
lakini anajikuta hajisikii tena ile furaha
kama mwanzo. Anajitahidi kujisikia vizuri
tena; lakini haiwezekani tena. Kwa nini?
Alipojiachilia kwenye kishawishi cha
hasira, mapepo walifanya bidii zote
katika muda huo kufunga lile tundu kule
juu. Na mara waliporudishia lile jiwe,
uwepo wa Bwana unakuwa umekatika,
yaani ile nguzo iliyokuwa inatokea
mbinguni na kumfunika inakuwa haimfikii
tena!
Mtu huyo hataacha kuwa mwana wa
Mungu. Lakini ule upako wa ziada
uliokuwa unaandamana naye maishani;
ule uwepo uliokuwa ukitenda mambo bila
yeye kutumia nguvu zozote, unakuwa
umekatika! Maana pepo wachafu
wanatafuta uliko udhaifu wako.
Kama udhaifu wa mtu ni kwenye masuala
ya mapenzi, adui ataandaa watu,
matukio, na mambo ambayo yatainua
hisia za mtu huyo za tamaa ya
kimapenzi. Na kama mtu huyo
atazikubalia hizo tamaa na kufungua akili
yake kuyapokea mambo hayo, na kuyalea
nafsini mwake, pale anapomaliza kila kitu
na kutaka kurejea tena kwenye hali ya
upako ili asonge mbele, anakuta kwamba
ule uwepo haupo tena. Labda unasema,
“Hii si vizuri kabisa.” Kumbuka tu Biblia
inasemaje, " Tena ipokeeni chapeo ya
wokovu. Vaeni dirii ya haki." Mara nyingi
hatuoni haja ya silaha hizi za kivita.
Lakini kumbuka Yesu alivyotuambia juu
ya namna ya kuomba "Usitutie
majaribuni, lakini utuokoe na yule
mwovu."
Kila mara unapopata mpenyo katika
maombi, unapofika mwisho, kumbuka
kuwa wewe bado ni kiumbe mwanadamu
aliye dhaifu. Kumbuka kuwa
haujakamilishwa bado. Mwombe Bwana,
useme, "Bwana, nimefurahia wasaa huu
wa maombi, lakini nitakapotoka nje
kwenye dunia, usiniongoze kwenye
majaribu. Usiruhusu niangukie kwenye
mtego wa ibilisi. Najua kuwa adui
anatega mitego kule nje. Sijui ni mitego
ya namna gani. Na ninajua kuwa bado
mimi ni dhaifu katika baadhi ya maeneo.
Kama nikiingia kwenye hali fulanifulani,
nitaanguka. Unilinde, Bwana. Unapoona
ninaelekea kule ambako kuna mitego
niliyotegewa, nifanye nielekee upande
mwingine. Uingilie kati, Ee, Bwana. Usiche
niende tu kwa nguvu zangu na uwezo
wangu. Niokoe na yule mwovu.”
Mungu anaweza kufanya hivyo. Lakini,
kama kuna kitu kibaya kitatokea,
ambacho kitakufanya uondoe macho
yako kwa Kristo, wewe sema tu, “Asante
Yesu.” Ndiyo sababu Mtume Paulo
aliandika, “Mshukuruni Mungu kwa kila
jambo.” Baadhi ya mambo si mazuri.
Yanaumiza, na tunashangaa kwa nini
Mungu anayaruhusu yatufikie. Lakini
kama tu tungejua kwa njia hiyo
anatuokoa na mambo yapi,
tungemshukuru. Tukijifunza kumwamini
Bwana, tutamshukuru kwa kila jambo.
Yule kijana aliendelea kusema kuwa,
unapopata mpenyo katika maombi,
majibu yako ni lazima yatakuja. Alisema
kuwa jibu mara zote huja, lakini mara
nyingi, huwa halifiki kwa mtu aliyeliomba.
Kwa nini? Ni kwa sababu ya mapambano
yaliyoko kwenye anga. Pia, majibu
yanaweza kuzuiliwa iwapo viumbe waovu
wa rohoni watafanikiwa kurejesha ule
mwamba na kuziba tundu ambalo
mwombaji alifanikiwa kulitoboa kwa njia
ya maombi yake.
Kisha aliongea jambo ambalo kwa kweli
lilitikisa imani yangu. Binafsi ilinibidi
niingie kwenye mfungo wa siku kumi, ili
kumwuliza Bwana kama hilo alilosema
lilikuwa na ukweli wowote. Basi sikiliza
haya: Kijana huyu alisema kuwa, kila
Mkristo anaye malaika ambaye
anamtumikia Mkristo huyo. Nasi
tunafahamu kuwa Biblia inasema kuwa
malaika ni roho wanaotutumikia.
(Waebrania 1:14). Alisema kuwa watu
wanapoomba, majibu huletwa kwa
mikono ya malaika. Malaika huleta
majibu, kama ambavyo tunasoma kwenye
kitabu cha Danieli. Kisha alisema jambo
ambalo ni gumu sana. Alisema kwamba,
kama yule anayeomba anafahamu silaha
za kiroho na amejivika silaha hizo, majibu
nayo huja kwa kupitia malaika ambaye,
naye amejivika kikamilifu kwa silaha
hizohizo.
Lakini, kama anayeomba hajali silaha za
kiroho, basi malaika nao wanakuja bila
silaha hizo. Wakristo ambao hawajali kile
ambacho kinaingia mawazoni mwao;
hawashindani kuangusha mawazo
yasiyofaa; malaika wao huja bila chapeo.
Silaha zozote utakazoacha kuzitilia
maanani duniani, malaika anayekutumikia
naye anakuwa hanazo. Kwa maneno
mengine, silaha zetu za kiroho hazitulindi
miili yetu, bali zinalinda vitu vile vya
kiroho tunavyofanikiwa kuvipata kutoka
kwa Bwana.
Malaika anapokuwa anakuja, mapepo
wanamtazama na kumkagua na kubaini
maeneo ambayo hajajifunika; na hayo
ndiyo maeneo ambayo watashambulia.
Kama hana chapeo kichwani, basi
watashambulia kichwani. Kama hana
dirii, watashambulia kifuani. Kama hana
viatu, watajaribu kutengeneza moto ili
kumwunguza miguuni.
Sasa, najua kuwa hili ni gumu kuamini;
mimi narudia tu kile ambacho kijana huyu
alisema. Kisha tulimwuliza, “Je, malaika
wanaweza kuungua moto?” Na unajua
alisema nini? Kumbuka kuwa huu ni
ulimwengu wa roho. Hizi ni roho kwa roho
zinapambana. Mapambano ni makali
sana, na pale wanapomshinda malaika
wa Mungu, jambo la kwanza
wanalokimbilia ni lile jibu alilobeba; na
wanalichukua hilo. Na hizi zinakuwa ni
zawadi ambazo hutolewa kwa watu
kupitia imani za siri, au uchawi.
Kumbuka kile ambacho Biblia inasema
kupitia kitabu cha Yakobo. Vipawa vyote
vyema hutoka kwa Mungu (Yakobo 1:17).
Kwa hiyo, shetani anapata wapi vitu
vizuri anavyowapatia watu? Baadhi ya
watu ambao hawawezi kupata watoto,
huenda kwa wachawi na waabudu
shetani, na wanapata mimba! Mtoto
anakuwa ametoka wapi? Je, shetani ni
muumbaji? HAPANA! Anaiba kutoka kwa
watu ambao hawaombi maombi yao hadi
mwisho.
Katika Biblia, Yesu alisema, "Ombeni bila
kukoma." Pia alisema, "atakapokuja
Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani
duniani? " Je, Yesu atakukuta bado
unangojea? Au utakata tamaa na
kumwacha adui aibe kile ambacho
umekuwa ukikiombea?
Na hawaridhiki tu na kuiba jibu la
maombi. Wanataka pia kumweka malaika
kifungoni. Na wanaanza kupambana
naye. Wakati mwingine wanafanikiwa
kumkamata na kumfunga malaika.
Inapotokea hivyo, Mkristo anakuwa kama
chakula chao duniani. Wanaweza
kumfanyia chochote maana hana ulinzi
tena kwenye ulimwengu wa roho.
Nilimwuliza kijana huyo, “Una maana
kuwa malaika anaweza kushikiliwa katika
ulimwengu wa giza?” Sasa alikuwa
anaeleza uzoefu wake, na akasema,
hawatamshikilia malaika kwa muda mrefu
kwa sababu ya Wakristo wengine ambao
wanaomba mahali pengine. Jeshi la ziada
litatumwa, na malaika atakuwa huru. Na
kama yule Mkristo anayehusika hajaomba
hadi kwenye mpenyo, basi atabakia
mateka. Ndipo shetani atatuma malaika
wake na malaika wa nuru kwa mtu huyu,
na hapo ndipo uongo na udanganyifu
unapotokea; maono ya uongo na unabii
wa uongo. Uongozi wa uongo, na kufanya
kila aina ya maamuzi mabaya. Na mara
nyingi, mtu wa namna hii anaweza kupata
mashambulizi na vifungo vya kila aina.
Niliondoka kwenye kile chakula cha jioni
huku na mawazo mengi sana. Nikasema,
“Bwana, sitaki hata kujaribu kuamini
jambo hili.” Linaondoa ujasiri na usalama
wangu wote! Nilipoenda kumlingana
Bwana, ilikuwa ni kwa siku kumi; na
Bwana alifanya mambo mawili. Kwanza,
si tu kwamba alithibitisha mambo hayo
niliyoyasikia kutoka kwa yule kijana, bali
pia alifungua akili zangu zaidi ili kuona
mambo mengine mengi zaidi ya yale
ambayo niliyasikia. Pili, aliniongoza
kuona kile ambacho tunatakiwa kukifanya
wakati mambo haya yanapotokea ili
tuweze kuwa washindi.
Alinipa mambo matatu:
Moja: namna ya kutumia silaha za vita
vyetu vya kiroho. Biblia inaziita silaha za
Mungu. Si silaha zetu. Tunapozitumia,
tunamruhusu Mungu kupigana kwa niaba
yetu.
Mbili: tambua uhusiano wa roho
zinazotutumikia, yaani malaika, na
maisha yetu ya kiroho. Na ni lazima kuwa
makini sana na kile kinachotokea mioyoni
mwetu; kama mwongozo wa kile
ambacho kinatakiwa kutokea rohoni
kutuhusu sisi.
Tatu: ni Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu
hatakiwi kuja kama mtumishi wetu,
kututumikia na kutuletea vitu mbalimbali.
Hakimbiikimbii kwa Baba kumweleza kile
ambacho tunataka. Hiyo ni kazi ya
malaika. Lakini Yeye husimama pamoja
nasi. Anafanya nini? Anatuongoza,
anatufundisha, anatutangulia,
anatusaidia kuomba inavyotakiwa. Na
mambo haya yanapotokea kwenye
ulimwengu wa roho, anatuambia. Wakati
mwingine anakuamsha usiku na
kukwambia, “Omba.” Wewe unasema,
“Hapana! Muda wangu haujafika.” Na
anasema, “Omba sasa!” Kwa nini inakuwa
hivyo? Ni kwa sababu Yeye anaona kila
kinachoendelea kwenye ulimwengu wa
roho. Wakati mwingine anasema, “Kesho
ni kufunga.” Wewe unasema, “Hapana,
nitaanza Jumatatu!”
Lakini kumbuka kuwa Yeye anaelewa kile
kinachoendelea kwenye ulimwengu wa
roho. Ni lazima tujifunze kuwa makini na
Roho Mtakatifu. Anatuongoza kwenye njia
za haki. Wapendwa, tuishie hapa. Labda
wakati mwingine tutaongea jinsi ambavyo
tunaweza kuomba hadi kupata mpenyo,
maana sasa tunajua mapambano
yaliyoko rohoni na jinsi ya kupenya; na
namna tunavyoweza kudumu tukiwa na
mpenyo tuliopata. Na mara tunapojifunza
hili, linakuwa ni jambo la furaha sana.
Tukumbuke tu jambo moja: vita si vyetu,
bali ni vya Bwana! Haleluya!
Hebu tusimame. Mwangalie mwenzio
machoni na utafakari ni mara ngapi
amekosa kile ambacho Mungu alikiandaa
kwa ajili yake. Lakini shikaneni mikono
kama inawezekana; watu wawili au
watatu, kisha tu muambiane, “Hakuna
haja ya kushindwa tena! Tunaweza
kushinda! Iko nguvu ya kutosha kushinda!
Yesu tayari ameshafanya kazi yote.”
Muombeane ninyi kwa ninyi ili Bwana
aweze kutusaidia kushinda. Hatutakiwi
kushindwa. Iko neema ya kutosha; nguvu
ya kutosha kuleta ushindi!
Asante Yesu.
**********************
http://draywadray.blogspot.com

Post a Comment

0 Comments