100/recent/ticker-posts
KANAANI MPYA - Lisikilizeni Neno la Bwana............. MAOMBI NA MAOMBEZI --- Tupigie; +255767-155-623 Ujumbe mfupi/Whatsapp; +255620-179-783

MAISHA YA WOKOVU

  MAISHA YA WOKOVU


draywadray.blogspot.com
Yesu anasema nasi, “kaeni ndani yangu nami ndani yenu” ambapo tunaona mawili, Yesu kukaa ndani yetu na sisi kukaa ndani ya Yesu. Katika sehemu iliyopita tumeona Yesu kukaa ndani yako, kwamba ni kumpokea Yesu ndani ya moyo wako; yaani “kuokoka”. Leo tunaona Yesu kukaa ndani yako; yaani “maisha ya wokovu”.
Yesu anasema, mkikaa ndani yangu “mtazishika amri zangu”. Kuzishika amri za Yesu ndiyo kuishi katika wokovu. Kwa hiyo ukiweza kuishi kwa kuzishika mari za Yesu unakuwa umeishi maisha ya wokovu tunayoyazungumzia.
Tumeona kwamba unapookoka, Yesu anakuwa ameingia ndani yako na sasa tunakwenda kujifunza maisha katika wokovu ambayo kwa lugha nyingine tunaita kukaa ndani ya Yesu.
Maisha ya wokovu ni maisha ya hapa duniani tangu mwanadamu anapookoka hadi atakapokufa (hatima ya maisha ya duniani). Baada ya maisha ya wokovu ni maisha ya milele ambapo tutaishi pamoja na Baba katika ufalme wake Mbinguni.
“Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.” UFU. 3:20-21
Bwana Yesu ni wa kwanza, anabisha hodi, ukifungua mlango (ukimruhusu aingie) yaani ukimwamini na kumkiri… anaingia ndani yako na kufanya makao. Atakula pamoja nawe, nawe pamoja Naye (kila utakachokuwa unafanya, atakuwa pamoja nawe), katika mawazo yako yupo nawe, katika matendo yako yupo nawe, na kila sehemu utakapokuwepo Yeye yupo nawe.
Akiisha ingia kwako inakupasa nawe ukae ndani yake, yaani uyaishi maisha ya wokovu kikamilifu kwa uangalifu mkubwa. “atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.” 1 YOH. 3:8-10
Yesu akikaa ndani yako nawe unapokaa ndani ya Yesu, unakuwa umeruhusu utatu wote mtakatifu kukaa nawe. Kwasababu hiyo, unakuwa na utukufu wa mbinguni, na mtembeo utakao tembea ni mtembeo wa kimbingu, maana akikaa ndani yako anayeishi sasa siyo wewe bali yeye aliye ndani yako na laiye ndani yako ni ufalme wote wa Mbinguni. Biblia inasema katika Wagalatia 2:20 kwamba; “nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilionao sasa katika mwili ninao tena katika imani ya mwana wa Mungu, ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwaajili yangu.”
Na kwasababu umefanyika mwana wa Mungu aliye hai, unakuwa na tabia maalum ya Mungu. Mungu wetu ni mtakatifu, kwa hiyo watoto wake waliozaliwa naye wanapaswa kuwa watakatifu. “…Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu…”
Maisha ya wokovu ni kupambana ili kudumu katika utakatifu. Utakatifu ni kutokutenda dhambi. Na kwasababu umeshatolewa kwenye ule utu wa kale, yaani kuishi kimwili na ukawa mfu kimwili na kuanza kuishi kiroho, vivyo hivyo unapaswa uenende kwa namna ya rohoni. Paulo katika waraka wake wa pili kwa Timotheo anasema “nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda” 2TIM. 4:7. Unaona hapa sasa, maisha ya wokovu ni maisha ya vita. Vita ni mapambano. Siyo maisha ya starehe na raha, bali ni maisha ya kusimama imara. Shetani kila kukicha anapambana kuiteka Imani yetu, sisi tunapaswa kuilinda hii Imani.
Haya maisha ya wokovu ni maisha ya utakatifu. Mtu anapookoka anakuwa mtakatifu (bila dhambi) na hivyo baada ya kuokoka mtu anapaswa kupambana kuishi katika utakatifu, na haya ndiyo maisha katika wokovu. “Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani. Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo.” KOL. 2:6-8.

MBINU KUU NNE ZA KUDUMU KATIKA WOKOVU:

  1. Neno la Mungu:

Ili kuishi maisha ya wokovu kwa ushindi unapaswa kusoma, kulishika na kulifuata neno la Mungu. Biblia inasema “ni kwa jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kuitii na kulifuata neno” ZAB.119:9, pia ukisoma 2TIM.3:16-17 Biblia inasema “kila andiko lenye pumzi ya Mungu linafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza na kuwaadibisha katika haki… ili mtu wa Mungu awe kamili, aweze kukamilishwa apate kutenda kila tendo lililo jema.”
Tumepata kusema kwamba maisha ya wokovu ni mapambano, maisha ya wokovu ni vita. Silaha yetu kubwa katika hiyo vita ni neno la Mungu. Biblia inasem ahivi “Neno la mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo” EBR.4:12
Mfano: Yoshua mwana wa Nuni alipokabidhiwa kundi la wana wa Israel alifikishe nchi ya ahadi, alipewa maagizo na Mungu. Aliambiwa, “kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapofanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana”.
Baada ya kufuata masharti hayo, Yoshua alikuja kuwa na mafanikio sana na ushindi mno. Tumesoma kuwa alivuka maji ya mto Jordan na pia aliangusha ukuta wa Jeriko na kuiteka miji yote ng’ambo ya Jordan. Hatimaye Yoshua anasema, “Mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana Mungu wetu, nyinyi chagueni hii leo mtakaye mtumikia” kwa maana ameiona siri ya ushindi alionao utokanao na Neno kukaa ndani yake.
Neno la Mungu likikaa ndani yako, utaishi maisha wokovu kwa ushindi siku zote. Utayaishi maisha ya wokovu bila kutetereka na kutikisika, utayaishi maisha ya wokovu bila kuyumba na kuzimia moyo. Hatimaye utaurithi ule uzima wa milele ambayo ndiyo ahadi tunayoishindania.
  1. Roho mtakatifu:

Ili kuishi kwa ushindi maisha ya wokovu, tunahitaji sana msaada wa Roho mtakatifu. Biblia inasema Basi nasema, “enendeni kwa Roho, wala hutazitimiza kamwe tamaa za mwili” GAL. 5:16, ukiendelea kusoma Biblia inasema, …kwa maana mwili hutamani ukishindana na roho…hata hamwezi kufanya mnayoyataka, lakini mkiongozwa na Roho mtakatifu hampo chini ya sharia tena… ukisoma YOH.14:25. Roho mtakatifu anatufundisha na kutukumbusha kuenenda sawasawa na Neno la Mungu. Unapaswa kulisoma Neno kila mara, kuliweka ndani yako Neno na kulitenda Neno; Roho mtakatifu ni mwalimu, anakufundisha Neno, ni msaidizi anakusaidia kuliweka ndani yako na anakukumbusha kuenenda sawasawa na Neno la Mungu.
Mfano: Petro Simon, mwanafunzi wa Yesu alikosa kuwa na ujasiri kuenenda na kukiri wokovu hata akamkana Yesu mara tatu… Lakini alipokuwa pamoja na kanisa la kwanza pale ghorofani Jerusalem, Roho mtakatifu alishuka na kuwajaza wote wakanena kwa lugha nyingine… Petro alipata ujasiri mkubwa sana akahubiri na kumkiri pamoja na kumshuhudia Yesu Kristo mbele ya wayahudi maelfu, wakabatizwa hapo watu takriban wanaume 3,000.
  1. Maombi:

Maombi ni silaha nzito sana ili tuwe na ushindi katika maisha yetu ya wokovu. Maombi hupenya pasipopenya silaha yoyote ile. Maombi ni silaha katika ulimwengu wa kiroho. Shetani anapambana nasi kila saa ili sisi tushindwe kuishi maisha ya wokovu.
Biblia inasema, “kesheni mkiomba, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi lakini mwili ni dhaifu”, MAT. 25:41 lakini pia ongezea EFE. 6:18, “Kwa sala zote na maombi, mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha katika jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote”
Maombi yanatuweka katika uwepo wa Mungu, yanatufanya tuishi tukiwa tumekaa na Mungu kila wakati. Katika maisha ya wokovu maombi yanatufanya kuzidi kukaa katika ulimwengu wa roho na kuishi kiroho. Ndiyo maana Bwana Yesu alitusihi kukesha katika kuomba, Paulo naye ansema “ombeni bila kukoma” 1THES.5:17 anasema dumuni katika kuomba… KOL. 4:2
Kutokana na maombi Mungu ametuahidi mambo mengi mazuri sana. MAT.7:7-11, LUK.18:1-8, YOH.6:23-27.
Biblia inasema, “hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahala pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri”, MDO. 4:31. Pia Biblia inasema, “…huu ndiyo ujasiri tulionao, tukiomba kitu chochote katika mapenzi yake atusikia, kama tunajua atusikia basi tunazo zile haja tumwombazo…” 1YOH.5:13-15.
  1. Kusanyiko/Kanisa:

Ili tuwe na ushindi katika maisha ya wokovu, ni muhimu sana kuwa washirika. Neno la Mungu linasema, “Kwakuwa walipo wawili watatu, wamekusanyika, kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao”, MAT.18:20
Bwana Yesu alipowatuma wanafunzi wake kwenda kuhubiri injili, aliwapanga wawili wawili na siyo mmoja mmoja. Biblia inasema “Basi baada ya hayo, Bwana Yesu aliweka na wengine sabini, akawatuma wawili wawili waende kila mji na kila mahala alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache…” LUK. 10:1-2 Kama isingekuwa ni umuhimu wa ushirika Bwana Yesu asingewatuma wawiliwawili, kwamaa anasema “mavuno ni mengi na watenda kazi ni wachache”. Aliwatuma wawili wawili kwasababu kila walipo wawili watatu au shirika kwa jina lake na Mungu yupo mahala hapo.
Mwandishi wa Ebrania anasema, “tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri. Wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia” EBR. 10:24-25, pia ukisoma YAK. 5:16. Biblia inasema “ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana mpate kuponywa…” Neno la Mungu linazidi kuweka bayana umuhimu wa ushirika katika maisha yetu ya wokovu.
Tunaona tena ni katika makusanyiko, mfano kusanyiko la Yerusalem walipoomba kwa bidii ndipo Roho mtakatifu alishuka, wanafunzi na kanisa la kwanza wakaanza kunena kwa lugha mbalimbali. Mungu alishuka kwa nguvu kubwa sana. Kuwepo katika ushirika kwa jina la Mungu kunakufanya kukaa katika uwepo wa Mungu maana yupo mahala hapo.

Post a Comment

0 Comments