SOMO: IMARISHA IMANI YAKO UNAPOINGIA KATIKA MSIMU WAKO MPYA.
DAY 1
Mwl:MWAKASEGE
Yakobo 1:2-4
Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.”
Sasa nataka uone hiki kipengele kinachosema kujaribiwa kwa imani yenu”
Jaribu si jaribu mpaka likufikishe njia panda yaani mahali pa kuamua kusimama na hiyo imani au kuacha, usonge mbele au urudi nyuma. Kama hujafika njia panda basi bado hujakutana na jaribu ujue umekutana na chagamoto tu na sio jaribu.
Leo nataka tuangalie kwamba IMANI YAKO INAKUWA KATIKA HALI GANI INAPOJARIBIWA KATIKA MSIMU MPYA? Tutatazama kutoka kwenye uhusiano wa Hajiri na Ishmael kwa mtiririko ufuatao.
JAMBO LA KWANZA
1. MSIMU MPYA UNALETA KIPINDI CHA IMANI ZA WATU KUJARIBIWA AU KUPIMWA
Ukisoma Mwanzo 21:1-3,5-7 utaona kwamba kuzaliwa kwa Isaka kulileta kicheko. Lakini pia kulileta jaribu la imani kubwa sana kwa Ibrahimu, Sara, Hajiri na Ishmael. Kwa sababu ukisoma kwenye Biblia utaona ya kwamba Isaka alizaliwa wakati Ibrahimu akiwa na miaka 100.
Baada ya kusubiri mtoto kwa muda mrefu ilikuwa ni sahihi sana baada ya kupata mtoto wakapata furaha/kicheko. Lakini hawakujua ya kwamba ule ulikuwa ni msimu mpya kwao ambao ungewapitisha katika jaribu la imani ambalo hawakutegemea.
Hilo utaliona pale ambapo walipokuwa wanafanya sherehe ya kufurahia jambo. Maandiko yanatuambia Sara alimuona Ishmael akidhihaki na hapo hapo Sara akasema mfukuze mjakazi huyu na mwanae maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu Isaka” Sasa haya maneno Biblia inasema yalikuwa mabaya machoni pa Ibrahimu. Na wakati alikuwa akihangaika namna ile Mungu aliiingilia kati na kumwambia neno hilo lisiwe baya bali amsikilize mke wake katika kuwafukuza watoke pale nyumbani kwake.
Jambo hili lilikuwa zito sana kwa Ibrahimu maana ataanzia wapi kumfukuza Hajiri? Je kosa lake ni lipi? Kwa sababu Hajiri alikabidhiwa kwa Ibrahimu ili alale nae na Sara. Kwa hiyo kwa jinsi ya kibinadamu Hajiri hakuwa na kosa lolote. Maana wao ndio waliomuomba ili awasaidie kupata mtoto na pia si hivyo tu Ishmaeli alikuwa na miaka 13 wakati huo alikuwa ni kijana na ni mtoto aliyetoka kwenye kiuno cha Ibrahimu.
Sasa ilikuwa ni uamuzi wa Ibrahimu kumsikiliza au kutomsikiliza Mungu ili uhusiano wa Ibrahimu na Mungu na mkewe uingie katika shida. Kwa kumsikiliza Mungu ni kumsikiliza mke wake na kumfukuza Hajiri na mwanae.
Kwa hiyo unaona kabisa hakikuwa ni kitu chepesi kwa sababu unaona jaribu lile lile lilikwenda kwa Sara kwa namna nyingine. Kwamba anawezaje kumtazama msichana ambaye yeye ndiye aliyemuomba kumsaidia kuzaa mtoto na mumewe? Kwa hiyo hakikuwa kitu chepesi kabisa kwake. Mahusiano ya Sara na watu waliokuwa wakimsaidia kazi mbalimbali pale nyumbani kwake na wao mahusiano yao na Sara yaliingia kwenye shida.
Kwa upande wa Hajiri na Ishameli, Ishmaeli alitahiriwa akiwa na miaka 13 maana yake aliingizwa kwenye imani ya Mungu wa Ibrahimu. Kwa namna hiyo hiyo hata Hajiri naye aliingia kwenye imani hiyo hiyo kwa sababu alikuwa ndani ya familia ya Ibrahimu.
Sasa jaribu lililokuwa kwa Ishmael ni kwamba anawezaje kuendelea kusimama na imani ya baba yake wakati Mungu wa baba yake alitoa kibali cha yeye kufukuzwa nyumbani kwao?
Hapa unaweza kufikiri ni kitu chepesi lakini wao hawakujua kuwa kuzaliwa kwa Isaka ilikuwa ni kuashiria ya kwamba kuna msimu mpya uliongia kwenye maisha yao yaani Ibrahimu, Sara, Hajiri, Ishmaeli na Wayahudi wote.
Na unaposoma kwenye maandiko ndipo unakuja kugundua ya kwamba ule ulikuwa ni mlango wa ugomvi mkubwa kati ya Isaka na Ishmael ambao wanagombana mpaka leo. Esau pacha wake na Yakobo alipoona mzee Isaka anamwelekeza namna ya kupata mke kwamba kwenda kule nyumbani kwa ndugu zao kwa Labani, Esau yeye hakupewa hayo maelekezo. Kwa hiyo Esau alijitafutia tu mke na Biblia inasema alienda kuoa kwa Ishmael.
Sasa fikiria tu ugomvi ambao Ishmael tayari anao na Isaka halafu mtoto wake ameenda kuoa kwa adui? Na kati ya uzao wa Esau ni Waamaleki waliokuwa wapinzani wa kwanza wa kivita wa wana wa Israel wakati wakitoka Misri kwenda Kaanani.
Lakini hata sasa Dunia inapita kwenye majira mapya, imani za watu zinapita kwenye majaribu makubwa sana. Msimu mpya ulianza mwaka 2019 mpaka sasa 2020, bado unaendelea. Na katika msimu huu mpya imani za watu wengi sana zimeyumba kutokana na mabadiliko hayo.
Turudi sasa kwa Ishmaeli, Ishmaeli alipewa baraka lakini nje ya agano. Maana yake Ishmaeli alinyimwa ardhi kwani ardhi iliyoko Israeli ni ya Isaka ndio maana hata Ibrahimu alipokufa urithi alipewa Isaka na watoto wa masuria walipewa vizawadi tu, hakuna aliyepewa ardhi.
JAMBO LA PILI
2. UNAHITAJI NENO LA MUNGU LA KUTOSHA ILI LIKUVUSHE KATIKA KIPINDI CHA KUJARIBIWA IMANI YAKO
Soma Mwanzo 21:14-16 na Mathayo 4:4
Fikiria ukiwa katikati ya kujaribiwa na unaletewa neno la faraja linalosema. Unapokula chakula kwa ajili ya kutunza mwili wako, kula na chakula kwa ajili ya kutunza imani yako. Kwa sababu mtu hataishi kwa mkate tu, bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
Ibrahimu aliambiwa awafukuze Hajiri na kijana wake Ishmaeli. Kumbuka hawa watu walikuwa wanamtegemea Ibrahimu kwa kila kitu maana hawakuwa na shamba au hela au mahali pa kwenda wakati ule.
Lakini Ibrahimu aliwafukuza na akawapa chakula na maji kidogo ili kiwasaidie njiani. Lakini tunaona ya kuwa wakiwa katika safari kuelekea wasikokujua. Kumbuka Ishmaeli alikuwa ni kijana wa miaka 13 wakati ule lakini akiwa katika safari alianza kudhoofika kiafya na Hajiri akamlaza chini ya kijiti. Ili asimwone mtoto wake akifa. Huenda walikuwa na maswali mengi kwa Mungu kuwa kwa nini hakumwandaa Hajiri mapema kama anajua atapitia mazingira hayo?
Unapopita kwenye kipindi kigumu hata baadhi ya mistari ya Biblia inakuwa taabu kutamka mfano ile Zaburi ya 23 ya “Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu…”
Huenda Ishmaeli alikuwa anatafakari shuhuda za Mungu wa baba yake namna alivyomsaidia tangu akiwa Uru ya Wakaldayo lakini sasa yeye yupo Jangwani anaelekea kufa kwa kwa kukosa maji wakati baba yake ana visima vya maji.
Inawezekana na wewe unapitia katika majira ya namna hii, Mungu anazungumza nawe kwa lugha iliyo nyepesi kabisa, hakikisha unapata chakula cha kutosha cha neno la Bwana ambacho kitakusaidia katika kipindi usichotarajia.
Mungu akitaka kukulisha kwa ajili ya safari, hakulishi tu safarini, bali anakulisha pia kabla ya safari na anakupa na chakula cha njiani.
Hajiri na Ishmaeli walipewa chakula cha njiani lakini kilikuwa hakitoshi na kiliisha mapema na pia hata mwilini mwao namo kiliisha.
Mungu anapokuletea neno katika maisha yako, usifikiri anakosea. Wengine wakipewa neno kama hilo kwa sababu kwa muda huo hawalihitaji wanalitupa. Hii ni sawa na kipindi cha Nuhu na watu wake ambao hawakutii neno la Mungu la msimu maana walikuwa hawaoni kama gharika itakuja.
JAMBO LA TATU
3. KATIKATI YA KIPINDI CHA KUJARIBIWA KWA IMANI YAKO USIPOTEZE MWELEKEO WA NJIA UNAYOPASWA KUIENDEA
Mwanzo 21:14
Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba.”
Ile kupotea ni kama vile mtu anaenda msituni au jangwani bila kujua anakoenda. Hata kwako katikati ya kujaribiwa kwa imani yako, usipoteze mwelekeo wa njia inayopaswa kuindea.
Waebrania 12:2-3
tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.”
Hapa anatupa jibu kuwa Eliya alichoka, akazimia moyoni mwake,maana yake alikata tamaa. Ndio maana aliomba aondolewe Duniani.
Pia tunamwona Eliya akipewa chakula na maji na Mungu kupitia Malaika, Eliya akala na akalala. Malaika akamwamsha mara ya pili akamwambia amka ule , unywe kwa sababu safari yako bado ni ndefu. Biblia inasema alienda na kile chakula kwa siku 40, kwa hiyo ilikuwa ration ya siku 40, lakini 40 ya Biblia ni nyingi na akafika mahali Mungu akamsemesha tena. Lakini kinywa cha Eliya kilikuwa bado kinalalamika kuwa nimebaki mwenyewe.
Ni hatari sana kula chakula cha Bwana ambacho hujui kazi yake ni nini. Pia usile chakula cha Bwana kwa sababu tu unanjaa. Maana unaweza ukala chakula chochote na popote, ndio maana Biblia inasema kutakuwa na njaa siku za mwisho. Maana neno ambalo litalokufaa wewe kuwa chakula litakuwa halipatikani.
Mtu yule ambaye anamjua Bwana hatakula chakula chochote kwa sababu tu ametindikiwa au yupo katika hali ngumu. Yesu alipita mahali pangumu kuliko unapopita wewe lakini aliiitazama furaha atakayoipata baada ya kustahimili msalaba na imani yake kwa Mungu ikawa thabiti.
Unapoangalia furaha uliyonayo utakapokufa ya kuwa utakaa na Bwana milele na milele! Haijalishi majaribu unayopitia huwezi kumwacha Bwana. Wakati unatazama utakuwa unatafakari habari za ukuu wake usije ukachoka wala kukata tamaa njiani.
Mama mjamzito hawezi kula chakula chochote kwa sababu ya njaa bali atakula chakula ambacho mtoto anakihitaji huko tumboni. Sasa kwanini unataka kula chakula chochote tu kwa sababu ya njaa? Ndio maana nakuambia katikati ya kujaribiwa kwa imani yako usije ukapoteza mwelekeo au ukaacha kitu ambacho Mungu kakupa kufanya. Ukifanya hivyo utashangaa unaishia jangwani na Kaanani haufiki.
Kuna watu wengi ambao wamepotea, kwa jinsi ya kiroho na kimaisha. Maana utamuona mtu hajui alipotokea, alipo na anakoelekea, hata ukimwambia rudi nyumbani hawezi kurudi.
JAMBO LA NNE.
4. JARIBU LA IMANI LINAWEZA KUKUTENGANISHA NA IBRAHIMU WAKO LAKINI LISIKUTENGANISHE NA MUNGU WAKE KATIKA YESU KRISTO.
Ibrahimu alikuwa ni mzazi mwenzake na Hajiri kwa mtoto wao Ishmael. Kwa jinsi ya kiroho alikuwa baba yao wa imani na mlezi wao. Pia Hajiri alikuwa ameajiriwa na Ibrahimu, kwa hiyo alikuwa ni mfanyakazi wake, alipozaa mtoto naye wakaingia kwenye undugu.
Jaribu la imani katika msimu mpya ni jaribu la ajabu sana kwa sababu linaweza kukutengenisha na Ibrahimu wako na ukashangaa Mungu akasema sawa. Katika ile hali ya kutenganishwa kwao akawapa chakula cha mwisho ili waondoke pale nyumbani kwake. Pia unakuja kuwaona wakati Ibrahimu akigawa mali za urithi akiwa hai. Pia ukisoma Biblia utaona kuwa baada ya Sara kufa Ibrahimu alioa mke mwingine aliyeitwa Ketura na alizaa naye watoto watano. Katika mazishi yake ya Ibrahimu Hajiri, Ishmaeli, Ketura na watoto wake pamoja na Isaka walikuwepo. Swali linakuja Ishmaeli na Hajiri waliwezaje kurudi kumzika Ibrahimu wakati aliwafukuza?.
Wakati mwingine Msimu mpya unadai watu waweze kukaa mbali kwa ajili ya kupanua kitu. Lakini unahitaji kumjua Mungu na kusikiliza anachosema la sivyo kitakuwa ni kigumu sana kwako. Maana litakuwa ni jaribu sana kwako badala ya kuwa mahali pa kupitia.
Wakati mwingine Mungu anataka ukue kwa sababu huwezi kusimama mahali kisa Ibrahimu wako amesimama je akizama utazama naye? Kukua katika imani maana yake Ibrahimu wako akiyumba unamwimarisha na kumtegemeza kwa njia ya maombi.
Kama umemuweka Ibrahimu kama mungu wako basi ujue ukiingia katika msimu mpya kuna kitu kitaingia katikati na kuwatenga. Sasa haijalishi Ibrahimu anatenganishwa na wewe kwa muda mrefu au mfupi ila hakikisha hutengani na Mungu wake aliyekupa nafasi ukamjua katika Kristo Yesu.
Kwa hiyo usimuache Yesu kwa sababu mwajiri wako aliye kuongoza kwa Yesu ndiye anakupunguza sasa kazini. Maana ni rahisi sana ukajiuliza kuwa inakuje mtu huyu ananiondoa kazini kama mtu ambaye hanifahamu kwa hiyo hata Mungu wake simtaki.
Ukifika mahali pa namna hiyo usikate tamaa bali imarisha imani yako katika Kristo Yesu. Ndio maana unaweza kuta wazazi wako wanakulea vizuri ili umjue Yesu lakini wakifa na imani yako inakufa pia. Kwa sababu uliweka imani yako kwa wazazi wako badala ya Mungu wa wazazi wako.
Kwa mfano msimu mpya unakuja kwako na Mchungaji wako anahamishwa lakini wewe kwanini unazira kwenda kanisani kwa sababu Mchungaji wako kahamishwa?. Sasa hapo unaacha unazira kumtumikia Mungu kwa sababu Mchungaji kahama.
Ukisoma habari za Ibrahimu wakati walipoambiwa amwondoe Ishmael nyumbani kwake hatuoni mahali akimsindikiza. Lakini Mungu akitaka imani yako iweze kusimama anakuchukua kama mtoto wa Tai 🦅 (Eagle) anavyochukuliwa katika viota vyao vizuri ambavyo huwa vinatengenezwa na miiba na manyoya ili viwe na joto ili wakae vizuri.
Viota vya Tai ni vizuri sana maana huwa na joto zuri sana ambalo linavifanya vile vitoto vya Tai vijisahau hata kujifunza kuruka vikikua kwa sababu tu viota vyao ni vizuri.
Mama yao anachofanya kuna wito ambao anawaita ili waweze kwenda juu yake ili akawafundishe kuruka. Sasa huwa hawataki kutoka kwa hiyo anaanza kutoa manyoya katika kiota ili ibaki miiba tu iwachome.
Sasa baada ya hivyo akiwaita tena kwa lugha yake huwa wanaruka haraka sana kwenda juu ya mabawa ya mama yao. Maana wanajua wakiendelea kubaki kwenye kiota kuna miiba itawachoma.
Sasa Tai akiwachukua pale anaruka nao mpaka juu sana. Na akifika huko juu anajipindua alafu akifuatilia kifaranga chake ili kisije kikadondoka mpaka chini. Kwa hiyo anakifanyisha zoezi mara mbili au tatu alafu anakirundisha kwenye kiota chenye miiba. Sasa utaelewa jinsi ambavyo kitakuwa kinasubiri muda wa kuruka maana angalau ndipo kinapata raha maana kwenye kiota sasa kuna miiba tu yale manyoya hayapo tena.
Sasa kwanini na wewe unataka Mungu akufanyie na wewe kama hivyo kukuwekea miiba ili ujifunze na kuruka?
JAMBO LA TANO
5. USIMKASIRIKIE MUNGU ANAPOSIKILIZA SAUTI YA KILE KILICHOBEBA BARAKA ZAKO KULIKO SAUTI YA MAOMBI YAKO.
Hii utaipata katika Mwanzo 21:14-19
soma hiyo mistari ila hapa tutaangalia
16-19
Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko.Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana.
Kumbuka nimekuambia kuwa jaribu la imani linaweza likakutengenisha na Ibrahimu wako. Ishmaeli na Hajiri walijua kabisa na Mungu wa Ibrahimu pia kawaacha. Maana Mungu alimwambia Ibrahimu mkubalie mke wako mfukuze Hajiri na Ishmaeli.
Sasa fikiria Ibrahimu anaulizwa na Hajiri anamuuliza je nimekukosea nini?.
Pia fikiria Ishmael anamuuliza baba yake kuwa je nimekukosea nini?
Halafu unanifukuza ili niende wapi?
Maana wewe ni baba yangu. Ibrahimu huenda akajibu kuwa mama yako mkubwa kasema mwana wa mjakazi hatarithi kama mwana wa muungwana yaani Isaka.
Ishmaeli anaweza akajibu akasema kama ni hivyo baba urithi sitachukua basi naomba nipeleke tu shule basi ili inisaidie. Na je huko ntakakoenda nani atanisaidia maana sikujui hata ninakokwenda?.
Ibrahimu huenda alijibu kwa kusema unajua Mwanangu yule Mungu ambaye nilikutambulisha kwake na ukatahiriwa naye kakubaliana na mama yako mkubwa kuwa na wewe uondoke. Na kaniambia nimtii anachosema. Ingekuwa ni mimi ungebaki ila Mungu kasema nimtii. Kwa maana hiyo Ishmaeli angesema ina maana Mungu naye kanifukuza? Ibrahimu angesema kabisaa ndio mwanangu.
Sasa fikiria wanaenda kule ambako wanaenda baada ya kufukuzwa na hawatagemei kama watakutana Mungu njiani.
Lakini kumbe Mungu yuko pale nao njiani.
Wakati Mungu alipokuwa anamsemesha Ibrahimu kuwa atazaa mtoto yeye alisema mimi ni mzee na mke wangu ni mzee. Mtumie Ishmaeli maana yuko hapa. Mungu alikataa akisema agano langu ntalifanya imara kupitia Isaka ambaye atakuja mwakani majira kama haya. Ila kwa sababu umeomba basi kumbariki ntambariki Ishmaeli lakini nje ya agano. Ina maana kuna kitu alibeba cha Mungu na Mungu hakutaka kife kirahisi. Maana kikifa ina maana na ushuhuda wake unapotea.
Hajiri hakujua kuwa baraka na msaada wa maisha yake ya baadae kuwa umefichwa ndani ya Ishmaeli. Wakati anamtelekeza Ishmaeli alikuwa anaweka mbali baraka zake. Maana ilimretea jaribu maana huenda angekuwa anasema "Ningekuwa na uwezo wa kumrudisha mtoto huyu tumboni ningemrudisha kabisa ila sasa sina namna".
Ukisoma biblia utaona kuwa Hajiri alipokaa mbali na mtoto wake alilia sana. Mungu alisikia kilio cha sauti ya kijana na sio maombi ya mama yake. Je umewahi kufikiri umeomba na kufunga unaona Mungu kama amenyamaza kabisa. Alafu baada ya muda kidogo anakujibu kuwa amesikia kilio cha mtoto wako.
Hapo unaweza ukamuuliza kuwa je ina maana Mungu umemsikiliza mtoto wangu badala yangu ina maana huyu mtoto kanizidi hali ya kiroho?
Umewahi kufikiri kuwa huenda kuna mahali pagumu unapita na unaamua kuacha na kutelekeza baraka ambayo Mungu kakuwekea kwenye kazi au mtu. Yaani kwa sababu tu ya mahali unapopita unaitelekeza baraka yako? Unasahau kuwa Mungu ndiye kaweka mbegu yake hapo, japo wewe unaona kama inakufa lakini kumbuka kuwa itachanua.
MAOMBI: Kwa wale ambao Wameacha vitu mbalimbali na kukata tamaa kwa sababu ya msimu mpya ili Mungu awatie nguvu kwa upya.
DAY 2
Leo nataka kuzungumza na wewe juu ya NAMNA YA KUTAMBUA WAOMBAJI WANAOWEZA KUYUMBISHA NA KUPOFUSHA IMANI YAKO KATIKA MSIMU WAKO MPYA NA UJUE CHA KUFANYA
Kwa kuangalia na kujifunza jambo hili tutaangalia mtiririko wa mambo mawili yafuatayo ambayo yatakuwa na mifano ndani yake:-
JAMBO YA KWANZA
1. KUNA UHUSIANO KATI YA MSIMU WAKO MPYA NA KUJITOKEZA WATU WA KUKUOMBEA
Mara nyingi utakapoingia katika msimu wako mpya utakuwa na msukumo wa kuomba sana na si kidogo. Na kwa wale ambao hawajui msukumo wa kuomba ni kwamba watasikia ndani yao kuna mzigo au mahangaiko fulani ni kama vile kuku anayetaka kutaga yai.
Na hii ni hali ya ki-Biblia kabisa wala usije kushangaa kwa sababu katika msimu mpya Mungu anaachilia kitu kipya, ngazi mpya, mawazo mapya, mipango mipya. Na kwa sababu hiyo huwa anaweka waombaji ambao watasimama pamoja na wewe kuhakikisha ya kwamba wanakusaidia kuomba. Na saa nyingine Mungu anaweka maombi ndani yako yatakayokusaidia kuomba ili Mungu aweze kukusaidia kujua njia ya kupita na kujua mikakati ya kutembea ndani yake na ili uweze kupita mahali palipo nyooka.
Lakini tatizo lililoko wala si jipya maana lipo ndani ya Biblia, huwa wanainuka waombaji kipindi hicho hicho ambao badala ya kuwa msaada kwako wanakuwa kikwazo. Na si watu wengi sana wanajua namna ya kuwatambua waombaji ambao wanakuwa vikwazo kwao. Na Mungu alipokuwa akinisemesha amenipa vitu vichache hivi niviachilie kwako maana wako wengi waliokwama na wapo ambao muda mchache wanaweza kukwama.
Ngoja nikupe aina chache kama mifano juu ya jambo hili la kwanza ili uweze kuona mahusiano hayo lakini ikilenga zaidi juu ya waombaji ambao wanaweza kuyumbisha na kupofusha imani yako katika msimu wako mpya na ujue cha kufanya:-
AINA YA KWANZA
I. WAOMBAJI WANAOTUMIA TATIZO ULILOWASHIRIKISHA KUKUNYIMA UHURU WA WEWE KUKUA KATIKA NEEMA YA KRISTO NA KATIKA NGUVU ZAKE
Soma 2Wakorintho 12:7-10 na ile 2Wakorintho 1:8-11 unganisha na Warumi 15:30-33 Hapa nataka uone ya kwamba kati ya waombaji ambao Mungu alikuwa amemuinulia Paulo kwa ajili ya kumuombea walikuwa wengi. Lakini kuna waombaji waliokuwa katika kanisa la Korintho na kanisa la Rumi walikuwa na kitu cha tofauti kidogo kuliko waombaji wengine. Kwa sababu Paulo alijifunua moyo wake kueleza matatizo yake na udhaifu aliokuwa nao na upinzani aliokuwa nao kwa namna ambavyo si watumishi wengi sana wanaweza kusema.
Paulo angekuwa anajua ya kwamba hizi Nyaraka zitasomwa mpaka leo kuna uwezekano mkubwa sana kuwa kuna mambo mengine angeweza kutokuandika kabisa. Aliandika akilenga wapendwa wake yaani watu ambao alikuwa anashirikiana nao na kule Korintho walikuwa wakishirikiana naye kwenye maombi alipokuwa akipita mahali pagumu. Pia hata alipokuwa na udhaifu ndani yake napo aliandika. Lakini hata shetani alipokuwa akipambana naye maandiko yanatumbia alikuwa akiwaandikia ili waweze kuomba kwa ajili yake.
Ukisoma hiyo mistari utaona habari ya mwiba ambao Paulo alikuwa nao yaani mwiba wa shetani. Na kumbuka Paulo ni mtumishi wa Mungu hakuficha na aliamua kuwaambia ukweli. Na kitu kingine ambacho ni kigumu alichowaambia ni kwamba alimuomba Yesu mara tatu lakini alimnyamazia kwa namna ambavyo hakutaka kuuondoa ule mwiba wa shetani na kumsemesha kitu kigumu sana kumwambia “Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu.”
Sasa wale kuna waombaji ambao walijua udhaifu wake na mahali alipokwama na shetani alipompiga. Pia walijua hata huduma yake wapi ilipokuwa ikikubalika na ilipokataliwa pia.
Sasa hao waombaji ambao waliokuwa wakijua vitu vyote kumhusu kwa lugha ya sasa naweza kusema ni rahisi sana wakachukua hayo matatizo na uwezo wake wa kutokuomba mwenyewe na kutafuta namna ya kumbana. Watambana kwa namna ambayo bila yeye mwenyewe kujua na kidogo kidogo wanamnyang’anya uwezo wa imani yake kusimama na kujikuta anategemea imani yao. Na ghafla imani yake inakosa kazi.
Na sasa kama ni wewe kwa wakati huu kupitia mfano huo wa Paulo imani yako inakosa kazi. Ikikosa kazi ni mahali pabaya sana na ukitaka kujua ya kwamba imekosa kazi utashangaa na utaona tu kuna mwingine hawezi kula mpaka mwombaji amesema. Pia kuna wengine huwa wanaenda mbali zaidi na kufika mahali pa kuwachagulia watu aina ya chakula. Hata kwenda kanisani ni mpaka mwombaji amwambie nenda ua usiende. Wakati mwingine wanaweza kukuchagulia mpaka kanisa la kusali hata kukuchagulia mke kama wewe ni kijana.
Au waombaji wa namna hii wengine wakiingia kwenye ndoa wao wanakuja kuingia katikati kushikilia hizo ndoa ziendelee, wanakuwa kama Yesu kwa kuzibeba hizo ndoa. Wengine wanabana hata muda wako, matumizi ya fedha (kutoa sadaka hata matumizi ya nyumbani kwako) wanakubana kwenye kila kitu unachotumia.
Paulo aliwaombea watu wakue katika fahamu zao lakini hawa ambao wanatengeneza utegemezi kwao, siku ukitindikiwa utafanyaje? Hiyo hali ikikukuta katika msimu wako mpya utafanyaje ili utoke hapo. Badala umuulize Mungu unabaki kumwuliza mwombaji wako.
Mungu anakuambia ili ufanikiwe ufanye mambo kadhaa, sasa unasema ngoja uende ukamwulize mwombaji wako halafu unarudi kwa Mungu kuwa mwombaji anasema aliyemsemesha sio Mungu. Hii yote ni kwa sababu umeweka imani yako pembeni na humtambui Mungu kwa jinsi anavyojifunua kwako kupitia neno lake kiasi ambacho unategemea mtu mwingine mwishoni anaweza kusababisha kuua huduma yako au watabeba wao kwani utajikuta hauwezi ukabeba hiyo huduma.
Ukiona hali kama hiyo fanya yafuatayo;-
i). Itisha/simamisha damu ya Yesu katikati yenu.
Au kama unamfahamu mtu wa namna hii omba damu ya Yesu iwatenganishe (huyo mtu na huyo mwombaji) uhusiano huo ufe kabisa. Baadaye wataona huyo mtu akifanikiwa haraka.
ii). Usiwashirikishe mambo yako.
Kwa maana wamegundua ya kwamba kila ukiwaeleza tatizo lako wao wanachukua kama mtaji. Baadaye waone tu mafanikio yako, na hata wakijaribu kubomoa tena, wewe simama katika damu ya Yesu lazima watashindwa tu. Wakilaani mafanikio yako, wewe bariki mafanikio yako kwa sababu siku iliyobarikiwa haiwezi kulaaniwa.
iii). Acha kuomba nao.
Ukiona unatamani kuonana nao jikaze tulia uombe mwenyewe.
iv). Omba Mungu akuinulie watu wengine wa kushirikiana nao.
Mungu anao uwezo wa kukupatia wengine watakaosimama pamoja nawe na kwa ajili yako.
AINA YA PILI
II. WAOMBAJI ULIOWATAFUTA WEWE WAKUOMBEE LAKINI SI MUNGU ALIKUPATIA WAKUOMBEE ILI WAZO ALILOKUPA MUNGU LIZALIWE NA LIFANYIKE
Ukisoma Wagalatia 4:19 Paulo anasema watoto akimaanisha aliwaombea kiasi ambacho mpaka walizaliwa ndani ya Kristo. Pia jinsi alivyowakuta hakupendezwa nao kwa sababu alijua Kristo hajaumbika ndani yao ndipo akaomba tena kwa utungu ambao Mungu aliuweka ndani yake ili kuzalisha wazo na mpango wa Mungu.
Mara nyingi Mungu anainua watu watakaosimama kwenye maombi ya namna hii. Mfano wake kwenye Biblia ni nabii Ana aliyekaa hekaluni mchana na usiku akiombea Yesu azaliwe kwani ilikuwa wazi na alishasoma (agano la kale) kwenye vyuo, manabii, torati, Zaburi. Mungu alimwinua yule mama aendelee kuomba bila kujua Mariamu aliko ila tu alijua kuna mtu kabeba huo ujauzito. Aliomba mpaka kile yule mtoto alipozaliwa. Sasa Mungu anaweza akakupa mwombaji mmoja au waombaji wengi. Sasa ubaya ni pale unapotafuta waombaji wengine bila msaada wa Mungu na wanakuja kukuingiza mahali pagumu sana.
Mfano wa Ibrahimu na Sara, Ukisoma Mwanzo 12:1-2 na ukiunganisha na Mwanzo 16:1-4 Utaona Mungu alimwambia Ibrahimu kuwa atakuwa baba wa mataifa wakati huo kabla ya Isaka kuzaliwa.
Sasa Mungu alikuwa anaona picha ya Isaka ndani ya Ibrahimu na alikuwa anamwona Yesu ndani ya Isaka, na kupitia Isaka ndipo sisi tunakuja kuzaliwa kwa kumpokea Yesu Kristo ambaye hilo wazo lilipitia ndani ya Ibrahimu (baba wa mataifa). Kwa lugha ya sasa hivi tungesema Ibrahimu na Sara walikuwa wanatafuta mwombaji atakayebeba hilo wazo Mungu alilowapa.
Si kila mwombaji amepakwa mafuta kuombea kila kitu, si kila mwombaji amepakwa mafuta kuombea kila wazo ulilonalo. Mungu ana namna ya kuwanyanyua watu na kuwaweka mahali na kuachilia maombi waweze kuomba. Saa nyingine ni vigumu sana kuwatambua unapopita mazingira kama ya Ibrahim aliyopitia na Sara. Kuna wakati wanaojitokeza ni wale walio karibu yako au kazini kwako au kanisani kwako. Kwa hiyo jifunze kumwaomba Mungu ili kama ni Mungu amekupa wazo, jifunze namna ya kwenda na kumuuliza Mungu hili wazo nimshirikishe nani na nani ambaye amempaka mafuta aweze kuomba pamoja nami.
Ukiwa na waombaji kama Hajiri mara nyingi hawapewi nguvu ndani yao ya kuhakikisha ya kwamba amekuombea mpaka mwisho. Hajiri aliweza kupata mtoto lakini inategemea kama wazo alilokupa Mungu lina muda mrefu au linapitia mahali pagumu watu wengine wanaacha kuomba, hawana nguvu ya kukusukuma uendelee kuomba, kwa sababu kile kilichoko ndani cha kuendelea kuomba hakina muunganiko na kile kilichoko mbele.
Inapofika mahali pa namna hiyo jifunze kumsikiliza Mungu. Maelekezo hayafanani bali fuata anachokuelekeza Mungu kwa kufuata amani ya Kristo ambayo inaamua ndani yako.
AINA YA TATU
III. WAOMBAJI WANAOTUMIKA KUTAKA KUKIANGAMIZA KILE WALICHOKIOMBEA KIKAZALIWA
Ukisoma Kutoka 1:15-16 Unaweza ukachukua huu mfano wa wazalishaji kuwa waombaji ambao wanafanya kitu ulichobeba kizaliwe. Sasa fikiria hawa ni waombaji na ghafla wazo la shetani linakuja ndani yao na kugeuza fikra zao na wanaingiwa wazo la kutaka kuua kile kitu ambacho kilizaliwa.
Kumbuka hili kuwa kuna wazaliwa wa agano ambao Mungu huwa habadilishi tu. Maana anasema kabla sijakuumba katika tumbo la mama yako nalikujua na kukutakasa. Watu wa namna hii ina maana Mungu anaingia gharama hata kabla hawajatungiwa mimba.
Sasa fikiria imani za Waebrania zingekuaje juu ya Mungu wao katika mazingira ya namna hiyo. Tuna waombaji wa namna hiyo ambao wanaanza vizuri kuomba ila baada ya muda wanabadilika.
NAMNA YA KUWATAMBUA WAOMBAJI AMBAO WALIANZA VIZURI NA SASA WAMEBADILIKA
1.Ghafla wanakuwa na hasira na kitu ambacho Mungu aliwatumia wakakiombea na kikazaliwa.
2.Utagundua kuwa kidogo kidogo wameanza kushirikiana kukuhujumu na wale watu ambao hawapendi mendeleo yako.
3.Hawana stamina ya kukaa na wewe unapopita katika shida wanakuwa kama Petro wakati ule wa Yesu.
Wakati ule Yesu alikuwa na waombaji watatu. Yaani Petro, Yohana na Yakobo. Hawa ndio waombaji alipanda nao mlimani kuomba alipogeuka sura na pia hawa hawa alienda nao katika Bustani ya Getsemane.
Lakini Yesu alipopita kwenye shida Petro alimkana Yesu na kukimbia. Waombaji ambao Mungu kakuinulia kwa ajili ya kukufunika unahitaji kuwatazama vizuri maana kuna wakati wanaweza wanaingiliwa na shetani kama Petro. Maana yake shetani alipata nafasi ndani ya Petro na Petro alimkana Yesu na kumkimbia, lakini yale maombi yakamrudisha.
HATUA ZA KUCHUKUA SASA UNAPOKUTANA NA WAOMBAJI WA NAMNA HII
1.Waombee waombaji wako ili wawe na hofu ya Mungu.
2.Waombee wakeshe katika sala ili wapate nguvu za kuomba.
3.Jiombee wewe uhodari na nguvu ili ikibidi waombaji wakiwa wamekuacha basi uombe wewe mwenyewe mpaka uvuke.
Soma Waefeso 6:10-11, Kutoka 1:15-21
JAMBO LA PILI
2. OMBA KWA JUHUDI MUNGU AKUPE WAOMBAJI AMBAO WATAKUOMBEA KWA JUHUDI KATIKA MSIMU WAKO MPYA NA AKUPE KUWATAMBUA.
Kwenye Luka 6:12-16 Hapa anaposema aliwaita wanafunzi wake sio wote 12. Maana kuna wanafunzi wake kati ya hao ambao wanaitwa mitume. Lakini Mungu alimpa watatu yaani Petro,Yakobo na Yohana kama Waombaji wake. Pia Yohana alikuwa ndio Msiri wake. Yote haya yalitoka kwenye maombi ya Yesu.
Kwa hiyo jifunze na wewe kuomba ili Mungu akuinulie watu sahihi ambao watasimama na wewe katika kuomba kwenye msimu huu mpya.
Maana kama ni wazo la msimu mpya Mungu kakupa ujue kuwa huwezi ukalibeba peke yako bali unahitaji watu wawili watatu ambao watasimama pamoja na wewe katika kuomba.
Watu hawa hawapatikani tu kwa kuwanyanyua bali kwa kuomba. Ukisoma kitabu cha Yohana 17 utaona ya kuwa Yesu anasema “Baba wale watu ulionipa”. Hawa watu alipewa na Mungu katika ile Luka 6 akiwa katika maombi.
Yesu alipewa watu ambao walikuwa katika wale wengi ambao walikuwa wanamfuatilia mara kwa mara lakini aliweza kuwatambua na akawapa majina. Katikati ya waombaji walikuwepo na mitume. Kwa hiyo hata kwako Mungu pia anaweza akakupa waombaji na akakuambia yule unayeweza kumshirikisha vitu ambavyo huwezi kuwaambia watu wengine. Ndio maana nimesema kuwa omba Mungu akupe kuwatambua.
DAY 3
Bwana Yesu asifiwe sana, baada ya kutazama Namna ya kutambua waombaji wanaoweza kuyumbisha na kupofusha imani yako katika msimu wako mpya na ujue cha kufanya Leo nataka nizungumze na wewe juu ya KUJIFUNZA KUUNGANISHA IMANI YAKO NA NGUVU ZA MUNGU
Kama hujapata somo la kipindi kilichopita basi jiunge katika kundi letu la Telegram ili uwe unapata masomo haya. Angalia link hapo juu bonyeza na kaangalie ndani nilipokuwekea link ya telegram na bonyeza ili uwe unafuatana nasi katika semina mbali mbali .
Leo tutajifunza jambo hili kwa mtiririko wa mambo yafuatayo:-
JAMBO LA KWANZA
IMANI YAKO NA NGUVU ZA MUNGU VINAHITAJIANA ILI UPATE MSAADA WA MUNGU
Na huu msaada wa Mungu inategemea wewe unao uhitaji maana wakati mwingine inawezekana ni kufanikiwa kimaisha au kufanya mapenzi ya Mungu au kutimiza kusudi Mungu au kufanikiwa kwenye msimu mpya kama sasa au unataka kupokea uponyaji katika mwili wako.
Marko 5:25-34
“Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule. Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu? Wanafunzi wake wakamwambia, Je! Wawaona makutano wanavyokusonga-songa, nawe wasema, Ni nani aliyenigusa? Akatazama pande zote ili amwone yule aliyelitenda neno hilo. Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote. Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena.”
Nataka nikuonyeshe mambo machache hapa kama manne hivi kutoka kwenye hii mistari.
Jambo la Kwanza
I. HUYU MWANAMKE ALIKUWA NA IMANI, PIA ALIKUWA NA UGONJWA KWA WAKATI MMOJA NA IMANI YAKE HAIKUMSAIDIA KUPONA UGONJWA WAKE.
Katika Marko 5:27 Biblia inasema “aliposikia habari za Yesu”.... Ina maana alisikia habari za Yesu akiwa anaumwa na kule kusikia zile habari alipata imani ndani yake. Kwa hiyo kilichomsukuma kwenda kwa Yesu ni imani aliyoipata baada ya kusikia japo alikuwa ni mgonjwa. Na hii ni kwa sababu imani huja kwa kusikia neno la Kristo na sio kwa kumuona Yesu.
Hivyo kwa jinsi ya ki-Biblia alikuwa na imani lakini pia alikuwa mgonjwa. Kwa sababu kama imani peke yake ingekuwa inamwezesha kupona basi pale aliposikia habari za Yesu basi angepokea uponyaji wakati ule ule.Maana tunaona Yesu akimwambia kwenye ule mstari wa 34 kwamba “Binti, imani yako imekuponya” ni imani yake ndiyo iliyomponya na si imani ya Yesu. Kumbuka leo tunajifunza KUUNGANISHA IMANI YAKO NA NGUVU ZA MUNGU
Jambo la Pili
II. YESU ALIKUWA NA UPAKO WA KUPONYA LAKINI SI KILA ALIYEMGUSA ALIVUTA UPAKO ULE
Na hili tunajua pale ambapo wanafunzi walipomshangaa sana Yesu alipouliza ni nani aliyemgusa mavazi yake. Wanafunzi walimwambia kuwa anaona makutano walivyomsonga sasa anasemaje kuna mtu kamgusa mavazi yake. Sasa Yesu hakuwa akizungumzia mguso wa mikono ya watu bali alikuwa akizungumzia mguso wa imani.
Jambo la Tatu
III. NI MPAKA YULE MWANAMKE ALIPOMGUSA KWA IMANI NDIPO NGUVU ZIKATOKA KWA YESU NA KUINGIA MWILINI MWAKE NA KUMPONYA
Na hii ni kwa sababu unaona kabisa maandiko yanatuambia kwamba “Naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule” kwa hiyo alipona msiba aliokuwa nao kwa njia ya imani. Kwamba kuna kitu alichokifanya ambacho is kilisababisha kuunganisha imani yake na nguvu iliyokuwa ndani ya Kristo.
Jambo la Nne
IV.ILIBIDI IMANI NA UPAKO (NGUVU ZA MUNGU ZILIZOKUWA NDANI YA YESU) VIKUTANISHWE INGAWA VYOTE VILIKUWA ENEO MOJA
Vyote vilikuwa eneo moja lakini bila kuviunganisha yule mama asinge pata msaada. Kwa hiyo unaweza ukawa na imani kwenye upande mmoja na unaweza ukawa na upako kwenye upande mwingine na vyote visikusaidie pamoja na kwamba vyote vipo mahali pamoja.
Waebrania 11:31
“Kwa imani Rahabu, yule kahaba, hakuangamia pamoja na hao walioasi; kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi kwa amani.”
Hizi habari ziliandikwa baada ya huyu dada kuacha ukahaba na kuhamia kwenye kabila la Waebrania. Mwandishi anaposema “Kwa imani Rahabu, yule kahaba,...” anamaanisha ya kwamba Rahabu alikuwa ana imani na alikuwa kahaba kwa wakati mmoja. Rahabu alipata hii imani kwa kusikia soma Yoshua 2:8-12
Ukisoma hapo, kwenye mstari wa 10 anasema “tumesikia” na mstari wa 11 anasema “tuliposikia” na mstari wa 9 anasema “mimi najua….” Hajasema sisi tunajua. Sasa maandiko yanasema kwa imani twafahamu (Waebrania 11:3) kwa hiyo ufahamu ukiingia, imani imeingia.Katika habari za Rahabu na watu wa Yeriko waliosikia ni wengi lakini waliopata imani katika kusikia ni mmoja tu yaani Rahabu.
Rahabu aliwaeleza wapelelezi kitu kilichowapata kabla ya wao kupata habari za Mungu wao, matendo anayoyafanya. Pamoja na ukahaba wake alikuwa anasikia habari za Mungu na hiyo ikaanza kumtengenezea imani ndani yake. Ndio maana akajua kabisa kuwa haijalishi amezaliwa katika familia ipi, lakini amejua Mungu wao ndio mkuu.
Ile imani haikumbadilisha Rahabu mpaka wale wapelelezi walipokuja walifika na nguvu za Mungu na upako ulikuwa juu yao. Ndipo Rahabu akatafuta namna ya kuunganisha imani aliyokuwa nayo na upako huo wa wana wa Israeli. Alianza kuwa na imani kabla wale wanaume hawajafika na walipoingia ndani kwake alijua kuwa hawatafuti ukahaba bali wameenda kumsaidia.
MFANO MWINGINE
Ukiwa unataka umeme nyumbani kwako (kwa ajili ya taa, kupikia, n.k) ukienda Tanesco watakuambia umtafute fundi atengeneze mfumo wa umeme hapo ndani kwako (kwa kufunga nyaya na mengine ya muhimu). Huyo fundi akimaliza wao watakuja kupima kama kazi imefanyika vizuri.
Ile kwamba umeweka nyaya kwenye nyumba yako inamaanisha una imani na umeme lakini hauna umeme ndani kwako.
Ukisoma Biblia utaona imani peke yake haitakusaidia kwa sababu haijaumbwa ifanye kazi peke yake. Ndio maana neno linasema.
1 Wakorintho 13:2
“Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.”
➖ Imani inafanya kazi pamoja na upendo kwani imani pasipo na matendo haizai. Hata Ibrahimu alirithi ahadi kwa kuvumilia kwa hiyo imani pia huja kwa kuvumilia na kwa uaminifu.
➖ Imani hufanya kazi pamoja na upako; Yesu alikuwa ana upako, yule mama alikuwa ana imani ndipo ziliposhirikiana akapokea uponyaji.
➖ Imani inafanya kazi na maombi , Marko 11:24
➖ Imani inafanya kazi na maneno, Marko 11:23
➖ Imani hufanya kazi na nyimbo, 2 Mambo ya Nyakati 20:22. Ni imani ilikuwa ndani ya wimbo, waliomba wakapewa neno, walipoanza kusifu nguvu za Mungu zikaanza kufanya kazi kwa ajili ya kuwakomboa na kuwapigania.
➖ Imani inafanya kazi na agano.
JAMBO LA PILI
2. ZIJUE NA ZITUMIE NJIA ZILIZOWEKWA NA BIBLIA KWA AJILI YA KUUNGANISHA IMANI YAKO NA NGUVU ZA MUNGU.
1.NJIA YA KWANZA, KUWEKA IMANI KWENYE MATENDO
Tukirudi kwa habari ya yule mama tunaona njia mojawapo ni kwa kuweka matendo alichokiwaza moyoni kwa imani.Soma Marko 5:27-28. Maandiko yanatuambia katika Waefeso 3:20 Kuwa Mungu anajibu kuliko tuyaombayo na tuyawazayo
Mawazo yanaweza kutengenezwa yakaachilia imani. Yule dada aliweka kwenye matendo alichokuwa anawaza moyoni mwake au analisema moyoni mwake kwa imani. Maana yake alikuwa na uhakika ya kwamba akikifanya kitatokea alichokuwa anakitarajia. Maandiko yanatuletea sentensi ya alichokuwa anakiwaza ya kwamba nikigusa pindo tu la nguo yake nitapona. Hiyo ilikuwa ni imani ikiongea ndani kwa kile alichokisikia juu ya Yesu.
Kwa hiyo kuna namna fulani alisikia habari za Yesu kwamba si lazima nikae naye nimuulize kibali kwamba nisimame uniombee. Kuna namna ambayo alijua kabisa nguo yake imebeba upako, kwa wayahudi wanaelewa nguo ya Kuhani imebeba upako.
Kwa mtu anayesoma Agano la kale anajua kabisa kuhani vazi lake lina upako, kwa hiyo siyo ajabu kuona yule mama akivizia vazi la Yesu.
USHUHUDA
Wakati fulani tulikuwa katika mkoa mmojawapo hapa nchini , kuna watu walikuwa na shida ya kutopata mtoto miaka mingi na mke wa yule baba kamweleza mume wake "Nasikia mwalimu ana semina huko mjini ngoja niende, nikipata nafasi ya kumwona nitamwambia shida yetu atuombee". Yule mama akaja na kuona kwamba kuniona sio rahisi na nguvu za Mungu zilikuwa zinapita kushoto na kulia.
Kwa hiyo likamwingia wazo moyoni akasema haiwezekani upako wote huu watu walioko hapa wanaondoka nao, kwa hiyo akategea muda ule tumemaliza semina akaja mwenyewe, akaja kwenye madhabahu hapo akachukua vumbi akabeba akaenda nanyo nyumbani. Alipofika nyumbani kwake, mume wake akamuuliza umeonana na Mwalimu? Yule man akasema hapana, nimemwona kwa mbali lakini kupata nafsi ya kuonana naye si rahisi lakini nimepata dawa. Akaulizwa kwani wanagawa dawa, akatoa lile vumbi, akasema sijawahi kuona nguvu za Mungu namna hiyo lazima kwenye ule udongo kulikuwà na nguvu za Mungu zinazobaki maana nina uhakika Mwakasege haondoki na Upako wate ule. Sasa mimi nimeona tukoroge tunywe huu udongo. Wakakoroga wakanywa, mwaka uliofuata wakatuletea mtoto waliyempata baada ya kunywa udongo walioutoa madhabahuni. Lakini usiige imani ya mtu.
2. NJIA YA PILI NI KWA KUOMBA
Unaweza kuunganisha imani yako na nguvu za Mungu kwa kuomba. Soma Marko 11:24,Luka 11:13 ………...Mkimwomba baba Roho Mtakatifu atawapa………...
Kuna kuomba kifupi kuna kuomba kwa kirefu, Elia aliomba mara saba nguvu za Mungu zikashuka kutengeneza wingu na mvua ikaja, saa nyingine unaomba maombi mafupi kama Petro "Bwana niokoe" na nguvu za Mungu zinashuka.
Lakini pia katika Matendo Ya Mitume 4:23-31 Hizi ni habari za akina Petro ambao walipata shida baada ya kumuombea mgonjwa. Walitishiwa ili wasiendelee kuhubiri na kulitaja jina la Yesu. Biblia inasema walirudi kwa wakwao wakawaeleza kilichotokea. Basi wale wenzao waliposikia. Biblia inasema wakampazia Mungu sauti zao wakaomba.
Katikati ya yale maombi walisema Mungu yaangalie matisho yao na wakasema nyoosha mkono wako. Walipokuwa wanaomba nguvu za Mungu ziliwashukia kwa upya na mahali pale walipokuwa pakatikisika na wakaanza kuhubiri tena neno la Mungu kwa ujasiri wote.
Kuna wakati ukipita katika msimu mpya unaona kila kitu kinaharibika na unaanza kuingiwa na hofu. Hofu yako inaweza ikashughulikiwa ukiweza kuunganisha imani yako na nguvu za Mungu katika maombi.
Ukiona nafsi yako imechoka maandiko yanasema Mungu anaweza akakutia nguvu kwa upya. Hata kama nafsi yako inakataa kufarijika endelea kuachilia neno la Bwana juu yake na tafakari shuhuda za Bwana. Biblia inasema Daudi alipokuwa anapita mahali pagumu alikuwa anatafakari shuhuda za Bwana. Maana yake tazama matendo makuu ya Mungu aliyokutendea tangu zamani. Hilo tatizo moja lisiondoe uaminifu wa Mungu juu yako.
JAMBO LA TATU.
3 MSALABA UNATUPA NAFASI YA KUWA NA VYOTE NDANI YETU YAANI IMANI NA NGUVU ZA MUNGU
Soma Yohana 1:14,12-13, Hapa tunaona kuwa neno ambalo unalisoma kwenye Biblia linaweza likajitokeza kama ilivyosomwa katika Biblia na ukakiona.
Ukienda katika Biblia ukiona namna neno alivyo fanyika mwili utaona katika kitabu cha Luka 1. Utaona namna Malaika Gabriel alipoenda kwa Mariam. Akimpelekea neno la imani la msimu ya kwamba atapata mimba na kuzaa mwana. Naye anaitwa Yesu..
Mariamu aliuliza litakuaje neno hili. Yaani neno litafanyikaje mwili?. Malaika akasema Roho Mtakatifu atakujilia juu yako na nguvu zake zitakufunika juu yako kama kivuli. Na kitakacho zaliwa kitakuwa kitakatifu. Kwa hiyo kilicho badilisha neno kuwa mwili ni nguvu za Mungu ambazo zilienda juu ya Mariamu.
Wakati Mungu anaumba ulimwengu Roho Mtakatifu alitulia juu ya maji, giza , mahali palipo haribika.
Kulikuwa na nguvu za Mungu lakini giza, uharibifu, ukiwa ulikuwa haujaondoka. Hii ni kwa sababu kama Roho Mtakatifu yuko mahali na hakuna imani hatokuwa na kitu cha kufanya. Ndio maana Roho Mtakatifu akitaka kufanya kazi mahali anahitaji imani na neno la Mungu.
Mungu alisema kuwe nuru, nuru ikaja lakini ukiwa ulikuwa bado uko palepale. Hii ni kwa sababu Mungu alikuwa hajashughulikia ukiwa. Maana pale Mungu alisema neno ambalo linashughulika na giza na sio ukiwa na ndio maana ukiwa ulibaki.
Mungu angeweza kusema giza kwa jina la Yesu toka, na lingetoka. Lakini kuondoa giza hakutengenezi nuru. Nuru inaondoa giza maana palipo na nuru giza linaondoka. Umeme ukikatika ndani kwako na giza likaingia, na umeme usipowaka basi ujue kuwa nuru haitakuja. Hata kama utaweza kemea giza kuanzia asubuhi mpaka jioni na nuru isije.
Soma na huo mstari wa 12 na 13 wa kitabu cha Yohana 1:12-13. Utaona ya kuwa unapookoka kuna vitu vitatu ambavyo vinaingia kazini kwa pamoja.
➖ Neema ya Mungu inafunuliwa juu yako
➖ Neno linakuja
Biblia inasema juu ya habari za neno la Mungu kuwa ni Roho, kwa hiyo linaachilia nguvu za Roho Mtakatifu ndani yako. Hapa ina maana chemchem za uzima zitatoka ndani yako.
Pia maandiko yanazungumzia juu ya kuzaliwa kwa roho, neno, neema na imani. Hapa nataka tuone kuwa tunaweza kupokea vitu vyote kwa wakati mmoja. Maana imani, neema na nguvu za Mungu zinaingia ndani yako
Hata kama imani yako ni ndogo kiasi gani, basi tambua kuwa inaweza hamisha milima.
Kwa hiyo hapo unahitaji kukua katika neema, imani na nguvu za Mungu ili uweze kuona matokeo yake. Kwa hiyo unahitaji nguvu za Mungu ili ziiingie ndani yako na ziweze kufanya kazi.
DAY 4
Karibu katika siku yetu ya nne na ya mwisho ya somo letu;
JIFUNZE NAMNA YA KULITAMBUA WAZO LA MUNGU NDANI YAKO KWA AJILI YA MSIMU WAKO MPYA
Na katika kujifunza jambo hili nataka tuangalie mtiririko wa mambo kama matatu hivi ambayo yana vitu kadhaa ndani yake:-
JAMBO LA KWANZA
1. WAZO LA MUNGU LINALOKUHUSU LINA THAMANI KUBWA SANA KWAKO
Zaburi 139:17-18
“Mungu, fikira zako zina thamani nyingi kwangu; Jinsi ilivyo kubwa jumla yake! Kama ningezihesabu ni nyingi kuliko mchanga; Niamkapo nikali pamoja nawe.”
Mtunga Zaburi kwa lugha nyingine anasema kwamba anapotembea ndani ya fikra hizo Mungu hamwachi na anakuwa naye na kila siku.
Ukisoma Zaburi 139:1-5,13-17,23-24 ule mstari wa 16-17 anasema “Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado. Mungu, fikira zako zina thamani nyingi kwangu”
Ukisoma kwenye Biblia ya Kiingereza mstari wa 16 anaposema “Chuoni mwako” maana yake Kitabuni mwako. Kwa hiyo kuna kitabu kinachohusu maisha ya kila mtu na kinaandaliwa kabla ya kuzaliwa kwa mtu. Kwa hiyo kila siku yako Mungu ameiandika na ameweka mawazo ambayo ndiyo anayotaka utembee nayo.
Ukisoma Yeremia 29:11 Mungu anasema Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.
Lile neno wazo kwenye Yeremia 29 imetafsiriwa kutoka kwenye neno mpango. For I know the plans I have for you, declares the Lord.
Kwa hiyo huyu ndugu anapozungumza juu ya wazo la Mungu kuliweka katika kila ukurasa juu yake, anazungumza juu ya maisha yake. Mungu aliyaratibu na aliamuru siku juu yake na kuweka mawazo yake kwa kila siku ambayo yanatakiwa kutekelezwa kila siku na mtu.
Ukisoma Waefeso 2:10 utaona ya kuwa kuna matendo ambayo Mungu alikwisha yatengeneza. Na tunapozungumza juu ya matendo hatuzungmzii tabia. Kwa hiyo unatakiwa kuenenda kila siku katika matendo ambayo Mungu alikwisha tuumbia ndani ya Kristo ambayo yapo kama mawazo na kuwekwa kwenye kitabu.
Ukisoma Zaburi 139 utaona yale mawazo ambayo Mungu ameyaweka ndani ya kile kitabu chake ndiyo ambayo yanampa kuumbika kama vile ambavyo Mungu amempangia.
Mithali 23:7a inatuambia “Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo”. Maana yake afikirivyo au awazavyo nafsini mwake ndivyo alivyo. Kwa hiyo mawazo yake ndiyo yanayomfanya awe jinsi alivyo.
Tukitaka kukujua unavyowaza tutatazama ulivyo, unavyoishi na unavyosema. Kwa sababu kinywa kinasema kitu kilichojaa moyoni. Kwa hiyo kama umekwama katika maisha yako basi jua umekwama katika mawazo yako.Huwezi ukavuka zaidi ya mawazo uliyo nayo ndani yako.
Ukisoma Waebrania 3:19 Utaona Mungu anazungumza juu ya wana wa Israeli wale ambao waliangamia jangwani. Walitoka Misri vizuri kabisa lakini Waebrania 3:18 inatuambia kuwa Mungu aliwatoa Misri lakini walishindwa kuingia Kaanani.
Pia katika Hesabu 13,14 tunaona kuwa walishindwa kwenda Kaanani kwa sababu waliona majitu walipoenda kuipeleleza nchi ya Kaanani. Na wakaogopa na kujiona kama mapanzi. Waliporudi waliwasimulia ndugu zao na zile habari ziliwapa kuogopa na kuwa na wasiwasi juu ya wao na watoto wao pia.
Mungu alikasirika sana juu yao kwa sababu walilinganisha ukuu wa Mungu na majitu waliyokutana nayo. Hawakujua ni kwa sababu gani Mungu aliwapeleka wapelelezi kule na lengo lake ni nini.
Biblia inatuambia walishindwa kuingia Kaanani si kwa sababu ya majitu au shetani bali ni kwa sababu ya kutokuamini kwao
Ukisoma Waebrania 4:1-2 utaona neno raha, sasa usifikiri ni raha ya kwenda mbinguni pekee. Yesu alituambia kwamba “njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha.
Jitieni nira yangu maana nira yangu ni laini tena ni nyepesi nami nitawapa raha nafsini mwenu”
kwa hiyo unaweza ukapata raha ya Yesu ukiwa hapa duniani na unaweza ukapata raha ya Yesu ukiwa umekufa na kwenda mbinguni.
Kwenye hiyo raha ambayo tumeiona kwenye Waebrania ni raha ya kutoka Misri kwenda Kanaani. Safari ile haikuwa safari ya kiroho kwa jinsi tunavyofahamu bali ilikuwa ni safari ya kiuchumi kwa sababu kilichowapeleka Misri ni njaa. Na kwa sababu hiyo hata kuondoka Misri ilibidi Mungu awape sababu ya uchumi akawaambia anawapeleka kwenye nchi iliyojaa maziwa na asali. Angewaambia sababu nyingine wangeweza kusema awaache wakae pale pale Misri.
Mungu aliwachukua Misri, wakapita Jangwani. Walipokuwa wanajiandaa kuvuka mto Yordani Mungu aliwapa kitendawili cha kwenda kufanya upelelezi katika nchi ya Kaanani na waliporudi wale wapelelezi kumi waliwakwamisha watu wengi sana kwa habari zao mbaya.
Hawa watu Mungu alikuwa akiwaandaa kwa ajili ya msimu mpya ambao ulikuwa mbele yao lakini wengi sana walikwama. Kilichowakwamisha kuingia kwenye msimu wao mpya ni kutofuatilia neno ambalo Mungu aliwapa katika msimu uliotangulia kwa ajili ya msimu mpya. Kuna neno alilowaletea wakiwa jangwani lakini lilikuwa ni la kuishi nalo Kanaani.
Maandiko yanasema kwamba “lilishindwa kuchanganyika na imani iliyokuwa ndani yao” siyo kwamba hawakuwa na imani. Biblia inazungumza kwa habari ya kutoka imani mpaka imani maana yake kuna ngazi za imani na viwango tofauti tofauti vya imani.
Ubaya wa hawa ndugu waling'ang'ania sana neno la msimu uliopita. Kwa kufanya hivyo imani yao haikuchanganya na neno la msimu mpya kwa hiyo wakakosa imani ya kuwaingiza katika msimu mpya. Biblia inasema walishindwa kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.
Hata sasa wapo wengi wameshikilia imani ya msimu uliopita kiasi ambacho hawana nafasi ya kupokea wazo au neno jipya ambalo Mungu anawapa. Na kwa sababu hiyo wanaishia jangwani hata kama wameshavuka Misri (kama ilivyo kwa Waisraeli). Yatupasa kujua thamani ya neno jipya katika msimu mpya huu.
JAMBO LA PILI
2. WAZO LA MUNGU LINALOKUHUSU LIMEBEBA VITU GANI KWA AJILI YAKO?
Hapa tutatumia andiko la Isaya 55:8-13.
“Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu. Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma. Maana mtatoka kwa furaha, Mtaongozwa kwa amani; Mbele yenu milima na vilima vitatoa nyimbo; Na miti yote ya kondeni itapiga makofi. Badala ya michongoma utamea msunobari, Na badala ya mibigili, mhadesi; Jambo hili litakuwa la kumpatia BWANA jina, Litakuwa ishara ya milele isiyokatiliwa mbali.”
Ukisoma hiyo mistari utaona vitu vingi sana ambavyo Mungu kaweka humu ndani kwa ajili yetu. Nakutajia angalau vitu 11 hivi kutokea hapa:-
i). Mpango wa Mungu kwa ajili yako. Isaya 55:8-9
ii). Mkakati wa kutekeleza mpango wa Mungu.
Watu wengi wanatafuta mpango wa Mungu lakini hawatafuti njia ya kulitekeleza. Kwenye wazo la Mungu kuna kifurushi ambacho kina vitu vyote ndani yake (njia na namna ya kulitekeleza, n.k)
iii). Upako wa kulainisha moyo wako ili kupokea na kubeba hilo wazo.
Anapozungumza kuhusu mvua na theluji ni sawa na maeneo mengine hasa yenye barafu wanaopanda wakati barafu ikiisha na ile ya mwishoni ndipo wanapanda sawa na sisi huku tunapanda wakati mvua ikishanyesha. Isaya 55:10
Tukizungumzia mvua ni juu ya Roho Mtakatifu kuwa anapoingia ndani yetu na kutusaidia analainisha mioyo yetu isiwe mioyo ya jiwe bali ya nyama kwa kutumia upako unaoitwa mafuta. Kazi mojawapo ya mafuta ni kulainisha na kazi ya upako ni kubeba wazo la Mungu kupitia nguvu za Mungu kwani huwa na uwezo wa kubeba kitu alichokusudia Mungu.
iv). Mbegu.
Yaani kibebeo cha maisha yako ya baadaye. Isaya 55:10, Yeremia 29:11
v). Chakula. Kibebeo cha maisha yako ya sasa. Isaya 55:10
Kumbuka kwa wana wa Israeli walikupokuwa Misri walikula wanachotaka ila walipokuwa jangwani walipewa mana, walipovuka Yordani mana ilikoma na walitakiwa kulima. Sasa watu wengi hata sasa wanadhani wataendelea kula kama walivyokuwa kwenye msimu uliopita wanasubiria mana, kware, miujiza, n.k lakini vyote hivi haviji.
Mungu alisema tutakula kila neno linalotoka katika kinywa chake. Muujiza ni kwa ajili ya kuingilia kati jambo fulani na ni kwa ajili ya Bwana na si kwa ajili yako. Kazi ya muujiza ikishakamilika tayari utaondoka na hautajirudia.
Neno la Mungu litakuchukua kwa mahali ambapo muujiza hautakuchukua kwani neno linajua kuuchukua na kukupeleka hadi mahali panapotakiwa ufike. Muujiza wa kupewa milioni 1 kila siku ni tofauti na kupewa wazo la kupata milioni 1 kila siku. Sasa Wazo ni kwa ajili ya mtu na muujiza ni kwa ajili ya Mungu. Watu wengine wanachukulia kuwa wazo lazima liwe biashara fulani, shamba au huduma. Kiujumla wazo linahitaji mchakato (process).
Mwaka huu 2020 tulikuwa na kongamano la 12 la maombi kitaifa - Dodoma. Miaka 12 iliyopita kongamano halikuwepo,pia kabla ya hapo miaka miwili tulipewa wazo hilo na Mungu kwa maana hiyo, kabla ya miaka 14 iliyopita kongamano halikuwepo. Lakini Mungu alikuwa anajua nini anataka, alipoteremsha ndani yetu tulidhani ni jambo rahisi sana kwa watu kufika tu Dodoma kutoka maeneo tofauti tofauti na tukafanya kirahisi lakini kumbe si hivyo. Taratibu zote hizi zipo ndani ya Biblia na Mungu alitupeleka taratibu mpaka lilipofanikiwa na kuendelea kuwepo hadi leo.
Wale waliosomea masomo ya Mipango na Maendeleo na Biashara wanajua jambo hili, wanafundishwa namna ya kumsaidia mtu mwenye wazo na kulitengenezea mpango mkakati (business plan). Wewe unawaeleza unachowaza halafu wao wanaandika. Usije ukasema hao walibuni ubunifu mpya; huo ubunifu uko ndani ya Biblia.
vi). Kuna neno lake kwako binafsi. Isaya 55:11
Anaposema ndivyo litakavyokuwa neno langu anamaanisha ni mawazo yake au mapenzi yake Mungu kwa mtu mmoja mmoja binafsi.Mungu anatupa mawazo yake ambayo yanafanana na neno lake.
Biblia ni neno la Mungu kwa watu wote ila lina neno maalum kwa kila mtu binafsi. Yesu asipokuwa wa kwako, amepoteza maana ya msalaba wake. Kwenye Biblia ni Mungu anazungumza na mtu binafsi.
vii). Kuna mafanikio yako binafsi. Isaya 55:11 “…..nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.” Kwa hiyo neno limebeba wazo la mafanikio kwa ajili yako ili kutimiza mapenzi yake kwa ajili yako na halitamrudia Mungu bila kukufanikisha. Kama unataka kufanikiwa tembea kwenye wazo la Mungu.
viii). Wazo la Mungu lina uwezo wa kukutoa ulipo. Isaya 55:12
ix). Kuna uongozi na ulinzi wa Mungu. Isaya 55:12 na Wafilipi 4:7
x). Wazo limebeba jina la Bwana ili lipate kujulikana kwa kila kitu unachofanya. Isaya 55:13 Ukitekeleza kitu ambacho Mungu amekuambia, utamletea Mungu utukufu ili ajulikane na kwa wengine.
xi). Kuna umilele.
Isaya 55:11 inasema
itakuwa ishara ya milele isiyokatiliwa mbali Ndani ya wazo kuna umilele, kwa tafsiri nyepesi kuna uwezo, muda na utekelezaji ndani ya wazo. Kwa hiyo wazo la Mungu huwezi kuliharakisha na kulisukuma unavyotaka maana lina muda wake.
Hivi ndivyo maandiko yanavyotuambia katika: Habakuki 2:2 … .Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, …..; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia. Ndio maana watu wengi wanapata shida linapokuja wazo la Mungu ndani yao na wanapotaka kuliharakisha, kwa kufanya hivyo wanaua vifaranga ndani yao.
Mhubiri 3:1
“Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.”
Lakini kule ndani yake ameandika lakini ndani yake ameweka umilele ndani ya mioyo yao. Unashangaa kwanza alikuwa ana maana gani?
Kumbuka kila kitu kimetoka kwenye eneo ambalo lilikuwa na umilele. Huko mbinguni hawana muda kama sisi tulio nao huku wana umilele.
Vitu vyote huku Duniani vimetokea kwenye umilele na vikapangiwa muda kwa hiyo lazima ujue ratiba ya Mungu aliyoweka! Imewekwa ndani ya mbegu, kwa sababu wazo lake ni mbegu.
JAMBO LA TATU
3. MUNGU ANALITAMBULISHAJE WAZO LAKE KWAKO?
Kwa sababu kama Mungu amehangaika kuweka wazo lake kwenye kitabu. Na huko mbinguni kuna vitabu vingi kwa kila mtu vingine ni virefu vingine vifupi. Hakuna kitu kibaya kama kufika mbinguni ukaonyeshwa kitabu chako ukakuta uliishi ukurasa mmoja tu, itakuwa ni hasara sana kwako.
Ukisoma kwenye Biblia kitabu cha Isaya 55:8 kwamba mawazo yangu si mawazo yenu inamaanisha si wazo lako. Ndio maana unakuta mtu anajiuliza huyu ni Mungu au mimi au ni shetani, ukiona hivyo ujue ni wazo jipya limeingia ndani inawezekana ni Mungu au shetani.Kwa sababu hata shetani aliingiza dhambi kwa mara ya kwanza kwa kupitisha kwenye fikra kwa sababu mfumo wa maisha unapitia huko.
Maandiko yanatuambia aliwadanganya kwenye fikra zao akina Adamu, kwa hiyo hata shetani bado anaweza kuingizia vitu vyake kwa kubana kwenye mlango wa fikra., Kwa sababu tuliruhusu dhambi, kusingekuwa na dhambi kungekuwa na wazo la Mungu peke yake na tusingekuwa tunahangaika.
Pia wazo la Mungu lipo juu sana kwa viwango sio sawa na la kwako. Biblia inasema njia zangu zi juu sana kuliko za kwako kwa hiyo haliwezi kuja sawa na kiwango chako. Mungu hawezi kukupa wazo linaloendana na pesa uliyonayo.Maana ikiwa hivyo utaacha kumtegemea Mungu.
1 Wakorintho 2:9
Lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.
Ukiwa kwenye orodha ya kupendwa na Bwana ndani ya Kristo kuna mawazo ambayo Mungu ameyaandaa si kwa ajili ya kila mtu. Kuna ubunifu ambao anawawekea watu wake tu.
Ukifuatilia juu ya ubunifu wa photocopy machine, aliyebuni wa kwanza ilikuwa kwa ajili ya kutoa karatasi za kurasa za Biblia na sio kwa ajili ya ofisi. Kama mbinguni kuna karatasi na vitabu haiwezekani huyu aliyebuni vitabu liwe wazo lake na katika huo ubunifu unatatua matatizo mengi sana na wewe unakula humo humo.
Kuna mahali inafika watu wanakutazama wanaona umefika mahali pazuri na wanatamani kufika ulipo. Lakini ghafla Mungu anakuletea wazo lingine ili uende ngazi nyingine. Lakini unapewa wazo jipya na kwa sababu unapenda sana ya mahali ulipo na unaogopa kupokea wazo jipya la Mungu. Kwa hiyo jifunze kutulia na kuomba.
Angalia Ayubu 20:2 Kwa hiyo mawazo yangu hunipa jawabu, Kwa ajili ya haraka niliyo nayo ndani yangu.
Mawazo yako sio ya Mungu yanakupa jawabu, kwa nini? Kwa sababu ya haraka! Isaya 28:16, ameweka jiwe kuu la pembeni na ameweka kule mwisho kipengele cha mwisho na aaminiye hatafanya haraka kwa sababu kila wazo la Mungu lina speed yake. Kwa nini unafanya haraka hupati muda wa kutafakari?
Yoshua aliambiwa alitafakari lile neno alilopewa, usiku na mchana ndivyo utakavyostawi na kufanikiwa sana. Alipewa kipengele cha kutenda na alipewa kipengele cha kunena lakini nilitaka uangalie kile kipengele cha kutafakari maana yake kulifikiria kwa ndani, kulichanganya kwa ndani, ujiulize maswali kwa ndani kwa sababu Roho Mtakatifu yuko huko ndani atajibu pamoja na wewe.
Jifunze kuomba kama vile Daudi alivyoomba katika Zaburi 139:24 .Pia omba kamaa Mithali 16:1-3. Mkabidhi kazi zako na kwenye mawazo yako atathibitisha kama ni yeye aliyekupa au si yeye. Jaribu kumkabidhi siku yako asubuhi uone au jioni kabla ya kulala utakuta kuna mawazo uliyopanga kesho yake yamepanguliwa. Kwa sababu ukishamkabidhi tu anaenda kwenye kitabu chake anachungulia anaona hili halipo, linaondolewa kwenye fikra zako linaletwa la kwako. Ukikabidhi ibada jumapili utaona kuna mahubiri yanapanguliwa na analeta yale aliyoyapanga.
Maandiko yanasema utaongozwa na amani, maana yake itakusaidia kujua hili wazo ni la Mungu au si la Mungu.
Marko 5:34
Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena.
Hapa nataka ujiulize swali kuwa kwa nini Yesu alimwambia enenda zako kwa amani? Ni kwa sababu kilichomsukuma kwenda kwa Yesu ni amani iliyoingia ndani yake ya kwenda kushika pindo.
Wazo la kwenda kushika pindo la Yesu halikuwa jepesi maana wakati ule walikuwa hawaruhusiwi hata kutoka nje ukiwa na hali ya namna ile. Pia ilikuwa kama wewe una hilo tatizo hata ukimgusa mtu mwingine naye anakuwa ni najisi. Huyu mwanamke alitumia njia mbalimbali kutafuta kupona lakini alishindwa.
Baada ya kusikia habari za Yesu kuwa anaponya alianza kupambana na wazo hilo ambalo limeingia ndani yake. Huenda alikuwa anajiuliza je nitamwelezaje Yesu kuwa nina hii shida maana huwa anakuwa na watu wengi sana? Je nitapata nafasi ya kumwona na kumweleza shida yangu ili anisaidie?
Basi wazo hilo la kwenda kwa Yesu lilipoingia ndani yake akaanza kutafakari mpaka akapata amani. Kupata amani maana yake kilikuwa ni kigezo cha kwamba asonge mbele na hilo wazo sawa sawa na Wakolosai 3:25a inayosema Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu;...
Pia Zaburi 34:14b inasema Utafute amani ukaifuatie. Maana yake katika kila kitu ambacho unataka kufanya tafuta amani ukiipata ifuate inakokupeleka. Kama husikii amani maana yake Yesu hayupo hapo kukuambia uendelee na hilo jambo. Na sio kwamba Yesu hataki bali ni huenda sio muda wake kwa wakati huo. Unahitaji uendelee kutafakari ili upewe sababu yake kwanini usifanye hilo ambalo unataka kufanya.
Yesu alimwambia yule mwanamke kuwa enenda zako kwa amani kwa sababu alipotakiwa kusema ushuhuda wake peupe ndipo ilimletea shida maana alisikia hofu na kutetemeka sana. Kwa sababu alijua gharama yake kuwa atakaposema kuwa alikuwa na shida ya kutokwa damu. Ina maana pia alivyopita ili kumfikia Yesu ina maana aligusa watu wengi sana na kwa maana hiyo aliwanajisi watu.
Sasa hapo alikuwa na hofu na kuhofia kuwa kwa maana hiyo ya Sheria za Kiyahudi kama wakuu wake wa dini wakisikia itakuaje. Na ndio maana alisikia hofu na kutetemeka ndani yake. Lakini amani iliyokuwa ndani yake ilimsukuma kusema ule ushuhuda. Baada ya kusema ule ushuhuda ile amani ambayo alikuwa nayo ilipotea.
Yesu alihakikisha anamwambia Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena. Aliposema namna hiyo amani ile ilirudi ndani yake. Yesu alisema amani yangu nawaachieni. Kwa hiyo yule dada pale alitoka kifua mbele kuwa haijalishi kavunja sheria za Kiyahudi ili apone ila sasa kapona. Kwa hiyo ile amani ambayo alikuwa nayo hamna mtu ambaye anaweza kumnyang'anya.
MFANO WA PILI
Ukisoma Waebrania 11:31 utaona kilichomsaidia Rahabu asiangamie na wale walioasi ni kwa sababu aliwapokea wale wapelelezi kwa amani. Alisikia amani ndani yake kwanza, sawasawa na maneno ya Yesu katika Mathayo10:12-13
Kwa hiyo lazima wale wapelelezi walipomsalimia walipata amani mioyoni mwao na Rahabu naye akapata amani ya kuwapokea. Hii itakusaidia sana hasa watu ambao wanataka kufanya biashara kuwa usimchukue tu mtu yeyote kwa sababu tu ni rafiki yako au ana hela bali sikiliza amani moyoni mwako kama ipo.
Pia sio kila mtu ni wa kumkaribisha nyumbani kwako. Kuna watu wengine ukitaka kuwakaribisha nyumbani kwako unasikia kukosa amani na utajua hapo kuna tahadhari Mungu anakupa.
Hata pia kama una gari lako, na mtu anakuomba lift njiani, na wazo likaingia la kutaka kumpa lakini ukasikia kukosa amani ongeza mwendo wa gari mpite kwa sababu huruma za kibinadamu zinaweza kukumaliza.
Biblia inasema mtaongozwa kwa amani. Na pia unaona hamna amani sasa wewe kwanini unafanya maamuzi? Huu ni msimu mpya Mungu anaweka mawazo mengi sana ndani ya watu. Sasa wanaweza wakakwama kwa sababu hawataki kuingia ndani ya Biblia ili kujua kuwa Mungu huwa anawekaje mawazo hayo ndani ya watu. Ukiwa na neno la kutosha ndani yako litakusaidia zaidi.
Ukisoma Waebrania 4:12 Utaona kuwa kadri neno la Mungu linavyokuwa ndani yako ni rahisi sana ukayatambua maneno ambayo yanakuja ndani yako. Pia ukiwa na neno la kutosha ndani yako unaweza mtazama mtu na ukajua kitu ambacho anawaza. Ukisoma Biblia unaona inasema Yesu alifahamu kitu ambacho wanawaza.
Sasa kama Yesu yupo ndani yako maana yake atafahamu kitu unachowaza.
Yesu ni neno kwa hiyo ukiwa na neno la kutosha inakuwa rahisi kuunganisha na kuweza kutambua mawazo ambayo mtu anawaza juu yako.
USHUHUDA
Kama wewe unafuatilia habari zetu mtandaoni utakuwa unalijua hili. Kuna watu wana nia nzuri sana sisi maana walisikia namna ambavyo nilieleza juu ya safari zetu za semina na namna ambavyo huwa tunachoka.
Kuna mtu mmoja wa Mungu alisikia hiyo habari na akapata wazo na akanipiga simu kuwa mwalimu tukununulie Helkopta? Pia aliandika na wazo hilo katika mtandao. Watu wengi sana waliitikia na kuwa tayari kushiriki kutoa pesa kwa ajili ya kununua Helkopta.
Kwa hiyo nilimuuliza Mungu kama kwa muda ule je ndio ambao nitapata Helkopta? Sasa sikuona katika ukurasa wa kitabu changu cha mbinguni kuwa kwa wakati ule ingekuwa muda wa kupata hiyo Helkopta.
Basi nikawashukuru sana wale ndugu lakini niliwaambia kuwa ule sio muda ambao Mungu kapanga kutupa Helkopta.
Ungeniuliza kwa jinsi ya kibinadamu nani asiyependa Helkopta. Maana hata hapa baada ya kumaliza tu semina kesho yake au siku hiyo hiyo naondoka zangu kwenda Arusha. Pia huwezi kujua kuwa Mungu aliniepusha na vitu vingapi kwa kutokuchukua helkopta kwa muda ule. Kama itakuja kutokea uko mbeleni sijui ila nataka kwenda hatua kwa hatua ambayo Mungu kanipangia. Kwa hiyo usifurahie vitu tu kwa sababu ni vizuri bali angalia ndani ya moyo wako kuwa je unapata amani au hupati.
MFANO WA TATU.
2 Mambo ya Nyakati 7:11
Hivyo Sulemani akaimaliza nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme; na yote yaliyomwingia Sulemani moyoni ayafanye nyumbani mwa BWANA, na nyumbani mwake mwenyewe, akayafanikisha.
Wakati hema la kukutania lilipokuwa linatayarishwa katika wakati ule wa Musa, Mungu alimpa maelekezo mpaka aina ya miti ambayo aitumie katika kujenga hema na Musa aliandika kila kitu. Katika ujenzi wa hekalu vitu vingi sana vilipita moja kwa moja katika moyo wa Sulemani na yeye ndio alikuwa anatoa maelekezo.
Wakati Musa anajenga hema hakupata msaada kutoka mahali popote, Sadaka zote zilitoka ndani ya wana Israeli. Lakini wakati Sulemani anajenga Hekalu kuna baadhi ya miti aliipata kutoka Lebanoni.
Hata kama unajenga nyumba yako sikiliza amani ya Mungu ndani yako. Usichukue tu ramani ya nyumba kwa sababu ulimtembelea jirani yako na ukaipenda ramani yake.
Watu wengi huwa wanajenga nyumba kwa kutazamia na hawana utulivu moyoni mwao wa kusikiliza amani ya Mungu. Sasa kama unajenga nyumba na Yesu anakuwa ni mwenyeji wako kwa kuiweka wakfu. Yesu alifika mlangoni na anasema mbona kuna chumba hukuweka?
Hii habari utaipata pia katika ile habari ya mwanamke mshunami ambaye alimwendea Elisha. Yule mama na mume wake walijua hawana mtoto kwa hiyo hawakuwa na sababu ya kujenga nyumba yenye vyumba vingi. Pia hawakuwa hata na mpango kukuribisha wageni.
Lakini watumishi wa Mungu walivyokuwa wanapita pale ndipo wazo lilikuja ndani yao ili wajenge chumba cha kuwahifadhi wageni. Je kama wasingekuwa na akiba ya kutengeneza chumba kingine ingekuwaje? Kwa maana hiyo ule muujiza ungewapita.
Pia nimeona hii mahali, pengi unaweza ukaenda mahali kwenda kuombea kiwanja chako. Wakati umemaliza na kumshukuru Mungu na kutafakari kidogo unaona Mungu anakuonyesha matumizi ya hicho kiwanja na anakuonyesha na nyumba ambayo utajenga namna itakavyokuwa. Ukiwa na utulivu wa kutosha uwe na uhakika kuwa utaenda kwa mchora ramani za nyumba na utamwonyesha kitu ambacho umeona.
Katika kipindi hiki cha msimu mpya kuna lugha muhimu sana ambayo unahitaji kumtegemea Mungu katika mambo mengi. Watu wengi sana walipokuwa wanaugua wakawa wanafikiria kwenda Ulaya na India. Lakini sasa ilitokea hali ambayo ilifanya hali kuwa ngumu kwenda. Sio kwamba zile nchi wanawakataa watu wasiende lakini ghafla mazingira yamekataa watu hawatakiwi kusafiri kwenda nje ya nchi. Pia hata hospitali zao zilijaa wakawa wanasema hata kama wewe sio mgonjwa mahututi usije hospitali.
Pia hata watoto ambao wako Ulaya uliokuwa unawategemea wakutumie pesa sasa wanasema ni miezi mitatu tuko ndani tu na hatuna kazi. Pia kuna wengine hapa nchini hawana kazi wanasubiri mambo yakae sawa baada ya ugonjwa huu wa COVID-19 kupita.
Lakini Mungu alikusemesha wewe mwenyewe kuwa uanze kuzalisha pesa za kwako lakini ulikuwa hutaki kusikia. Sasa unashangaa hali imekuwa ngumu, lakini kumbuka Mungu alishakusemesha mapema kuwa mana karibu inakatika jifunze namna ya kulima.
Jifunze kuomba na kutafakari, katika mambo yote hata kwenye kutoa sadaka, Biblia inasema toa kama ulivyokusudia moyoni mwako. Maana yake Mungu ataweka wazo la kutoa sadaka ndani yako.
Mungu akubariki sana

0 Comments