100/recent/ticker-posts
KANAANI MPYA - Lisikilizeni Neno la Bwana............. MAOMBI NA MAOMBEZI --- Tupigie; +255767-155-623 Ujumbe mfupi/Whatsapp; +255620-179-783

UMUHIMU WA MALEZI KWA MTOTO Sehemu ya pili

 

UMUHIMU WA MALEZI KWA MTOTO


 

SEHEMU YA PILI

VITU VINAVYOWEZA KUAMUA MWANAO AWE MTU WA AINA GANI WA BAADAE

 

  1. ANACHOLISHWA AKIWA MTOTO (Anachofundishwa
  2. ANACHOSIKIA AKIWA MTOTO
  3. KINACHOMZUNGUKA

 

1.ANACHOLISHWA AKIWA MTOTO (anachofundishwa)

Mithali 22:6

Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.

Nakusalimu tena katika jina takatifu la Yesu,

Nikukaribishe tena katika  mwendelezo wa somo letu ambalo tumejifunza siku chache nyuma linalosomeka kama UMUHIMU WA MALEZI KWA MTOTO.

Ni imani yangu kwamba kila mtu anao wajibu wa kusimama kama mzazi au mlezi kuhakikisha tunapata kizazi kilicho bora kiroho na kimwili,haijalishi mtoto huyo umemzaa mwenyewe ama hukumzaa.

Kwenye sehemu ya kwanza ya  somo lililopita nilieleza tofauti kati ya mzazi na mlezi na kwa maana hiyo nisingependa kurudia maelezo hayo nikiwa na imani ya kwamba yalijitosheleza na kila aliyefatilia alipata kuelewa lakini kwa ufupi tu ili Yule ambaye hakupata nafasi ya kusoma somo hilo aweze kuelewa,

Nilisema, kuna tofauti kati ya mzazi na mlezi,

Kitu kimojawapo cha yule anayelea ni kumsaidia anayelelewa ili hasikate tamaa, kwasababu katika safari yoyote kuna kukata tamaa au kukatishwa tamaa au kuvunjika moyo.

 

KWAHIYO mtu yeyote aliyebeba roho ya kukulea, atahakikisha yupo karibu na wewe, atakuombea wakati wote, atakutia moyo, atakwambia songa mbele, hatakulaumu bali atakushauri, katika kipindi kigumu atazungumza na wewe kama vile matatizo ni mepesi hata kama yeye mwenyewe anaona ni magumu, na mwisho wa yote atakuhimiza kuweka tumaini lako kwa Bwana hata kama kuna sehemu nyingine ya msaada ulitarajia.

 

 

Turudi katika somo letu katika kipengele kinachozungumzia namna ambavyo anachofundishwa mtoto au kulishwa kwa lugha ya kibiblia jinsi ambavyo kinaweza kumfanya kuwa mtu wa aina Fulani wa baadae.

Biblia inasema  Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.

Vitu viwili viko hapo kwanza katika malezi ambayo mtoto anapokea yanaweza kumfanya aiendee njia ipasayo ama njia hisiyopaswa maana sio kila aina ya malezi yanamfaa mtoto,lakini ni wajibu wa mzazi kuhakikisha mtoto anakua katika njia ambayo kwayo inampa Mungu utukufu kupitia huyo mtoto.

Sasa biblia inaposema, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee,haimaanishi kwamba pamoja na malezi bora unayompa basi hautakutana na changamoto katika kumlea.kinachohimizwa hapa ni kupanda mbegu ndani yake pasipo kuchoka hata kama huoni matokeo halisi kwa wakati huo kama ulivyotegemea kutegemeana na namna unavyomlea,maana kuna saa unaweza kumwambia pita kulia na yeye akapita kushoto.

Ukiona hivyo kisikupe shida moyoni wala hisiwe sababu ya kuacha kumuelekeza katika njia bora lakini zaidi sana malezi yako kwa huyo mtoto yaambatanishwe na maombi maana wazazi na walezi wengi wamepata shida katika eneo hili,pindi wanapoona mtoto haelekei kule ambako wao wanaona ni salama huwa wanaachana na suala la malezi na kubaki kuwaombea, na mimi nimewasikia wazazi wengi wakilaumu namna ambavyo watoto wao wamekuwa wakaidi na wakiacha tumaini lao kwa Mungu wakiamini kwamba atashugulika nao,sipingi kwamba Mungu hawezi kushughulika nao lakini kufikiri hivyo ni kukimbia majukumu na wajibu wako kama mzazi kwasababu pamoja na kwamba Mungu anaweza kushughulika nao lakini kanuni ya kiroho iko palepale kwamba        imani pasipo matendo imekufa

KWAHIYO kwa kuamini tu kwamba  Mungu atamsaidia pasipo kuunganisha imani yako na matendo ya kimalezi inaweza ikakusaidia tu kwa sababu Mungu ni wa rehema lakini njia kubwa ya kuleta matokeo chanya  ni kudumu katika  kumuombea huku ukiunganisha imani hiyo ya kumuombea na kutokuacha kumpa malezi bora au kumuelekeza katika njia impasayo kwa msaada wa roho mtakatifu,hata kama unaona haendi sawasawa lakini husijaribu kuacha kimojawapo katika hivyo na ukaamini kimoja kitakuvusha,(IMANI NA MATENDO).

 

Jambo hilo la kutofautiana kimalezi baina ya watoto na wazazi/walezi  husababisha wakati mwingine wazazi/walezi kuwa wakali kwa watoto wao na kupelekea saa nyingine watoto kukosa uhuru kwa wazazi wao lakini biblia inasema,

wakolosai 3:21

Ninyi akina baba msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

 

waefeso 6:4

Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana.

 

Kwa maana hiyo mzazi anaweza kuwa sababu kuu ya mtoto kukata tamaa na kumuondoa kwenye kusudi la Mungu kupitia aina ya malezi anayompatia.

Ndiyo maana japokuwa ni mtoto lakini husijaribu kuenenda naye kama mtoto na kumchukulia dhaifu kwa kila eneo maana unachokilea sio yeye bali ni kile kilichoko ndani yake ndicho kinaweza kubadilisha hali yake ya nje na adui anawinda kilichobebwa  ndani yake,kwahiyo matokeo yoyote utakayoyaona kwa mtoto wako ujue yameanzia ndani kabla ya kutoka nje,hivyo sehemu ya kwanza ya kushughulika nayo ni kumtengeneza ndani maana akipona ndani uwe na uhakika na nje amepona.

 

Biblia inaposema wazazi wasiwachokoze watoto haina maana wasiwaonye bali waonywe katika hekima na si kila aina maonyo au adhabu inaweza kufanyika msaada kwao kuwafanya waelekee katika njia sahihi,maana kuna kumuadhibu mtoto kwa hasira na kuna kumuadhibu mtoto kwa lengo la kumsaidia na kumuonesha njia hiyo anayoiendea sio salama kwake.

Kwahiyo husijaribu kumudekeza mtoto ukifikiri unamsaidia,sizungumzii hekima ya namna hiyo bali nazungumzia hekima ya maonyo ambayo ndani yake imebeba kitu cha msaada kwa ajili ya huyo mtoto,kwa maana kwamba maonyo utakayompa yasimumtoe katika kusudi la Mungu bali yafanyike msaada wa kumsogeza kwenye nafasi yake sawa na mapenzi ya Mungu baba,lakini hakuna msaada wowote unaotoka katika kumdekeza mtoto.

Ndiyo maana maandiko yanasema,

Mithali 23:13-14

Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa.

Utampiga kwa fimbo, Na kumwokoa nafsi yake na Kuzimu

Kwahiyo unaweza ukamdekeza mtoto ukifikiri unamsaidia kumbe unampeleka kuzimu pasipo kujua,

 

Katika kipengele hiki cha kwanza nimalize kwa kusema haijalishi unamuona mtoto wako anapotea ama anakukatisha tamaa kwa kiasi gani lakini husijaribu kumtenga wala kumkatia tamaa wala kumuweka mbali na wewe maana katika saa ambayo hukutaraji neema ya Mungu itadhihirika juu yake,

Namimi nafahamu wako wazazi wameumizwa sana na watoto wao kiasi ambacho wanaweza kujuta kuwapata,

Ni kweli kwamba hakuna mzazi anaweza kujisikia vizuri kwa kuona mtoto wake ni mwizi,mlevi,kahaba,mtu hasiyefaa wala kuwa na maadili katika jamii,kila mzazi anatamani aone mtoto wake akiwa mfano wa kuigwa katika jamii inayomzunguka lakini sio wote wanaoona matokeo haya kwa watoto wao,

lakini niko hapa kukwambia husikate tamaa kwa ajili ya mtoto wako ile kwamba yuko hai bado liko tumaini kwa Bwana la kumvusha hapo alipokwama na kumpeleka kwenye nafasi yake.

Neema ya Mungu iliyo kuu mno haijakoma,katika somo hili sehemu ya kwanza nilisema ikiwa Rahabu Yule kahaba alihamishwa kutoka kwenye ukahaba wake mpaka kwenye kuamini uwe na uhakika hata mwanao anaweza kuhamishwa saa yoyote lakini kubwa kuliko husiache kupanda mbengu njema ndani yake huku ukidumu katika kumuombea sawa na Neno la Mungu katika,,,

Mithali 19;18

Mrudi mwanao, kwa maana liko tumaini; Wala usiikaze nafsi yako kwa kuangamia kwake.

 

 

2.ANACHOSIKIA

Warumi 10:17a

Basi, imani chanzo chake ni kusikia…..

IMANI ndiyo inajenga msingi wa kile tunachokiamini kukiishi,sasa ikiwa hivyo ndivyo maana yake kile unachoruhusu mtoto wako akisikilize ndicho kitakachojenga msingi wa yeye awe mtoto wa aina gani katika jamii kwa sababu biblia imetuambia imani huja kwa kusikia.

Huko mtaani nimepishana na watoto wengi sana wakiwa na uwezo mkubwa sana wa kuimba  nyimbo za wa wasanii wa bongo fleva kwa ustadi mkubwa kuliko jinsi ambavyo wanaweza kuimba nyimbo za kumtukuza Mungu.

Nilibaki na huzuni moyoni  lakini Sikuwahi kuwalaumu kwasababu hiyo ndiyo aina ya malezi wanayoyapata kutoka kwa wazazi wao,

Ukiwa kama mzazi tafuta kujua ni faida gani anaipata mwanao kwa kumsikilizisha nyimbo au video ambazo ndani yake hazina msaada wowote kwake zaidi ya kumshawishi kutamani kuyaishi yale anayoyaona kwenye televisheni au anayoyasikiliza kwenye simu,radio nk.

Biblia inasema,

Wakolosai 3:16

“Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.”

Sasa ni mara ngapi umemfundisha na kumuonya mtoto wako kwa zaburi na nyimbo na tenzi za rohoni au ni mara ngapi umemfundisha mwanao kumwimbia Mungu wake na kumueleza ukuu wake na namna ambavyo anaweza kusimama naye hata kama wewe mwenyewe haupo,

Watoto wengi wamekuwa mayatima wa kiroho kwa kukosa wazazi ambao wanaweza kuwasaidia kukua kiroho badala yake wanawafanya kuwa watoto wa kisasa kwa kigezo kwamba ni zama za utandawazi,

Sikia utandawazi ambao unakupeleka jehanamu una faida gani kwa kwako na kwa kizazi chako???

Kuna saa mtoto ataharibikiwa kutokana na hicho anachokisikia lakini huo utandawazi hautakuwa na msaada wowote wa kumsaidia kumkwamua alipokwama zaidi sana wewe mzazi ndiye utakayebaki na maumivu moyoni na diye utakuwa mtu wa kwanza  kulaumiwa pindi tu kile ulichomjaza mtoto kitakapoanza kuleta madhara katika jamii inayomzunguka,maana utakachokipanda kwa mwanao ndicho utakachokivuna baadae sasa inategemeana ni chema au kibaya,ndivyo biblia inavyosema katika

                                                  Wagalatia 6:7                                                                                                                                                                                                    “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.”

Kuna tofauti kati ya kusikia kinachosemwa  NA kuelewa kinachosemwa,ndiyo maana unaweza ukasikia kilichosemwa lakini husielewe kilichobebwa ndani ya hicho ulichokisikia,              Daniel 12:8a “Nami nikasikia, lakini sikuelewa;…….

KWAHIYO husitegemee kumuona mwanao akienenda katika njia njema ikiwa hujamuandaa kukaa mkao wa yeye kuiendea njia hiyo uliyokusudia aiendee,maana kabla ya kuenenda kinachotangulia ni maamuzi na maamuzi ni matokeo ya alichokielewa baada ya kusikia.

 

MFANO 1;

Mithali 23:19-21

 Sikia, mwanangu, uwe na hekima, Na kuuongoza moyo wako katika njia njema. Usiwe miongoni mwao wanywao mvinyo; Miongoni mwao walao nyama kwa pupa. Kwa maana mlevi na mlafi huingia umaskini, Na utepetevu humvika mtu nguo mbovu.

Mithali 23:29-30

Ni nani apigaye, Yowe? Ni nani aliaye, Ole? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye mguno? Ni nani aliye na jeraha zisizo na sababu? Ni nani aliye na macho mekundu?Ni wale wakaao sana kwenye mvinyo; Waendao kutafuta divai iliyochanganyika.

Sasa fikiri tu ikiwa hukuwahi kumfundisha mwanao madhara ya pombe akingali bado mdogo,unategemea atakayebeba jukumu lako ni nani lakini je ufahamu wa mtoto kukaa mbali na pombe ataupata wapi?, mara nyingi tunalalamika kwa kutokea katika familia masikini lakini familia nyingi umasikini wa mwilini umetokana na umasikini wa rohoni ambao mizizi yake haikushughulikiwa mapema,maana pengine kama mtoto angejifunza mapema madhara ya pombe na matokeo yake hasingejikuta huko na kupelekea kuharibikiwa na kujidhalilisha utu wake kwa kujivika nguo mbovu ya ulevi maana hakuna mtu anamsikilizaga mlevi wala kumuheshimu,sasa kama ni baba haheshimiki kwa ajili ya ulevi wake uwe na uhakika na familia yake itadharaulika kwasababu heshima familia inategemeana ni nani  ni mlango wa hiyo familia na sote tunajua baba ndiye kichwa cha familia,sasa ikiwa kichwa kimeinama maana yake utukufu wa Mungu haupiti.

 

MFANO 2;

Mithali 23:22-24

 Msikilize baba yako aliyekuzaa, Wala usimdharau mama yako akiwa mzee.Inunue kweli, wala usiiuze; Naam, hekima, na mafundisho, na ufahamu.Baba yake mwenye haki atashangilia; Naye amzaaye mtoto mwenye hekima atamfurahia.

Nimewaona watoto wao wakiwanenea maneno ya kashfa wazazi wao,na kuwadharau,maneno hayo juu ni maonyo kwa mtoto lakini mimi nitayatumia kwa ajili ya mzazi kumuandaa mwanae,maana ukiwa kama mzazi ukiona umeshindwa kumfanya mwanao akusikilize maana yake akuheshimu,maana yake umemfungulia mlango wa kukudharau kwasababu ni wajibu wako kama mzazi kuachilia hekima na mafundisho na maarifa kwa mtoto wako ili kumjengea msingi bora wa kesho yake iliyo njema na yenye matumaini,na biblia inaniambia Naye amzaaye mtoto mwenye hekima atamfurahia.                                               Kuzaa ni jambo moja lakini kumfanya mtoto awe mwenye hekima na maarifa ni jambo la pili ambalo kila mzazi anao wajibu wa kushughulika nalo kuhakikisha mtoto wake anakuwa na maisha bora ya baadae yenye msingi imara uliofungamanishwa katika kristo.

Biblia inasema “Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo.                                                                                                                                                                 ”1 Wakorintho 3:11

 

 

 

3.KINACHOMZUNGUKA

1 Wakorintho 5:10-11

Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang'anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia.

Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang'anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye.

Ni watu gani wanaomzunguka mtoto wako na wanampa nini na je wanachompa kinaacha mbegu gani ndani yake?

Familia nyingi wamehamisha jukumu la malezi kutoka kwao kama wazazi na kulihamishia kwa wadada wa kazi,mdada ambaye wamekutana naye ukubwani,hawaelewi background ya maisha yake na hata hawajui msingi wa malezi yake mwenyewe umejengwa katika nini,

Na wengine wamepeleka watoto wao kwa bibi zao na babu zao na mashangazi na wajomba nk

Sina maana kwamba watu hao ni wabaya lakini nahoji uhakika wako kama mzazi kama watu hao wanaweza kumpa malezi bora mwanao yanayoweza kusababisha kusudi la Mungu ndani ya huyo mtoto likasitawi.

 

Litaendelea………………………

 

unaweza kufatilia sehemu ya kwanza ya somo hili kwa kubonyeza linki hii hapa chini            

UMUHIMU WA MALEZI KWA MTOTO sehemu ya kwanza

Post a Comment

1 Comments