IRUDISHE IMANI YAKO MAHALI INAPOSITAHILI ‘Reposition your faith to its right place’
Bwana Yesu asifiwe mwaka huu wa 2021, kuliko alivyosifiwa mwaka jana wa 2020.
Heri ya mwaka mpya.
Ujumbe nilionao kwako,toka madhabahuni pa Mungu kwa mwaka huu ni: Irudishe na Iweke imani yako mahali inapostahili’! Au kwa muhtasari kwa kiingereza – ‘Reposition your faith to its right place’!
Hii ni kwa sababu,ulimwengu wote,tupo katika msimu mpya. Na mambo yanayotokea katika mwanzo wa misimu mipya, huwa yana tabia ya kuyumbisha imani za watu.
Je, imani yako ipo mahali inapotakiwa kuwapo? Je, imani yako ikiyumba utajuaje? Na unairudishaje imani iliyoyumba,na kuiweka mahali inapostahili kuwapo? Dalili za imani iliyoyumba ni zipi? Ngoja nikupe mifano michache ya dalili hizo:
Dalili ya 1: ‘Kufikiri moyoni mwako ya kwamba, kwa kuwa jambo limekushinda wewe, na limewashinda watumishi wa Mungu, basi, hata Mungu wao limemshinda!’
Ukiona umefikia mawazo ya namna hii, katika kupata utatuzi wa jambo linalokusumbua, ujue imani yako haiko tena kwa Mungu, hata kama unaomba! Soma Marko 9:14 – 27. Huyu baba wa mtoto,aliyekuwa na pepo bubu,alifikia mawazo kama haya!
Rudisha imani yako kwa Mungu,kwa kutubia kutokuamini kwako (Marko 9: 22 – 24); na anza tena kutafakari,na kuamini mistari ya biblia,inayotujulisha kuwa, hakuna lisilowezekana kwa Mungu (Luka 1:37, Yeremia 32:12,27, Mathayo 19:26).Na ya kwamba Mungu anajibu maombi (Waebrania 11:6).
Dalili ya 2: ‘Unapoanza kulalamika moyoni mwako,kana kwamba Mungu amekusahau, na unadhani ndio maana hajibu maombi yako, na kutoyaondoa matatizo yako!’
Ukiwaza namna hii, ni dalili ya kuwa, imani yako imeondoka, mahali inapotakiwa kuwapo! Ndicho kilichompata Habakuki. Soma Habakuki 2:1 – 4.
Habakuki alijikuta analalamika mbele za watu (Habakuki sura ya 1), na mbele za Mungu (Habakuki 2:1); kwa sababu alipoteza imani inayokuja na maono ya Mungu juu ya eneo lao. Na kwa kuyumba kwa imani yake, alijikuta uwezo wake wa kuendelea ‘kumsubiri’ Mungu unapotea! Uvumilivu unapotea!
Na ile Mungu kumwambia Habakuki,mwenye haki ataishi kwa imani yake (Habakuki 2:4),ina maana alitaka ajue ya kwamba,kulalamika kwake ilikuwa ni ishara ya kuwa,imani yake haikuwa mahali ilipotakiwa kuwapo.
Ikiwa unapitia hali ya imani yako kuyumba kama ya Habakuki, hata kama wewe ni mwombaji kama Habakuki,rudisha imani yako mahali inapostahili, kwa kutafakari Ahadi ya Mungu inayokupa “maono” ya Mungu, yaliyobeba jibu la mazingira mabaya yanayokuzunguka! Soma tena Habakuki 2:1 – 4. Na msome pia Ibrahimu katika Warumi 4:18 – 21 na Waebrania 6:11 – 18.
Dalili ya 3: ‘Unapojikuta unapoteza utulivu, na amani moyoni mwako, kwa sababu unapita mahali pagumu kimaisha, au kiutumishi, au kikazi, au kibiashara, au kimahusiano, au kiuchumi, au kisiasa!’
Hali hii,iliwapata wanafunzi, wakiwa na Yesu ndani ya boti, huku bahari ikiwa imechafuka sana. Ni dhahiri walipoteza utulivu,na amani mioyoni mwao. Yesu aliwauliza: “Imani yenu iko wapi?”
(Luka 8:22 – 25).
Swali hilo lilionyesha ya kuwa, imani yao haikuwa mahali ilipotakiwa kuwapo! Ingawa walikuwa na Yesu ndani ya boti, bado wali – “panic” – maana yake walikosa utulivu,na amani mioyoni – wakidhani watazama!
Kumbuka: Unaweza ukawa na Yesu, lakini imani yako isiwe,mahali ambapo anaweza kuitumia kukusaidia.
Imani yao waliiweka kwenye ‘uzoefu’ wao,katika kusafiri baharini. Na ‘uzoefu’ uliposhindwa kuwasaidia, wakapoteza amani, na utulivu.
Ikiwa unapitia hali kama ya namna hii, ujue imani yako imepigwa dhoruba, na haipo mahali inapotakiwa. Irudishe imani hiyo mahali pake,kwa kukua katika kumjua Yesu, na neno lake linasema nini juu ya uwezo wake,juu ya mazingira mabaya unayopitia.
Ukisoma Luka 8:25 – utaona wanafunzi wakiulizana: “ni nani huyu basi hata anaamuru pepo na maji, navyo vyamtii?” Ni dhahiri walimjua Yesu na uwezo wake katika maeneo mengine, lakini hawakumjua Yesu na uwezo wake katika jambo gumu walilokuwa wanapitia wakati ule? Je, wewe unamjua Yesu kwa kiwango gani, na uwezo wake kwa kiasi gani, juu ya eneo hilo ambalo unapita mahali pagumu?
Dalili ya 4: ‘Unapojikuta unapoteza imani yako ya kuendelea na juhudi zako, za kufanya kile ambacho huoni matunda ya juhudi zako, hata kama unajua, Mungu amekuamini na amekukabidhi ukifanye!’
Soma Luka 13:6 – 8. Mtu huyu ni mfano wa mtu aliyekabidhiwa kazi na Mungu, lakini kwa miaka mitatu mfululizo,kazi ile haikuzaa matunda yaliyotakiwa. Lakini,unaona mtu yule hakupoteza imani yake,juu ya kuendelea na juhudi za kuifanya kazi ile. Ndipo akaomba aongezewe mwaka mwingine!
Je, umejikuta unakata tamaa, kwa kuwa tu, kazi uifanyayo haikuzalii matunda yanayotakiwa? Usikate tamaa! Unapokata tamaa kuendelea kulifanya jambo, ambalo Mungu amekupa ulifanye, ujue imani yako haiko mahali inapotakiwa kuwapo “kiutendaji” (Yakobo 2:17,20).
Rudisha imani yako mahali inapotakiwa kuwapo, kwa kutokuchoka kutenda,au kufanya kile ambacho,Mungu amekupa ukifanye,kwa sababu utavuna kwa wakati wake (Wagalatia 6:9)!
Dalili ya 5: “Unapojikuta unaikubalia tabia mbaya uliyonayo, kuinyima imani nzuri uliyonayo,fursa ya kumpa Mungu nafasi akutoe katika maisha uliyonayo, na kukuingiza kwenye msimu wako mpya kimaisha, au kikazi, au kiutumishi, au kibiashara, au kisiasa, au kimahusiano, au kiuchumi!”
Habari ya Rahabu, yule kahaba, inatupa kujua ya kwamba, mtu anaweza akawa na tabia mbaya isiyompendeza Mungu, na wakati huo huo akawa na imani nzuri inayompendeza Mungu! Soma Waebrania 11:31.
Mazingira aliyoishi Rahabu,yalimpa urahisi wa kuona fursa ya kutumia tabia mbaya aliyokuwa nayo, kuliko kuona fursa nyingi za kuitumia imani yake nzuri aliyokuwa nayo. Lakini moyoni mwake, aliazimu kutokubali imani yake hiyo, iyumbishwe na tabia mbaya aliyokuwa nayo. Tena, wala hakukubali imani yake, iyumbishwe na maneno ya waliomzunguka, waliokuwa wanamtuhumu,na kumshambulia,juu ya tabia yake mbaya aliyokuwa nayo!
Fursa moja ilipotokea ya imani yake kutumika, hakusita kuitumia. Tabia mbaya aliyokuwa nayo, haikumzuia kuitumia imani yake, kutumia fursa ya ‘kutoa sadaka’ ya kukaribisha ‘watumishi’ wa Mungu! Mungu akaitumia imani ya Rahabu kumtoa kwenye ukahaba, na kumpa msimu mpya na maisha mapya.
Je, una tabia ambayo si nzuri machoni pa Mungu, uliyoingia nayo mwaka huu,hata kama si inayofanana na aliyokuwa nayo Rahabu? Na je inafanya imani uliyonayo kwa Yesu, iwe mahali ambapo huwezi kuitumia ipasavyo katika msimu huu mpya?
Irudishe imani yako katika nafasi inayostahili kuwapo,ndani ya moyo wako, ili uweze kuitumia kwa faida.Rahabu aliitunza imani yake, katikati ya tabia mbaya aliyokuwa nayo, kwa kuendelea kutafakari shuhuda za Mungu wa Israeli, alizokuwa anazisikia. Na wewe fanya vivyo hivyo. Soma Yoshua 2:1, 8 – 11.
Rahabu aliiweka imani yake mahali ambapo, alipopata fursa ya kumtolea Mungu sadaka, aliitoa bila kusita, na akiwa na amani. Mungu akaitumia sadaka ile,kumtoa kwenye mazingira ya maisha mabaya ya msimu wake uliokuwa umetangulia, na kumwingiza kwenye msimu mpya uliokuwa umeandaliwa na Mungu kwa ajili yake. Soma Waebrania 11:31. Na wewe fanya vivyo hivyo!
Rahabu aliiweka imani yake mahali ambapo, ilikuwa rahisi kujiambatanisha na Mungu wa Israeli kiagano, kwa njia ya maombi. Na Mungu akaonyesha uaminifu wake wa kushika agano lake, kwa kujibu ombi la kiagano la Rahabu. Soma Yoshua 2:12 – 21 na Yoshua 6:17, 23. Na wewe fanya vivyo hivyo.
Na ndani ya maombi hayo ya Rahabu,kulikuwa na toba yake.Na wewe usiache kuitubia tabia mbaya uliyonayo.
Wewe uliyesoma ujumbe wa salamu hizi, nakuombea, ili kama imani yako haiko mahali pake kwa ajili ya misukosuko ya msimu mpya, Mungu akujalie na akuongoze cha kufanya ili imani yako,irudi mahali inapotakiwa kuwapo.
Heri ya Mwaka 2021.
NAKUTAKIA BARAKA ZA BWANA

0 Comments