100/recent/ticker-posts
KANAANI MPYA - Lisikilizeni Neno la Bwana............. MAOMBI NA MAOMBEZI --- Tupigie; +255767-155-623 Ujumbe mfupi/Whatsapp; +255620-179-783

MUNGU AKUPE KUONA FURSA KATIKATI YA MAGUMU

MUNGU AKUPE KUONA FURSA KATIKATI YA MAGUMU

1 Wafalme 17:10-13,15,16

¹⁰Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa.¹¹ Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako.¹² Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe.¹³ Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao.

¹⁵ Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi.¹⁶ Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.


LENGO LA SOMO

1.Ni kutambua ukuu wa Mungu katikati ya magumu. 

2.Ni kuona fursa mpya katikati ya kuchoka. 

3.jinsi ya kutembea katika magumu pasipo kufarakana na Mungu.


Bwana wetu Yesu apewe sifa,

Karibu katika somo letu leo nililolipa kichwa cha MUNGU AKUPE KUONA FURSA KATIKATI YA MAGUMU.


miongoni mwa mambo yanayokatisha tamaa na kunyonya nguvu za Mungu ndani ya mwamini ni pamoja na kuomba alafu husijibiwe kama ulivyotegemea wakati huo unapita katika wakati mgumu.

Inahitajika mafuta ya pekee ya kukuwezesha kutembea katika wakati huu kwasababu ukishajibiwa tofauti na ulivyotegemea ni rahisi sana kuvunjika moyo na kuingiwa na huzuni na kukosa amani ya moyo.


KWA MFANO

               Unaenda mbele za Mungu kumuombea mgonjwa na pengine mgonjwa huyo ni wa karibu sana kwako pengine ni mke, mme, mtoto au mzazi alafu Mungu anakujibu anakwambia "hatopona hakika atakufa" na kweli mgonjwa anakufa na wakati huo wewe mwenyewe unayo maandiko ya kusimamamia kile unachokiomba na pengine unamwambia Mungu yakuwa wewe ulisema "mtaweka mikono juu ya wagonjwa nao watapa afya" Lakini sauti ya Mungu inarudia "hatopona hakika atakufa"Na wakati huo unajua kabisa Yakwamba Mungu si mwanadamu hata aseme uongo maana yake hawezi kujipinga.


Unapofika saa ya namna hii, unaomba ukitegemea chanya alafu inatokea hasi ni rahisi sana kuanza kukemea ukifikiri ni shetani amezungumza kumbe ni Mungu amenena.


USHUHUDA

Wakati fulani nilipita katika kipindi kigumu kiuchumi na hali hiyo ikanipelekea nishindwe kumudu mahitaji muhimu binafsi ya kila siku, Ikanilazimu niende mbele za Mungu na nilimuomba Mungu anifungulie milango ya kazi ili angalau nipate kipato kitakachonisaidia na kuniwezesha kukabiliana na hali hiyo  lakini akanijibu alinijibu kitu cha ajabu sana akasema, "katikati ya wakati mgumu unaouishi tafuta fursa zinazopatikana katika mazingira hayo yanayoonekana ni magumu kwako, na kupitia fursa hizo zinazoonekana dhaifu nitazifanya kuwa imara na kupitia hizo kiu yako ya kutafuta kazi itakoma"

Sasa husije ukafikiri ilikuwa rahisi kwangu kupokea majibu hayo, maana ananijibu hivo wakati huo sina hata pesa ya kufungua hata kibanda cha nyanya,lakini nimesoma na vyeti ninavyo ndani.

Kwahiyo kabla ya kuomba Mungu anifunulie hizo fursa ilikuwa ni lazima kwanza niombe Mungu anipe upako au mafuta ya kutembea katika hiyo hali maana vinginevyo hisingekuwa rahisi kabisa kwangu kupokea hayo majibu.


Ndivyo ambavyo wana wa Mungu wengi wamekwama sehemu moja kwa kufikiri kwamba Ni lazima Mungu akujibu kama ambavyo wewe unatazama mazingira yanayokuzunguka.

Biblia inasema Mtumishi wa Mungu Eliya anamwambia yule mama mjane akampe mkate na hata baada ya kumwambia hivo, mama anajaribu kujitetea kwa kumtazamisha Eliya hali ya akiba ya chakula alichobaki nacho lakini hata baada ya kunena hivo mbele ya Eliya bado Eliya alikazana kumwambia amuandalie kwanza yeye kabla ya yeye huyo mama mwenyewe na mtoto wake.


Kwa majibu hayo ya Eliya kwa mama mjane ilikuwa ni rahisi kwa mama yule kufikiri kwamba huyu mtumishi wa Mungu hana huruma kabisa maana anaomba chakula ambacho hicho ndo akiba ya mwisho na wakati huo yuko mtoto mdogo ambaye angalau ilitakiwa apewe kipaumbele kwanza yeye.

Ndivyo ambavyo tumepishana na baraka za Mungu mara nyingi lakini Mungu hatazami kama tunavyotazama, maana maandiko yanasema,

“Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani.” Isaya 43:19

Maana yake, 

        • katikati ya kukata tamaa kwetu Mungu ataweka tumaini.
        • Katikati ya kuchoka kwetu Yeye atatutia nguvu kwa upya.
        • Katikati ya huzuni Yeye ataachilia kicheko.
        • Katikati ya giza nene Nuru yake itaangaza.
        • Katikati ya Kufikiri kwetu na kuwaza  kwetu na kuamua kwetu kunapofika mwisho yeye ataachilia maarifa mapya yenye ushindi. 


 Baada ya majibishano ya muda mfupi mama yule alimua kufanya kama ambavyo Eliya alimwambia na maandiko yanasema baada ya hapo ile akiba iliyoonekana ni ya mlo mmoja tu ilidumu kwa siku nyingi maana yake walikuwa wanapika kila siku lakini chakula hakipungui.

Lakini mama huyu husije ukafikiri ilikuwa rahisi sana kwake bali alimtazama aliyeko mbele yake na nani kamtuma na zaidi alikuwa na imani vinginevyo hisingekuwa rahisi kufanya maamuzi ya namna ile akijua baada ya hapo ni kifo kinafuata kwake na kwa mwanae lakini katikati ya wakati mgumu aliokuwa nao alitumia vyema ipasavyo FURSA aliyoipata ambayo kwayo muujiza mkubwa ulitendeka tofauti na ambavyo angeamua kubaki na akiba yake na baada ya hapo akafa lakini kwa kutii tu sauti ya Mungu pasipokuangalia ugumu wa mazingira yanayomzunguka kwa wakati huo alipata neema  ambayo inakuja na FURSA ya kupata nafasi yake ya kuendelea kuishi na kwa hakika aliuona  wema wa Mungu. 


Niko hapa kukwambia wewe unayejiona unapita katika wakati mgumu na pengine hakuna hata mmoja aliye upande wako au hakuna hata mmoja wa kukutia moyo au mambo ni shwari kabisa lakini bado unahitaji Mungu akufungue macho ya rohoni upate kuona FURSA zinazokuzunguka tofauti na wanavyoona watu wengine maana fursa zinaweza kuwepo nyingi lakini si kila fursa inaweza kukufaa na njia pekee ya kutambua nafasi yako kifursa ni kumuomba Mungu akufunulie ili husienende kwa kupapasa. 

Maana pamoja na kupita katika wakati mgumu lakini faida moja wapo ya kutembea na Mungu katika wakati huo mgumu ni pamoja na kujua hatima ya hali unayoipitia kwa wakati huo tofauti na mtu anayepita katika wakati mgumu kwa kutumia akili zake maana Ukiwa na Mungu atahakikisha nuru yake inaangaza hata kama unapita katika wakati wa giza na hivyo kukusaidia wewe kuona vyema mahali unapopakanyaga lakini pia ile kujua tu kwamba unaye Mungu inaachilia ujasiri ndani yako na nguvu ya kusonga mbele  hata kama watu wote wamekukimbia na weliobaki wanakulaumu kama AYUBU  na unapita katika giza lakini utashinda maana hakika unajua hatima yako ni njema na ya ushindi tofauti na mtu anayetumia akili zake, yeye katika giza atatembea kwa kupapasa maana yake kwa kubahatisha sasa katika kutembea kwa kupapasa unaweza kujikuta unakanyaga msumali au unagusa moto na hivyo kufanya safari yako kuwa ngumu na mwisho utajikuta unakata tamaa na kughairi safari na kurudi nyuma.

Maandiko yanasema, 

“Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.”Zaburi 119:105


    1. Kwahiyo huwezi kushinda vita ya aina yoyote kama huna neno la Mungu ndani yako.
    2. Huwezi kuchukua maamuzi kama ya mama mjane kama huna Neno la Mungu ndani yako.
    3. Huwezi kupenya kwenye majaribu kama huna neno La Mungu ndani yako
    4. Huwezi kutofautisha Sauti ya Mungu na ya shetani katikati ya majaribu Kama huna Neno la Mungu ndani yako.
    5. Huwezi kuona Fursa za kutoka kwako kama huna Neno la Mungu ndani yako.

Kwasababu maandiko yanasema katika Neno ndiko penye "taa ya miguu yetu" maana yake usalama wa tunapopakanyaga umefungamanishwa katika ufahamu wa Neno la Mungu, ndiyo maana ni ngumu sana kuendesha gari kama hukuwahi kuendesha lakini ni rahisi mno kwa mwenye ufahamu na eneo hilo la kuongoza gari.

Pengine hujaelewa lakini ilikuwa ni ngumu sana kwa shedrack, meshaki na abednego kukanyaga katika moto na wakatoka wakiwa wazima kama wasingekuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu Mungu wanayemuamini na uwezo wake katika mahali hapo walipokuwa wanapita. Kuokoka au kuamini tu haikuwasaidia bali walitakiwa wawe na ufahamu wa kutosha kwa maana ya Neno la Mungu ndani yao litakalowapa uhakika wa kuvuka ng'ambo ya pili.


Ile kusema "Ni mwanga wa njia yangu" inamaanisha wakati wowote unaoweza kuupitia utakuwa na wepesi wa kutembea katika huo kwa maana iko nuru au mwangaza mbele yako unakusaidia kuona unapoelekea.

Wakristo wengi leo wanafikiri wakishampokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yao ndio kusema kwamba wamemaliza kazi lakini sivyo.

Nami nataka nikwambie leo ya kwamba ukiwa mkristo wa namna hii dumu ukifunga na kuomba husije ukapita katika majaribu na ni ngumu pia kukaa katika wokovu na husipite katika majaribu kwasababu maandiko yanasema "Yesu alikuwemo chomboni lakini dhoruba ilitokea"

Kwahiyo kuwa katika wokovu haimaanishi dhoruba haitakupata maana wako watu wanayo imani ya namna hiyo na wamekalilishwa hivyo lakini inapofika saa ya majaribu wao ndio wa kwanza kurudi nyuma kwasababu ndani yao taa imezima maana yake Neno la Mungu limesinyaa  au halimo kabisa ndani yao na inapofika saa wanapita katika wakati mgumu safari yao ya ushindi inakuwa fupi sana kwasababu kilichotakiwa kusimama kama mwanga wa kuwaangazia wanakokuelekea hakipo au kimezima au mwanga wake ni hafifu.

Kwa maana hiyo husijaribu kuishi pasipo neno la Mungu ndani yako maana hata kama yuko mtu anayekuombeaga ukipita katika magumu lakini iko siku mtu huyo atakuwa hayupo na hapatikani kwenye simu au yuko busy au naye anapita katika wakati mgumu  kiasi hawezi kumbeba mtu mwingine au huko mbali naye na hivyo hautapata msaada wa kukuvusha hapo na adui atapata nafasi ya kukuvuruga kwa maana hapana kizuizi. 


Nimalize kwa kusema "omba Mungu akufungue macho ya rohoni na akupe mafuta ya kuona fursa ambazo zipo katika hayohayo unayoyaona ni mazingira magumu kwako."


Mungu wangu mwema akubariki sana na akutendee mema na roho mtakatifu akafanyike mwalimu kwako katika somo hili ili upate kuelewa kwa kina zaidi ya hapa.

Panapo wakati mwingine tutakuja na somo jingine kadri roho mtakatifu atakavyotuongoza. 


"Amen"

Post a Comment

0 Comments