100/recent/ticker-posts
KANAANI MPYA - Lisikilizeni Neno la Bwana............. MAOMBI NA MAOMBEZI --- Tupigie; +255767-155-623 Ujumbe mfupi/Whatsapp; +255620-179-783

SOMO: JIEPUSHE NA MAKOSA YAFUATAYO UKITAKA KUVUKA KWA USHINDI - C. Mwakasege


SOMO: JIEPUSHE NA MAKOSA YAFUATAYO UKITAKA KUVUKA KWA USHINDI  - C. Mwakasege

Haya siyo mahubiri wala mafundisho ya kawaida, Mungu anazungumza na mtu mmoja binafsi. Fikiria ni mwanzoni mwa mwaka na Mungu anakutembelea na kuzungumza nawe juu ya mambo yaliyoko mbele yako mwaka huu.

Marko 4:35-41

Siku hiyo kulipokuwa jioni, Yesu akawaambia, Na tuvuke mpaka ng'ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyokuwa katika mashua. Na mashua zingine zilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakaipiga mashua hata ikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?


Mungu anazungumza nasi kupitia maneno haya juu ya makosa ambayo tunatakiwa kuyakabili kama tunataka kuvuka kwa ushindi mwaka huu. Hii ni kwa sababu kila mwaka unapoanza ni msimu mpya na matarajio mapya kwa kazi unayofanya kama ya huduma na kazi zingine. 


Kama tulivyosoma kwenye mistari hii, Yesu alikuwa na wanafunzi wake katika boti akizungumza nao mambo ya ajabu sana akiwaambia “Na tuvuke mpaka ng’ambo”kwa hiyo Mungu anaweza kukuambia “tuvuke mpaka mwaka ujao".

Kwa sababu uko pamoja nasi siku ya leo Mungu anataka kusema nawe kuhusu makosa Saba ya kujiepusha ili uvuke mwaka huu kwa ushindi. 


KOSA LA KWANZA

1.USIENDE NA USIISHI KWA MAZOEA MWAKA HUU.

Nakuambia hili kwa sababu kwenye maandiko imeandikwa 

Marko 4:35

Siku hiyo kulipokuwa jioni, Yesu akawaambia, Na tuvuke mpaka ng'ambo. Wakauacha mkutano, *wakamchukua vile vile alivyokuwa katika mashua*. Na mashua zingine zilikuwako pamoja naye.

Usije ukajikuta unata kwenda kama hawa wanafunzi maana waliishi kwa mazoea. Sasa siwezi kushangaa sana maana ukipata nafasi ya kwenda Israel na ukaona lile eneo la Ziwa Galilaya  ambalo Yesu na wanafunzi walikuwa ndani ya Boti kwa ajili ya safari utashangaa sana.

Ukisoma hizi habari utaona ya kuwa dhoruba ilitokea kama marambili au maratatu hivi. Pia kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Yohana, kuna vitu vingine vilimhusu Yesu na wanafunzi wake havikuandikwa ndani ya Biblia maana vingeandikwa vyote hata vitabu visingetosha Dunia nzima.

Katika safari zetu za Israel mpaka mwaka huu 2016 nimeenda kama mara 23 hivi. Kila safari zote huwa napanda Boti katika ziwa Galilaya. Sasa unaweza ukaelewa  ninapozungumza habari hizi.


Kila wakati tukiwa hapo huwa pia napata nafasi ya kuzungumza neno la Bwana. Kila wakati ninapo pita pale na kusoma habari hizi Mungu huwa ananisemesha kitu kipya.


Hawa watu walipanda kwenye boti kimazoea wakiwa na Yesu kwa sababu tu kasema na tuvuke mpaka ng'ambo. Kwa hiyo walipanda nae kikawaida kabisa, hii ni sawa na watu kutoka mwaka mmoja na kuingia mwingine kimazoea kwa sababu hata miaka iliyopita waliweza kuingia kimazoea hivyo hivyo. 

Biblia inasema Wanafunzi wengi wa Yesu aliopanda nao boti wengi wao walitokea katika jamii ya wavuvi. Kwa hiyo kazi ya kusafiri ziwani au kuendesha boti ilikuwa ni kazi waliyoizoea. Hata kuingia ndani ya Boti hakikuwa kitu cha ajabu sana kwao.

Pia hata kusafiri na Boti kwenda ng'ambo nyingine pia hakikuwa kitu cha ajabu kabisa kwao kilikuwa ni kitu cha kawaida kabisa. Pia Biblia inasema siku ile kulikuwa na Boti zingine pale, kwa hiyo  ilikuwa ni kawaida kabisa kwao.

Kwa hiyo wanafunzi waliingia ndani ya boti kwa mazoea. Hii ndio maana nakuambia katika hili jambo la kwanza kuwa Usije ukafanya makosa kama haya kwa kwenda na kuishi kimazoea kwa sababu kuna gharama kubwa sana.

Mazoea yanakutengenezea mazingira ya kujitegemea na hayakupi nafasi ya kumtegemea Mungu. Kwenye Biblia hakuna kitu kinachoitwa kujitegemea bali kuna  kumtegemea Mungu. Pia mazoea yanakuondolea sababu ya kuomba kwa hiyo unajikuta huombi. Hata unakuta watu wanasafiri kwa basi  na  hawaombi kabisa muda wa safari.

Pia hata wakiamka asubuhi unakuta hawaombi hata katika shughuli zao napo huwa hawaombi. Siku ukiwakuta wanaomba ni kwa sababu kuna shida au kuna pressure fulani hivi ambayo inawasukuma kuomba. Hii yote ni kwa sababu ya mazoea maana mazoea huwa  yanaondoa msukumo ndani yao  wa kuomba. 

Mazoea yanakupa ndani yako mfumo wa kutokujiandaa  kwa ajili ya mazingira mengine bali mazoea yanakufanya uwe katika  mazingira yale yale.  Kuishi kwa mazoea kunakufanya usiwe na mpango wa kubadilika  sababu mazoea hayana mpango wa kubadilika na  yanatarajia kuishi kama jana na kutembea na Yesu kama jana. Kwa hiyo hayakuandai  kwa ajili ya mabadiliko na ndio maana ni hatari sana kuishi kwa mazoea.

Pia mazoea hukufanya uone ya kwamba ule ujuzi ulionao uone kuwa  unatosha na hujisikii kwenda kujiendeleza.  kwa sababu mazoea ndani yake yanatengeneza kitu kinachoitwa ujuzi fulani. Mfano mtu amejifunza kushona viatu mtaani kwa sababu anapata hela sasa na kwa sababu ya kuzoea kushona  hasikii msukumo ndani yake wa kutaka  kujiendeleza. Hata katika shughuli zingine (za biashara hata huduma za kufundisha neno la Mungu kama hizi zetu) kwa sababu ya mazoea watu hawana msukumo wa kusoma au kujisomea zaidi. Kama sisi wahubiri kwa sababu tu ya kuzoea kufundisha neno la Mungu  unakuta hata huulizi kitu Mungu ili akusemeshe kitu cha kwenda kufundisha ila wewe unajipangia tu. 

Nilipokuwa naanza huduma miaka ile ya 80 Mungu alinisemesha kuwa Nisiende na kuiishi kwa mazoea”. Hili jambo Mungu amekuwa akinikumbusha mara kwa mara. Madhabahu ya Jumapili hii na Jumapili nyingine haiwezi kufanana hata ya asubuhi na mchana au jioni ni tofauti kabisa, siwezi kutumia mazoea ya asubuhi nihudumu mchana. Hairuhusiwi kabisa kwenda na kuishi kwa mazoea, Biblia imekataza.  Kwa hiyo kuepuka kosa hili ili uanze mwaka mpya  hakikisha usije ukaenda na kuishi kwa mazoea.



KOSA LA PILI. 

2.USIDHANI KUWA NI RAHISI KUZUIA BAHARI KUCHAFUKA


MARKO 4: 37

Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakaipiga mashua hata ikaanza kujaa maji.”


Biblia inasema Yesu alikuwepo ndani ya boti, usidhani ya kwamba kuwa na Yesu ndani yako bahari haitacha kuchafuka. Katika safari zote nilizokwenda Israeli kati ya safari 27 ni mara mbili tu nilikutana na mawimbi, wakati mwingine ile bahari ilikuwa shwari kabisa. 


Kosa kubwa sana ambalo watu wengi wanalifanya wakiwa na Yesu hawatarajii matatizo. Hata kama unamtumikia Mungu usije kudanganywa kuwa hautapata matatizo  kuwa ukiwa ndani ya boti yako bahari haitachafuka. Usikubali hivyo lazima kuna muda bahari itachafuka tu.


USHUHUDA

Siku moja nilikuwa mahali fulani kumtembelea mtumishi mmoja mke wake alikuwa amelelazwa hospitali. Sasa akawa anasema kwanini Mungu ameruhusu hili wakati namtumikia namna hii,kwa hiyo akaanza kulia. Nikamwambia kaa hapo nikusimilie habari zangu. Nikamsimulia mapito ya yangu niliyopita. Wakati namsimulia  akafuta machozi yake akawa ananisikiliza. Baada ya kumaliza kumsimulia akasema mwalimu haya unapitia wewe mwenyewe au ni ya mtu mwingine?


Nikamwambia haya ni mapito ninayopitia mimi. Akasema haiwezekani, akauliza sasa unapataje nguvu ya kuendelea kuwahubiria wengine? Nikamwambia waulize wengine wanaendeleaje na kazi wakati wana matatizo nyumbani kwao.


Usije ukamchukia Mungu kwa sababu unapitia magumu eti kwa sababu wewe ni Mkristo au umeokoka au unamtumika Mungu, kwenye biblia hakuna kitu kama hicho. Labda kama hujajua ya kwamba Yesu kuwa ndani ya gari, haibadilishi hali ya barabara. Kama barabara ina mashimo na unamwendesha Rais hakubadilishi hali ya barabara ikichafuka imechafuka. 


Kwa hiyo hata ukiwa na Yesu ndani ya Boti usifikiri ya kwamba upepo utamwagopa, au labda utaacha. Japo Yesu anaweza fanya kitu ila jua kuwa upepo unaweza tokea. Ile kwamba umeanza na Yesu mwaka huu haina maana kuwa bahari haitachafuka.


KOSA LA TATU.

3.USIMRUHUSU YESU ALALE AKIWA MAISHANI MWAKO 

Sababu Biblia inazungumza katika ile mstari wa 38,

MARKO 4:38

Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?

Unaweza ukawa na Yesu na ukamwacha akalala. Sasa Biblia imetukataza kuruhusu kitu cha namna hiyo, katika Luka 18:1-8 Biblia inasema kuwa imetupasa kumuomba Mungu siku zote wala tusikate tamaa. Na imekuwa ikizungumza kwa wale wenye haki wa Mungu ambao wamekuwa wakimuomba Mungu  usiku na mchana. angalia ule mstari wa 7 wa Luka 18. 


LUKA 18 :7

Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? 


ZABURI 121:1-8

“Nayainua macho yangu niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi?  Msaada wangu hutoka kwa BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi.   Hatauacha mguu wako usogezwe; Akulindaye hatasinzia;  Naam, hatasinzia wala hatalala, Yeye aliye mlinzi wa Israeli.  BWANA ndiye mlinzi wako; BWANA ni uvuli katika mkono wako wa kulia.   Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku.   BWANA atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako.   BWANA atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.”


Unaona Biblia ikituhimiza kwamba Mungu halali, lakini unaweza ukamwacha akalala. Biblia inasema “Yeye aliye mlinzi  hasinzii wala halali maana yake ana nafasi ya kukusiliza saa yoyote.  Lakini hawa wanafunzi wake kwa nini  walimwacha alale?


Biblia inasema katika

ISAYA 62:6-7

Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha Bwana, msiwe na kimya;  wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani.

Anazunguza juu ya kuzungumza na Mungu masaa yote yaani usimwache Mungu anyamaze.Sasa swali linakuja, hawa watu kwanini walimuacha akalala? Nimetafakari na nimegundua majibu makubwa mawili. 

I. Walimchukua Jinsi alivyo katika chombo, Biblia inasema walimchukua vile vile alivyo  maana yake walimchukua kama abiria. Hakumchukua kama Bwana na mwokozi wa maisha yao .Kama ilivyo watu wengi wanamchukua Yesu kama abiria na kumzungusha duniani ili awafikie watu. Kwa hiyo anakuwa abiria mioyoni mwao.

Labda kwa sababu walivyomtazama Yesu wakati ule wao ni tofauti na sisi kwa wakati huu. Maana Yesu alikuwa wa rika lao walijua familia anayotoka na walimuona kama kiongozi wa huduma na sio kama Bwana na Mwokozi wa maisha yao. Na kama alikuwa kiongozi wa huduma ina maana akina Petro walikuwa walinzi wake na sio Yesu kama mlinzi wao.

Kwa hiyo kama anaingia kwenye boti walimuona kama kiongozi wa huduma maana ni kawaida kwa kiongozi wa huduma kuwekewa walinzi kwa hiyo na wao waliona labda anatakiwa kulindwa. Lakini hata katika maisha haya, ni rahisi sana kumchukulia Yesu kama abiria, na unamwacha analala ina maana hana kazi za kufanya kumbuka nimekuambia kwenye kosa la kwanza kuwa USIENDE KWA MAZOEA.


Sasa utajiuliza kwanini walienda kumuamsha usifikiri walimuamsha ili atulize dhoruba la hasha, kwanza hata walikuwa hawajui kama anaweza kutuliza dhoruba, Maana pia kwanini hawakumpa yeye Yesu aendeshe chombo? Ni kwa sababu walivyomtazama walijua katokea katika nyumba ya useremala kwa hiyo hawezi endesha Boti. Kwa hiyo lazima uwe mwangalifu sana kuwa Yesu anakazi gani maishani mwako? usimchukue kama abiria katika maisha yako yaani asiwe na kazi ya kufanya.



KOSA LA NNE

4.USITEGEMEE IMANI ILIYOKUSAIDIA KUBEBA MIZIGO YAKO YA JANA IKUSAIDIE PIA KUBEBA MIZIGO YA LEO

Tunaona katika mstari wa 39-41

MARKO 4:39-41

Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?

Swali la kwanza la kumuuliza Yesu na mimi ningekuwepo ningeuliza kuwa unaposema hamna Imani Bado una maana gani?. Kwa sababu hawa watu walimuamini, maana tunaona alikesha usiku kucha akiomba Mungu kupata wanafunzi na Petro na akina Mathayo waliacha kazi zao na wakaja kufanya nae huduma. 

Sasa ilitakiwa wamuulize kuwa aliposema hawana imani bado alikuwa na maana gani? Kwa sababu hawa watu wasingekuwa wanashirikiana naye kama wangekuwa hawamuamini.. Maana walikuwa wanaenda nae kila mahali.

Lakini kwa kufuatana na swali hilo, walitakiwa kuwa na imani ya aina fulani ambayo ingewasaidia wakati wanapanda boti  maana inaonesha kuwa hawakuwa na imani nyingine ambayo ingewasadia katika kipindi ambacho wangetakiwa kuvuka katika Boti walipopata dhoruba. Kuna imani iliwapeleka ng’ambo  na walitaka kuitumia hiyo hiyo kuvuka ng’ambo nyingine kwa maana hiyo Yesu aliwauliza hamna imani bado? Maana yake walihitaji imani nyingine ya kuwavusha hapa maana wanakutana na mazingira tofauti tofauti na inatakiwai imani nyingine. Pia imani iliyokuvusha mwaka jana ni tofauti na imani itakayokuvusha mwaka huu kwa hiyo huwezi kutumia imani ya mwaka jana kuvuka mwaka huu.

Ndio maana walishangaa kuwa huyu ni nani basi hata bahari na upepo vyamtii. 



KOSA LA TANO

5.USIANZE SAFARI YA MAISHA YA MWAKA HUU BILA YA KUWA NA UHAKIKA KUWA YESU YUKO PAMOJA NA WEWE.


MARKO 6:45-52

Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande mashuani, watangulie kwenda ng’ambo hata Bethsaida, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Hata alipokwisha kuagana nao akaenda zake mlimani kuomba.  Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa katikati ya bahari, na yeye yu peke yake katika nchi kavu. Akawaona wakitaabika kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita. Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe, kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope. Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao; kwa maana hawakufahamu habari za ile mikate, lakini mioyo yao ilikuwa mizito.


Biblia inasema mara akawalazimisha “Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande mashuani, watangulie kwenda ng’ambo hata Bethsaida, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Hata alipokwisha kuagana nao akaenda zake mlimani kuomba” sasa huu mstari ukisoma kwa kiswahili unaweza usipate msisitizo wake sana ila ukiangalia kwa upana wake unaweza pata maana kidogo.  Lile neno akawalazimisha maana yake ni kulikuwa na ubishi katikati yao uliomfanya Yesu asiende pamoja nao.  Na wao wakawa tayari kuondoka bila Yesu. Kama walikuja  wote kwenye boti walitegemea anarudije peke yake? 

Biblia inasema waliondoka, sasa unaweza kuelewa wakati ule sijajua walivyokuwa wanamtazama Yesu kiasi ambacho wanaweza kudiriki kuondoka na kumuacha ng'ambo nyingine. Mtu yeyote anayemfahamu Yesu tunayemsema na anayesemwa kwenye Biblia hawezi kufanya kosa la namna hiyo kwa kujua.

Na hapa haijalishi mmegombana kiasi gani usije ukakubali kuanza safari bila Yesu. Musa aligoma wakati ule wana Israeli walivyomkasirisha Mungu na kutengeneza ndama na kuiabudu. Mungu akakataa akasema mtaenda na malaika uso wangu hauwezi kwenda nanyi maana nikishuka nitawaangamiza lakini Musa akamwambia Mungu uso wako usipoenda nami usituchukue hapa. Musa alikuwa anajua kuwa gharama ya kuchukua hatua moja katika maisha yake na safari yake bila kuwa na uhakika ya kwamba uso wa Mungu uko pamoja naye, wengi wangefurahi kuwa wako pamoja na malaika lakini unajua kama malaika wako, na Mungu ameshusha kiwango chake cha uwepo maana yake ameshusha kiwango chake cha heshima katika ile safari na Musa alikataa na kwa maana nyingine alisema siendi safari hii wala sisogei.


Sasa ni watu wachache sana ambao wanayo hiyo hali hii ya kutaka kusafiri kwa staili hiyo wengi sana husema kama Yesu hataki kwenda na mimi hiyo ni juu yake nitaendelea peke yangu kwani kabla sijakutana naye si nilikuwa naishi kwa hiyo asiniwekee masharti hapa ya kutaka niende naye. Na kuna watu wengine ambao wameanza mwaka huu staili hiyo Yesu huyu walioanza naye mwaka jana hawamtaki kwa sababu aliwabanabana sana kwenye maisha yao na kuona kwa sasa ni ghasia kwenda naye.

Sijajua kikundi ulicho nacho na wenzako ulionao wanakushabikia kiasi gani kwamba unaweza ukaenda bila Yesu. Sababu ni rahisi sana wenzako wakakubana ukaanza safari yako mwaka huu bila Yesu. 

Lakini pia inawezekana kuwa ni maswala ya mazaoea tu kiasi ambacho ukafikiri ya kwamba Yesu yuko pamoja na wewe kumbe hayuko pamoja na wewe, kumbuka habari za Mariam na Yusufu waliondoka Yerusalem bila kujua ya kwamba Yesu yuko katikati yao iliwachukua mwendo wa muda mpaka walipoanza kuona mgawanyiko wa kundi ndipo wanamtafuta mtoto. Sasa inakuaje watu mnaanza safari bila kuwa na uhakika kuwa mtoto mko nae. Mpaka mfike mwishoni mwa safari ndio mnagundua mtoto hamko nae pamoja. Huwa najiuliza swali maana huwa nasikia kwenye semina zetu watoto wanatangazwa kuwa hawawoni wazazi wao. Huwa nashangaa inakuaje mtu uende na mtoto na usiwe makini kuwa mtoto uko nae hapo.


Matendo ya Mitume 17:28

“Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake.”

Usijaribu kutembea bila Yesu maana ndani yake tunakwenda, tunaishi na tunakuwa na uhai wetu.


Biblia inasema  pasipo yeye hatuwezi fanya jambo lolote

Yohana 15:5

“Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.”

Siyo kwamba hatuwezi kufanya lolote lakini hatuwezi kufanya lolote katika kiwango ambacho Mungu anakitarajia. Kama unataka Mungu akutazame aone matunda utakayomzalia mwaka huu na aweze kuyafurahia inamaanisha lazima ahusike kwa sababu tawi peke yake haliwezi likazaa lazima liunganike na Yesu.

Jiulize swali umemzalia Mungu kiasi gani tangu tuanze Januari? Kuna kitu gani ambacho unaweza kuonyesha katika maisha yako na watu wakazama na kusema Yesu alikuwa pamoja naye. Wengine wamebeba mazoea ya wokovu wakifikiri wamembeba Yesu, wengine wamebeba dini wakifikiri wamembeba Yesu.

Jifunze kumsikiliza Mungu anasema kitu gani na si swala la mazoea. Iwe ni katika kupanga ratiba zako au umeitwa na watu au kusafiri hauhitaji mazoea maana kila mahali unaposimama pana ujumbe wake.

Huwezi kufanya kosa la kuingia Januari kwa mazoea, huwezi fanya kosa la kuingia Januari kwa kutegemea imani ya mwaka jana, huwezi kufanya kosa la kuingia Januari huna uhakika ya kwamba uso wa Bwana uko pamoja na wewe huwezi kumaliza hata siku moja.

Kama uso wa Bwana unaenda pamoja nawe uwe na uhakika na neema yake iko juu yako.



KOSA LA SITA

6. USIMUACHE YESU AKUPITE HATA KAMA ANATAKA KUKUPITA

Marko 6:48

“Akawaona wakitaabika kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita.”

Ukiendelea kusoma hapa utaona kuwa walifikiri ni kivuli, halafu walipomwona hawakufurahi walifadhaika, sasa unaweza kuelewa kwamba hawa watu hawakuachana vizuri kwa sababu hawakumtegemea YESU kutokea na hata alipotokea hawakufurahi. Lakini pia unaweza ukaelewa ni kwanini YESU kawakuta hawa wanavuta makasia wanahangaika akataka kuwapita na hawa ni watu wake amewakuta katikati ya shida kwanini awapite?  Ndio maana nakuambia usifanye kosa la namna hiyo hata kama anataka kukupita.

Kwa sababu inawezekana kabisa ukapita kwenye eneo,kipindi fulani cha maisha na inawezekana kabisa wale unaowategemea wote kwa pamoja hamjafikia imani mnayotakiwa kuwa nayo haijalishi mko wangapi kama hamna hiyo imani mnayotakiwa kuwa nayo kwenye hicho kipindi mtakwama. Ndio maana wote wale walikwama, Biblia inazungumza kuwa walipata shida kwa sababu kwenye kile kipindi walijaribu kuvuta makasia. Haijalishi utavuta kasia halafu unashangaa anataka kukupita, usije kumruhusu akupite.

Ukisoma habari za Bathimayo alipokuwa kwenye  mlango wa Yerusalem, nilisoma ile habari Alafu nikashangaa sana YESU alipita na kumponya upofu wa Bathimayo Lakini hakurudi tena Yeriko. Kwa maana alikuwa anaendelea na shughuli zake na kwa sababu alikuwa ni kipofu kwa hiyo hakuweza kumfuata Yesu kule aliko na Biblia inasema aliposikia kelele akauliza wakamwambia Yesu wa Nazareth anapita Biblia inasema “Bathimayo akaanza kupiga kelele Yesu mwana wa Daudi unirehemu” na kila akipiga kelele sauti inaenda juu na ilikuwa juu kiasi ambacho wale watu waliokuwa wanamzunguka wakaona anawakera wakamwambia”Nyamaza unapoteza muda tu huoni alivyozungukwa na watu wengi unafikiri atakusikia” sikia kuna sauti ya kilio ya kawaida na sauti ya kilio ya imani na sauti ya Imani itamsimamisha YESU haijalishi amezungukwa na watu wengi kiasi gani, lakini anapoisikia lazima atapiga breki na kusema “Mwiteni aje hapa" .

Ndio maana unahitaji kung’ang’ana mbele za Bwana na kumwambia Mungu nisaidie usiniache. Sijajua kwa upande wako Lakini unapokaa kwenye uwepo wa Mungu namna hii labda kama unaenda kanisani, au kwenye mkutano na watu ni wengi sana na sio rahisi sana kukutana na kila mtu alieko mahali pale. YESU hategemei mhubiri kukuhudumia unaweza ukaita ukasema “Yesu hii ibada ni ya kwangu nimeisubiri hii siku usinipite"

Nimeona watu wa namna hiyo kwenye mikutano yetu.


USHUHUDA I 

Wakati fulani tulikuwa Mbeya kwenye semina, Wakati tunamaliza semina ili twende mahali pengine, nikaletewa meseji inasema Mtafute huyu mtu aliyetoka Tukuyu. Kutoka Tukuyu  kuja kwenye semina Mbeya mjini  ni kama kilomita 100 hivi na alimleta mtoto wake aliyepooza na  hanyanyuki. Wakati wa semina alinyanyuka na alirudi nyumbani anatembea. Mimi nilikuwa sijui ila nilileletewa meseji kuwa mtafute huyu mtu upate ushuhuda wake. Sikia mimi sikujua Lakini YESU alijua na lazima alimpigia Mungu kelele hii zamu isinipite. Kisikusumbue ni watu wangapi wanakusumbua, mazingira yanayokuzunguka, kwa YESU ipo rehema na DAMU yake itakufunika.


USHUHUDA II

Miaka ya themanini wakati Mungu ameweka wito mzito ndani yangu nilipita kwenye kanisa la Anglikana sio mara nyingi utakuta watu wanasali kanisani mchana nilikuwa naenda ule muda wa Break nasali kwa muda wa saa moja Alafu narudi kazini,. Nilikuwa ninaomba maombi sio mepesi sana nikamwambia Mungu”unapopita mji huu kutafuta watumishi au mtu utakaosimama nao naomba usinipite haijalishi madhaifu yangu lakini usinisahau na unitumie unavyotaka”

Kwa sababu Mungu hamtafuti alie kamili  anamtafuta alie tayari, au wachafu yeye atawasafisha kwa Damu yake, na hamna sababu ya kuwa na hofu kama una hofu tengeneza maisha yako.


USHUHUDA III

Wakati fulani baba akiwa ameugua ghafla akalazwa kule Nkwarungo Kiilimanjaro na nilipofika pale madaktari wakaniita ili kunieleza hali yake. Nilimtoa  Mbeya kwa ndege kumleta kwa matibabu Kilimanjaro maana alianguka ghafla tu. Sasa nilipokuwa hospitali Nkwarungo  madaktari wakasema hawajuia kwanini anaendelea kuishi maana kuna damu imevuja kwa ndani baada ya mpasuko na wakasema tutamfanyia  operation. Nikasema haina shida ili mradi tu mkitaka kufanya hivyo nijue.

Tukaelekea wodini aliko baba, tulikuwa na  mama mzazi, kabla ya kuanza kuzungumza na baba mama akaniita pembeni kidogo akasema nafikiri kuna shida hapa maana madaktari wanapita sana hapa mara kwa mara kuchukua vipimo kila baada ya muda mfupi..kwa hiyo kimemsumbua sana baba yako hebu jaribu kuongea nae. 

Basi nikaenda alipolazwa baba, nikavuta kiti nikakaa karibu na mahali alipokuwa amelazwa nikamuuliza  “baba unaogopa kufa? maana nimeomba kwa Mungu akuongezee muda wa kuishi lakini kama unaogopa kufa tutengeneze na Mungu” Biblia inasema kufa kwetu ni faida kwa hiyo ndani yako kama unaogopa kufa kuna shida mahali. Mbinguni  ni nyumbani kwa Mkristo  na kifo ni mlango wa kukupeleka nyumbani (Mbinguni), japo mwili lazima utapiga kelele tu.



KOSA LA SABA.

7.YESU AKIAMUA KUTOITULIZA DHORUBA USIMKASIRIKIE BALI ENDELEA KUOMBA  NA KUFUATA MAELEKEZO YAKE.

Hili ni eneo ambalo unahitaji kulielewa sana kwa sababu si kila mtu atapita mahali ambako pako shwari.

Kila mtu anapita kwenye dhoruba yake na si kila dhoruba ni mbaya.

Warumi 8:28.

28 Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.

Simama kwenye kusudi la Mungu shetani hawezi kukuzamisha atajaribu kila namna lakini atashangaa ukisimama kwa upya.

Kuna matatizo mengine Mungu anayaruhusu kwa ajili ya kukujengea msuli wako kwa ajili ya mambo yaliyopo mbele yako.

Yesu aliomba “kikombe hiki kiniepuke” alikuwa anajua kabisa angeweza kuamuru jeshi la malaika kumtetea na kumpigania, angeweza kuwatoroka, lakini Biblia inasema mbigu zilinyamaza kwa sababu Mungu hakuwa na mpango wa kumwondolea msalaba,kwa sababu msalaba ungeondolewa hakuna mahala tungekombolewa.

Mungu akinyamaza usikasirike, endelea tu kuomba kwa sababu inawezekana ni jambo bado majira yake.

Tatizo tunatembea katika majira ambayo tunahisi tunapopata matatizo tunahisi tumepungukiwa imani lakini kumbe hatujajua ni sehemu ya safari au sehemu ya maisha.

Hakuna mtu hapa Duniani atayekuambia matatizo ni mazuri. Lakini tunapotembea hapa Duniani hakuna mtu yeyote ambaye hatakutana na matatizo, kwa hiyo usijaribu kuishi na mawazo kwamba hautakutana na matatizo.

Hata Yesu anazungumza juu watu ambao wanamsikiliza kwamba nyumba zao zitapigwa na dhoruba lakini yule anayelisikiza Neno la Bwana na kulitenda ni kwamba dhoruba itakuja na kuipiga nyumba lakini haitaanguka, kwa sababu alifuatilia maelekezo ambayo alikuwa amepewa.

Wenzake na Daniel yaani Meshack, Shadrack na Abedinego wakiwa Babeli walipotakiwa kuisujudia ile sanamu walikataa wakaendelea kumwabudu Mungu wao. Wakashitakiwa wakapelekwa mbele ya mfalme,wakamwambia mfalme hujui uhusiano tulionao na Mungu wetu. Wakasema sisi tuko tayari kufa kwenye hili tanuru la moto hata Mungu akitunyamazia kwenye hili tanuru tuko tayari kufa kwa ajili yake waliingizwa kwenye tanuru la moto

Walimkuta mtu anasura kama ya Mwana wa Adamu na kumbe ni Yesu alikuwa anawasubiri ndani ya tanuru la moto. Kwanini asiwasaidie nje hadi kawasubiri waingie ndani ya tanuru la moto? Jibu ni watu wengine watajuaje ya kuwa yupo Mungu ambaye anaweza waokoa watu hata katika shida kubwa namna hiyo!

Ni rahisi sana kumziria Mungu unapopita kwenye matatizo na hakusaidii.Lazima kuna sababu fulani wewe endelea kuomba, usichoke,wala usikate tamaa, lakini endelea kufuata maelekezo anayokuelekeza katikati ya dhiki hiyo.Ndio maana wakati mwingine anakupitisha kwenye bonde la uvuli wa mauti, ila hakuondoi , anahakikisha unapita.

Wale wanafunzi walifadhaika kwa sababu Yesu alitembea juu ya dhoruba na mawimbi hakuyatuliza. Kwa sababu waliwahi kumwona akituliza dhoruba, lakini leo anawaona wanahangaika hawasaidii. Walifikiri angetuliza dhoruba ila yeye anatembea juu ya ile ile dhoruba 

Walifadhaika kwa sababu walimzoea Yesu anayewaondolea matatizo si Yesu anayewapitisha kwenye matatizo.


Yesu anaweza kuja kwenye maisha yako na  akatembea katikati ya matatizo yako,ili kukupitisha.Shida ni kuwa kila tatizo unamwona shetani na shetani anaweza kutumia hayo mazingira akakuvuruga kweli.Lakini unaweza ukaamua katikati ya shida ukamwona Yesu,kwa sababu yupo hapo hapo. Anasema “niite katikati ya matatizo nami nitakuokoa” lakini anapokuja anatembea juu ya majaribu.

Hapa ndio mwisho wa hili somo.Hakikisha somo hili unaliweka kwenye matendo. ubarikiwe sana. Nakutakia mwaka wa baraka maishani wako uweza wa Mungu uwe juu yako na ufanikiwe katika kila ulifanyalo.

Post a Comment

0 Comments