100/recent/ticker-posts
KANAANI MPYA - Lisikilizeni Neno la Bwana............. MAOMBI NA MAOMBEZI --- Tupigie; +255767-155-623 Ujumbe mfupi/Whatsapp; +255620-179-783

KARAMU AU SHEREHE YA WAMWAMINIO YESU KRISTO


KARAMU AU SHEREHE YA WAMWAMINIO YESU KRISTO

Mwl:Jovin John

KANAANI MPYA MINISTRY

Karamu au Sherehe ya wamwaminio Yesu Kristo ni malipo kwa ajili ya watakatifu wote walioliamini jina la Bwana wawapo duniani.

Isaya 25: 6-9

“Na katika mlima huu Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana. Naye katika mlima huu  atauharibu uso wa sitara iliyowekwa juu ya watu wote, na utaji ule uliotandwa juu ya mataifa yote.Amemeza mauti hata milele na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote, na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote maana BWANA amenena hayo. Katika siku iyo watasema, tazama huyu ndiye Mungu wetu, ndiye tuliyemungoja atusaidie, huyu ndiye BWANA tuliyemngoja, na tuushangilie na kuufurahia wokovu wake”

Hii itakuwa ni siku ambayo kila aliaminiye jina la Bwana na akauhuishi utakatifu atafurahi na kushangilia maana mateso, dhiki, huzuni, njaa, matatizo na magonjwa havitakuwepo tena.

Itakuwa ni furaha baada ya mateso na adha ya ulimwengu huu, na  ni wakati ambapo kila chozi litafutwa nasi tuliokombolewa tutarukaruka kama ndama wawapo zizini.

Isaya 35: 10

“Na hao waliokombolewa na BWANA watarudi , watafika Sayuni wakiimba, na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao, nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia”

Hapa ndipo kila mtu aliyeliamini na kuliitia jina la Bwana na kuachana na matendo mabaya ya dunia ataifurahia thawabu yake ya kuishi maisha ya Utakatifu duniani, nayo furaha itatawala katika nyuso za watakatifu nao wataona malipo yao ya kumngoja Bwana kwa zaburi huku wakiutunza utakatifu na wajapodhihakiwa na kutukanwa lakini hawakuiacha ile neema waliyopewa mara moja na MUNGU.

Taabu, dhihaka, masumbuko, matukano, shida na adha za kila namna walizokutana nazo  katika wokovu si bure, malipo yake yatakuja kwa muda ambao aujua Mungu.

1Wakorintho 15: 58

“ Basi ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA siku zote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu sio bure katika Bwana”

Ndugu zangu katika Kristo yatubidi kuimarika na kuzidi kuitenda kazi ya Mungu hususani katika ulimwengu huu ambao umejaa machukizo ya kila namna ukitawaliwa na tamaa za kila na namna, litangazeni jina la Bwana wala msilionee aya kwa maana yeye ndiye aliyeumba Mbigu na nchi na vitu vyote ni mali yake, yeye ndiye mwanzo na mwisho ajuaye mwanzo na mwisho wa kila mmoja.

Kwa pamoja tuzidi kusonga mbele tukiilinda na kuithamini ile neema tuliyokabidhiwa mara moja idumuyo katika kuutunza utakatifu, huku tukiingoja siku ile ambayo kila mtu atapewa taji yake na Bwana atamlipa kila mtu sawasawa na matendo yake.

Isaya 35: 3-4

“ Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea, wambieni walio na moyo wa hofu, jipeni moyo, msiogope, tazama Mungu wenu atakuja na kisasi na malipo ya Mungu, atakuja na kuwaokoa ninyi”

Lakini je tunawaza nini juu ya Bwana?Kuna wengine ambao wamekata tamaa kutokana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika maisha ya huduma na kuutunza utakatifu, yamkini wengine kugeuzwa Imani na kusema kuwa huenda Mungu hayupo. Aidha kuibuka kwa adha mbalimbali katika ulimwengu huu mfano magonjwa kama Corona (COVID 19) imekengeusha Imani ya baadhi ya watakatifu wakihoji kwamba Mungu angelikuwepo na anasikia maombi ya watakatifu asingeacha umati wa watu unaoendelea kuangamia kwa adha hizi za dunia.

Hakika haya ni mawazo ambayo yanamfedhehesha Mungu ila yeye yupo na kazi zake zadumu hata milele naye atabaki kuwa Mungu kwa wote wenye mwili.

Nahumu 1: 9

“ Mnawaza nini juu ya BWANA? Yeye atakomesha kabisa, mateso hayatainuka mara ya pili”

Mawazo ya Bwana si kama yetu, yeye atuwazia mema kila kukicha, maana yeye ndiye aliyetuumba na hatamuacha hata mmoja ambaye ameliamini jina lake mpaka siku ile ya karamu iliyoandaliwa.

Isaya 55: 8-9

“ Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu, asema BWANA. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu”

Hivi ndivyo Mungu wetu atuwaziavyo na awaza kumpa kila mtu vile apendavyo lakini mwisho wa yote atuwazia mwisho mwema wa kuisherekea ile karamu nzuri iliyojaa vinono na urojorojo.

Tusikubali kikiri udhaifu na kushindwa tukaikosa karamu au sherehe iliyoandaliwa kwa ajili yetu na mwokozi wetu Yesu Kristo.

 Imefika wakati sasa hata aliye dhaifu na aseme mimi ni hodari.

Yoeli 3:9-10

“ Tangazeni haya kati ya mataifa, takaseni vita, waamsheni mashujaa, watu wa vita na wakaribie, na wapande juu. Yafueni majembe yenu yawe panga, na miundu yenu iwe mikuki, aliye dhaifu na aseme, mimi ni hodari”

Simama imara, fanya kazi ya Bwana, tunza utakatifu karamu inayoandaliwa na Bwana wetu Yesu Kristo sio ya kukosa.

Mungu akubariki sana karibu tena katika kipindi kijacho.


UBARIKIWE SANA

Post a Comment

0 Comments