100/recent/ticker-posts
KANAANI MPYA - Lisikilizeni Neno la Bwana............. MAOMBI NA MAOMBEZI --- Tupigie; +255767-155-623 Ujumbe mfupi/Whatsapp; +255620-179-783

KUSHINDA KATIKA NYAKATI ZA KUSHINDWA - Mwl Jovin John

KUSHINDA KATIKA NYAKATI ZA KUSHINDWA

KANAANI MPYA MINISTRY 

Bwana Yesu Asifiwe!!!

Danieli 6:12-17

“Ndipo wakakaribia wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, katika muda wa siku therathini, ila kwako Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika. Basi, wakajibu wakasema mbele ya mfalme, yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale walioahamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku. Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli; akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa. Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee, mfalme ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lolote lililo marufuku, wala amri yeyote iliyowekwa na mfalme. Basi, mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli katika tundu la simba. Mfalme, akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya. Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu, naye mfalme akalitia muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lolote katika habari ya Danieli”.

 

Danieli mtumishi wa Mungu baada ya kutenda kazi kwa uaminifu katika ofisi ya mfalme, hatimaye maadui zake wakatafuta namna ya kumtoa katika ile nafasi, ndipo wanakosa upenyo maana kwa uaminifu aliokuwa nao Danieli na bidii katika utumishi wake basi alimpendeza sana mfalme. Ndipo wakapata upenyo wa kupitia imani yake kwa Mungu na kupitisha sheria ya mtu awaye yote asiweze kumwabudu Mungu katika nchi ile isipokuwa wamwabudu mfalme. Danieli akasema hili haliwezekani kamwe na kuendelea kumwabudu Mungu wake huku amefungua madirisha akipiga magoti na kuomba kila siku mara tatu. Tazama sasa kama ilivyo hukumu ya mtu atakayekengeuka sheria iyo ni kutupwa katika tundu la simba, Danieli anakamatwa na kutupwa katika tundu hilo lenye simba wenye njaa kali. Nini hatma ya Danieli fuatilia ushuhuda huu……………..

 

Ushindi wa Danieli

Danieli 6: 19-23

“Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba. Naye alipokaribia akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena akamwambia Danieli; Ee Danieli mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa? Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma, malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme sikukosa neno. Basi, mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli akatolewa katika lile tundu, wala dhara lolote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake”

 

Je waona ambavyo Danieli  ni kama aliachwa kwanza na Mungu wake mpaka akatupwa katika tundu la simba wenye njaa kali?, lakini wakati wa mwisho ndipo Mungu anamuokoa hivi ndivyo ilivyo akili yetu inapofikia mwisho ndipo Mungu anapoanzia. Ni wakati ambao maadui zake Danieli walidhani imekwisha na hawatamuona tena Danieli lakini hawakujua kuwa, Mungu wake aliyekuwa akimtumikia aweza kufanya chochote na kwa muda wowote. Na huu ndio ushindi katika nyakati za kushindwa.

 

Je unajua nini kilitokea kwa Shedrack, Meshack na Abednego baada ya kukataa kuisujudia sanamu aliyoisimamisha mfalme?

Tufuatilie ushuhuda huu…..

Danieli 3: 8-23

“Basi baadhi ya Wakaldayo wakakaribia, wakaleta mashtaka juu ya wayahudi. Wakajibu, wakamwambia mfalme Nebukadreza, Ee mfalme, uishi milele, Wewe Ee mfalme, ulitoa amri ya kwamba kila mtu atakaposikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, ni lazima aanguke na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu; na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa katika tanuru ya moto uwakao. Wako Wayahudi kadha wa kadha uliowaweka katika mambo ya wilaya ya Babeli , yaani, Shadraka, na Meshaki, na Abednego; watu hawa Ee mfalme, hawakukujali wewe  hawaitumikii miungu yako, wala kuabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha. Basi Nebukadreza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao shadraka, Meshaki na Abednego……………………”

 

Shadraka, Meshaki na Abednego wakatupwa katika tanuru ya moto tena ambayo imetiwa moto mara saba zaidi ya desturi yake, nao wakaanguka katika ile tanuru ilhali wamefungwa. Hatma ya watumishi wa Mungu ambao hawakuiacha imani yao na kumwabudu Mungu halisi. Je yuko wapi Mungu waliyemwabudu na kumtumikia? Mbona awaacha hata wakatupwa katika tanuru la moto?

Haya ni maswali ambayo mtu aweza kujiuliza sawa na wale waliowashitaki sambamba na mfalme walivyokuwa wakijiuliza lakini hawakujua kuwa Mungu yupo kazini na lile tanuru la moto kwake yeye ni kitu kidogo maana hata hao waliolitengeneza na kutia moto wapo chini ya mkono wake. Hatimaye analidhiirisha hili mwishoni na kutengeneza uhalisia wa somo letu kwa leo… KUSHINDA KATIKA NYAKATI ZA KUSHINDWA.

 

Ushindi wa Shadrack, Meshaki na Abednego

Danieli 3: 24-30

“ Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu wakamwambia, kweli, Ee mfalme, Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu……………………”

 

Je wataka kusikia habari za Sara mkewe Ibrahimu aliyejua ya kwamba hatapata mtoto daima na kwamba Ibrahimu atakosa mrithi kutoka kwake. Na hata Ibrahimu mwenyewe alijua ya kwamba hatapata mtoto kamwe kutoka kwa Sara mkewe, na Mungu alipomwambia alicheka. Malaika walipomwambia Sara habari za kuzaa mtoto alicheka pia maana aliiona kama ndoto ya mchana maana hata umri wake wa kuzaa ulishapita?

Ibrahimu acheka alipoambiwa na Mungu habari za kupata mtoto kwa Sara mkewe

Mwanzo 17: 15-17

“ Mungu akamwambia Ibrahimu, Sarai mkeo, hutamwita jina lake Sarai, kwa kuwa jina lake litakuwa Sara. Nami nitambariki, na tena nitakupa mwana kwake, naam, nitambariki, naye atakuwa mama wa mataifa, na wafalme wa kabila za watu watatoka kwake. Ndipo Ibrahimu akaanguka kifudifudi akacheka, akasema moyoni, Je! mtu wa umri wa miaka mia, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye miaka tisini atazaa?” 

 

Sara naye akacheka alipoambiwa na malaika habari za kupata mtoto

Mwanzo 18: 1-15

“ …………………………….Akamwambia, hakika nitakurudia wakati huu mwakani, na tazama , Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwaiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee?...........................”

Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Sara na Ibrahimu hakuna  aliyeamini kwa umri wao ya kwamba watapata mtoto, matumaini yalikwishapotea kabisa kiasi cha kukaribia kukengeuka imani maana twaona hata Mungu alipomwambia Ibrahimu habari za kupata mtoto alicheka huku na Sara naye akicheka aliposikia malaika wakimuahidi kupata mtoto. Mungu wetu hachelewi wala hawai ndivyo tunavyoweza kusema kwa ushuhuda huu na pale unapokata tamaa yeye ndipo hapohapo yupo kazini.

 

Ushindi wa Ibrahimu na Sara kupata mtoto

Mwanzo 21: 1-3

“ BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema. Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. Ibrahimu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia”

 

Je umewahi kufuatilia habari za wana wa Israeli kutoka Misri kwenda Kanaani na katika sehemu ambayo walifika huku hawaoni njia ya kusonga mbele, mbele yao kuna bahari, nyuma yao Farao na jeshi lake wanakuja kuwateka tena kuwaangamiza au kuwarudisha nchi ya mateso (Misri)....…

Kutoka 14: 9-12

“…………………… Hata Farao alipokaribia wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama Wamisri wanakuja nyuma yao, wakaogopa sana, wana wa Israeli wakamlilia Bwana. Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa uko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri? Neno hili silo tulilokuambia huko Misri tukisema, tuache tuwatumikie Wamisri maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani”

 

Wana wa Israeli hawaoni njia nalo tumaini lao kurithishwa nchi ya ahadi iliyojaa maziwa na asali  likapotea ghafra. Wakaanza kumnungunikia Musa aliyekuwa kiongozi wao. Je wafanye nini kama sio kusubiria kifo aidha kutupwa baharini katika bahari iliyopo mbele yao au kuuliwa na kundi kubwa la Farao linalokuja na hasira kwa ghadhabu kuu?. Lakini mwenyezi Mungu yupo kazini hakuwaacha kamwe na pale walipodhania ndio hatma yao ya maisha ndipo Mungu anatokeza ushindi.

 

Ushindi wa wana wa Israeli

Kutoka 14:21-22

“ Musa akanyoosha mkono wake juu ya bahari; BWANA akaifanya bahari irudi nyuma kwa upepo wa nguvu utokao mashariki, usiku kucha, akaifanya bahari kuwa nchi kavu, maji yakagawanyika. Wana wa Israeli wakaenda ndani kati ya bahari katika nchi kavu, nayo maji yalikuwa ukuta kwao mkono wa kuume, na mkono wa kushoto”

 

Niseme nini kwa habari za Yona ambaye alimezwa na samaki naye akakaa ndani ya tumbo la samaki siku tatu haoni nuru na anapumua kwa shida lakini mwisho akamwomba Mungu, naye Mungu siku ya tatu akasema na samaki akamtapika Yona nchi kavu, nikukumbushe pia habari za wana wa Israeli kudhihakiwa na kupigwa na Goliathi na kufikia hatma ya kukata tamaa ya kuwa hawamuwezi Goliathi lakini mwisho Mungu anatokeza ushindi tena kupitia kwa mtu waliyemdharau (Daudi),

 Hana naye mke wake Eli ilhali akiwa amekwisha kukata tamaa ya kwamba hatapata mtoto ndipo anapata mtoto katika ukongwe wake na kumwita jina Samweli na ndipo tutakuwa na ushuhuda mkubwa kabisa juu ya utendaji wa Mungu nyakati za mwisho tukikumbuka habari za Lazaro aliyekufa na kufufuliwa, Dorkas aliyekufa na kufufuliwa, mwanamke yule aliyekuwa anatokwa na damu miaka kumi na miwili akaponywa, viwete wakitembea, vipofu wakiona, waliopooza wakipona, wenye ukoma wakitakasika na miujiza mingi katika agano jipya lakini katika wakati ambao hawakujua kama wangeweza kutendewa hivyo. Mungu wetu hachelewi wala hawahi na hakika katika nyakati tunapodhania ya kwamba tumeshindwa yeye ndipo anapofungua mlango wa ushindi.

Yamkini unapitia magumu, shida, adha, dhihaka, matukano, magonjwa na taabu za kila namna na umefikia wakati wa kukata tamaa, ujumbe huu ukurudishie imani na matumaini sasa kwa Mungu wetu ukijua kuwa yeye yupo na aona taabu yako, naye asikia maombi na kilio chako, vumilia, ungoje ushindi wako kwa zaburi maana  pale akili inapofikia kikomo yeye ndipo anapoanzia. Hakika upo ushindi katika uvumilivu na imani. Soma neno la Mungu na angalia kwa jinsi ambavyo watu wengi ushindi wao ulipatikana mwisho, Mungu hajachelewa kwako atajibu kwa wakati wake.

 

Ubarikiwe sana na karibu katika kipindi kijacho

Mwl: Jovin John

 

 

Post a Comment

0 Comments