100/recent/ticker-posts
KANAANI MPYA - Lisikilizeni Neno la Bwana............. MAOMBI NA MAOMBEZI --- Tupigie; +255767-155-623 Ujumbe mfupi/Whatsapp; +255620-179-783

TOFAUTI YA MAOMBI NA MALALAMIKO MBELE ZA MUNGU

TOFAUTI YA MAOMBI NA MALALAMIKO MBELE ZA MUNGU

 Hesabu 21:5-6

Watu wakamnung'unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu.

Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa.

WEB: DRAYWADRAY MINISTRY

WhatsApp Group

KWAHIYO   Popote penye MANUNGUNIKO pana ADHABU,

Fikiri tu kwa nafisi yako ni mara ngapi umemnungunikia Mungu ukifikiri na kuwaza kwamba amekuacha na hajari kuhusu hapo unapopapitia,

Kuna saa Mungu anaweza kujibu kulalamika kwako na kuna saa Mungu anaweza kujibu hitaji lako,. Kwasababu sio kila aina ya majibu unayoyapata baada ya maombi ukafikiri ni salama  sana kwako, angalia kwanza wakati unaomba hicho kilichojibiwa ulikuwa umevaa nini, je ni moyo wa unyenyekevu wa kuachilia mapenzi ya Mungu? Au ni moyo uliojaa malalamiko kutegemeana na kipindi unachokipitia?


NGOJA TUSOME HII

Hesabu 11:5, 10,13,16,18, 19,20,33

Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu;.......................Basi Musa akawasikia watu wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema yake; na hasira za Bwana zikawaka sana; Musa naye akakasirika................... Nipate wapi nyama ya kuwapa watu hawa wote? Kwani wanililia, wakisema Tupe nyama, tupate kula.................Kisha Bwana akamwambia Musa, Nikusanyie watu sabini, miongoni mwa wazee wa israeli, ambao wewe wawajua kuwa ndio wazee wa watu hawa, na maakida juu yao; ukawalete hata hema ya kukutania, wasimame huko pamoja nawe........................... Kisha uwaambie watu hawa, Jitakaseni nafsi zenu kabla ya kesho, nanyi mtakula nyama; kwa maana mmelia masikioni mwa Bwana, mkisema, Ni nani atakayetupa nyama, tule? Maana huko Misri tulikuwa na uheri. Basi kwa sababu hiyo Bwana atawapa nyama, nanyi mtakula..........................Hamtakula siku moja, wala siku mbili, wala siku tano, wala siku kumi, wala siku ishirini;.....................lakini mtakula muda wa mwezi mzima, hata hapo nyama hiyo itakapotoka katika mianzi ya pua zenu, nanyi mtaikinai, kwa sababu mmemkataa Bwana aliye kati yenu, na kulia mbele zake, mkisema, Tulitoka Misri kwa maana gani?................................Kisha hapo hiyo nyama ilipokuwa ikali kati ya meno yao, hawajaitafuna bado, hasira za Bwana ziliwaka juu ya watu, Bwana akawapiga watu kwa pigo kuu mno.


Unaweza kusoma sura ya 11 yote ukipata nafasi, utaweza kuelewa kiundani sana habari hii lakini ninachotaka tutazame hapa ni nini watu hawa waliomba na walikuwa kwenye hali gani wakati wanaomba lakini pia ni nini Mungu aliwajibu, 


Ukisoma hiyo sura yote utaelewa kwamba watu hawa walimnungunikia Musa kiongozi wao Na Mungu aliyewatoa katika nchi ya utumwa na kufika hapo na ni ukweli kwamba hakuwahi kuwaacha kabisa isipokuwa kuna aina ya mazingira aliyokuwa akiwapitisha kutokana na na aina ya kulalamika kwao na wakati huo wao wakifikiri ndio wanaomba. 


Tuache hizo habari zote za nyuma bali tutazame hili hapo juu ambayo ndo pointi ya msingi, kuna aina ya watu pindi tu wanapopita kwenye magumu hujiona kama Vile Mungu amewaacha au amechelewa kujibu au hajali, kila mtu na tafsiri yake lakini kwa tafsiri hizo ndizo ambazo hupelekea kuanza kulalamika na Popote penye MALALAMIKO ni ishara kwamba pana MAUMIVU na popote penye maumivu lazima kuna kitu kilitangulia kabla ya hayo maumivu. sawa na zaburi inayosema;

“Nimedhoofika na kuchubuka sana, Nimeugua kwa fadhaa ya moyo wangu.”Zaburi 38:8

Kwahiyo mwili ukidhohofu ni dalili kwamba moyo umeshindwa kubeba hicho.


Turudi kwenye somo,

katika mazingira ya namna hii utakutana na;

Aina mbili za kujibiwa kwako;


AINA YA KWANZA

1.unaweza kujibiwa kutokana na unyenyekevu wako na kiwango chako cha imani na nguvu ndani yako ya kuachilia mapenzi ya Mungu, 

ukienda kwa mfumo huu uwe na uhakika Mungu hawezi kuacha kujifunua kwako na haya ndiyo majibu yadumuyo kwasababu ndani yake hubeba mapenzi ya Mungu kwako na sio mapenzi yako na zaidi sana hufunikwa na amani ya kristo, tunaposema amani ya Kristo tunamaanisha hata kama Mungu akikujibu tofauti na ulivyotegemea bado utabaki salama moyoni na utakuwa na amani ya moyo na utaendelea kuwa pamoja naye pasipo kumkasirikia wala kujisikia mnyonge.

KWA MFANO

1 Samweli 1:1-28

¹⁰ Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana akalia sana.

¹¹ Akaweka nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.

²⁰ Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa Bwana.


Huyu ni mwanamke ambaye alidumu katika ndoa yake kwa muda mrefu sana na maandiko yanasema mme wake alikuwa na wake wawili lakini mwanamke huyu alikuwa mke wa kwanza lakini hakupata watoto na maandiko yanasema Bwana alifunga tumbo lake. {kama ambavyo anaweza kuzuia jambo fulani lisitokee kwako kwa wakati unaoutaka wewe kwa ajili ya hatima yako ya baadae iliyo njema}

Baada ya muda mumewe akaamua kuoa mke mwingine aliyeitwa penina na mwanamke huyu akawa sababu ya huzuni kwa mke mkubwa aliyeitwa Hana maana maandiko yanasema mke huyu wa pili baada ya kuolewa alipata watoto wakike na wakiume maana yake ni wengi lakini kwa muda wote huo yule mke mkubwa aliyeitwa Hana hakuwa amepata watoto bado na biblia inasema mke mdogo akawa akimsikitisha na kumchokoza mke mkubwa kwa kutokuzaa kwake kwa lugha nyepesi alikuwa akimdharau na kumsimanga kama ilivyo jamii ya leo na kama walivyo wanawake wengi leo wanapojiona wamezaa na wengine hawajazaa huanza kuwakebei wenzao na kuwaona hawana maana pasipokuelewa hatima ya hao wanaowacheka na kuwadharau imebeba kitu gani kwa familia,jamii na hata taifa kwa ujumla. 

Biblia inasema mwanamke huyu akaishi katika hali ya huzuni na akawa mtu wa machozi,

Analia kwa sababu ya kukosa mtoto kama ilivyo shahuku ya kila mwanamke aliye kamili lakini pia analia kwa ajili ya matusi,manyanyaso na masimango kutoka kwa mke mwenza lakini zaidi pia lazima kuna namna jamii ilimchukulia na yako maneno yamkini aliyasikia mtaani na yakamuumiza moyo maana hata alipokuwa katika kuomba katika hekalu maandiko yanasema;

1 Samweli 1:12-16

Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za Bwana, Eli akamwangalia kinywa chake.Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa.Ndipo Eli akamwambia, Je! Utakuwa mlevi hata lini? Achilia mbali divai yako.Hana akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za Bwana.Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa.


Sijui kama unaelewa wakati aliokuwa anaupitia katika hali ya huzuni na kulia kwingi anaamua kukimbilia hekaluni/kanisani kwa ajili ya kupeleka huzuni yake mbele za Mungu na akiwa katika kuomba mtu ambaye angetakiwa kumtia moyo na kumpa maneno ya kumjenga kiroho na kumpa ujasiri kwa jinsi ya rohoni lakini mtu huyohuyo anamuuliza swali ambalo leo mchungaji au padre au shekhe akimuuliza swali hilohilo  muumini ambaye yupo katika hali hiyo ni rahisi sana kumpoteza na katika mia watakaoulizwa swali hilo  pengine ni wachache wanaoweza kuendelea kuabudu mahali hapo chini ya huyo mtumishi wa Mungu. 

Biblia inasema Eli ambaye ni kuhani wa Bwana akamuuliza mwanamke Hana akasema;

14 Ndipo Eli akamwambia, Je! Utakuwa mlevi hata lini? Achilia mbali divai yako.

Fikiri tu kwa namna ya kibinadamu upo katika hali kama hiyo na ndani yako una uchungu na huzuni alafu mtu ulitegemea akupe neno la faraja anakuuliza swali kama hilo na kuzidisha huzuni ndani yako maana nyumbani ni huzuni na kanisani nako unakutanana maneno ya kukuvunja moyo tena kutoka kwa kiongozi wa kanisa, kwa hali hiyo ni rahisi kuhama kanisa, ni rahisi kumuacha Mungu, ni rahisi sana kumuona kuhani hana roho wa Mungu nk. 

Lakini maandiko yanaonyesha Hana alizidi kuwa mnyenyekevu mbele za huyo kuhani na mbele za Mungu na mwisho wa yote Biblia inasema;

“Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa Bwana.” 1 Samweli 1:20

Kwenye ule msitari wa 28 Hana anasema;

1 Samweli 1:26-28

Akasema, Ee bwana wangu, kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyesimama karibu nawe hapa, nikimwomba Bwana.

Naliomba nipewe mtoto huyu; Bwana akanipa dua yangu niliyomwomba;

kwa sababu hiyo mimi nami nimempa Bwana mtoto huyu; wakati wote atakaokuwa hai amepewa Bwana. Naye akamwabudu Bwana huko.


Ile kumrudisha kwa Bwana ilikuwa ni kuondoa nadhiri aliyoiweka kwa Bwana, lakini jambo hili lilikuwa linampa Mungu utukufu na hivyo hakuna namna ambavyo Bwana angemuacha, na mtoto samweli akafanyika mtumishi wa Mungu na maandiko yanasema;

1 Samweli 3:19-20

Samweli akakua, naye Bwana alikuwa pamoja naye, wala hakuliacha neno lake lo lote lianguke chini.

Nao Waisraeli wote, toka Dani mpaka Beer-sheba, walitambua ya kwamba huyo Samweli amewekwa kuwa nabii wa Bwana.

ni kweli umechelewa kupata mtoto lakini je nani angejua katika tumbo la mama huyu Hana aliyekuwa akichekwa na kusimangwa kama katika tumbo hilohilo angetokea nabii wa MUNGU?

Nimekueleza yote hayo upate kuelewa faida iliyo ndani ya majibu ya maombi unayoweza kupeleka mbele za Bwana kwa unyenyekevu na kwa kuachilia mapenzi ya Mungu. 

Hana alipata jina kupitia unyenyekevu wake na kuachilia mapenzi ya Mungu kwa kila mazingira aliyokuwa anapitia, hakutazama ni wangapi wako upande wake au hawapo kabisa bali alimtazama Mungu na hata alipojibiwa bado matokeo ya majibu hayo aliyarejesha mbele za Bwana na kuyafanya kama sehemu ya sadaka kwa Bwana na alimtukuza Mungu kwa ajili ya mtoto wake lakini pia na Mungu alimfanya samweli kuwa mtumishi wake akasimama katika Israeli. 

  • Sasa ni mara ngapi umeomba ukaishia njiani kwa kukosa uvumilivu. 
  • Ni mara ngapi umeomba na hata baada ya kujibiwa hukumbuki kuunganisha sadaka ya shukurani kwa Bwana kama sehemu ya kuunganisha hicho ulichokipata na Mungu. 
  • Ni mara ngapi umeweka nadhiri kwa Bwana na baada ya kupata ulichokihitaji ukamsahau Mungu na mambo yalipoharibika ukaanza kumlaumu na kunungunika. 

Maana kupata unachokihitaji kwa Bwana ni jambo la kwanza na kukifanya kiwe sehemu ya Mungu ni jambo la pili maana yake hakikisha kile Bwana anachokubariki kinakufaa wewe lakini kinabaki na utukufu wa Mungu juu yake na kama hakiwezi kuwa na utukufu wa Mungu maana yake hujakiunganisha na Mungu; {mungu hana sehemu katika,hiyo bishara yako au uzao wako au mashamba yako nk}

  • Sijui kama ulishawahi kujiuliza kwanini watoto wanawekwa wakifu kwa Mungu makanisani wakati kabla ya watoto hao kupatikana watu hao waliomba kabla ya uchumba, wakaomba baada ya ndoa na wakaomba uzao mwema.  

  • Lakini pia sijui kama ulishawahi kujiuliza kwanini Mungu alimtokea ibrahimu na akamuhaidi mtoto na hata baada ya huyo mtoto kuzaliwa ambaye ni isaka kuzaliwa na kukua Mungu huyohuyo aliyemleta huyo mtoto anamwambia tena ibrahimu akamtoe sadaka kwa Bwana. 


Unaweza kuomba unavyoweza na Bwana akajibu kwasababu ni kanuni ya kiroho kwamba “Ombeni, nanyi mtapewa;.......” Mathayo 7:7 lakini kama hicho ulichokipata hakitamrudishia Mungu utukufu unaweza ukakimiliki lakini bado kisikufae,lazima tujifunze kuwa na moyo wa shukrani ili kwamba Bwana aendelee kuweka ulinzi juu ya vile ambavyo ametubariki.

“shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.”

   1 Wathesalonike 5:18 


AINA YA PILI

2.unaweza kujibiwa kutokana na kulalamika kwako maana yake unahitaji kuona Mungu akikutendea jambo fulani kwa faida yako na kwa mapenzi yako, na kwasababu zako tu. 

Majibu ya namna hii huwa hayana faida kwa Mungu kwasababu kinacholetwa kwako ni mapenzi yako au tamaa yako na sio makusudi ya Mungu na wewe, yale majibu ya kwenye namba moja huwa yana faida pande zote mbili kwa maana faida upande wako na faida upande wa Mungu yaani utapata kilicho haja ya moyo wako lakini kikiwa ndani ya mapenzi ya Mungu na Mungu pia atapata utukufu kutokana na hicho alichokujibu. Lakini haya majibu ya namba mbili yana faida kwako tu na bahati mbaya huwa hayadumu kwasababu hayana muunganiko na Mungu ambao ni endelevu na nyuma yake huwa kuna adhabu pia inayotokana na manunguniko na kutokutanguliza mapenzi ya Mungu katika hicho unachokiomba, kwasababu ukishaanza kuomba jambo lolote kwa sababu maalumu alafu jambo hilo likachelewa kuja ni rahisi sana kuanza kulalamika maana unatazama faida upande wako peke yako. 


Unaweza husielewe kwa haraka lakini 

  • wako watu walimuomba Mungu awafanikishe na kuwafungulia milango ya baraka lakini baada ya Muda watu hao walifirisika na hali zao za mwisho zikawa mbaya kuliko za mwanzo,sasa inategemea unamuomba Mungu akupe mtaji wa kufungua biashara kwasababu ipi maana swali la kujiuliza hapa ni hili kwamba, ninamuomba Mungu anipe mtaji nifungue biashara alafu nikishapata hiyo biashara sehemu ya Mungu katika hiyo biashara ni ipi????? 

Na Mungu akishaona sehemu yake katika hiyo biashara unayoiomba ndani ya moyo kabla ya kuipata hawezi kuacha kukupa. 


  • Wako watu waliingia katika ndoa na wakakaa muda mrefu pasipo watoto wakaamua kwenda mbele za Mungu na baada ya hapo matumbo yao yakafunguliwa na wakapata watoto lakini uzao wao haukudumu kwasababu kila baada ya Muda kupita watoto wao walifariki kwasababu mbalimbali na wengine walikua lakini katika hali ya ukengeufu na kupelekea maumivu kwa wazazi wao. 

Swali ni lile lile kwamba uliomba hao watoto kwa sababu zipi? 

Je ulimuomba Mungu akupe watoto baada ya kuona wadada wenzako wote wamepata watoto na wewe bado?? 

Je ulimuomba Mungu akupe watoto kama njia ya kuleta amani ndani ya ndoa baada ya kuona mmeo anaanza kukusumbua na mawifi wanakusimanga?? 

Je ulimuomba Mungu akupe watoto ili na wewe upate heshima kama mama??? 

Sikia Hana alikuwa anayapitia yote hayo lakini alipoenda mbele za Bwana na Bwana akamsikia na kumjibu mtoto yule hakumtumia kama fimbo ya kuwachapia waliokuwa wanamcheka wala hakumuona kama sehemu ya kufuta machozi yake bali alimrudisha kwa Bwana na akamfanya awe sehemu ya utumishi katika Nyumba ya Mungu, ndivyo Bwana anavyotaka na hiyo ndiyo kanuni ya kiroho na alichokifanya Hana kumpeleka samweli Nyumbani mwa Bwana hakikuwa  tofauti na tukio la ibrahimu kumtoa  isaka kama sadaka kwa Mungu. 


  • Wako watu walienda mbele za Mungu kuomba kazi na baada ya muda milango ikafunguka na wakapata kazi lakini hawakudumu kazini na hata waliodumu walifanya kazi katika mazingira magumu. 

Yamkini ulikuwa na nia njema na hiyo kazi lakini hukuifanya au hukuiunganisha kazi hiyo na Mungu. 

Jiulize tu kazi hiyo ilimpa utkufu Mungu kwa kiwango gani na saa ingine hata zaka hukutoa, hata kanisani hukuonekana tena baada ya kupata hiyo kazi. 


  • Wako watu huenda mbele za Mungu kuomba kuhuishwa upya roho zao kwa maana ya toba lakini baada ya muda hali zao au maisha yao ya kiroho huwa mabaya zaidi kuliko ya mwanzo kabla ya toba, namaanisha hurudi tena dhambini tena kwa nguvu na kwa kasi mpya kuliko mwanzo. 

Swali la msingi ni kuwa kitu gani kilikusikuma ukaomba toba je ulitaka maisha ya utakatifu mbele za Mungu au katika huduma yako au liko jambo ambalo ili uweze kulipata ilikuwa ni lazima uwe mtakatifu na baada ya kulipata umuhimu au sababu ya maisha matakatifu ikapotea??? 

sio mpango wa Mungu kumuachilia mtu kwenye dhambi lakini ukienda kuomba toba kwa mzaha na kwasababu zako binafsi huko ni kujidanganya na shetani atakusakama kuliko kawaida maana biblia inasema;Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. luka 11:26  lakini zaidi sana Ukienenda kimwili na matokeo yake yatakuja kwa jinsi ya mwilini na ukienenda kiroho na matokeo yake yatakuja kiroho maana yake katika mwili pana uharibifu lakini katika roho pana uzima wa milele ndivyo maandiko yanavyosema,Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. wagalatia 6:7-8

Sasa sina maana kwamba kila mtu aliyekwama kwenye maeneo yote hayo kwamba hiyo ndio sababu lakini najaribu kukutazamisha kwamba ukipeleka maombi yako mbele za Mungu kwa kutanguliza mapenzi yako na kiu ya namna unavyotamani kuona hicho unachokiomba kukiona kikitokea kwako, alafu ukasahau kutanguliza mapenzi ya Mungu na kuwa na moyo wa shukrani mbele za Mungu baada ya kukubariki  uwe na uhakika Mungu anaweza akakujibu kweli lakini majibu hayo yanaweza yasidumu au yakaja kwa kiwango kidogo tofauti na namna ambavyo ungeyaunganisha tena mbele za Mungu ili Mungu azidi kuwepo kwenye hilo kuhakikisha linakua na kuzidi kuwa bora katika mapenzi ya Mungu lakini pia ukiunganisha jambo lolote na Mungu maana yake unaruhusu ulinzi wa Mungu ukae juu yake,


najua pengine Sio rahisi sana ukaelewa lakini watazame wana wa israel hapo juu tulikosoma biblia inasema walianza kukumbuka vyakula walivyokuwa wanapata katika nchi ya utumwa na wakasahau yakwamba hapo walipo wako safalini kupelekwa katika nchi ya maziwa na asali ambapo huko ndiko nyumbani haswa na sio utumwani tena, lakini pia wakasahau muda wote ambao Mungu ametembea nao kwenye safari yao akiwalisha Mana jangwani na anawapitisha njia ndefu ili kuwaepusha vita nyingi ambayo wangekutana nayo njiani lakini  inafika saa wanakosa moyo wa shukrani  mpaka wanakidhihaki chakula cha Mungu alichokishusha kwao, 

Biblia yangu inaniambia Mungu alikasirika na Musa akakasirika, ndipo Mungu aliposhuka na akajibu kulalamika kwa hao watu, akawapa walichokitaka lakini ukisoma msitari wa 33 utaona chakula kile alichowapa kutokana na kulalamika kwao nyuma yake kilikuwa kimebeba adhabu kwasababu biblia inasema Bwana akawapiga kwa pigo kuu mno.

Walitazama haja za mioyo yao lakini hawakutazama mapenzi ya Mungu kwao ni nini.na zaidi hawakuwa na moyo wa shukurani kwa Bwana katika yale alitenda kwao. 


Yamkini kuna sehemu nyingi tunakwama kwasababu tunapeleka malalamiko mbele za Mungu na sio maombi na hivyo Mungu anajibu kulalamika kwetu.

Hata hivyo Rehema za Mungu ni kuu  mno, bado tungali na nafasi ya kuomba mapenzi ya Mungu kudhihirika kwetu katika yale ambayo tungetamani kumuona akijifunua kwetu.

Zaidi sana tuombe msaada wa roho mtakatifu pale tunapokielekea kiti cha rehema ili pengine kama kuna sehemu tulienda mbele za Mungu na tukatanguliza mapenzi yetu basi Bwana akumbuke rehema na aturehemu na atupe nafasi nyingine tena na kuachilia moyo wa shukrani ndani yetu hata kama hakutujibu kama tulivyotaka bado nafasi yake ndani yetu hisibadilishwe na chochote. 


Mungu wangu akubariki sana

MASOMO MENGINEYO




























Post a Comment

0 Comments